1,2,3,4. Ninaapa kwa pepo zinazo timua mawingu, zikayasukuma
kwa nguvu, huku zikibeba mizigo mizito ya maji, zikawa zinakwenda kwa wepesi
kwa amri ya Mwenyezi Mungu, zikawa zinagawanya riziki kwa ampendaye Mwenyezi
Mungu.
5,6. Hakika hayo mnayo ahidiwa, nayo ya kufufuliwa na mengineyo,
ni hakika ya kweli itakayo tokea, na kwamba kwa yakini malipo kwa vitendo
vyenu yatakuwa tu hapana hivi wala hivi.
7,8. Ninaapa kwa mbingu zenye njia zilizo wekwa baraabara, kwamba
nyinyi msemapo mnayo yasema ni maneno ya kugongana.
9. Huacha kuamini hiyo ahadi ya kweli na malipo yatakayo kuwa huyo
anaye acha, kwa sababu amekhiari kufuata pumbao la nafsi yake kuliko akili
yake.
10,11. Wameteketea waongo wanao sema katika khabari za Kiyama kuwa
ni mambo ya dhana na kukisia tu, ambao kwamba wamezamishwa katika ujinga,
wameghafilika na dalili za yakini.
12. Wanauliza kwa kejeli, kwa kuwa wanaona hayawi hayo: Lini itakuwa
hiyo siku ya malipo?
13. Siku watapo simamishwa Motoni wakichomwa!
14. Wataambiwa: Onjeni adhabu yenu hii ambayo duniani mlikuwa mkiihimiza
iwe.
15. Hakika walio mt'ii Mwenyezi Mungu na wakamkhofu watakuwa wananeemeka
katika Mabustani na chemchem za Peponi ambazo haziwezi kusifika hakika
yake.
16. Wakipokea thawabu na takrima wanazo pewa na Mola wao Mlezi. Hakika
hao kabla ya hapo walikuwa duniani ni wenye kufanya mambo mazuri kwa kutimiza
waliyo takiwa wayafanye.
17,18. Walikuwa kulala kwao usiku ni kuchache, na wakikesha sana
kwa ibada, na mwishoni mwa usiku walikuwa wakiomba maghfira.
19. Na katika mali yao wakiweka fungu maalumu lilio thibiti kwa ajili
ya wenye haja, wanao omba na wanao jizuilia kuomba kwa kujiteta.
20. Na katika ardhi zipo dalili nyingi zilizo wazi zinazo pelekea
yakini, kwa mwenye kuitafuta njia.
21. Na hali kadhaalika katika nafsi zenu zipo Ishara zilizo wazi.
Je! Mmeghafilika nazo, hamzioni?
22. Na katika mbingu ipo amri ya riziki zenu na kukadiriwa mnayo
ahidiwa.
23. Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi kwamba hakika yote
hayo mnayo yakanya kuwa, yaani kufufuliwa, kulipwa, kuadhibiwa wanao kadhibisha,
na kuwalipa thawabu wachamngu, yote hayo bila ya shaka ni ya kweli thaabiti
kama hivyo kusema kwenu ambako hamna shaka nako kuwa mnasema.
24,25. Unakijua kisa cha Malaika, wageni wa hishima wa Ibrahim? Pale
walipo ingia kwake na wakamtolea Salamu, na yeye akawajibu kwa Salamu,
na kuwambia kuwa ni watu asio wajua.
26,27. Akenda kwa mkewe naye ana khofu, akaja na ndama aliye nona.
Akawakaribisha, nao hawakula. Akasema kwa kuto wajua hakika yao: Mbona
hamli?
28. Akahisi katika nafsi yake khofu kuwaogopa. Wakasema: Usiogope.
Na wakampa bishara kuwa atapata mwana mwenye ilimu nzuri.
29. Akatokea mkewe akipiga kelele alipo isikia ile bishara, akijipiga
uso wake kwa mkono wake, kwa kuona muhali hayo na kustaajabu, na akasema:
Mimi ni kizee, na tasa. Itakuwaje nizae?
30. Wakasema: Hivyo ndivyo alivyo kwisha hukumu Mola wako Mlezi.
Hakika Yeye ni Mwenye hikima katika kila anayo hukumu, ni Mwenye ujuzi
ambaye hapana linalo fichikana kwake lolote.
31. Ibrahim akasema: Mna kazi gani tena baada ya khabari hii nzuri,
enyi wajumbe?
32,33,34. Wakasema: Kwa hakika sisi tumetumwa kwa kaumu iliyo pita
kiasi katika uasi, tuwatupie mawe ya udongo, ambayo hapana anaye yajua
yalivyo ila Mwenyezi Mungu. Mawe hayo ni makhsusi na maalumu kwa Mola wako
Mlezi kwa ajili ya wanao pindukia mipaka katika mambo machafu.
35,36. Basi tukahukumu tuwatoea kwenye mji huo walio amini. Lakini
hatukukuta ila nyumba moja tu ndiyo ya Waislamu.
37. Na katika mji huo tumeacha alama ya maangamizo ya watu wake,
ili wapate kuzingatia wanayo ikhofu adhabu chungu.
38. Na katika kisa cha Musa yapo mawaidha. Tulipo mtuma kwa Firauni,
na tukatilia nguvu kwa kumpa ushahidi ulio wazi.
39. Firauni akapuuza kumuamini Musa kwa kutegemea ati nguvu zake.
Akasema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu!
40. Tukamchukua yeye na hao anao jitapia kwao, tukawatumbukiza baharini,
naye ni mwenye kuyatenda hayo ya ukafiri na inda anayo laumiwa kwayo.
41. Na katika kisa cha A'di yamo mawaidha pia. Tulipo wapelekea upepo
usio kuwa na kheri yoyote.
42. Upepo huo haupiti kwa kitu chochote ila hukiacha kama fupa lilio
nyambuka.
43,44. Na katika kisa cha Thamudi ipo Ishara. Walipo ambiwa: Stareheni
katika majumba yenu kwa muda maalumu. Wakajivuna na wakatakabari wasifuate
amri ya Mola wao Mlezi. Basi radi ikawaangamiza nao wanaiona kwa macho
yao inavyo tokea.
45. Basi hawakuweza kuinuka. Wala hawakuweza kujipigania kuijikinga
na adhabu.
46. Na kaumu ya Nuhu tuliihiliki kabla ya hawa. Hakika hao walikuwa
watu walio toka nje ya ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
47,48. Na mbingu tumeipanga kwa nguvu, na bila ya shaka Sisi ni waweza
zaidi ya hayo. (1) Na ardhi tumeikunjua, na Sisi ni wenye kuitengeneza
vizuri kama kitanda.
(1) Aya hii tukufu inaashiria maana za kitaalamu nyingi; miongoni
mwazo ni kwamba Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la ameumba ulimwengu huu
mkunjufu kwa nguvu. Na Yeye ni Muweza kwa atakayo. Na maana ya mbingu katika
Aya hii ni kila kilicho juu ya kitu na kikakifunika. Basi kila kilicho
zunguka sayari na nyota na mkusanyiko wa jua katika sehemu hii inayo onekana
ya ulimwengu kimetanda kupita inavyo kadirika na akili, wala haiwezi kupimika.
Kwani masafa yao hukisiwa kwa mamilioni ya miaka ya mwangaza. Na mwaka
mmoja wa mwangaza kwa ilivyo thibiti kwa ilimu za kisasa katika karne hii
ya ishirini ni masafa yanayo kwenda mwangaza kwa mbio za kilomita 300,000
kwa nukta moja ya dakika. Na ibara ya Aya tukufu (Na hakika Sisi
ndio twenye kuutanua) inaashiria hayo, yaani kutanda huko kwa ulimwengu
kunako staajabisha tangu kuumbwa kwake.
Kama vile vile kuwa kukunjuka huko kungali kunaendelea, na hayo
sayansi ya sasa imethibitisha vile vile. Na imejuulikana kwa nadhariya
ya kutanda ambayo katika mwanzo mwanzo wa karne hii imethibiti kuwa ni
kweli kiilimu, na ufupi wake ni kuwa ulimwengu unaendelea kukua na kupanuka,
na kila sayari za mbinguni zinajitenga wenyewe kwa wenyewe.
49. Na kila kitu tumekiumba namna mbili, yaani kwa jozi, ili mpate
kukumbuka muuamini uwezo wetu.
50,51. Basi fanyeni haraka kuendea kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
Wala msimfanye mungu mwengine kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu. Hakika mimi
nimekujieni kwa amri ya Mwenyezi Mungu kukuonyeni kwa uwazi matokeo ya
ushirikina.
52. Hivyo ndivyo ilivyo kuwa hali ya mataifa yote kwa Mitume wao.
Hakuja Mtume kwa watu wa kabla ya kaumu yako ila walimwita: Mchawi au mwendawazimu.
53. Je! Mmeusiana, mmeambizana, nyinyi kwa nyinyi kusema hivyo ndio
maana mnalirejea hilo kwa hilo? Bali hao ni watu walio pindukia mipaka,
ndio wakawafikiana katika kuwashutumu Mitume!
54. Basi wapuuzilie mbali hawa wenye inda! Wewe hulaumiki usipo wajibu
kitu.
55. Wewe dumisha kukumbusha, kwani ukumbusho huwazidisha Waumini
kufumbua macho na kuwa na nguvu za yakini.
56. Wala sikuwaumba majini na watu kwa jambo la kuniletea Mimi manufaa,
bali ili waniabudu, na kuniabudu Mimi ni manufaa kwao.
57. Sitaki kwao riziki, kwani Mimi si mhitaji kwa walimwengu wote;
wala sitaki wanilishe, kwani Mimi ndiye ninaye lisha, wala silishwi.
58. Hakika Mwenyezi Mungu peke yake, ndiye mdhamini wa kuwapa riziki
waja wake, na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Aliye imara, hashindiki.
59. Hakika hao walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na kukanusha
wana fungu lao la adhabu mfano wa fungu la wenzao katika kaumu zilizo kwisha
pita. Basi wasifanye haraka kuhimiza adhabu ishuke kabla ya wakati wake.
60. Basi maangamio yatawapata wenye kuikataa siku yao waliyo ahidiwa, kwa sababu ya shida na vitisho viliomo katika siku hiyo.