1,2. Ninaapa kwa nyota inapo tua kwa kuchwa, ya kwamba
Muhammad hakuiacha Njia iliyo sawa ya kufuata Haki, na wala hakupata kuitakidi
upotovu.
3. Wala halitoki katika anayo yatamka ya Qur'ani kwa mapendo ya nafsi
yake.
4. Hii Qur'ani anayo itamka si chochote ila ni Wahyi (Ufunuo) ulio
toka kwa Mwenyezi Mungu anamfunulia yeye.
5. Aliye mfundisha ufunuo huu ni mwenye nguvu nyingi.
6,7. Ambaye ametua akili zake na maoni yake, akasimama sawa sawa
katika sura yake; naye yuko upande wa juu katika mbingu upeo wa macho wa
mwenye kuangalia.
8,9. Kisha Jibrili alimkaribia, na akazidi kukaribia, hata akawa
ukaribu wake ni kiasi ya mipinde miwili, bali karibu kuliko hivyo.
10. Jibrili akamfunulia mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, alicho
mfunulia, nao ufunuo huo ni jambo lenye shani kubwa na athari ya mbali
kabisa.
11. Moyo wa Muhammad haukukanya yale macho yake yaliyo yaona.
12. Hivyo nyinyi mnamkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu na mnabishana
naye kwa aliyo yaona kwa macho yake?
13,14,15,16,17. Na bila ya shaka Muhammad alimwona Jibrili kwa sura
yake mara nyengine, katika pahala pasipo juulikana ila na Mwenyezi Mungu
tu, ambapo amepaita Sidratul muntahaa, "Mkunazi wa Mwisho". Na akasimulia
kuwa hapo ndio ipo Jannatul Ma-awa, Bustani inayo kaliwa. Vikafunikwa na
kuzibwa, kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu, visio weza kuelezwa. Jicho la Muhammad
halikubabaika kwa aliyo yaona, na wala hakukiuka mpaka ya aliyo amrishwa
kwa kuona kwake huko.
18. Hakika ameona mengi katika Ishara za Mwenyezi Mungu na maajabu
yake makubwa makubwa.
19,20. Je! Mmeyajua hayo, na mkayafikiri ya kina Lata na Uzza na
Manata, huyo mwengine wa tatu, mlio wafanya kuwa ni miungu wa kuwaabudu?
21. Mkagawa, nyinyi muwe na watoto wa kiume, na mkamfanyia Mwenyezi
Mungu awe na watoto wa kike!
22. Huo basi ni ugawaji wa dhulma, mnamgawia Mwenyezi Mungu kile
mnacho kichukia nyinyi wenyewe!
23. Hayo masanamu yenu si chochote ila ni majina tu yasiyo na maana
yoyote ya kiungu. Mmeyatunga nyinyi na baba zenu kwa kufuata pumbao lenu
la upotovu. Mwenyezi Mungu hakuteremsha nayo hoja yoyote ya kusadikisha
huo uzushi wenu mnao wadaia. Na hawa hawafuati ila ni dhana tu, na kipendacho
nyoyo zao zilio potoka na kuacha maumbile yaliyo sawa. Na hakika yalikwisha
wajia kutoka kwa Mola wao Mlezi yenye uwongofu, laiti wangeli ufuata huo!
24,25. Mwanaadamu hapati kila anacho kitamani, ya kupata uombezi
wa haya masanamu au mengineyo anayo yatamani kwa nafsi yake. Kwani mambo
yote, ya duniani na Akhera, ni ya Mwenyezi Mungu peke yake.
26. Na malaika wengi wa mbinguni, juu ya ubora wa vyeo vyao, haufai
kitu uombezi wao isipo kuwa baada ya kupewa idhini huyo mwombezi na Mwenyewe
Mtukufu, na kumridhia huyo mwenye kuombewa.
27. Hakika hao wasio iamini Akhera ndio bila ya shaka wanao sema
kuwa Malaika ni wanawake. Wanasema: Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu!
28. Na kwa kauli hii hawana ujuzi wowote. Hawafuati kitu ila dhana
zao tu zilio potoka, na dhana haifai kitu mbele ya haki.
29. Basi jitenge nao hao makafiri walio ipuuza Qur'ani na ikawa hamu
yao si chochote ila uhai wa duniani tu, wakiyakataa yenye maslaha nao.
30. Hayo wanayo yafuata katika itikadi zao, na vitendo vyao ndio
ukomo walio yafikilia katika ilimu. Hakika Mola wako Mlezi anamjua vyema
anaye shikilia upotovu, na anamjua vyema aliye elekea kupokea uwongofu.
31. Na ni vya Mwenyezi Mungu pekee vyote viliomo katika mbingu na
ardhi, kwa kuviumba na kuvidabiri, ili awalipe walio potea wenye kufanya
viovu vitendo vyao, na awalipe walio hidika watu wema kwa malipo yaliyo
mema.
32. Wema hao ndio wale wanao jitenga na madhambi yenye adhabu kubwa
kubwa, na yanayo chukiza mno. Lakini Mwenyezi Mungu husamehe dhambi ndogo
ndogo. Hakika Mola wako Mlezi ni Mkuu wa kughufiria, naye anajua vyema
hali zenu. Kwani Yeye ndiye aliye kuumbeni kutokana na ardhi, na mlipo
kuwa mimba matumboni mwa mama zenu katika hali zenu mbali mbali za kukua
na kugeuka. Basi msikae mkijisifu nafsi zenu kuwa mmesafika kwa kujigamba
na kujifakhari. Na Yeye ndiye Mjuzi mkubwa kabisa wa kila mwenye kumcha
na akajisafisha nafsi yake kweli kweli kwa uchamngu wake.
33,34,35. Je! Umezingatia ukamwona anaye puuza kuifuata Haki, na
akatoa kidogo katika mali, na khalafu akakata kabisa kutoa? Je! Huyo anayo
ilimu ya kujua mambo ya ghaibu, basi kwa hivyo ndio anayajua yanayo mpelekea
kuiacha kuifuata Haki, na akafanya ubakhili wa mali?
36,37,38. Kwani huyo hakuambiwa yaliomo katika Vitabu vya Musa na
Ibrahim, aliye fika ukomo wa kutimiza aliyo agana na Mwenyezi Mungu, ya
kwamba hapana mtu ataye mbebea dhambi mwenginewe?
39. Na kwamba mtu hapati ila malipo ya vitendo vyake mwenyewe.
40. Na kwamba vitendo vyake vitakuja tangazwa, na ataviona Siku ya
Kiyama, iwe ni kumtukuza mtenda mema, na kumkebehi mtenda maovu.
41. Kisha kila mtu atalipwa malipo anayo stahiki.
42. Na kwamba kwa hakika ni kwa Mola wako Mlezi, wala si kwa mwenginewe,
ndio miadi ya kurejea.
43. Na Yeye peke yake ni Mwenye uweza wa kuufanya uso uonyeshe furaha
au maudhiko, na pia ni Mwenye kuziumba sababu za starehe na dhiki.
44. Na hakika ni Yeye, ndiye Mwenye kuondoa uhai, na kuuleta.
45,46. Na Yeye ndiye aliye umba vitu kwa jozi, yaani dume na jike,
binaadamu na wanyama, kutokana na manii yanayo miminwa.
Makusudio ya Aya hii tukufu ni kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu
Mtukufu kwamba Yeye ameumba waume na wake katika wanaadamu na wanyama wote
kutokana na tone ya manii ambayo humo humo mna ume na uke. Na juu ya udogo
wake na udhaifu wake ndio chemchem ya uhai. Umuujiza wa Qur'ani unadhihirika
katika Aya hii tukufu ukikumbuka kuwa ulimwengu ulikuwa haujui mpaka hivi
karibu kuwa katika maji ya mwanamume ndio zimo mbegu "sperms" na katika
maji ya mwanamke mna vijiyai "ova", ndio vikikutana vijidudu vya manii
ya mwanamume na vijiyai vya mwanamke vikawa kitu kimoja ndio hiyo
huwa mimba. Ukweli huu ulitajwa na Qur'ani kabla ya kuvumbuliwa na ilimu
za Sayansi.
47. Na juu yake Yeye ndio kufufua baada ya kifo.
48. Na Yeye ndiye anaye toa kinacho tosheleza, na akaridhisha kwa
kinacho kinaisha na cha kuweka akiba.
49. Na hakika Yeye ndiye Mola Mlezi wa hii nyota kubwa inayo itwa
Shii'ra (Sirius, Dog Star).
Makusudio hapa ni Nyota hiyo inayo itwa Ash-shi'ra Alyamaaniya,
au wanavyo ita Wazungu Sirius au Dog Star. Nyota hii inang'ara kwa nguvu
zaidi kuliko nyota zote ziliomo katika kikundi cha nyota kinacho itwa Alkalbu
l-akbar, kwa Kizungu Canis Major au Greater Dog. Nyota hiyo ndiyo inayo
zagaa sana mbinguni, na huonekana kusini ya mstari wa kati wa mbinguni
kiasi ya daraja 18. Na kwa jina hilo la Nyota ya Mbwa ikijuulikana hata
miaka elfu tatu ilio pita. Katika mabaki ya michoro ya Mafirauni wa Misri
imeashiriwa pia. Mwenyezi Mungu ameitaja khasa kwa kuwa Waarabu walikuwa
wakiiabudu hapo kale, na pia Wamisri wa zamani, kwani kutokea kwake upande
wa mashariki katikati ya mwezi wa Julai kabla ya kuchomoza jua kulikuwa
kunawafikiana na wakati wa mafuriko ya Misri ya kati, yaani katika tukio
muhimu kabisa katika ulimwengu huo wa kale. Na tukio hili huenda ndilo
lilio fanya kuanzisha kuwekea kiwango urefu wa mwaka katika dunia nzima.
Kwani kudhihiri Nyota ya Shiira kabla ya kuchomoza jua hakutokei ila mara
moja tu katika mwaka. Basi huu ndio mwanzo wa mwaka mpya.
50,51. Na Yeye ndiye aliye wateketeza kina A'di wa mwanzo, kaumu
ya Nabii Hudi. Na akawateketeza Thamudi, kaumu ya Nabii Saleh. Hakuwabakisha.
52. Na aliwaangamiza kaumu ya Nuhu kabla ya kuwaangamiza A'di na
Thamudi. Hakika hao walikuwa wamekithiri kudhulumu, na wamezidi kwa uasi
kuliko A'di na Thamudi.
53. Na miji ya kaumu Lut'i iliyo pinduliwa juu chini, ni Yeye Mwenyezi
Mungu ndiye aliye ipindua.
54,55. Akaizunguka kwa kuiadhibu kama alivyo izunguka. Basi katika
neema za Mola wako Mlezi una shaka nayo ipi?
56. Hii Qur'ani ni onyo katika jinsi ya yale yale maonyo ya kale
waliyo onywa kwayo watu walio tangulia.
57,58. Kiyama kimekaribia; na wala hapana wa kuujuulisha wakati kitapo
tokea ila mwenyewe Mwenyezi Mungu.
59,60,61. Hivyo nyinyi mnapinga kila la kweli? Na mnaistaajabia
kwa kuikaataa hii Qur'ani? Na mnacheka kwa kejeli na maskhaara, wala hamlii
kama wafanyavyo wenye yakini, nanyi mmo katika pumbao na kutakabari?
62. Basi msujudieni Mwenyezi Mungu aliye iteremsha Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu wote, na muabuduni Yeye tu peke yake Mwenye kutukuka kwa utukufu wake.