1. Ametukuka, na amezidi baraka zake Mwenye kumiliki
peke yake uwezo wa kuendesha mambo ya viumbe vyote. Na Yeye, juu ya kila
kitu, anao uwezo ulio timia.
2. Ambaye ndiye aliye umba mauti na uhai kwa makusudio anayo yataka
Yeye, ili akufanyieni mtihani ni yupi katika nyinyi anaye fanya vitendo
sawa, na mwenye niya safi. Na Yeye ni Mwenye kushinda, wala hashindiki
kwa kitu, Mwenye msamaha kwa wenye upungufu.
3. Yeye ndiye aliye zizua mbingu saba zilizo pandana kwa mpango mmoja
sawa sawa. Huoni tafauti yoyote katika uundaji wa Mwenyezi Mungu, ambaye
rehema yake imeenea kwenye viumbe vyake vyote. Basi hebu tazama tena, unaona
khitilafu yoyote?
4. Kisha tazama tena, na tena! Jicho lako linakurejea mwenyewe bila
ya kugundua aibu yoyote, nalo limechoka.
5. Na hakika Sisi tumeipamba mbingu hii ya karibu, unayo iona kwa
macho, tumeipamba kwa nyota zinazo ng'aa. Na tumefanya katika hizo vimondo
vya kuwapopolea mashetani; na Akhera tumewaandalia adhabu ya moto unao
waka.
Mbingu ni kila kilicho juu yetu kikatufunika. Amesema Ibn Sayyidih:
Hiyo ni bahari ya anga na vyombo vyote viliomo ndani yake na vimondo.
Na sura wanayo iona wakaazi wa duniani katika masiku yaliyo safi ni kama
qubba la kibuluu lilio pambwa kwa nyota na sayari kama kwamba ni taa, kama
unavyo ziona nyota za mkia, au vimondo, vinakwenda angani vikiungua huko
juu ya ardhi. Na hilo qubba la kibuluu si chochote ila ni matokeo ya mwangaza
wa jua na nyota pamoja na takataka za vumbi zinazo ning'inia katika hewa,
na sehemu za hewa molecules zinazo tawanyika. Haya mbali na yanayo onekana
katika mwangaza nafsi yake ambayo huipamba mbingu hii ya karibu, kama vile
zile rangi nzuri nzuri za wakati wa kuchwa jua, au wakati wa kuchomoza
jua alfajiri, na mianga ya njia za nyota, miangaza ya kaskazini, na miangaza
ya katika sehema za Polar regions. Na hayo yote yanayo onekana ni matokeo
ya kuingiliana mwanga pamoja na funiko la anga la ardhi na uwanja wake
wa smaku, magnetic field.
6. Na kwa ajili ya wasio muamini Mola wao Mlezi tumewawekea adhabu
ya Jahannamu. Na huo ndio mwisho muovu kweli kwao.
7,8. Wakitiwa humo watasikia sauti mbaya ya kuchusha, na huo moto
unatokota kwa ukali, unakaribia kukatika na kutawanyika kwa wingi wa kuwaghadhibikia.
Kila likitumbukizwa kundi mojapo kati yao walinzi wake huwauliza kwa kuwakejeli:
Kwani hakukujieni Mtume kukuhadharisheni na mkutano wa siku hii ya leo?
9. Na wao watajibu: Ametujia mwonyaji, lakini sisi tulimkanusha tukamwambia
mwongo, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakukuteremshia chochote wewe wala
Mitume wenginewe. Nyinyi mnao dai Utume si chochote ila ni watu walio potoka,
na mko mbali na haki.
10. Na watasema: Lau kuwa tulikuwa tunasikia kama inavyo faa asikie
mwenye kutaka ukweli wa mambo, au tunafikiri tunayo itiwa, tusinge kuwa
miongoni mwa watu wa Motoni.
11. Basi wataungama kukadhibisha kwao na kukufuru kwao. Watu wa Motoni
wamepotelea mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu!
12. Hakika wenye kumkhofu Mola wao Mlezi, na hali wao hawamwoni,
watafutiwa madhambi yao, na watapata thawabu kubwa kwa mema yao.
13. Na ficheni kauli yenu, au itangazeni. Yote mawili kwa Mwenyezi
Mungu ni sawa, kwani Yeye ni Mkuu wa kuyazunguka yote kwa kuyajua, Mjuzi
wa vinavyo ficha vifua.
14. Kwani Muumba si Mwenye kujua mambo yote ya waja wake? Na Yeye
ni Mjuzi wa dogo na kubwa
15. Yeye ndiye aliye ifanya ardhi dhalili inakut'iini. Basi tembeeni
pande zake kote kote. Na kuleni katika riziki zake zinazo toka ndani
yake. Na kwake Yeye peke yake ndio kufufuliwa na kulipwa.
16. Je! Mmejiaminisha na Mwenye Ufalme wa mbinguni, kuwa hatakukatieni
ardhi, akakuchukulieni kwa ghafla kwa mtikiso mkubwa?
17. Bali, mmejiaminisha na Mwenye Ufalme wa mbinguni, kuwa hatakupelekeeni
upepo wa kukupopoeni kwa changarawe? Hapo basi mtakijiua kitisho cha onyo
langu kwenu!
18. Na hakika walikwisha wakanusha Mitume wao hao walio kuwa kabla
ya kaumu yako. Basi ghadhabu yangu juu yao ilikuwa hali gani kwa nilivyo
waangamiza na kuwashika!
19. Wameingia upofu? Wala hawakuwaangalia ndege walio juu yao, vipi
wanavyo kunjua mbawa zao mara kwa mara, na mara nyingine wakizikunja? Hapana
anaye washikilia wasianguke ila Mwingi wa Rehema. Hakika Yeye ni Mwingi
wa ujuzi na khabari kwa kila kitu. Anakipa kila kitu jambo kwa mujibu
wa maslaha yake.
Kukunjua huku ni kukunjua ndege mbawa zake bila ya kuziendesha. Katika
kuruka kwa ndege ipo miujiza ambayo haikufahamika baadhi yake ila baada
ya kuendelea ilimu ya kuruka na nadhariya ya kutembea katika hewa.
Lakini katika yanayo staajabisha ni kupita ndege katika anga na mbawa zote
mbili zimetulia mpaka apite upeo wa macho. Na ilimu imevumbua kuwa ndege
wanao kunjua mbawa zao hupanda juu ya mikondo ya hewa inayo saidia inayo
timbuka ama kwa kupigana dafrau na kiziwizi fulani au kwa kunyanyuka nguzo
za hewa imoto. Ukiwa upepo ni mzuri hizo nguzo za hewa husimama wima na
ndege hupaa kwa namna ya mzunguko kama skurubu. Na ukiwa mkali hizo
nguzo hugeuka kuelekea juu na ndege huruka bila ya kupiga mbawa kwa njia
ya sawa moja kwa moja na kufikia mbali.
Na ndege kwa jumla wana sifa maalumu, katika hizo ni kuwa ni wepesi,
na wana umbo la nguvu, na nyoyo zao ni madhubuti, na kadhaalika mzunguko
wao wa damu, na vyombo vya kuvutia pumzi, na namna lilivyo pimika umbo
lao, na vikawa sawa sawa viwiliwili vyao kwa kusahilisha kuruka katika
hewa. Na sifa hizi Mwenyezi Mungu Mjuzi Mwenye kuona kawajaalia ndege ,
kwa ajili ya kuwahifadhi hao ndege katika hewa pale wanapo kunjua mbawa
zao au wanapo zikunja.
Ama videge vidogo vinavyo tegemea kuruka kwao juu ya mbio, hivyo hupiga
mbawa zao kwa chini na mbele ili vipate kujisukuma na kupaa. Na hayo ni
dharura kwa sababu ya kuruka kwao. Kisha huzikunja mbawa zao, lakini nao
wanabaki kuwa wanaruka kwa zile nguvu za msukumo wao.
Na hivyo linawafikiana umbo lao hao ndege wa kila namna na muundo wa
kifundi wa miili yao kwa kuwazesha kuruka na kujilinda sawa wakati wa kuruka.
20. Bali ni nani huyo mwenye nguvu kwenu atakaye kulindeni na adhabu
asiye kuwa Mwenyewe Arrahman, Mwingi wa Rehema? Makafiri hawamo ila katika
udanganyifu tu kwa hayo wanayo yadhania.
21. Bali ni nani huyo atakaye kuruzukuni kwa yanayo kupeni uhai wenu
na starehe zenu, ikiwa Mwenyezi Mungu akizuia riziki zake asikupeni? Bali
makafiri wamekakamia katika kutakabari kwao na kuikimbia Haki.
22. Je! Hali itageuka? Mwenye kwenda akijikwaa na kusinukia juu ya
uso wake ni mwongofu zaidi katika mwendo wake, au yule anaye tembea sawasawa
kwenye njia isiyo kwenda upogo?
23. Sema: Huyo aliye kuumbeni nanyi hamjakuwa chochote, na akakupeni
usikizi na kuona, na fahamu ambazo ni sababu za vitendo vyenu na uwongofu
wenu - ama ni kuchache mno kushukuru kwenu kwa neema hizi kumshukuru huyo
aliye kupeni.
24. Sema: Huyo ndiye aliye kutawanyeni katika ardhi, na kwake Yeye
peke yake ndio mtarejea kwa ajili ya kukuhisabuni na kukulipeni.
25. Na wanasema wanao kanya kufufuliwa: Yatatokea lini haya ya kukusanywa
watu? Twambieni yatakuwa lini, kama nyinyi mnasema kweli!
26. Ewe Muhammad! Sema: Ujuzi wa hayo ni wa Mwenyezi Mungu peke yake.
Ama mimi ni mwonyaji miongoni mwa waonyaji tu.
27. Watakapo yaona hayo yaliyo ahidiwa yapo karibu nao, nyuso za
makafiri zitajaa huzuni na unyonge, na wataambiwa kwa kuwakejeli na kuwatia
uchungu: Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyataka yaje kwa haraka!
28. Sema: Nambieni, ikiwa Mwenyezi Mungu akinifisha mimi na Waumini
walio pamoja nami, kama mnavyo tamani yawe, au akaturehemu akaakhirisha
ajali yetu, na akatusamehe asituadhibu, maana itakuwa katuokoa katika hali
zote mbili, basi nani atakaye wakinga makafiri na adhabu chungu wanayo
istahiki kuipata kwa sababu ya ukafiri wao, na kudanganyika kwao na miungu
yao?
29. Yeye huyo ndiye Arrahman, Mwingi wa Rehema, tunaye msadiki sisi,
na nyinyi hamumsadiki. Yeye tu peke yake ndiye tunaye mtegemea, na nyinyi
mnawategemea wenginewe. Mtakuja jua itakapo teremka adhabu ni kundi gani
kati yetu lilio tengeka mbali na Haki.
30. Sema: Hebu nipeni khabari, maji yenu yakitoweka chini ya ardhi msiweze kuyapata kwa namna yoyote, ni nani asiye kuwa Mwenyezi Mungu atakaye kuleteeni maji ya dhaahiri yanayo miminika anayo weza kuyapata kila atakaye?