1. Vitu vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi
vinamtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisio laiki naye. Na Yeye ndiye Mwenye
kushinda ambaye hashindwi na kitu. Mwenye hikima katika mipango yake na
vitendo vyake.
2. Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliye watoa walio kufuru miongoni mwa
Watu wa Kitabu, nao ni Mayahudi wa ukoo wa Banu Nnadhir, kutoka kwenye
majumba yao wakati wa kuwatoa mara ya kwanza katika Bara Arabu. Enyi Waislamu!
Hamkudhania kuwa watatoka kwenye nyumba zao kwa sababu ya nguvu zao. Na
wao wenyewe walidhani kwamba ngome zao zitawalinda na mashambulio ya Mwenyezi
Mungu. Mwenyezi Mungu akawatokea katika upande wasio utarajia, na akawatia
katika nyoyo zao fazaa kubwa, wakawa wanabomoa nyumba zao kwa mikono yao
ili zibaki kuwa magofu tu, na kwa mikono ya Waumini wapate kuzivunja zile
ngome. Basi enyi wenye akili, chukueni somo katika haya yaliyo washukia
hawa.
3. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakuwahukumia kuwatoa majumbani kwao
kwa sura hii ya kuchusha, basi hapana shaka angeli waadhibu katika dunia
kwa shida zaidi kuliko huko kuwatoa. Na Akhera, wao watapata adhabu ya
Moto, mbali huku kutolewa majumbani kwao duniani.
4. Hayo yaliyo wapata duniani na yanayo wangojea Akhera ni kwa sabau
ya kuwa wamemfanyia uadui Mwenyezi Mungu na Mtume wake, uadui mkubwa mno.
Na mwenye kumfanyia uadui Mwenyezi Mungu basi hawezi kupenya kuikimbia
adhabu yake. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
5. Enyi Waislamu! Mitende yoyote mliyo ikata au mkaiacha imebaki
kama ilivyo kuwa, basi ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hapana lawama juu
yenu katika hayo, ili awape nguvu Waumini, na awahizi wapotovu walio ziacha
sharia zake.
6. Na aliyo yaleta Mwenyezi Mungu na akayarudisha kwa Mtume wake
katika mali ya Banu Nnadhir hamkuyapigia mbio nyinyi kwa farasi wala ngamia.
Lakini Mwenyezi Mungu huwapa madaraka Mitume wake kwa awatakao katika waja
wake bila ya kupigana vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mtimilivu wa uweza juu
ya kila kitu.
7. Alicho rudisha Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake katika mali ya watu
wa vijiji hivi bila ya kuwatimua farasi au ngamia, vitu hivyo ni vya Mwenyezi
Mungu na Mtume wake, na jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri. Haya
ni hivyo ili yasiwe mali yakizunguka katika mikono ya matajiri peke yao
katika nyinyi. Na anacho kupeni Mtume katika hukumu basi kishikeni, na
anacho kukatazeni basi kiwacheni. Na jilindeni na kughadhibika kwa Mwenyezi
Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
8. Na hivyo yale mali ya watu wa vijiji aliyo yarudisha Mwenyezi
Mungu kwa Mtume wake wapewe mafakiri katika Wahajiri, walio kimbilia Madina,
ambao wametolewa majumbani kwao na mali yao huko Makka. Wao wanataraji
ziada kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika riziki zao na radhi. Na wanamsaidia
Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa nafsi zao na mali yao. Hao ndio Waumini
wa kweli.
9. Na Ma-ansari, watu wa Madina walio mnusuru Mtume na Wahajiri,
ambao wamekaa Madina katika maskani zao, na Imani yao ikawa safi kabisa
kabla ya kufika Wahajiri, wanawapenda wale wageni Waislamu walio hamia
kwao, na wala hawahisi ubaya wowote katika nafsi zao kwa walicho pewa Wahajiri
katika ngawira. Bali wanawakadimisha Wahajiri kuliko nafsi zao, ijapo kuwa
wakiwa wao nao ni wahitaji. Na mwenye kuhifadhika, kwa uweza wa Mwenyezi
Mungu, asione ubakhili katika nafsi yake, basi watu kama hao ndio wenye
kufuzu kwa kila walipendalo.
10. Na Waumini walio kuja baada ya Wahajiri na Ansari husema: Mola
wetu Mlezi! Tusamehe dhambi zetu, sisi na ndugu zetu walio tutangulia katika
Imani. Wala usijaalie kuwa katika nyoyo zetu husda kuwahusudu walio amini.
Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe umefika ukomo katika upole na kurehemu.
11. Hebu huwaangalii hao wanaafiki ukastaajabu? Kazi yao ni kuwakariria
kauli ndugu zao walio kufuru katika Watu wa Kitabu - nao ni hao Banu Nnadhir
- kuwaambia: Wallahi! Mkilazimishwa kuihama Madina, basi hapana shaka na
sisi tutatoka pamoja nanyi. Wala hatutamt'ii katika jambo lenu mtu yeyote
daima dawamu. Na pindi ikiwa Waislamu watakupigeni vita, basi hapana shaka
sisi tutakusaidieni. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hakika wanaafiki
hapana shaka ni waongo katika hizo ahadi zao wanazo zitoa.
12. Wakitolewa Mayahudi, wanaafiki hawatatoka pamoja nao. Na wakipigwa
vita hawatawanusuru. Na pindi wakiwasaidia basi hapana shaka watatoka mbio
warudi kinyume nyume, wala hawatawanusuru.
13. Hakika, enyi Waislamu, mna kitisho zaidi katika vifua vya wanaafiki
na Mayahudi kuliko wanavyo mwogopa Mwenyezi Mungu. Hayo ni kwa sababu hakika
wao ni watu wasio jua ukweli wa Imani.
14. Mayahudi hawapigani vita nanyi kwa pamoja ila wawe katika miji
iliyo jengewa ngome, au wajifiche nyuma ya kuta. Vita vyao baina ya wao
kwa wao ni vikali. Utawadhani kuwa wameshikamana, wote ni wamoja. Kumbe
hakika nyoyo zao zimefarikiana mbali mbali. Wao ni wenye sifa hizo, kwa
sababu hao ni watu wasio zingatia nini utakuwa mwisho wa mambo.
15. Mfano wa Bani Nnadhir ni kama mfano wa walio kufuru kabla yao
karibuni. Hao walionja hapa hapa duniani matokeo ya ukafiri wao na kuvunja
kwao mapatano. Na Akhera watapata adhabu ya uchungu mkali.
16. Mfano wa wanaafiki kuwashawishi Banu Nnadhir wamuasi Mtume wa
Mwenyezi ni kama mfano wa Shetani pale anapo mghuri mtu aiache Imani, akamwambia:
Kufuru! Na alipo kufuru akasema: Mimi niko mbali nawe, kwani mimi ninamkhofu
Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
17. Ikawa basi marejeo ya Shetani na huyo anaye mzaini ni kuishia
Motoni wabaki humo milele. Na kudumu humo dawamu ni malipo ya wenye kuasi
wakaikiuka Njia ya Haki.
18. Enyi mlio amini! Jiwekeeni kinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu
kwa kujilazimisha kumt'ii Yeye. Na kila nafsi izingatie a'mali gani ya
kuikadimisha kwa ajili ya Kesho. Na jilazimisheni kumcha Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari vilivyo kwa yote myatendayo. Naye atakulipeni
kwa hayo.
19. Enyi Waumini! Msiwe kama wale walio sahau haki za Mwenyezi Mungu,
na Yeye akawasahaulisha nafsi zao, kwa kuwajaribu kwa mitihani, na wakawa
hawajui linalo wafaa na linalo wadhuru. Hao ndio walio toka wakaacha ut'iifu
wa Mwenyezi Mungu.
20. Hawawi sawa watu wa Motoni wanao teswa, na watu wa Peponi wanao
neemeshwa. Watu wa Peponi peke yao ndio wenye kufuzu kwa kila walipendalo.
21. Lau tungeli iteremsha hii Qur'ani juu ya mlima wenye nguvu basi
ungeli uona huo mlima, juu ya nguvu zake, unanyenyekea na unapasuka kwa
kumwogopa Mwenyezi Mungu. Na hiyo ni mifano tunawaelezea watu ili wapate
kuzingatia matokeo ya mambo yao.
22. Yeye Mwenyezi Mungu ambaye hapana wa kuabudiwa kikweli
isipo kuwa Yeye peke yake, Mwenye kujua lilio pita na lilioko sasa. Yeye
ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
23. Yeye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye, Mwenye
kumiliki kila kitu kwa hakika, Aliye safika na kila upungufu, Aliye takasika
na kila lisio mwelekea, Mwenye kusalimika na yote ya upungufu, Mwenye kuwaamini
na kuwasadiki Mitume wake aliyo wapa nguvu kwa miujiza, Mlinzi Mwenye kuangalia
kila kitu, Mwenye kushinda basi hashindwi na chochote, Mkubwa wa shani
katika nguvu na utawala, Mwenye kutukuka na kila kisicho kuwa laiki na
uzuri wake na utukufu wake, Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wanayo mshirikisha
nayo.
24. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye kuviumba vitu vyote tangu mwanzo bila ya ruwaza ya kuigia iliyo tangulia, Mwenye kuvipa sura kama vilivyo kwa mujibu wa atakavyo Yeye. Yeye ndiye Mwenye Majina Mazuri, Mwenye kutakaswa na kila kisicho kuwa laiki yake na kila kilichoko katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye kushinda, asiye shindwa na kitu. Mwenye hikima katika kupanga kwake na sharia zake.