1,2,3,4,5,6. Ninaapa kwa mlima wa T'ur ulioko katika
Sinai. Kwenye mlima huo ndio Nabii Musa a.s. alisemezwa. Na naapa kwa Kitabu
kilicho teremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kilicho andikwa katika kurasa
zilio nyepesi kuzisoma, na kwa Nyumba iliyo jengwa kwa sababu ya wenye
kuizunguka kwa ibada na wenye kusimama na kurukuu na kusujudu kwa Sala,
na naapa kwa mbingu iliyo nyanyuliwa bila ya nguzo, na bahari iliyo jaa.
7,8. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi waliyo ahidiwa makafiri bila
ya shaka itawateremkia hapana hivi wala hivi. Hapana wa kuizuia isiwafikilie.
9,10. Siku mbingu itapo tikisika kwa mtikiso mkubwa, na milima itapo
ng'oka kutoka hapo ilipo kwa kuonekana khasa.
11,12. Maangamio makubwa yatawapata siku hiyo hao wanao kadhibisha
Haki, ambao katika upotovu ndio mchezo wao wanapo chezea.
13. Siku watakapo sukumwa kuingizwa Motoni kwa nguvu.
14. Wataambiwa: Huu ndio Moto mlio kuwa mkiukanusha duniani.
15. Je! Bado mnaendelea kuukanya. Huu Moto mnao uona ni uchawi, au
hamwoni tu?
16. Uingieni, mpate kuonja vukuto lake. Mkivumilia shida zake, au
mkitovumilia, kwenu ni mamoja. Hakika leo mtayakuta mliyo kuwa mkiyatenda
duniani.
17. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani yenye wasaa, hapana
awezae kuyaeleza yalivyo, na neema kubwa kadhaalika.
18. Wakistarehe na neema alizo wapa Mola wao Mlezi, na Mola wao Mlezi
akawalinda na adhabu ya Moto.
19. Wataambiwa: Kuleni chakula mpendacho, na kunyweni kwa raha, kuwa
ni malipo ya vitendo mlivyo vitenda duniani.
20. Wakikaa nao wameegema juu ya makochi yaliyo pangwa kwa safu.
Na tutawaoza wake weupe wenye macho ya vikombe wazuri.
21. Na walio amini, na wakastahiki vyeo vya juu, na vizazi vyao wakawafuata
katika Imani, na wao hawajafikia daraja zile za baba zao, tutawakutanisha
nao hao dhuriya zao, wapate kutulia nyoyo zao. Na wala hatuwapunguzii chochote
katika thawabu za vitendo vyao. Wala wazazi hawatobeba chembe katika makosa
ya dhuriya zao. Kwa sababu kila mtu amefungamana kwa rahani na vitendo
vyake visio bebwa na mwenginewe.
22. Na tutawazidishia matunda mengi, na nyama kama waipendayo.
23. Huko Peponi watakuwa wakipeana kwa mapenzi bilauri zilio jaa
vinywaji visio leta maneno yasiyo na maana wala vitendo vya dhambi, yaani
havilevi na kuondoa akili.
24. Na watakuwa wakiwapitia vijana walio wekwa kwa kuwatumikia, kwa
weupe wao na usafi wao kama lulu iliomo ndani ya chaza.
25. Na watu wa Peponi watakabiliana wakiulizana wao kwa wao khabari
za hayo mambo makuu wanayo yapata na sababu zake.
26,27. Kabla ya neema hizi sisi tulikuwa pamoja na ahali zetu tukiiogopa
adhabu ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akatufadhili kwa rehema yake,
na akatukinga na adhabu ya Moto.
28. Hakika sisi kabla ya haya tulikuwa duniani tukimuabudu Yeye tu.
Yeye peke yake ndiye Mhisani Mkunjufu wa rehema.
29. Wewe endelea na kukumbusha kama unavyo fanya. Kwani wewe, kwa
neema ya Mwenyezi Mungu aliyo kuneemesha kukupa Unabii na akili iliyo timia,
si kuhani anaye toa khabari za ghaibu bila ya ilimu, wala si mwendawazimu
unaye sema usiyo yasadiki.
30,31. Bali ati wanasema huyu ni mtunga mashairi, tunaye mngojea
afikiwe na mauti! Waambie kwa kuwatisha: Ngojeeni, na mimi nami ni katika
wanao ngojea mwisho wa hali yangu na hali yenu!
32. Bali ndio akili zao zinawaamrisha waseme maneno hayo yanayo gongana.
Kwani kohani na mtunga mashairi ni watu wenye fahamu na akili; na mwendawazimu
hana akili. Lakini hawa ni watu walio pita mipaka katika inadi zao.
33. Bali ati wanasema: Muhammad ameizua hii Qur'ani! Bali hawa kwa
ukaidi wao hawaamini tu.
34. Basi nawalete masimulizi kama haya ya Qur'ani, ikiwa wao ni wasema
kweli kuwa Muhammad kaizua.
35. Kwani wao wameumbwa bila ya kuweko Muumbaji, au wao wamejiumba
wenyewe, basi kwa hivyo ati ndio hawamtambui Muumbaji wa kumuabudu?
36. Kwani wao ndio walio ziumba mbingu na ardhi kwa uumbaji mzuri
wa pekee wa namna hii? Bali wao hawana na yakini na lolote lilio
mwajibikia Muumbaji. Na kwa hivyo ndio wanamshirikisha.
37. Kwani wao wanazo khazina za Mola wako Mlezi wanazo zisarifu watakavyo?
Au wana nguvu za kutenda watakavyo, na kupanga mambo kama wapendavyo?
38. Bali wanacho kipandio cha kupandia mpaka mbinguni wakasikiliza
anayo yahukumia Mwenyezi Mungu? Kama hivyo, basi nawamlete huyo mtu wao
anaye sikiliza atoe hoja iliyo wazi kuthibitisha madai yake.
39. Ati Mwenyezi Mungu ndiye mwenye mabinti, kama mnavyo zua, na
nyinyi ndio mna watoto wa kiume kama ndio mnavyo penda?
40. Kwani wewe unawaomba chochote kuwa ni ujira wa kuwafikishia Ujumbe
wako, ndio wamethakilika na hizo gharama wakalalimika?
41. Bali kwani wao wanao ujuzi kujua mambo ya ghaibu, yaliyo fichikana,
na hivyo wanaandika kutoka hayo wayatakayo?
42. Au wanataka kukufanyia vitimbi tu na kuuharibu Ujumbe wako? Basi
hao walio kufuru ndio wanao stahiki kutumbukia katika vitimbi vyao.
43. Au wao wanae mungu wa kuabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu atakae
walinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo
wanayo mshirikisha naye!
44. Na wakiona kipande cha mbingu kinwaangukia kuwaadhibu wao husema,
kwa inda tu: Ni mawingu yaliyo bebana!
45. Waache bila ya kuwajali mpaka watakapo ikuta siku yao watapo
angamizwa.
46. Siku ambayo hila zao hazitawakinga hata na chembe ya adhabu,
wala hawatapata wa kuwanusuru.
47. Na hakika hao walio dhulumu watapata adhabu mbali na hii waliyo
teseka nayo hapa duniani, lakini wengi wao hawajui hayo.
48. Wewe isubirie hukumu ya Mola wako Mlezi ya kuwapa muhula hao,
na wewe kupata maudhi yao. Kwani hakika wewe umo katika hifadhi yetu na
ulinzi wetu. Basi vitimbi vyao havitokudhuru wewe. Na mtakase kwa kumsifu
Mola wako Mlezi unapo amka.
49. Na tafuta usiku usiku nafasi ya kumsabihi, yaani kumtakasa, Mwenyezi Mungu, na mtakase pia wakati zinapo kuchwa nyota, yaani alfajiri.