1,2,3. Ameita, mwenye kuita, kuhimiza kama kufanya kejeli,
iletwe upesi adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo hapana shaka itawashukia
makafiri. Wala hapana chochote cha kuzuia adhabu hiyo, kwani hiyo inatoka
kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu, ambako huko ndiko zinatoka nguvu zinazo
simama, na hukumu inayo tekelezwa.
4. Malaika na Jibrili wanapanda kwenda kunako toka amri yake kwa
siku ambayo urefu wake ni miaka khamsini elfu kwa mujibu wa hisabu ya miaka
ya duniani.
5,6,7. Basi, ewe Muhammad! Subiri uwastahamilie hizo kejeli zao,
na kuhimiza kwao adhabu, kwa subira isiyo kuwa na mbabaiko ndani yake wala
mashtaka. Hakika hao makafiri wanaiona hiyo Siku ya Kiyama ni kitu cha
muhali kutokea. Na Sisi tunaona kuwa ni jambo jepesi katika uweza wetu,
wala halina uzito wowote.
8,9,10. Siku mbingu itakapo kuwa kama fedha iliyo yayuka, na milima
itakapo kuwa kama sufi iliyo tiwa rangi na ikapigwa, wala jamaa hamuulizi
jamaa yake: Nini hali yako? Kwa sababu kila mmoja kajishughulikia nafsi
yake!
11,12,13,14. Watakuwa wakijuulishana wao kwa wao mpaka wajuane baraabara,
na ilhali hapana amuulizae mwenzie kitu. Kafiri atatamani lau ange pata
kujikomboa nafsi yake na adhabu hiyo Siku ya Kiyama kwa kumtoa mwanawe
awe ni fidia yake, au mkewe, au nduguye, au jamaa zake aliyo khusiana nao,
na wote waliomo duniani, apate kuokoka yeye tu!
15,16,17,18. Ewe mkosefu! Wacha hayo unayo yatamani ya kutaka kujikomboa
kwa fidia! Hakika huo moto, unawaka kweli! Utakubabua mikono yako, na miguu
yako, na viungo vyako vyote, utanadi kwa jina la huyo aliye iacha Haki,
na akaacha ut'iifu, na akakusanya mali akayaweka katika mabweta yake, wala
hakutoa haki ya Mwenyezi Mungu iliomo katika hayo mali!
19,20,21,22,23. Hakika tabia ya binaadamu ni papara, mwingi wa kupapatika,
na kutoridhika akifikiwa na lolote la karaha na uzito, na ni mwingi wa
kuzuia na kunyima akipata kheri na neema. Isipo kuwa wanao sali, ambao
wanadumisha Sala zao, hawakikosi hata kipindi kimoja. Hao Mwenyezi Mungu
huwakinga, na huwawezesha kutenda yaliyo kuwa ya kheri.
24,25. Na wale ambao katika mali yao ipo haki iliyo ainiwa iliyo
wekwa kwa ajili ya masikini mwenye kuomba kutaka msaada, na anaye jizuilia
kuomba pia. (Katika wanao zuilika kuomba wanaingia si wenye kustahi na
kuona vibaya tu, bali pia wasio weza kuomba kama watoto wachanga, wagonjwa,
na wanyama pia.)
26,27,28. Na wale wanao isadiki Siku ya Malipo, basi wanajitayarisha
kwa ajili yake; na wale wanao iogopa adhabu ya Mola wao Mlezi basi wanajikinga
nayo wala hawajitii katika jambo la kuwaletea adhabu hiyo. Kwani hakika
adhabu ya Mola wao Mlezi hapana hata mmoja anaye weza kuaminika nayo isimpate.
29,30,31. Na ambao wanazihifadhi tupu zao hata hawaemewi na matamanio
yao. Lakini kwa wake zao na masuria wao hawazihifadhi; kwa sababu hapo
hawalaumiwi kuifuata tabia ya maumbile. Basi mwenye kutafuta starehe ya
maingiliano kwa wasio kuwa wake na masuria, basi hao tena ni wenye kuikiuka
halali na kuingia katika haramu.
32,33,34. Na hao wenye kuzihifadhi amana za sharia na amana za waja
wa Mwenyezi Mungu, na walio lazimika nayo kwa Mwenyezi Mungu na kwa watu
bila ya kukhuni wala kupunja, na ambao kwa shahada zao wamesimama sawa
sawa kwa haki bila ya kuficha wanalo lijua, na wanao hifadhi Sala zao wakizisali
sawasawa kwa ukamilifu -
35. Watu wenye sifa kama hizo nzuri watakuwa ni wenye kuhishimiwa
mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu huko Peponi.
36,37,38. Kitu gani kinawapelekea hao walio kufuru kukujia mbio mbio
kutoka kuliani na kushotoni kwa makundi? Je, kwani kila mmoja wao ana tamaa
ya kuingia kwenye Pepo yenye neema, baada ya kusikia kuwa Mwenyezi Mungu
amemuahidi Mtume wake na Waumini kuwatia Peponi?
39. Basi nawaache hiyo tamaa yao ya kuingia Peponi. Hakika Sisi tumewaumba
wao kutokana na maji ya kudharauliwa.
40,41. Naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote, na magharibi zote
za siku, na sayari na hidaya, kwamba hakika bila ya shaka Sisi tuna uweza
wa kuwaangamiza, na kuwaleta walio wat'iifu zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko
wao. Wala Sisi hatushindwi kubadilisha huko.
Huenda ikawa inakusudiwa kwa "mashariki zote" na "magharibi zote"
ni maeneo ya mamlaka ya Mwenyezi Mungu yote ambayo hayana mpaka kama ilivyo
ashiriwa katika Aya 137 ya Surat Al-A'araf: "Na tukawarithisha watu walio
kuwa wanadharauliwa mashariki za nchi na magharibi zake ambayo tuliitia
baraka", kuonyesha sehemu zote za hiyo nchi inayo tajwa.
Na huenda ikawa makusudio yake ni mashariki za jua na mwezi na nyota
zote na sayari, na magharibi zao, kwa ajili ya kuonyesha vile vile ufalme
wa Mwenyezi Mungu wote. Na kwa hivyo inadhihirika kwetu kuwa vyombo vinavyo
kwenda katika qubba la mbingu vinachomoza kwenye upeo wa mashariki na kuchwa
kwenye upeo wa magharibi, au kwa uchache vinazunguka kutoka mashariki kwendea
magharibi kuizunguka nyota ya Pole, katika sehemu ya kaskazini ya dunia.
Kwani umbali wa Pole kwa nyota ni mdogo kuliko pahala unapo angalia, basi
nyota hapo haichomozi wala haichwi, bali hupiga duru ndogo kuizunguka North
Pole. Na kwa hiyo Aya inaashiria saa za usiku. Rejea kwenye kauli ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu: " Na alama na kwa nyota wao wanaongoka." Na kwa udhaahiri
wa kuchomoza na kuchwa ipo ishara ya kuzunguka kwa dunia, na hiyo ni neema
kubwa kabisa katika neema za Mwenyezi Mungu juu ya maisha katika sayari
hii. Kwani bila ya kuzunguka kwa dunia juu ya msumari-kati wake nusu ya
dunia ingeli pigwa na jua mfululizo muda wa nusu mwaka kaamili, na ingeli
nyimwa mwangaza kabisa nusu nyengine. Kwa hivyo uhai kama tulivyo uzoea
usinge kuwako.
Na tukifanya hizo mashariki na hizo magharibi ni za jua peke yake,
wachilia mbali nyota nyengine na sayari, basi itakuwa ishara ni kule kuchomoza
jua kila siku pahala pengine na kuchwa pahala pengine kila siku, au hata
katika kila dakika linapo pita juu ya dunia. Kwani jua kila dakika linakuchwa
pahala na linachomoza pahala papili mfululizo. Na haya ni katika mipango
ya Mwenyezi Mungu na miujiza ya uweza wake. Tazama pia maoni ya wataalamu
juu ya Aya ya 5 katika Surat Assaffat, na Aya 17 ya Surat Arrah'man.
42. Basi waachilie wakiporojoka katika upotovu wao, na wakicheza
na dunia yao, mpaka wakutane na siku yao waliyo ahidiwa kupewa adhabu.
43,44. Siku watakapo tolewa makaburini mbio mbio kumwendea huyo ataye waita, kama kwamba wamemweka ufundo na wakimuabudu duniani walivyo kuwa wakimkimbilia badala ya Mwenyezi Mungu, macho yameinama chini, hawawezi kuyanyanyua, yamegubikwa na unyonge na udhalili. Hiyo ndiyo siku waliyo kuwa wakiahidiwa duniani na wao wakiikanusha.