1,2. Qaaf. Hii ni harufi katika harufi za alifbete iliyo
fungulia Sura hii kama ilivyo ada ya Qur'ani katika kufungulia Sura kadhaa
wa kadhaa kwa harufi kama hii, ili kuwakabili makafiri kama wanaweza kuleta
mfano wake, na pia kuwazindua watu wasikilize yanayo somwa. Ninaapa kwa
Qur'ani yenye ubora, na utukufu, na hishima kwamba hakika Sisi tumekutuma
wewe, ewe Muhammad, ili uwaonye watu kwa hii. Na watu wa Makka hawakuamini,
bali walistaajabu kutokea Mtume miongoni mwa jinsi yao akiwaonya kuwa watafufuliwa.
Makafiri wakasema: Jambo hili hatulijui, na la ajabu!
3. Ati baada ya kwisha kufa na tukawa udongo, tutafufuliwa tena?
Huko kufufuliwa baada ya kufa ni marejeo yaliyo mbali, hayawi.
4. Sisi hakika tunajua vipi ardhi inavyo vimeza viwiliwili vyao baada
ya kufa. Na Sisi tunacho Kitabu kinacho dhibiti na kuhifadhi kila kitu
hata kidogo.
5. Wao hawayazingatii aliyo kuja nayo Mtume, bali walimkadhibisha
mara tu bila ya kuzingatia na kufikiri. Basi wao wamo katika hali ya kubabaika,
hawana utulivu.
6. Wameghafilika hata hawaitazami mbingu ilivyo nyanyuliwa juu yao
bila ya nguzo? Vipi tumetengeneza ujenzi wake, na tukaipamba kwa nyota,
na haina nyufa za kuitia kombo!
Mbingu ni kote kulio juu yetu, na ndani yake vimo vitu vya namna
mbali mbali, vinaogelea katika njia zao, nyota na sayari. Na hayo
ni kwa nidhamu ya uangalizi mkubwa, na mshikamano ulio timia, na vilevile
zinafuata kwa mpango wake kuwafikiana na kanuni za mvutano, basi hazitelezi.
7. Na ardhi tumeikunjua na tukaisimamisha milima iliyo kaa imara
na kuthibiti kwenda chini. Na tukaijaalia kumea kila namna ya mimea mizuri
ya kuwafurahisha watazamao.
Gamba lilio funika ardhi katika mwahali maalumu limetuna, ndio hiyo
milima. Na pengine limedidimia ndio sakafu ya chini ya bahari. Na uzani
wa vitu hivi vizito vinalingana wenyewe kwa wenyewe. Na ni katika uwezo
wa Mwenyezi Mungu na hikima yake kupatikana kulingana huku kwa uzani, na
ukawa umethibiti kwa kupenya madda za ardhi zilizo fanyika hilo gamba jembamba
chini ya mat'abaka ya juu juu. Na hayo ni kutoka kuliko kuwa kuzito kwendea
kuliko kwepesi.
8. Tumejaalia hayo aone na akumbuke kila mja mwenye kurejea kwa Mola
wake Mlezi, akafikiri Ishara za uwezo wake.
9. Na kutoka mbinguni tukateremsha maji yenye kheri nyingi na baraka,
na kwa hayo tukaotesha mabustani yenye miti, na mauwa, na matunda, na tukatoa
kwa hayo nafaka za makulima ya kuvunwa.
10. Na mitende mirefu mirefu, yenye makole ya tende yaliyo pandana
kwa wingi.
11. Tumeotesha hiyo ili iwe ni riziki kwa waja wetu, na tukaihuisha
kwa maji ardhi iliyo kauka mimea yake. Hali kadhaalika ndivyo kufufuliwa
wafu kutoka makaburini.
12,13,14. Kabla ya hawa, kaumu nyingi ziliwakadhibisha Mitume-
kaumu ya Nuhu, na kaumu nyengine iliyo kuwa ikiitwa "Watu wa
Rassi", na wa Thamudi, na wa A'di, na wa Firauni, na kaumu Lut'i, na kaumu
iliyo kuwa maarufu kwa jina la "Watu wa Machakani", na kaumu ya Tubbaa'
- wote hao waliwakadhibisha Mitume wao. Kwa hivyo wakastahiki maangamizo
niliyo waahidi.
15. Kwani kutaka kwetu kulipungua, au uwezo wetu ulitetereka, hata
tukashindwa kwa kule kuumba kwa mara ya kwanza, tusiweze tena kuwarejeza?
Hasha! Hatukushindwa, nao wanatambua hayo. Bali wao wana shaka tu na wanadanganyikiwa
na huku kuumbwa kupya baada ya kufa.
16. Ninaapa: Bila ya shaka tumemuumba mtu, na Sisi tunajua hata anayo
semezwa na nafsi yake. Na Sisi kwa kuzijua hali zake zote, ni karibu kuliko
mshipa wake wa damu ulioko shingoni mwake. Na hicho ndicho kitu kilicho
karibu mno naye.
17. Watakapo kutana Malaika wawili walinzi, mmoja anakaa kuliani,
na mwingine anakaa upande wa kushoto, wakiviandika vitendo vyake.
18. Halimtoki neno ila yuko karibu naye Malaika tayari kuandika
neno lake.
19. Na yatapo kuja machungu ya kukata roho, kwa haki isiyo
na shaka ndani yake, hilo ni jambo la kweli ulilo kuwa ukilikimbia.
20. Na baragumu litapulizwa kwa mpulizo wa kuwafufua watu. Kupulizwa
huko kutakuwa siku hiyo ya kuteremka adhabu waliyo ahidiwa.
21. Na kila nafsi njema na mbaya, itakuja na pamoja nayo wa kuichunga
kuipeleka kwenye mkusanyo, na wenye kuwatolea ushahidi wa vitendo vyao
22. Wataambiwa, kumtisha huyo mwenye kukadhibisha: Hakika wewe huko
duniani ulikuwa umeghafilika kabisa na haya unayo sononeka nayo hivi sasa.
Basi Sisi tumekuondolea pazia lilio kuwa likikuzuia usiyaone mambo ya Akhera.
Basi jicho lako hii leo linaona kwa nguvu.
23. Na Shetani wake aliye kuwa mwongozi wake duniani, atasema: Kafiri
huyu alioko kwangu yuko tayari kuingia Jahannamu kwa kupotezwa nami.
24,25. Malaika wawili wataambiwa: Watieni katika Jahannamu kila aliye
pita mipaka kwa ukafiri, na aliye pita mipaka kwa inadi, na akaacha kuifuata
Haki, na akapita mipaka kuzuia kheri, mwenye kudhulumu akaipindukia Haki,
mwenye kumtilia shaka Mwenyezi Mungu Mtukufu na aliyo yateremsha.
26. Aliye mfanya mungu mwengine wa kumuabudu pamoja na Mwenyezi Mungu.
Basi mtupeni huyo katika adhabu yenye mwisho wa ukali.
27. Shetani atasema kumrudi yule kafiri: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi
siye niliye mfanya awe mwenye kua'si, lakini yeye mwenyewe alikuwa katika
upotovu wa mbali na haki. Na mimi nilimsaidia tu kwa kumpotoa.
28. Mwenyezi Mungu Mtukufu atawaambia makafiri na wenzi wao: Msigombane
mbele yangu hapa pahala pa hisabu na malipo. Na Mimi nilikuleteeni mbele
duniani onyo juu ya kukufuru kwenu kuukataa Ujumbe wangu niliyo utuma kwenu.
Nanyi hamkuamini.
29. Hapana la kugeuza kauli ilioko kwangu na onyo langu kuwatia makafiri
Motoni, wala Mimi si Mwenye kuwadhulumu waja. Kwani simuadhibu mja yeyote
bila ya makosa.
30. Siku tutapo iambia Jahannamu kwa kuwatia kiwewe makafiri: Je!
Umejaa? Nayo Jahannamu iseme kwa kuwaghadhibikia: Wapo wengine zaidi wa
kuwaongeza katika hawa wenye kudhulumu?
31. Na Pepo iliyo pambwa italetwa karibu kwa ajili ya wenye kumcha
Mola wao Mlezi, kwa kufuata amri zake na kuyaepuka makatazo yake, iletwe
pahala pasipo kuwa mbali nao.
32. Haya ndiyo malipo ya kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu,
aliye mwingi wa kuhifadhi sharia zake.
33. Mwenye kukhofu adhabu ya Mwenyezi Mungu ambaye rehema yake imeenea
juu ya kila kitu, na Yeye haonekani, na akaja Akhera na moyo wa aliye kwisha
rejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
34. Itasemwa kwa hishima yao: Ingieni Peponi kwa amani. Hiyo siku
mtakapo ingia Peponi ndiyo siku ya kubakia milele isiyo na mwisho.
35. Hao wachamngu watapata kila wakitakacho huko Peponi. Na Sisi
tunazo neema za kuzidi kuliko yanayo mpitikia mtu kuyawaza.
36. Na wengi tumekwisha wateketeza kabla ya hawa wanao kadhibisha
katika mataifa yaliyo kwisha pita. Wao walikuwa na nguvu na madaraka zaidi
kuliko hawa. Wakaizunguka miji wakishughulika kuchungua na kutafuta. Je!
Walipata pa kukimbilia wasiangamizwe?
37. Hakika kwa waliyo tendewa hao wa kaumu zilizo kwisha pita ni
mawaidha kwa mwenye moyo wa kufahamu hakika ya mambo, au akasikiliza uwongofu
naye akili zake anazo.
38. Ninaapa: Hakika tumeziumba mbingu na ardhi na viumbe viliomo
baina yao katika siku sita. Na hatukupata kuchoka.
Rejea mambo yaliyo khusu maana ya neno "Siku" za uumbaji katika
maelezo ya kitaalamu juu ya Aya za idadi 9 mpaka 12 katika Sura ya "Fuss'ilat".
41:9-12
39,40. Ikiwa haya yamebainika, basi, ewe Mtume, yastahamilie hayo
wayasemayo hao wanao kanusha, ya uwongo na uzushi kukhusu Utume wako. Nawe
mtakasishe, Msabbih, Muumba wako na Mlezi wako na kila upungufu,
ukimhimidi wakati wa alfajiri, na wakati wa alasiri, kwani ibada nyakati
hizo ni jambo kuu. Na pia mtakasishe, Msabbih, katika saa za usiku, na
baada ya Sala.
41,42. Na sikiliza khabari ninazo kwambia katika hadithi za Kiyama
kwani shani yake ni kubwa. Siku atapo nadi Malaika wa kunadi kutoka pahala
pa karibu na hao wanao itwa. Siku watapo sikia mpulizo wa pili wa Haki,
nao ni wa kufufuliwa watu. Hiyo ndiyo siku ya kutoka kwenye makaburi.
43. Hakika Sisi, peke yetu, ndio tunao huisha viumbe vyote, na tunavifisha
duniani. Na kwetu Sisi, peke yetu, ndio marejeo Akhera.
44. Siku itakapo wapasukilia ardhi, na watoke humo mbio mbio wakikimbilia
mkutanoni...Hilo jambo kuu la kuwakusanya wote ni dogo na jepesi kwetu.
45. Sisi tunajua kuliko yeyote hayo wayasemayo ya uwongo juu yaliyo khusu Utume wako. Wala wewe hukutumwa uwalazimishe kwa unayo yataka. Ila wewe ni mwonyaji basi mkumbushe kwa Qur'ani Muumini mwenye kuiogopa adhabu yangu ili ukumbusho umfae..