1. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Msiwafanye
maadui wangu na maadui wenu kuwa ni wenzenu mkiwapa mapenzi ya kweli, na
hali wao wameyakataa yaliyo kujieni nyinyi ya kumuamini Mwenyezi Mungu
na Mtume wake na Kitabu chake. Wamemtoa Mtume na wamekutoeni nyinyi kwenu
kwenye majumba yenu, kwa sababu ya Imani yenu kumuamini Mwenyezi Mungu,
Mola wenu Mlezi. Mnapotoka makwenu kwenda pigana Jihadi katika Njia
yangu na kutaka radhi yangu, basi msifanye urafiki na adui zangu, mkawapa
mapenzi kisirisiri. Na Mimi nayajua vyema yote mnayo yaficha na mnayo dhihirisha.
Na yeyote mwenye kumfanya adui wa Mwenyezi Mungu kuwa ndiye rafiki yake
basi ameikosea Njia Iliyo Nyooka.
2. Wakikutana nanyi na wakakuwezeni, uadui wao kwenu unadhihiri,
na wanakunyoosheeni mikono yao na ndimi zao kukudhuruni. Na wanatamani
muwe makafiri kama wao.
3. Hawatakufaeni kitu jamaa zenu wala watoto wenu mlio wafanya kuwa
ni marafiki, na hali wao ni adui wa Mwenyezi Mungu na adui zenu.
Katika Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atakutengeni mbali mbali. Atawatia
maadui zake Motoni na marafiki zake Peponi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuyaona yote myatendayo.
4. Nyinyi mna kiigizo kizuri cha kukiiga katika Ibrahim na walio
amini pamoja naye, pale walipo waambia watu wao: Hakika sisi tunajitenga
nanyi, na tunajitenga na hiyo miungu ya uwongo mnayo iabudu badala ya Mwenyezi
Mungu. Sisi tunakukataeni, na umekwisha dhihiri uadui na kuchukiana baina
yetu na nyinyi. Hayo hayataondoka kabisa mpaka mumuamini Mwenyezi Mungu
peke yake. Lakini kauli ya Ibrahim kumwambia baba yake: Nitakutakia maghfira,
na similiki kwa Mwenyezi Mungu kitu chochote - kauli hiyo si ya kufuatwa.
Kwani hayo yalikuwa kabla hajajua huyo baba yake kashikilia kuwa adui wa
Mwenyezi Mungu wala hageuki. Ilipo dhihiri kwake kuwa hakika huyo ni adui
wa Mwenyezi Mungu alijitenga naye. Enyi waumini! Semeni: Mola wetu Mlezi!
Kwako Wewe ndio tunategemea, na kwako Wewe tunarejea, na kwako Wewe ndio
mwisho wetu Akhera.
5. Mola wetu Mlezi! Usitujaalie tukawa katika hali ya kuwa katika
fitina za walio kufuru. Na tusamehe madhambi yetu, ewe Mola wetu Mlezi!
Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu usiye shindika, Mwenye hikima katika kutasarafu
kwake.
6. Enyi Waumini! Bila ya shaka katika Ibrahim na walio kuwa pamoja
naye, kipo kiigizo kizuri kwenu kwa vile walivyo wafanyia uadui maadui
wa Mwenyezi Mungu. Kiigizo hicho ni kwa mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi
Mungu na Siku ya Mwisho. Na mwenye kupuuza kufuata haya basi kajidhulumu
nafsi yake. Kwani hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa mwenginewe. Yeye
ni Mwenye kustahiki peke yake sifa zote njema.
7. Asaa Mwenyezi Mungu akajaalia yawepo mapenzi baina yenu na hao
makafiri walio ni maadui zenu, kwa kuwapa tawfiki, kuwawezesha, kuingia
katika Imani. Na Mwenyezi Mungu ana uweza ulio timia, ni Mkunjufu wa maghfira
kwa mwenye kutubu, ni Mwenye kuwarehemu waja wake.
8. Mwenyezi Mungu hakukatazini kwa makafiri wasio kupigeni vita wala
kukufukuzeni makwenu kuwakirimu na kuwapa mawasiliano mema. Hakika Mwenyezi
Mungu anawapenda watu watendao ihsani na mawasiliano.
9. Ila Mwenyezi Mungu anakukatazeni wale walio kupigeni vita katika
Dini ili kukuzuieni nayo, na wakakulazimisheni kutoka majumbani kwenu na
nchi yenu, na wakasaidia katika kukutoeni huko, msiwafanye hao kuwa ndio
wenzenu wa kusaidiana nao. Na wenye kuwafanya hao ndio wasaidizi wao, basi
hao ndio wenye kujidhulumu nafsi zao.
10. Enyi mlio amini! Wakikujieni wanawake Waumini walio hama kukimbia
nchi ya ukafiri, basi wachungueni ili mpate kujua ukweli wa Imani yao.
Mwenyezi Mungu anajua zaidi ukweli wa Imani yao. Mkiwaona kama ni Waumini,
basi msiwarudishe kwa waume zao makafiri. Wanawake Waumini si halali kwa
makafiri, wala wanaume makafiri si halali kwa wanawake Waumini. Na
wapeni waume wa kikafiri mahari waliyo yatoa kwa wake zao walio hamia kwenu.
Wala hapana ubaya kwenu kuwaoa wanawake hao walio hamia kwenu mkiwapa mahari
yao. Wala msiwazuie kwa kifungo cha ndoa wanawake makafiri walio bakia
katika mji wa ukafiri au walio fungamana nao. Na takeni kwa makafiri mahari
mliyo yatoa kwa wenye kufungamana na mji wa ukafiri. Na wao hao watake
kulipwa walicho toa kuwapa wake zao walio hama wakaja kwenu. Hukumu hiyo
ni kwa mujibu wa sharia ya Mwenyezi Mungu, anayo kufafanulieni. Na Mwenyezi
Mungu anajua vyema maslaha ya waja wake, ni Mwenye hikima katika kutoa
sharia.
11. Na wakitokea baadhi ya wake zenu wakakukimbieni kwenda kwa makafiri,
kisha mkapigana nao vita, basi wapeni walio kimbiwa na wake zao kiasi cha
mahari waliyo yatoa. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.
12. Ewe Nabii! Wakikujia wanawake Waumini kukuahidi kwamba hawatamshirikisha
Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini, wala hawatwauwa
watoto wao, wala hawatawabandikiza waume zao watoto wao (wa haramu) kwa
uzushi na uwongo wanao uzua baina ya mikono yao na miguu yao. (yaani matumboni
mwao, au kwa ndimi zao na tupu zao); wala hawendi kinyume nawe katika jambo
jema unalo waitia, basi pokea ahadi zao juu ya hayo, na waombee msamaha
kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe na kurehemu.
(Mtume s.a.w. haamrishi ila jema, lakini sharia hapo inasema
kuwa mtawala yeyote hut'iiwa akiamrisha jema tu. Ama kwa lilio ovu, Mtume
s.a.w. amesema: "Hapana kumtii kiumbe katika kumuasi Muumba.")
13. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake, msiwafanye kuwa rafiki zenu watu ambao Mwenyezi Mungu amewaghadhibikia. Hao wamekata tamaa na Akhera na yote yatakao kuwapo huko, ya kulipwa na kuhisabiwa, kama makafiri walivyo kata tamaa kufufuliwa waliomo makaburini.