1. Ewe Nabii! Mkitaka kuwapa talaka wanawake, basi wapeni
talaka kwa kukabiliana na eda zao, (yaani wakati wa tahara kabla ya kuwaingilia),
na idhibitini eda, na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Msiwatoe
watalaka katika nyumba zao walimo pewa talaka. Wasitoke humo ila ikiwa
wamefanya kitendo kichafu wazi. Hukumu hizo zilizo tangulia ni alama za
Mwenyezi Mungu amezifanya ni sharia kwa waja wake. Na Mwenye kukiuka mipaka
ya Mwenyezi Mungu basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui pengine Mwenyezi
Mungu labda ataleta jambo usilo litaraji baada ya talaka hiyo, na wakapendana.
2. Wakikaribia walio achwa mwisho wa eda zao warejeeni mkae nao kwa
wema na ihsani, au farikianeni nao bila ya madhara. Na washuhudisheni kuwarejea
na kufarikiana watu wawili waadilifu miongoni mwenu, na toeni ushahidi
kwa mujibu wake kwa kumsafia Mwenyezi Mungu. Hayo mliyo amrishwa ndiyo
anayo waidhiwa mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na mwenye
kumkhofu Mwenyezi Mungu akazishika amri zake na akaepuka makatazo yake
atamjaalia njia ya kutokana na kila dhiki.
3. Na atamtengezea sababu za kupata riziki kwa jiha ambazo hata hazimpitikii
katika fikra zake. Na mwenye kumwachia mambo yake yote Mwenyezi Mungu basi
Yeye ni Mwenye kumtosha, hana haja ya mwengine. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kutimiza alitakalo, ni Mwenye kutekeleza alipendalo. Amejaalia
kila kitu na wakati wake, wala haupitikii, na kipimo hakivuki.
4. Na wenye eda ya talaka miongoni mwa wanawake walio sita kuingia
myezini kwa utu uzima, kama hawajui wahisabu vipi eda yao, basi eda yao
ni miezi mitatu. Na wale ambao hawaingii hedhi kabisa ni kadhaalika.
Na wenye mimba, eda yao inakwisha wanapo jifungua. Na mwenye kumcha Mwenyezi
Mungu, na akazitimiza hukumu zake Mwenyezi Mungu atamsahilishia mambo yake.
5. Sharia hizo ni amri ya Mwenyezi Mungu, si ya mwenginewe. Amekuteremshieni
Yeye. Na mwenye kumcha Mwenyezi Mungu kwa kuzihifadhi hukumu zake humfutia
makosa yake, na akayafanya makubwa malipo yake.
6. Wawekeni wanawake waliomo edani humo humo katika nyumba zenu,
kwa kadiri ya uwezo wenu. Wala msiwaletee madhara yoyote, kuwaletea dhiki
katika maskani. Na ikiwa wana mimba basi watoleeni gharama za kuwakimu
mpaka wazae. Wakikunyonyesheeni watoto wenu hao watalaka, basi wapeni ujira
wao. Na amrishaneni mambo mazuri ya kusameheana na kuacha kutaabishana.
Na ikitokea kati yenu dhiki na taabu, basi baba atafute mnyonyeshaji mwengine
badala ya mama aliye achwa.
7. Atoe mwenye nafasi nzuri ya riziki kwa mujibu alicho kunjuliwa
na Mwenyezi Mungu, na mwenye dhiki ya pato atoe kwa kadiri alicho mpa Mwenyezi
Mungu. Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ila kwa mujibu alicho mpa. Mwenyezi
Mungu atajaalia baada ya dhiki faraji.
8,9. Na miji mingi ambayo watu wake wamefanya ujabari na wakapuuza
amri ya Mola wao Mlezi na Mitume wake, tukaihisabia kwa hisabu kali kwa
kuchungua kila walilo litenda na kujadiliana nao, na tukawaadhibu
adhabu ya kuchusha iliyo mbaya, wakagugumia malipo maovu ya mambo yao.
Na ukawa mwisho wa mambo yao ni kukhasiri kukubwa mno.
10,11. Mwenyezi Mungu amewaandalia watu wa miji ya watu walio
fanya ujabari adhabu ya mwisho wa ukali. Basi tahadharini na ghadhabu ya
Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili sawa, ambao mnasifika kwa Imani. Amekuteremshieni
mtu mwenye utukufu na cheo, Mtume anaye kusomeeni Aya za Mwenyezi Mungu
zenye kukubainishieni baina yaliyo kweli na ya uwongo, ili awatoe walio
amini na wakatenda mema kutoka kwenye giza la upotovu kwenda kwenye mwangaza
wa hidaya. Na mwenye kumsadiki Mwenyezi Mungu, na akatenda vitendo vyema
atamtia katika Bustani zinazo pita kati yake mito. Watakaa humo milele.
Mwenyezi Mungu kamfanyia ihsani Muumini mwema kwa kumpa riziki iliyo njema.
12. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye umba mbingu saba, na ardhi mfano wa hizo. Amri yake inapita kote, ili mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni mtimilivu wa uweza, na kwamba Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.