1. Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya huyo mwanamke
anaye kurejea wewe kwa shauri ya mumewe aliye jitenga naye kwa kudai ati
anamwona kama mgongo wa mama yake, na akamlalamikia Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu anayasikia hayo maneno mnayo jibizana. Hakika Mwenyezi Mungu
anayasikia vyema yote ya kusikiwa, anayaona vyema yote ya kuonekana.
Imepokelewa kuwa Sahaba mmoja, aitwaye Aus bin Ass'amit, aliudhika
na mkewe aitwaye, Khola bint Tha'labah, akamwambia: "Wewe kwangu mimi kama
mgongo wa mama yangu." Na katika siku za Ujahiliya ilikuwa ndio mwanamke
kesha harimika kwa mumewe. Mwanamke akenda kumpa khabari Nabii s.a.w.,
na Mtume akamwambia: "Sijaamrishwa kitu katika kesi yako. Na sioni ila
ni kuwa kweli umekwisha harimika kwake." Mwanamke akajadiliana na Mtume
s.a.w. na akamrejea tena, na akawa anamshitakia Mwenyezi Mungu Mtukufu
kwa kukhofu kufarikiana na mume na kupotea mwanawe. Haukupita muda ila
ikateremka Aya hii na tatu zilizo baada yake.
2. Enyi Waumini! Hao miongoni mwenu wanao jitenga na wake zao kwa
kuwashabihisha katika kuharimikiana nao kuwa ati ni kama mama zao, ni wakosa.
Wake zao sio mama zao. Ukitaka haki mama zao ni wale walio wazaa tu. Na
hakika wanao watenga wake zao kwa kusema hivyo wanasema kauli inayo chusha,
inayo udhi katika murwa mwema, na ni uwongo ulio tokana na haki.
Na hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mkuu wa kusamehe na kughufiria
kwa yaliyo kwisha pita kwenu.
3. Na wale wanao watenga wake zao na kisha wakarejeza kauli yao,
wakayaona makosa yao, na wakataka kubaki na wake zao, basi
juu yao kumkomboa mtumwa kabla ya kugusana. Hayo aliyo yawajibisha Mwenyezi
Mungu, ya kukomboa mtumwa, ni mawaidha kwenu mnawaidhiwa ili
msirejee tena katika makosa hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua
vilivyo myatendayo.
4. Na asiye pata mtumwa wa kumkomboa, basi yampasa afunge miezi miwili
mfululizo kabla hawajagusana. Na asiye weza kufunga hivyo basi itampasa
awalishe masikini sitini. Tumeyalazimisha hayo ili mpate kumuamini Mwenyezi
Mungu na Mtume wake, na mtende kwa mujibu wa Imani hiyo. Na hiyo ndiyo
mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikiuke. Na makafiri watapata adhabu yenye
machungu makali.
5. Hakika wanao mfanyia inda Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kupingana
nao watatupiliwa mbali kama walivyo tupiliwa mbali walio kuwa kabla yao.
Na Sisi tumekwisha teremsha dalili zilizo wazi za kuonyesha Haki. Na hao
wapinzani watapata adhabu ya kuwafedhehesha mno.
6. Siku Mwenyezi Mungu atapo wafufua wote baada ya kwisha kufa kwao,
na awape khabari za yale waliyo yatenda. Mwenyezi Mungu amewawekea yote
na ameyahifadhi, na wao wameyasahau. Na Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa yote
na anayajua yote.
7. Kwani hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo mbinguni na
yaliomo katika ardhi, na wala hapana siri ya watu watatu ila Yeye Mwenyezi
Mungu ndiye wane wao kwa kuyajua kwake wanayo fanyia siri, wala hawawi
watano ila na Yeye ndiye wa sita wao. Wala duni kuliko hivyo, wala kuzidi
hivyo, ila Yeye yuko pamoja nao, anayajua hayo wanayo yanong'ona, popote
walipo. Kisha Siku ya Kiyama atawapa khabari kwa kila walilo litenda. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kutimia ujuzi wake.
8. Ewe Mtume! Huwaoni hao walio katazwa kufanya njama za siri wao
kwa wao kwa mambo ya kutia shaka katika nyoyo za Waumini, kisha wakayarejea
yale yale waliyo katazwa? Na wanafanya njama kwa madhambi wanayo yatenda,
na uadui wanao uazimia, na uasi dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na wanapo
kuja kwako wanakuamkia kwa kauli ya kupotoa, sivyo anavyo kuamkia Mwenyezi
Mungu. Na wao husema katika nafsi zao: Mbona Mwenyezi Mungu hatuadhibu
kwa haya tunayo yasema ikiwa huyu ni Mtume kweli? Inawatosha hao Jahannamu.
Wataingia humo waungue kwa moto wake. Na marejeo maovu yalioje marejeo
yao.
Ilikuwako sulhu baina ya Waislamu na Mayahudi katika mji wa Madina.
Na ikawa akipita mtu katika Waislamu kwao Mayahudi hunong'ona wao kwa wao
ili adhani yule Muislamu kuwa wao wanapanga njama za kutaka kumuuwa, au
lolote la kumdhuru apate kugeuza njia asiwapitie tena. Mtume s.a.w.
akawakataza hayo, lakini hawakuacha mtindo wao, wakayarejea yale yale waliyo
katazwa. Na wakawa akija Mtume s.a.w. wakimwamkia kwa maamkio ya kumuapiza.
Ndiyo ikashuka Aya hii.
9. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Mnapo sema siri,
basi msiwe mkisema siri katika mambo ya madhambi, na kufanya uadui, na
kwenda kinyume na Mtume. Semeni siri katika mambo ya kheri, na kuepukana
na madhambi. Na mwogopeni Mwenyezi Mungu ambaye kwake Yeye tu, si kwengineko,
ndio mtakusanywa baada ya kufufuliwa.
10. Hakika kusema siri kwa kuchochea shaka shaka ni katika kuzainishwa
na Shetani, ili apate kuingiza huzuni katika nyoyo za Waumini. Wala hayo
hayawezi kuwaletea madhara yoyote wao ila kwa kupenda Mwenyezi Mungu. Basi
Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu peke yake.
11. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Mkitakiwa baadhi
yenu kuwafanyia nafasi wenzenu mnapo kaa katika majlisi zenu, basi wafanyieni
nafasi. Na Mwenyezi Mungu atakufanyieni nyinyi nafasi. Na mkitakiwa kuondoka
pale mlipo kaa basi ondokeni. Mwenyezi Mungu hutukuza vyeo vya Waumini,
na wale walio pewa ilimu kwa daraja nyingi. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari
za mnayo yatenda.
12. Enyi mlio msadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wake! Mkitaka kusema
siri na Mtume wa Mwenyezi Mungu, basi kabla ya mazungumzo yenu hayo tangulizeni
kutoa sadaka. Hivyo ndio kheri yenu, na ni usafi zaidi kwa nyoyo zenu.
Lakini ikiwa hamkupata cha kutoa sadaka, basi hakika Mwenyezi Mungu ni
Mkunjufu wa kusamehe, Mwenye kukusanya rehema zote.
13. Mnachelea kujilazimisha kutoa sadaka kabla ya mazungumzo yenu
na Mtume wa Mwenyezi Mungu? Na ikiwa hamkutoa, na Mwenyezi Mungu akakusameheni,
basi hifadhini kushika Sala na kutoa Zaka, na mt'iini Mwenyezi Mungu na
Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za vitendo vyenu, naye atakulipeni
kwavyo.
14. Ewe Mtume! Huwaoni wanaafiki walio wafanya marafiki watu ambao
Mwenyezi Mungu ameghadhibika nao. Hawa wanao fanya urafiki si katika nyinyi,
na hao wanao fanywa ni marafiki pia si katika nyinyi. Na wanaapa kwa uwongo,
na huku wanajua kuwa wao ni waongo.
15. Mwenyezi Mungu amewatengenezea hawa wanaafiki adhabu ya mwisho
wa ukali. Hakika vitendo vyao walivyo kuwa wakivitenda, vya unaafiki, na
kuchukua viapo vya uwongo, ni viovu mno.
16. Wamefanya viapo vyao kuwa ndio viwe ni kinga ya kuwakinga wasiuliwe
wenyewe, na watoto wao wasiwe mateka, na mali yao yasiwe ngawira. Kwa hayo
wakaizuilia Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watapata adhabu ya fedheha.
17. Mali yao na watoto wao hayatawalinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu
hata chembe. Hao ni watu wa Motoni, wa kudumu humo milele.
18. Siku atapo wafufua Mwenyezi Mungu wote watamwapia kuwa hakika
wao walikuwa ni Waumini, kama wanavyo kuapieni nyinyi hivi sasa. Na wanadhani
kuwa kwa kuapa kwao huku ni ujanja utakao wafaa. Ama kweli, hakika hawa
wamefika ukomo wa uwongo!
19. Shetani amewatawala na amewasahaulisha kumdhukuru Mwenyezi Mungu
na kuukumbuka utukufu wake. Hao ndio kundi la Shetani. Ama kweli, hakika
kundi la Shetani ndilo lilio fikilia mwisho wa kukhasiri.
20. Hao wanao mfanyia inda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hao ndio
katika hisabu ya walio fikilia ukomo wa udhalili.
21. Mwenyezi Mungu amekata hukumu: Bila ya shaka Mimi na Mtume wangu
tutashinda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu zilizo timia, hashindwi
na yeyote.
22. Huwakuti watu wanao msadiki Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho wanapendana na wenye kumfanyia uadui Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au ni watoto wao, au ni ndugu zao, au ni jamaa zao. Hao ambao hawafanyi urafiki na wanao mpinga Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu ameithibitisha Imani katika nyoyo zao, na amewaunga mkono kwa nguvu zinazo tokana naye Yeye Mwenyewe, na atawatia katika Mabustani yapitayo mito kati yake wakikaa humo milele. Neema zake haziwakatikii. Mwenyezi Mungu amewapenda hao, na wao wamempenda. Hao ndio wanao ambiwa kuwa ni katika Hizbullahi, yaani Kundi la Mwenyezi Mungu. Hakika ni kweli Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufuzu.