1. Ewe Muhammad! Wanapo kujia wanaafiki, wanasema kwa
ndimi zao: Tunashuhudia kuwa hakika wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu anajua kwamba wewe ni Mtume wake; na Mwenyezi Mungu anashuhudia
kwamba wanaafiki hapana shaka ni waongo katika kujidai kwao wanaamini,
kwani hawasadiki katika nyoyo zao.
2. Wamezifanya yamini zao za uwongo ni kinga, au ngao za kujikingia
ili wasichukuliwe kuwa ni makafiri. Basi wakajizuia wenyewe wasiishike
Njia ya Mwenyezi Mungu Iliyo Nyooka. Hakika ni mabaya mno hayo wanayo yatenda
ya unaafiki na kujitia imani ya uwongo.
3. Hayo waliyo yafanya ndiyo mazoea ya kudhihirisha yasiyo ya kweli,
na kuapa yamini za uwongo, kwa sababu hao wameamini kwa ndimi zao, kisha
wakakufuru katika nyoyo zao, basi nyoyo zao zimepigwa muhuri kwa ukafiri
huu. Hao hawafahamu yepi ya kuwaokoa na adhabu za Mwenyezi Mungu.
4. Na ukiwaona miili yao inakupendeza kwa uzuri wao, na wakizungumza
unavutika kuwasikiliza kwa utamu wa maneno yao. Kumbe wao juu ya yote hayo
nyoyo zao zitupu, hazina Imani ndani yake. Kama magogo yaliyo egemezwa,
hayana uhai wowote. Wao hudhania kila linalo zuka basi linawalenga wao,
kwa sababu wanaitambua hali yao ya unaafiki. Hao ndio maadui, basi tahadhari
nao. Mwenyezi Mungu kesha wafukuza kwenye rehema yake. Vipi wanavyo iacha
Haki wakauendea unaafiki wanao ushikilia?
5. Na wakiambiwa: Jongeeni, apate Mtume wa Mwenyezi Mungu kukuombeeni
msamaha, hutikisa vichwa vyao kwa kejeli, na utawaona wanageuka kwa kiburi
hawataki kut'ii.
6. Ni sawa kwa hawa wanaafiki, ukiwaombea msamaha, au ukito waombea.
Kwa sababu hao hawauachi unaafiki wao. Basi Mwenyezi Mungu hatawasamehe
kabisa. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi kuwapeleka kwenye Haki wale wanao
kataa kufuata amri yake na kumuamini.
7. Hao wanaafiki ndio wanao waambia watu wa Madina: Msitoe chochote
kuwapa hao Waumini walio na Mtume wa Mwenyezi Mungu ili wapate kumwacha!
Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye khazina zote za mbinguni na duniani, na
riziki zote ziliomo humo. Lakini wanaafiki hawajui hayo.
8. Wanaafiki wanasema kwa kutoa ahadi: Tukirejea Madina hapana shaka
kikundi chetu, ambacho ndicho chenye nguvu zaidi, kitakitoa kikundi cha
Waumini ambao ni wanyonge! Nguvu anazo Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na
Waumini; sio hawa wanao jitia kuahidi. Lakini wanaafiki hawajui kitu.
9. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Yasikuhangaisheni
mali yenu, na watoto wenu, hata mkaacha kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kutekekeleza
aliyo kuamrisheni kuyafanya. Na wenye kushughulishwa na mali zao na watoto
wao wakaacha hayo, basi hao ndio watao kuwa wamekhasiri Siku ya Kiyama.
10. Enyi Waumini! Toeni katika mali tuliyo kuruzukuni upesi upesi
kabla mmoja wenu hayajamfikia mauti akasema kwa majuto: Ewe Mola wangu
Mlezi! Hebu hunipi muhula kidogo, nikapata kutoa sadaka, na nikawa
miongoni wa watu wema watendao vitendo vyema?
11. Wala Mwenyezi Mungu hampi muhula mtu yeyote ukisha fika wakati wake wa kufa. Na Mwenyezi Mungu ni Mkamilifu wa kujua yote myatendayo, na Yeye atakulipeni kwa hayo.