1. Kiyama kimekaribia na mwezi utapasuka hapana hivi
wala hivi.
2. Na makafiri wakiona Ishara, yaani muujiza mkubwa, wao hupuuza
wakaacha kuuamini. Bali husema: Huu ni uchawi wa daima unaendelea!
3. Na wamewakanusha Mitume na wakafuata yaliyo zainishwa na matamanio
yao. Na kila jambo huishia mwisho wake linapo tulia na kuthibiti.
4. Na ninaapa kuwa zimewajia makafiri khabari za mataifa yaliyo tangulia
zenye ukweli wa uumbaji ambazo zina mikemeo ya kutosha.
5. Haya yaliyo wajia ni hikima kubwa na lengo la kufikia mbali. Lakini
maonyo yataleta faida gani kwa wanao zipinga hikima hizo?
6. Ewe Muhammad! Waachilie mbali hawa makafiri, nawe ngojea
siku atapoita mwitaji wa Mwenyezi Mungu kuitia jambo ambalo nafsi inalichukia
mno!
7. Macho yao yatainamia chini kwa wingi wa kitisho, wakitoka makaburini
kama kwamba ni nzige walio tawanyika, kwa wingi wao na mbio zao.
8. Wakimkimbilia huyo mwitaji, wakimtazama kwa unyonge na unyenekevu,
macho yao yanamwangalia yeye tu. Makafiri watasema Siku ya Kiyama: Hii
leo ni siku nzito, siku ya shida!
9. Kabla ya makafiri wa Makka walikwisha kanusha kaumu ya Nuhu. Walimkadhibisha
Nuhu, mja wetu na Mtume wetu, wakamsingizia kuwa ana wazimu. Wakaingiza
baina yake na kufikisha kwake Ujumbe kila namna ya maudhi na vitisho.
10. Nuhu akamwomba Mola wake Mlezi akisema: Hakika mimi nimeshindwa
na hawa watu wangu, basi wapatilize hawa kwa ajili yangu!
11,12. Basi tukaifungua milango ya mbingu ikamimina maji yasiyo katika;
na tukaipasua ardhi kwa chemchem zikitibuka maji. Yakakutana maji ya mbinguni
na maji ya ardhi kuwahiliki, kama alivyo kadiria Mwenyezi Mungu Mtukufu.
13,14. Tukampakia Nuhu katika jahazi la mbao zinazo fungwa pamoja
kwa kamba, kama mtepe. Likawa linakwenda baharini chini ya hifadhi yetu,
kuwa ni malipo kwa Nuhu ambaye watu wake waliendelea kuukanya wito
wake.
15. Na tumeliacha hilo tukio na kuzamishwa makafiri na kuokolewa
Waumini liwe ni mawaidha, lakini yupo mwenye kuwaidhika?
16. Jee, vipi ilikuwa adhabu yangu na onyo langu kwa wakhalifu.
17. Ninaapa, tumeifanya Qur'ani iwe sahali kukumbukwa na kutoa mawaidha.
Lakini je, yupo wa kuwaidhika?
18. Kina A'di walimkadhibisha Mtume wao Hudi. Je, hali gani adhabu
yangu na onyo langu lilikuwa kwa wendao kinyume!
19,20. Sisi kwa yakini tuliwapatiliza kwa upepo ubaridi unao vuma,
katika siku ya ukorofi wa daima, ukiwang'oa watu na kuwatupa nao wamekufa,
kama vinavyo ng'olewa vigogo vya mitende na mizizi yake.
21. Hali gani adhabu yangu na onyo langu lilikuwa kwa walio kwenda
kinyume!
22. Na bila ya shaka Sisi tumeifanya sahali Qur'ani kwa ajili ya
mawaidha na mazingatio, basi je, yupo wa kuwaidhika?
23. Thamudi walikadhibisha maonyo ya Nabii wao, Saleh.
24. Wakasema: Hivyo aje mtu tu katika sisi, watu wa kawaida, asiye
na watu, nasi tumfuate? Tukimfuata huyo basi bila ya shaka sisi tutakuwa
mbali mno na haki, na tutakuwa tuna wazimu basi.
25. Uteremshiwe wahyi kwake yeye katika sisi na hali wapo wanao stahiki
zaidi? Bali huyo kazikdi katika uwongo, mwenye kukanya neema.
26. Karibu watakuja jua siku itapo wateremkia adhabu ni nani mwongo
anaye ikanya neema. Wao au Saleh, Mtume wao?
27. Hakika Sisi tunampelekea Mtume wetu Saleh ngamia mke, awe ni
mtihani wao. Basi wangojee, na uwatazame watafanya nini. Na subiri,
uvumilie maudhi yao mpaka itapo kuja amri ya Mwenyezi Mungu.
28. Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao na ngamia. Kila
mmoja wao atakuwa na zamu yake aje kunywa katika siku yake.
29,30. Wakamwita mtu wao mmoja akapania kumchinja yule ngamia, akamchinja.
Basi vipi ilikuwa adhabu yangu na onyo langu kwa hao wakhalifu walio kwenda
kinyume na amri.
31. Sisi tuliwapatiliza kwa ukelele mmoja tu, wakawa kama miti mikavu
anayo ikusanya yeyote atakaye kujengea boma la uwa wake.
32. Na bila ya shaka Sisi tumeisahilisha Qur'ani iwe nyepesi kwa
ajili ya mawaidha na kuzingatia. Lakini je, yupo wa kuwaidhika?
33. Kaumu Lut'i nao walikadhibisha maonyo ya Mtume wao.
34,35. Hakika Sisi tuliwapelekea upepo mkali wa kuwatupia changarawe.
Isipo kuwa watu wa Lut'i walio amini. Hao tuliwaokoa na adhabu hii mwisho
wa usiku, kwa kuwapa neema iliyo toka kwetu. Neema kama hizo kubwa kubwa
ndivyo tunavyo walipa wenye kuishukuru neema yetu kwa imani yao na ut'iifu.
36. Na hakika Lut'i aliwahadharisha watu wake vipi mshiko wetu ulivyo
mkali, wakatilia shaka maonyo yake kwa kuwa wanamwona mwongo.
37. Wakamtaka awape wageni wake wawatende fiili yao, tukayafuta macho
yao kuwa ni malipo kwa hilo walilo litaka. Basi waambie kwa kuwakejeli:
Igugumieni adhabu yangu, na maonyo yangu!
38,39. Na asubuhi mapema ikawashitua adhabu ya kuthibiti milele.
Wakaambiwa: Igugumieni adhabu yangu na maonyo yangu!
40. Na hakika tumeifanya Qur'ani ni sahali kwa ajili ya mawaidha
na mazingatio. Je! Yupo anaye waidhika?
41. Na watu wa Firauni yaliwajia maonyo ya mfululizo.
42. Walikadhibisha Ishara zetu na miujiza yetu waliyo kuja nayo Mitume
wetu. Tukawaangamiza kwa maangamizo ya nguvu yasiyo shindika, ya uwezo
mkubwa.
43. Ati nyinyi, makafiri, mna nguvu zaidi kuliko hao wa kaumu zilizo
tangulia ambao wameangamizwa? Au nyinyi mmetolewa makosani kwa ilivyo teremka
katika Vitabu vya mbinguni?
44. Bali ati wanasema hawa makafiri: Sisi ni kikundi kilicho ungana
chenye nguvu juu ya maadui wake, hakishindwi.
45. Kikundi hicho kitashindwa, na watakimbia mbio wakifurushwa.
46. Bali Kiyama ndio miadi ya adhabu yao. Na Kiyama ni kizito
zaidi, na kichungu zaidi.
47. Hakika wakosefu kutokana na hawa na hao watakuwa katika hilaki
na Jahannamu inayo waka moto.
48. Siku watapo bururwa kifudifudi katika Moto wakiambiwa: Hilikini
kwa machungu ya Jahannamu na joto lake!
49. Hakika Sisi tumeumba kila kitu. Tumeviumba kwa kukadiria inavyo
hitajia hikima.
50. Na haikuwa amri yetu tukitaka kitu ila neno moja tu, nalo ni
kusema: "Kuwa", nacho huwa, papo hapo kama kupepesa kwa jicho.
51. Na bila ya shaka Sisi tumekwisha waangamiza wengine walio fanana
nanyi katika ukafiri. Je! Yupo aliye waidihika?
52. Na kila kitu walicho kifanya duniani kimeandikwa katika madaftari,
kimeambatishwa nao.
53. Na kila dogo na kubwa katika vitendo limeandikwa. Hakipotei kitu.
54. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani yenye shani kuu, na
mito ya namna mbali mbali.
55. Katika baraza ya Haki, hakuna porojo huko wala madhambi, kwa Mwenyewe Mfalme Mtukufu wa uweza.