1. Ewe Nabii! Kwa nini unajikhini nafsi yako alicho
kuhalalishia Mwenyezi Mungu? Unataka kuwaridhi wakezo, na Mwenyezi Mungu
ni Mwingi wa kusamehe, Mkunjufu wa kurehemu.
2. Amekuwekeeni Sharia ya kuondoa viapo vyenu kwa kafara. Na Mwenyezi
Mungu ni Bwana wenu, Mwenye kutawala mambo yenu, na Yeye ni Mtimilivu wa
ujuzi, basi anakuwekeeni Sharia zenye kheri yenu, naye ni Mwenye hikima
katika kuweka Sharia zake.
3. Na taja pale Nabii alipo msimulia jambo kwa siri mmoja katika
wake zake, na alipo ifichua. Na Mwenyezi Mungu akamjuvya Nabii wake kuwa
imefichuliwa. Akamjuvya baadhi, na akamzuilia - kwa staha - baadhi
nyengine. Alipo mjuvya, akasema yule mke: Nani aliye kwambia haya? Akasema
Nabii: Ameniambia Mwenye kujua kila kitu, asiye fichika kitu.
4. Mkirejea nyinyi wawili kwa Mwenyezi Mungu nanyi mmejuta basi itakuwa
mmefanya waajibu wenu wa kutubu, kwa sababu nyoyo zenu zilikuwa zimeacha
jambo analo lipenda Mtume wa Mwenyezi Mungu, nalo ni kuweka siri. Na ikiwa
mtasaidiana kinyume chake kwa mambo ya kumuudhi, basi hakika Mwenyezi Mungu
ni Msaidizi wake, na Jibrili, na Waumini wanao sifika kwa wema, na Malaika
baada ya msaada wa Mwenyezi Mungu nao ni wenye kumsaidia.
5. Asaa Mola wake Mlezi akikuacheni, enyi wakeze, atamwoza badala
yenu wake wengine walio wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu kwa ut'iifu, wenye
kusadiki kwa nyoyo zao, wanyonge mbele ya Mwenyezi Mungu, wenye kurejea
kwa Mwenyezi Mungu kwa toba, wenye kumuabudu kwa kujidhalilisha kwake,
wendao kila njia za ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu, wajane na bikra.
6. Enyi mlio amini! Jihifadhini nafsi zenu na ahali zenu na Moto,
ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanao simamia kazi yake na kuwaadhibu
waliomo humo ni Malaika wakali, na wana nguvu katika muamala wao. Na wao
hutekeleza lile wanalo amrishwa, wala hawakawilishi.
7. Wataambiwa makafiri Siku ya Kiyama: Msitafute udhuru leo! Hapana
shaka mnalipwa mliyo kuwa mkiyatenda.
8. Enyi mlio amini! Rejeeni kwa Mwenyezi Mungu, muache madhambi yenu,
mrejee kweli kweli kwa ikhlasi. Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu
yenu, na akakutieni Peponi kwenye kupita mito chini ya majumba yake na
miti yake, Siku atakayo inyanyua Mwenyezi Mungu hadhi ya Nabii na walio
amini pamoja naye. Nuru yao hao itakuwa inakwenda mbele yao, nayo itakuwa
kuliani mwao, nao watakuwa wakisema kwa kujikaribisha kwa Mwenyezi Mungu:
Ewe Bwana wetu, Mwenye kumiliki mambo yetu! Tutimizie nuru yetu, mpaka
tuongoke kufikia Peponi. Na tusamehe dhambi zetu. Hakika Wewe ni Mtimilivu
wa uweza juu ya kila kitu.
9. Ewe Nabii! Pambana kwa Jihadi na hao walio tangaza ukafiri wao,
na wanaafiki walio uficha ukafiri wao, kwa kila unacho kimiliki, nguvu
na hoja. Na kuwa mkali juu ya makundi yote mawili hayo katika Jihadi yako.
Na makaazi ya hao ni Jahannamu. Na marejeo maovu ni hayo marejeo yao!
10. Mwenyezi Mungu ametaja hali ya ajabu inayo juulikana kuwa ni
hali zinazo fanana kwa wanao kufuru. Nayo ni hali ya mke wa Nuhu na mke
wa Lut'i. Hao walikuwa chini ya ulinzi wa waja wawili katika waja wema.
Nao wakawakhuni kwa kupanga njama dhidi yao, na kufichua siri zao kwenda
wambia kaumu zao. Na waja wema wawili hawakuweza kuwakinga wake zao kwa
lolote katika adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na wakaambiwa hao wake wawili walipo
angamizwa: Ingieni Motoni pamoja na wanao ingia!
11. Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano kwa Waumini kisa cha mke wa Firauni
alipo sema: Mola wangu Mlezi! Nijengee kwako nyumba karibu na rehema yako
Peponi, na uniokoe na utawala wa Firauni na vitendo vyake vilivyo pita
mipaka katika dhulma, na uniokoe na kaumu ya wanao fanya uadui!
12. Na Mwenyezi Mungu amewapigia Waumini mfano wa Mariamu binti wa Imrani, ambaye amehifadhi utupu wake, tukampulizia humo katika roho yetu, akashika mimba ya Isa. Naye akayasadiki maneno ya Mwenyezi Mungu, nayo ni amri zake, na makatazo yake, na Vitabu vilivyo teremshwa juu ya Mitume wake. Na yeye alikuwa miongoni mwa idadi walio dumu juu ya ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. (Huku kupuliziwa Mariamu roho ya Mwenyezi Mungu si kiroja, kwani wanaadamu wote wamepuliziwa kadhaalika. Soma Surat Al-H'ijr Aya 28-29 inapo simuliwa alipo umbwa mtu na akapuliziwa kutokana na roho ya Mwenyezi Mungu.)