1,2.Arrah'man, Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema amemfundisha
mwanaadamu Qur'ani na akaifanya iwe nyepesi kwake kuisoma na kuifahamu.
3,4. Yeye amemuumba mwanaadamu, na akamfunza kubainisha, kudhihirisha
yaliyo ndani ya nafsi yake, kinyume na makhaluku wenginewe.
5. Na jua na mwezi zinakwenda katika njia zake za mbinguni kwa mujibu
wa hisabu na vipimo visio kwenda pogo.
Aya hii tukufu inataja mwendo wa jua na mwezi kwa kufuata nidhamu
madhubuti tangu Mwenyezi Mungu Mtukufu alipo umba. Wala haukujuulikana
mpango huu madhubuti ila karibuni, kiasi ya miaka 300 iliyo pita. Hapo
ndipo ilipo dhihiri kuwa mwendo wa jua kama unavyo onekana kuzunguka ardhi,
na mwezi kuzunguka ardhi, nyendo hizo zinatimia kwa vipimo vya falaki kufuata
kanuni za mvuto. Na hizo ni hisabu za ndani kabisa, na khasa kwa mintarafu
ya mwezi.
6. Na mimea isiyo na vigogo, na miti inayo simama juu ya vigogo vyake,
yote hiyo inamt'ii na kumnyenyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kila alitakalo
kwao.
7,8. Na mbingu ameziumba kwa kuziweka juu, na akaweka uadilifu ili
mipaka isikiukwe.
9. Na wekeni mizani kwa uadilifu katika kila muamala wenu, wala msipunguze
mizani.
10. Na ardhi ameikunjua na amewatandikia viumbe wanafiike kwayo.
11. Katika ardhi yapo matunda ya namna nyingi, na imo mitende ambayo
ina mafumba ambayo ndani yake ndio imo thamra ya hizo tende.
12. Na katika ardhi zipo nafaka zenye makapi. Hiyo ni riziki yenu
na wanyama wenu. Na humo pia ipo mimea yenye harufu nzuri nzuri.
13. Neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi ambayo nyinyi, makundi
mawili, watu na majini, mnaikataa?
14,15. Ameumba jinsi ya kiutu kwa udongo mkavu usio chomwa kama wa
vyungu. Na ameumba jinsi ya kijini kutokana na ndimi za moto.
16. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi ambayo mnaikataa?
17. Mola Mlezi wa matokeo mawili ya jua, na Mola Mlezi wa machwea
jua mawili.
Yaweza kuwa hapa makusudio yake ni matokea mawili ya jua na mwezi,
na machwea mawili ya jua na mwezi. Na hivyo inaashiriwa muujiza wa usiku
na muujiza wa mchana. Tazama pia maoni ya wataalamu juu ya Aya 71, 72,
na 73 katika Sura Al Qas'as' inayo anzia kwa kauli yake Mtukufu: "Sema:
Mwaonaje kama Mwenyezi Mungu akiufanya usiku ukukalieni moja kwa moja mpaka
siku ya Kiyama.."
Na yafaa pia kuwa Aya hiyo inaashiria jua peke yake, nalo ndilo
tegemeo la maisha katika sayari hii ya ardhi, na hapo makusudio yake ni
kuchomoza na kuchwa kwake siku za baridi, na kuchomoza na kuchwa kwake
siku za joto. Na hivyo ndivyo walivyo fasiri wengi.
Kuonekana huku ni kwa sababu ya kuinama msumari-kati wa mzunguko
wa ardhi kwa mnasaba wa kulizunguka jua kwa kiasi ya daraja 523.5.
Kwa hivyo nusu ya kaskazini ya dunia, kwa mfano inainamia upande wa jua
wakati wa joto, basi mchana huwa mrefu na usiku huwa mfupi mpaka ufikiliwe
mwisho wake. Hapo jua huchomoza mwisho wa umbali kaskazini, na huchwa hivyo
vile vile. Kisha jua huanza kurejea kusini kidogo kidogo kila siku mpaka
lifike kati ya dunia na mashariki na magharibi ya kweli. Tena nusu hii
ya kaskazini huzidi kuinama na kuliacha jua, na usiku huwa mrefu na mchana
ukawa mfupi, na kuonekana jua linaendelea kusini zaidi mpaka kufikia ukomo
wa kusini, na kisha hurejea tena kaskazini siku baada ya siku mpaka lifike
katikati tena kwenye mashariki na magharibi ya kweli kweli. Sehemu ya kusini
ya dunia inakuwa kinyume cha hivyo. Na haya yanayo onekana huzidi
kudhihiri kila ukenda kaskazini zaidi, na kusini zaidi. Na hapana shaka
kuwa mpango huu wa hikima ni kwa maslaha ya hali za maisha juu ya dunia,
kwani kutokana na hayo ndio inapatikana misimu mbali mbali na kwa
hivyo miongo ya ukulima na kuvuna, na mambo yote yanayo onekana katika
maisha ya wanyama na mimea.
18. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
19,20. Mwenyezi Mungu anazipeleka bahari mbili, ya maji matamu na
maji ya chumvi, yanakaribiana bali yanagusana khasa juu yao. Lakini baina
yao kipo kizuizi kwa kudra ya Mwenyezi Mungu, kinacho zuia yasichanganyikane.
21. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
22. Humo hutoka lulu na marijani mnazo zifanya kuwa ni pambo la
kulivaa.
Tazama maoni ya wataalamu juu ya Aya 12 katika Sura Faat'ir. (35:12)
23. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
24. Na yake Yeye majahazi yaliyo undwa kwa mikono yenu, yanayo kwenda
baharini, makubwa yamenyanyuka juu kama vilima.
25. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
26,27. Kila kilioko juu ya ardhi kitaondoka, na atakabakia Mwenyezi
Mungu tu, Mwenye utukufu na kuneemesha.
28. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
29. Wote waliomo mbinguni na waliomo katika ardhi wanamwomba
haja zao Mwenyezi Mungu. Kila wakati Yeye yumo katika jambo, hutukuza na
huangusha, hutoa na hunyima.
30. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
31. Tutakushughulikieni kwa kukusudia kukuhisabieni, enyi majini
na watu Siku ya Kiyama.
32. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
33. Enyi makundi ya majini na watu! Ikiwa mnaweza kutoka pembezoni
mwa mbingu na ardhi kwa kukimbia, basi haya tokeni! Lakini hamwezi kutoka
ila kwa nguvu na kahari; na hayo hamna uwezo nayo!
Mpaka sasa imethibitika kuwa inahitaji juhudi kubwa mno na nguvu
hata kuweza kutokana na mvuto wa ardhi kwa kwendea huko nje ya anga na
mvuto, na kupatikana baadhi ya kufuzu kulikagua anga. Ni kwa muda
mchache sana kwa kulinganisha na ukubwa wa ulimwengu, ndio imetumiwa
juhudi kubwa ya wataalamu wa sayansi katika sehemu mbali mbali za uhandisi,
na hisabu, na ufundi, na ilimu za jiolojia, mbali na chungu ya mali yaliyo
tumiwa na bado yangali yanatumiwa kwa jambo hilo. Na hayo yanaonyesha kwa
dalili ya kukuta kuwa kuweza kuingilia maridhawa katika mbingu na
ardhi, ambayo yanafika mamilioni ya miaka ya mwangaza, ni muhali kwa watu
na majini.
34. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
35. Mtamiminiwa ndimi za moto na shaba iliyo yayushwa, basi hamtaweza
kujilinda na adhabu hiyo.
Shaba inakubaliwa kuwa ni katika maadeni za mwanzo kujuulikana na
binaadamu tangu zama za zamani, na inasifika kuwa daraja yake ya kuyayuka
iko juu sana, kiasi ya daraja 1083 za Centigrade. Basi ikimiminwa maadeni
hii iliyo yayuka juu ya mwili wa mtu, ndio inafananishwa na adhabu iliyo
kuu, na uchungu mkali.
36. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
37. Siku itapo pasuka mbingu ikawa nyekundu iliyo tibuka kama mafuta
yanayo ungua.
38. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
39. Basi siku itapo pasuka mbingu, siku hiyo haulizwi mtu wala jini
dhambi zake.
40. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
41. Wakosefu miongoni mwa watu na majini watajuulikana kwa alama
za kuwatambulisha. Basi watakamatwa washikwe kwa nywele za utosi na kwa
miguu watumbukizwe katika Jahannamu!
42. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
43,44. Wataambiwa kwa kuwashitua: Hii ndiyo Jahannamu waliyo kuwa
wakiikadhibisha wakosefu miongoni mwenu. Watakuwa wakizunguka baina ya
moto na maji ya ukomo wa kuchemka.
45. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
46. Na mwenye kukhofu uweza wa Mola wake Mlezi atakuwa nazo Bustani
mbili.
47. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
48. Bustani hizo zina matawi ya kufurahisha mazuri.
49. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
50. Katika Bustani hizo mtakuwa na chemchem zinazo pita maji kama
wapendavyo.
51. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
52. Humo mtakuwa namna mbili ya kila matunda.
53. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
54. Wametegemea na kutua juu ya matandiko ambayo bit'ana yao ni ya
at'ilasi, hariri nzito; na matunda ya hizo Bustani mbili yatakuwa karibu
kwa mwenye kuyachuma.
55. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
56. Katika hizo Bustani watakuwamo wake wenye kuhifadhi macho yao
hawawaangalii ila waume zao tu, walio bikra hawajakaribiwa kabla yao na
mtu wala jini.
57. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
58. Wanawake hao kwa uzuri wao na usafi wao wa rangi ni kama yakuti
na marijani.
59. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
60. Malipo ya vitendo vyema hayawezi kuwa ila kwa thawabu njema.
61. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
62. Na mbali ya Bustani hizo zilizo kwisha tajwa, zipo mbili nyenginezo.
63. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
64. Za kijani, iliyo koza mno rangi yake hata ikawa inaingia katika
weusi.
65. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
66. Ndani humo zimo chemchem mbili zinazo furika maji yasiyo katika.
67. Basi neema ipi katika neeema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
68. Humo itakuwamo miti ya matunda mbali mbali, na mitende, na mikomamanga.
(mikudhumani).
Huenda huku kutajwa khasa tende na komamanga kwa kuwa ni matunda
bora kuliko mengineyo kama zilivyo thibiti kwa mujibu wa wataalamu.
Kwa kuchambuliwa tende kwa ujuzi wa kimyaa imeonakana kuwa ina sukari
75 katika mia takriban, na aghlabu yake ni sukari ya miwa. Na vile vile
zimo sukari zilio geuka (yaani sukari ya matunda Fructose na sukari ya
zabibu Glucose) Nayo ni nyepesi kuungua katika mwili, na kwa hivyo humpa
mtu nishat'i ya kufanya kazi vizuri viungo na kuupa mwili joto. Na pengine
labda ndiyo hikima ya Mwenyezi Mungu kumuamrisha Mariamu ale tende ili
arejeshe nguvu zake baada ya machungu ya kuzaa. Mbali na hayo, tende inayo
sehemu kubwa katika Calcium (chokaa), na chuma, na fosfori (Phospohorus),
ambazo mwili unahitajia. Na imo pia kiasi maalumu ya Nicotinic acid,
ambayo ni vitamini ya kulinda maradhi ya Pelagra, na vitamini A na B. Na
zimo pia Protein na mafuta. Na vitu hivi vinaifanya tende kuwa ni chakula
chenye manufaa ya kukamilika.
Ama komamanga (au kudhumani kwa Kiswahili cha kaskazini) imo katika
kokwa zake au maji yake sehemu kubwa (ukilinganisha na matunda mengineyo)
ya Lemonic acid ambayo inasaidia inapo ungua katika mwili kupunguza athari
ya ukali acidity au "humudha", katika mkojo na damu inayo sabibisha kuepukana
na maradhi ya Naqras, au gout (kuumwa viungo aghlabu kidole gumba cha mguu),
na kufanyika mawe katika mafigo. Juu ya hayo katika maji ya komamanga zimo
sukari namna mbali mbali si haba (11 katika mia) zilizo nyepesi kuungua,
na zenye kuleta nishat'i ya kufanyia kazi. Kadhaalika maganda ya komamanga
yana maada ya kukausha ya kuzuia kuhara Tannin inayo linda matumbo madogo
(chango) na yanayo yasibu wakati wa kuwa na maradhi ya kuhara. Kadhaalika
maganda ya komamanga hutumika kuuwa minyoo, michango
69. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
70. Humo watakuwamo wake wenye tabia njema, wenye nyuso za kupendeza.
71. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
72. Wazuri wa macho, wenye kutawishwa ndani ya makhema yao.
73. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
74. Hawajakaribiwa na mtu wala jini kabla ya waume wao.
75. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
76. Wameegemea juu ya viti vya enzi vyenye makava ya kijani na mazulia
mazuri mazuri yaliyo fanywa kwa ufundi wa ajabu.
77. Basi neema ipi katika neemza za Mola wenu Mlezi mnayo ikataa?
78. Limetakasika jina la Mola wako Mlezi Mwenye utukufu na wingi wa neema.