1. Kila kiliomo katika mbingu na kiliomo katika ardhi
kinamtakasa Mwenyezi Mungu na kila kisicho kuwa ni laiki yake. Na Yeye
peke yake ndiye Mwenye kuvishinda vitu vyote, Mwenye hikima iliyo fika
ukomo.
2. Enyi mlio amini! Kwa ajili ya nini mnasema kwa ndimi zenu yasiyo
hakikishwa na vitendo vyenu?
3. Mwenyezi Mungu anachukia mno kuwa nyinyi mnasema msiyo yatenda.
4. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao pigania kutaka kulinyanyua
Neno lake nao wameshikamana kitu kimoja, kama kwamba wao ni jengo lilio
simama imara.
5. Ewe Muhammad! Kumbuka pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi
watu wangu! Kwa nini mnaniudhi mimi, na hali nyinyi mnajua kwamba hakika
mimi ni Mjumbe niliye tumwa na Mwenyezi Mungu nije kwenu? Walipo endelea
na kuiacha Haki, Mwenyezi Mungu alizipotoa nyoyo zao zisipokee uwongofu.
Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu walio toka kwenye ut'iifu wake.
6. Na kumbuka pale Isa bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili!
Hakika mimi ni Mtume nimetumwa kwenu, mwenye kusadikisha yaliyo nitangulia
yaliomo katika Taurati, na kukupeni bishara ya Mtume atakaye kuja baada
yangu. Jina lake ni Ahmad. Alipo kuja huyo Mtume aliye bashiriwa kwa Ishara
zilizo wazi wakasema: Haya uliyo tujia nayo ni uchawi dhaahiri!
(Kwa ushahidi wa kubashiriwa Nabii Muhammad s.a.w. katika vitabu vya
Kikristo na Kiyahudi, tazama: Kumbukumbu la Torati 18.19-22, na Injili
ya Yohana 16.5-14.)
7. Na nani aliye zidi kwa udhaalimu kuliko huyo aliye mzulia uwongo
Mwenyezi Mungu, naye anaitwa aingie katika Dini ya Kiislamu, Dini ya haki
na kheri? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu walio shikilia dhulma.
8. Wana wa Israili wanamzulia Mwenyezi Mungu uwongo, ili ati wapate
kuizima nuru ya Dini yake kwa vinywa vyao, kama anaye taka kuizima nuru
ya jua kwa kuipulizia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuikamilisha nuru yake
kwa kuitimiza Dini yake hata hao makafiri wakiudhika.
9. Mwenyezi Mungu ndiye aliye mtuma Mtume wake, Muhammad, pamoja
na Qur'ani ambayo ni uwongofu kwa watu wote, na Uislamu ambao ndio Dini
ya haki, ili autukuze juu ya dini zote, ijapo kuwa washirikina wataudhika.
10. Enyi mlio amini! Nikuongozeni kwenye biashara kubwa ambayo itakuokoeni
na adhabu yenye machungu makali?
11. Biashara hii ni kuwa mumuamini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake,
na mpigane Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi
zenu. Hayo aliyo kuonyesheni ndiyo kheri yenu ikiwa nyinyi mnajua.
12. Muamini na mpigane Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, ili
akusameheni madhambi yenu, na akutieni katika Bustani zinazo pita kati
yake mito, na maskani nzuri katika Bustani za milele. Hayo ndiyo malipo
makubwa.
13. Na neema nyengine ambazo Waumini Mujahidina wanazo zipenda, ni
msaada utokao kwa Mwenyezi Mungu na ushindi wa karibu utakao kuleteeni
kheri zake. Na ewe Muhammad! Wabashirie Waumini kuwa watapata malipo haya.
14. Enyi mlio amini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu anapo kutakeni Mtume wa Mwenyezi Mungu muwe wasaidizi wake. Kama walivyo kuwa masahaba wa Isa wasaidizi wa Mwenyezi Mungu alipo sema: Nani wa kunisaidia mimi kwa Mwenyezi Mungu? Basi kundi moja katika Wana wa Israili lilimuamini Isa, na kundi jengine likamkataa. Sisi tukawapa nguvu walio amini juu ya maadui zao walio kufuru. Basi kwa kuwapa nguvu kwetu wakawa ni wenye kushinda.