1,2. Kiyama ni Tukio litakalo tukia kwa haki, yaani
kwa kweli. Ni nini hicho Kiyama kitacho tokea kweli?
3. Na kitu gani kitacho kujuvya ukweli wake, na kitacho kupa sura
ya kitisho chake na shida zake?
4. Kina Thamudi na kina A'di walikanusha Kiyama kinacho wagutua walimwengu
wote kwa kitisho chake na shida zake.
5. Ama Thamudi basi walihilikiwa kwa tukio lilio pindukia mipaka
yote kwa ukali wake.
6. Na ama A'di waliangamizwa kwa upepo ubaridi na mkali,
7. Mwenyezi Mungu aliwasalitisha nao muda wa masiku saba, na siku
nane zilizo fuatana mfululizo, utaona walio patikana na upepo huo wamekuwa
maiti kama magogo ya mitende yaliyo kuwa matupu ndani yake. ("Masiku" ni
wingi wa "Usiku"; "Siku" wingi wake ni "Siku" vile vile.)
8. Je! Unamwona yeyote aliye bakia katika hao?
9. Akaja Firauni, na mataifa mengine yaliyo kufuru kabla yake, na
wale jamaa walio acha mwendo wa haki na vitendo vya maumbile wakafanya
vitendo vichafu kabisa hata miji yao ikapinduliwa juu chini.
10. Kila umma katika hawa walimuasi Mtume wa Mola wao Mlezi. Naye
Mwenyezi Mungu akawashika kwa kuwaadhibu kwa mshiko ulio zidi ukali.
11. Maji yalipo zidi ukomo wake, na yakapanda juu ya milima katika
tukio la tofani ya Nuhu, Sisi tulikupandisheni, yaani kwa kuwapandisha
wazee wenu wa asli, katika safina inayo kwenda baharini.
12. Ili kulifanya tukio hilo la kuwaokoa Waumini na kuwazamisha makafiri
liwe zingatio na mawaidha kwenu, na lihifadhiwe na kila sikio lenye kuhifadhi
linalo sikia.
13,14. Litakapo pulizwa barugumu kwa mpulizo mmoja, na ardhi na milima
ikaondolewa pahala ilipo, na ikavunjwa mara moja,
15,16. Siku hiyo ndiyo kitashuka cha kushuka, na mbingu zitapasuka
kwa kuondoka hukumu zake na sharia zake, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu
baada ya kuwa madhubuti zenye nguvu.
17. Na Malaika pembezoni mwake, na wapo Malaika wanane siku hiyo
watakao beba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi, juu ya Malaika hawa wengine.
18. Siku hiyo ndio mtaletwa kwa ajili ya kuhisabiwa. Wala haifichikani
siri yenu yoyote mliyo kuwa mkiificha.
19. Ama mwenye kupewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia,
atasema akiwatangazia furaha yake walio karibu naye: Chukueni msome kitabu
changu!
20. Mimi nilikuwa na yakini tangu duniani kuwa nitapata hisabu yangu,
basi nikajitayarisha nafsi yangu kwa mkutano huu.
21. Basi huyo atakuwa katika maisha yaliyo enea kupendeza.
22. Katika Bustani ya pahali na daraja ya juu.
23. Matunda yake yakaribu kwa kuyachuma. (kuyatunda).
24. Kuleni na mnywe kwa kula na kunywa kusio na karaha, wala maudhi,
kwa sababu ya vitendo vyema mlivyo kwisha vitanguliza katika siku za duniani
zilizo pita.
25,26. Ama mwenye kupewa kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto atasema
kwa majuto na huzuni: Laiti kuwa sikupewa kitabu changu, wala sikuijua
hisabu yangu!
27. Laiti kuwa kule kufa niliko kwisha kufa kungeli kuwa ndio kumalizika
kwangu kwa mwisho, wala nisingeli fufuliwa tena!
28,29. Hapana chochote nilicho kimiliki duniani kilicho nifaa. Uzima
wangu umenipotea, na nguvu zangu zimenitoka.
30,31,32. Wataambiwa walinzi wa Jahannamu: Mshikeni, na mfungeni
mikono yake kwenye shingo yake. Kisha msimtie popote ila ndani ya Moto
wa Jahannamu, kisha mfungeni kwenye mnyororo mrefu kabisa.
33,34. Hakika huyo alikuwa hamsadiki Mwenyezi Mungu Mtukufu, wala
hamhimizi yoyote kuwalisha masikini.
35,36,37. Basi hii leo huyu kafiri hana jamaa wa kumtetea, wala hana
chakula ila usaha wa watu wa Motoni, ambao kwa hakika ni mchanganyiko wa
damu na usaha. Hawakili chakula hicho ila wakosefu walio kusudia kufanya
maasi yao, na wakakamia kuendelea nayo.
38,39,40. Basi naapa kwa mnavyo viona katika vinavyo onekana, na
msivyo viona katika ulimwengu wa ghaibu, kwamba hakika Qur'ani bila ya
shaka inatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ulimi wa Mjumbe mwenye cheo cha juu.
41. Wala Qur'ani si maneno ya mtunga mashairi kama mnavyo dai. Ama
nyinyi ni chache mno imani yenu ya kuwa Qur'ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu.
42. Wala Qur'ani haisemi kwa maneno ya kumunyia munyia kama wanenavyo
makuhani mlio wazoea. Ni uchache mno kukumbuka kwenu na kuzingatia khitilafu
zilioko baina ya Qur'ani na maneno ya makuhani.
43. Hii ni uteremsho unao toka kwa Mwenye kuwaangalia walimwengu
wote kwa kuwaumba na kuwalea.
44,45,46. Na lau kuwa angeli dai kitu chochote ambacho tusicho kisema
basi bila ya shaka tungeli mshika akitoe kama mtu anavyo mkamata mtu kwa
mkono wa kulia akammaliza hapo hapo. Kisha bila ya shaka tungeli mkata
mshipa wake wa moyo, afe saa ile ile. (Biblia inasema katika Kumbukumbu
la Torati 18.20 "Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu,
ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine,
nabii yule atakufa.")
47. Na hapana yeyote katika nyinyi, hata ange kuwa na nguvu namna
gani, angeli weza kuzuia adhabu yetu isimfikilie.
48. Na hakika Qur'ani ni mawaidha kwa wanao fuata amri za Mwenyezi
Mungu, na wanaepuka makatazo yake.
49. Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba kati yenu wapo wanao
ikanusha Qur'ani.
50. Na kwamba hakika hiyo bila ya shaka ni sababu ya majuto ya wanao
ikataa, wakati watapo iona adhabu yao, na neema za wenye kusadiki.
51. Na hakika Qur'ani bila ya shaka ni Haki iliyo thibiti, isiyo
na shaka yoyote.
52. Basi mtakase Mola wako Mlezi, na dumisha kudhukuru jina lake.