1,2,3. Kitakapo tukia Kiyama haitatokea nafsi yoyote
ya kukadhibisha kutukia kwake. Kiyama hicho kitawateremsha chini walio
waovu, na kitawanyanyua juu walio wema.
4,5,6. Ardhi itakapo tikiswa, na ikatetemeshwa kwa nguvu, na milima
ikavurugwa teketeke, ikawa vumbi la kupeperushwa,
Aya hizi tukufu zinaeleza hadi gani vitakuwa vitisho vitavyo uteremkia
ulimwengu kitapo fika Kiyama. Na katika vitisho hivyo ni hayo masaibu ya
dunia yatakayo athiri ardhi na mat'abaka yake. Kwani hii ardhi tunayo ishi
juu ya mgongo wake si yenye kutulia na kukaa sawa kwa utimilivu. Kwani
hiyo imeundwa kwa mat'abaka ya majabali yaliyo ingiliana ovyo. Huenda baadhi
yao yakateremka yakaachana na mengineyo yaliyo jirani nayo. Na huwa hiyo
inayo itwa kupasuka kwa mat'abaka ya ardhi, Geological cleavage kama inavyo
tokea katika maeneo kadhaa wa kadhaa. Mpasuko huu ulikuwa na ungali kuwa
ndio asili ya chini kabisa ya zilzala, mitetemeko, mikubwa kwa kuathirika
na nguvu za kudidimiza na kuvuta zinazo fuatana na mat'abaka ya ardhi yanapo
vunjika. Basi mizani ya utulivu ya nguvu hizi inapo geuka kwa kuathirika
na mambo mengineyo ya nje huenda zikafunguka nguvu za mtikiso mkubwa ndio
ikatokea mitetemeko na mitikisiko ya ardhi, ambayo hubomoa kila kitu kiliopo
juu ya ardhi karibu na ilipo anzia hiyo zilzala. Na hapo tena hutokea uharibifu
mkubwa mno.
Na hayo maelezo ya kisayansi hayageuzi kitu, wala hayako mbali na
nadhari ya kidini. Kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu huenda akajaalia
sababu za maumbile za kawaida zikajumuika kwa njia tusiyo izoea sisi ili
zikiingiliana kwa njia ya kutisha ndio sababu ya kuharibika dunia. Hapo
maelezo ya kisayansi yanafuatana na Aya zenye kuonya kwa vitisho hivyo
vikuu. Na yote hayo yanatokana kwa Mwenyezi Mungu. Na hutokea kwa idhini
yake Mwenyezi Mungu kutimiza hukumu yake katika dunia yetu.
7. Na mkawa nyote siku hiyo namna tatu kwa mujibu wa vitendo vyenu;
8,9. Basi watu wa mkono wa kulia, watu wa cheo kilio bora, utukufu
ulioje huo wa hali yao! Na watu wa kushotoni, hao ni watu wa cheo duni,
uovu ulioje wa hali yao!
10,11,12. Na walio tangulia mbele katika mambo ya kheri duniani ndio
watakuwa mbele katika vyeo vya Akhera. Hao ndio walio karibishwa mbele
kwa Mwenyezi Mungu. Mola wao Mlezi atawatia katika Bustani zenye neema.
13,14. Hawa walio karibishwa mbele ni kundi la wengi katika mataifa
yaliyo tangulia na Manabii wao, na wachache katika umma wa Muhammad ukiwalinganisha
na hao.
15,16. Juu ya viti au vitanda vilivyo nakishiwa kwa nakshi
za vito vya thamani, wakivitegemea kwa raha na utulivu huku wakielekezana
nyuso kwa ziada ya mahaba.
17,18. Wakiwazungukia kwa kuwakhudumia vijana watakao baki milele
hivyo hivyo, nao wamechukua vikombe na mabirika yaliyo jaa vinywaji vya
Peponi, na bilauri zenye mvinyo kutoka chemchem zinazo miminika,
19. Vinywaji hivyo haviwaletei kuumwa kichwa wala kutokwa akili kwa
ulevi.
20,21. Na matunda ya kila namna wanayo yapenda na wanayo yaona; na
nyama za ndege kama zinavyo tamani nafsi zao.
22,23,24. Na wanawake wenye macho ya vikombe, kama mfano wa lulu
zilio hifadhiwa katika chaza, kwa usafi wao na urembo wao. Watapewa haya
kuwa ni malipo kwa mambo mema waliyo kuwa wakiyatenda duniani.
25,26. Huko Peponi hawatasikia maneno yasiyo kuwa na maana,
wala masimulizi ya kumtia dhambini mwenye kuyasikia. Ila watalo sikia ni
kauli ya wao kwa wao: Tunakusalimuni kwa Salama.
27. Na watu wa mkono wa kulia, hapana ajuaye nini malipo ya watu
wa kuliani.
28,29,30,31,32,33,34. Katika miti ya mikunazi iliyo katwa miba yake,
na migomba iliyo pangika na ndizi zake zimepandana juu ya mikungu, na kivuli
kilicho enea wala hakiondoki, na maji yanayo miminika karibu yao popote
wayatakapo, na matunda ya namna nyingi na kabila nyingi yasiyo tindikia
wakati wowote, wala hazuiwiliwi ayatakayo, na matandiko yaliyo nyanyuliwa
ya starehe.
35,36,37,38. Hakika Sisi tulianza kuwaumba Mahurulaini mwanzo, na
tukawafanya kuwa ni vijana, wenye kupendwa na waume zao, wenye umri ulio
karibiana, wa tayari kwa neema ya watu wa kuliani.
39,40. Watu wa kulia ni wengi katika mataifu yaliyo kwisha tangulia,
na kikundi kikubwa katika umma wa Muhammad.
41. Na watu wa kushoto, hapana anaye jua nini adhabu ya watu wa kushoto.
42,43,44. Watakuwa kwenye upepo umoto utakao wazunguka, unao penya
katika tundu za mwili, na maji yaliyo chemshwa motoni wayanywe na wamiminiwe
vichwani, na katika kivuli cha kiza cheusi cha moshi umoto, hapana ubaridi
wa kupunguza joto la hewa, wala huruma ya kuwaletea nafuu wanapo vuta pumzi.
45. Hakika hao kabla ya haya walikuwa wamepita kiasi katika kustarehea
neema za duniani, wamepumbaa hawataki kumt'ii Mwenyezi Mungu Mtukufu.
46. Na walikuwa wameshikilia daima kufanya dhambi kubwa kabisa, kwani
waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba kabisa Mwenyezi Mungu hatamfufua aliye
kufa.
47. Na walikuwa wakisema kwa kukanusha kurejea tena: Ati tutafufuliwa
baada ya kwisha kufa, na baadhi ya miili yetu ikisha kuwa udongo na mengine
mifupa iliyo chakaa? Ati sisi tutarudishwa tuwe hai mara ya pili?
48. Ati tutafufuliwa sisi na baba zetu wa zamani walio kwisha kuwa
udongo ulio tapanyika na umepotea katika ardhi?
49,50. Waambie kwa kuwajibu kukanusha kwao: Hakika wa zamani na wa
mwisho, ambao nyinyi ni katika jumla ya hao, nyote mtakusanywa katika wakati
wa siku malumu, na wala hamtoipita.
51,52,53. Kisha nyinyi, enyi mnao ipinga Njia ya Uwongofu, mnao kanusha
kufufuliwa, bila ya shaka mtakula mti wa Zaqqumu katika Jahannamu, na mtayajaza
matumbo yenu kwa shida ya njaa.
54,55. Mtakunywa juu ya mlicho kila maji yenye kutokota, yasiyo ondoa
kiu, na mtakunywa kwa wingi na pupa kama anavyo kunywa ngamia mwenye kiu
kisicho katika kiu chake kwa maji.
56. Hayo yaliyo tajwa ya mateso mbali mbali ndio karamu yao waliyo
andaliwa kwa siku ya malipo.
57. Sisi tulianza kukuumbeni mlipo kuwa si chochote, basi hebu hamkiri
uweza wetu wa kukurejesheni tena baada ya kukufufueni?
58,59. Hamuangalii manii mnayo itia katika tumbo la uzazi? Ni nyinyi
ndio mwenye uweza juu yake na kuilea mpaka ikawa mtu, au ni Sisi ndio twenye
makadara hayo?
60,61. Sisi tumekuhukumieni mauti, na tumeweka wakati makhsuri wa
kufa kwenu. Na wala Sisi si wenye kushindwa kukubadilisheni sura zenu,
na kuzileta nyengine, na tukakuumbeni katika umbo jengine na sura nyengine
msiyo ijua.
62. Bila ya shaka mmekwisha yakinika kuwa Mwenyezi Mungu alikuumbeni
mara ya kwanza, basi je, hamkumbuki kwamba Mwenye kuweza hayo ni Mweza
zaidi wa kufanya tena.
63,64. Je! Hamuangalii mbegu mnayo ipanda katika ardhi? Ni nyinyi
mnao ifanya imee au ni Sisi peke yetu ndio tunaifanya imee?
65,66,67. Tungeli taka tungeli ifanya mimea hiyo iwe mabua na mapepe
yaliyo katika katika kabla haijapevuka, mkawa mkistaajabu tu kwa uovu ulio
isibu, huku mkisema: Hakika sisi tumepata khasara baada ya juhudi yetu.
Bali sisi hatuna bahati, tumenyimwa riziki.
68,69. Je! Hamyaoni maji matamu mnayo yanywa? Ni nyinyi mnayo yateremsha
kutoka mawinguni, au ni Sisi ndio Wenye kuyateremsha kuwa ni rehema juu
yenu?
Katika Kiarabu limetajwa neno Almuzni. Maana yake ni mawingu yanayo
leta mvua. Na kitendo cha kunyesha mvua kinahitajia mambo yaliyo khusiana
na hali ya hewa maalumu ambayo mwanaadamu hana mamlaka nayo, au kuyaleta
kwa juhudi zake. Kwa mfano zinahitajiwa pepo zinazo kwenda kwa mkondo zilizo
baridi juu ya nyengine zilizo za joto, au hali za kuondoka utulivu katika
anga.
Na watu wamejaribu kuinyesha mvua kwa mawingu yanayo pita kwa njia
ya ufundi, lakini juhudi hizo mpaka sasa ni majaribio, na lilio thibiti
katika sayansi ni kufuzu kwa majaribio hayo ni kudogo mno, na hata hivyo
kunalazimu ziwepo hali maalumu za maumbile zinazo saidia.
70. Lau tungeli taka tungeli yafanya hayo maji yakawa ya chumvi yasiyo
nyweka. Basi mbona hamumshukuru Mwenyezi Mungu aliye yajaalia matamu yenye
kunyweka?
71,72. Je! Hamuuoni moto huo mnao uasha? Ni nyinyi ndio mlio uotesha
mti wake, na mkautia ndani ya huo mti moto, au ni Sisi ndio tulio uumbia
hivyo, kadhaalika?
73. Sisi tumeufanya huu moto uwe ni ukumbusho wa Moto wa Jahannamu
mtapo uona, na uwe ni manufaa kwa wasafiri wa msitu na nyika, wakinafiika
kwa kupikia chakula chao na kuotea moto wakati wa baridi.
74. Basi dumisha kusabihi, kutakasa, kwa kulidhukuru jina la Mola
wako Mlezi aliye Mkubwa, kwa kumtakasa na kumshukuru kwa neema hizi nzuri.
75,76. Basi ninaapa kweli kwa maangukio ya nyota pale zinapo tua
mwisho wa usiku wakati wa Tahajudi, ibada za usiku, na kustaghafiru.
Na hakika bila ya shaka hicho ni kiapo kikubwa chenye maana ya kufikia
mbali, lau kuwa mnafikiri makusudio yake.
Aya mbili hizi zinabainisha hadi ya umuhimu wa kiapo hichi kikubwa.
Kwani nyota ni vitu vyenye kutoa mwangaza wenyewe, na nyota ya karibu mno
kwetu sisi, nayo ni jua, ni kiasi ya masafa ya miaka 500 ya mwangaza. Na
nyota ifuatayo kwa ukaribu iko mbali nasi kwa kiasi cha miaka 4 ya mwangaza
takriban. Basi nguvu tunazo zitumia kutokana na jua ndizo zinazo tuwezesha
kuishi. Lau kuwa umbali wa jua kutokana na ardhi ni duni ya hivyo au zaidi
ya hivyo basi hapana shaka kuwa maisha yangeli kuwa taabu, bali ni muhali.
Kadhaalika ukubwa wa nyota unakhitalifiana. Zipo nyota kubwa mno hata ukubwa
wake unaweza kukusanya hii ardhi na jua juu ya umbali wao.
Vipo vikundi vya nyota vinavyo itwa A'naqiid vinaogelea angani zikivuka
Njia ya Maziwa The Milky Way mara kwa mara. Wakati wa kupita kwake zikasadifiana
kukutana na kikundi cha jua na zikagongana basi hakika hapo itakuwa ndio
maangamizo na kumalizika kwa kweli. Hata ikikaribia nyota moja katika nyota
zitokazo kwenye jua basi hayo pia yataleta kuharibika mizani na kupelekea
maangamizo na kumalizika ulimwengu.
Kwa hivyo basi hakika Ishara za mazingatio na uweza wa Mwenyezi
Mungu zinaonekana katika ulimwengu huu alio uumba Mwenyezi Mungu Subhanahu
wa Taala na akaupanga.
77,78. Hakika hii bila ya shaka ni Qur'ani yenye manufaa mengi, imo
katika ubao ulio hifadhiwa Al-lauhu-lmahfudh, usio karibiwa na yeyote ila
Malaika walio karibishwa kwa Mwenyezi Mungu. (Kwa watumiaji Computer wanaweza
kukisia kuwa hiyo Al-lauhu-lmahfudh ni kama Disk iliyomo ndani ya Computer
na haigusi mtu, na Misahafu tunayo iona, na kuisoma, ni kama yapigwayo
chapa kutoka hiyo Disk.)
79,80. Hawaigusi Qur'ani Tukufu ila walio t'ahirika na najisi na
hadathi, vitengua udhu; imeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mola Mlezi
wa viumbe vyote.
81. Je! Mnapuuza? Ni Qur'ani hii tukufu ndio nyinyi mnaidharau?
82. Na badala ya kuishukuru riziki yenu ndio mna ikadhibisha?
83,84,85. Basi je! Ikifika roho ya mmoja wenu kwenye mapitio ya pumzi,
na nyinyi inapo fika roho kwenye koo nanyi mnamwangalia huyo anaye kufa,
na Sisi tuko karibu zaidi kwa huyo aliye kabiliwa na mauti na tunaijua
zaidi hali yake kuliko nyinyi, lakini nyinyi hamjui hayo wala hamhisi.
86,87. Basi je! Ikiwa nyinyi si wenye kunyenyekea kwa Ungu wetu,
mrudishieni roho yake huyo aliye kabiliwa na mauti ikiwa nyinyi mwasema
kweli kwamba nyinyi mnazo nguvu na hamshindwi.
88,89. Ama akiwa huyo aliye kabiliwa na mauti ni katika walio tangulia
walio karibishwa basi mwisho wake ni raha, na rehema, na riziki njema,
na Pepo yenye neema.
90,91. Ama akiwa katika watu wa mkono wa kulia, basi ataambiwa kwa
maamkio na takrima: Unapewa salamu kutokana na watu wa kuliani.
92,93,94. Na ama akiwa ni katika wa kushoto, wanao kanusha, walio
wapotovu, basi atakirimiwa maji ya moto hadi ya kuchemka, na kubabuliwa
na moto wa mwisho wa ukali.
95. Hakika haya yaliyo tajwa katika Sura hii tukufu bila ya shaka
ni kiini cha yakini iliyo thibiti, isiyo ingiliwa na shaka.
96. Tanguliza tasbihi kwa kumdhukuru Mola wako Mlezi aliye Mkubwa, kwa kumtakasa na kumshukuru kwa neema zake.