1. Enyi mlio amini! Msitangulie na kulikata jambo
lolote la kidini na la kidunia bila ya kukuamrisheni Mwenyezi Mungu na
Mtume wake. Na jiwekeeni kinga ya nafsi zenu isikupateni adhabu ya Mwenyezi
Mungu kwa kufuata sharia yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia
baraabara yote mnayo yasema, ni Mwenye kuyajua vilivyo mambo yote.
2. Enyi mlio amini! Msinyanyue sauti zenu juu ya sauti ya Nabii anapo
sema na nyinyi mnasema. Wala msipambanishe sauti zenu na sauti yake, kama
mnapo semezana nyinyi kwa nyinyi, kwa kuchelea visiharibike vitendo vyenu
bila ya nyinyi wenyewe kutambua.
3. Hakika wanao teremsha sauti zao katika baraza ya Mtume wa Mwenyezi
Mungu kwa kumtukuza yeye, hao peke yao ndio Mwenyezi Mungu amezisafisha
nyoyo zao kwa uchamngu. Kwa wengineo si hivyo. Nao watapata msamaha mkubwa
kufutiwa madhambi yao, na thawabu zilizo fika ukomo wa kufika kwake.
4. Hakika hao wanao kuita kwa makelele nawe uko vyumbani mwako wengi
wao hawafahamu yanayo takikakana kukuhishimu na kukutukuza kwa makamo yako.
5. Na lau kuwa hao wangeli ngojea, kwa kukufanyia adabu, mpaka ukatoka,
bila ya shaka ingeli kuwa ni bora zaidi katika Dini yao. Na Mwenyezi Mungu
ni Mkubwa wa kusamehe, Mwenye rehema kunjufu.
6. Enyi mlio amini! Akikujieni mtu ambaye yuko nje ya sharia ya Mwenyezi
Mungu akakupeni khabari yoyote, basi chungueni mjue ukweli wake, kwa kuchelea
msije mkawaletea watu madhara, kwa kutojua hali yao. Hapo tena baada ya
kwisha dhihiri kuwa hawana makosa mkaingia katika majuto ya daima, mkatamani
yasingeli kuwa.
7,8. Na jueni, enyi Waumini, kwamba Mtume yuko nanyi. Basi
mkadirieni kama anavyo stahiki kadiri yake, na msadikini. Lau yeye angeli
wafuata walio wachache wa Imani kati yenu katika mambo mengi, basi hapana
shaka mngeli ingia katika mashaka na hilaki. Lakini Mwenyezi Mungu amewapendezesha
Imani wale walio kamilika katika nyinyi, na akaipamba katika nyoyo zenu.
Basi jilindeni na kujipamba na yasiyo takikana. Na amekufanyeni mchukie
kukufuru neema za Mwenyezi Mungu, na kutokana na sharia zake, na kwenda
kinyume na amri zake. Hao tu, peke yao, ndio wanao ijua njia ya uwongofu
na wameishikilia. Na hiyo ni fadhila tukufu na neema kubwa ya Mwenyezi
Mungu juu yao. Na Mwenyezi Mungu amekizunguka kila kitu kwa ujuzi wake,
ni Mwenye hikima ya kupita mpaka katika kuendesha kila jambo.
9. Na ikiwa makundi mawili ya Waumini yanapigana, basi enyi Waumini,
yapatanisheni. Ikiwa moja ndilo linalishambulia la pili, na likakataa kupatanishwa,
basi lipigeni hilo linalo shambulia, mpaka lirejee kwenye hukumu ya Mwenyezi
Mungu. Likirejea basi wapatanisheni kwa insafu. Na fanyeni uadilifu baina
ya watu wote katika kila jambo. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wenye kufanya
uadilifu.
10. Hakika wote wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni ndugu,
Imani imezifanya nyoyo zao pamoja. Basi patanisheni baina ya ndugu zenu
kwa kufuata udugu wa Imani. Na jiwekeeni nafsi zenu kinga cha kukinga adhabu
ya Mwenyezi Mungu, kwa kufuata amri yake, na kuepuka anayo yakataza, na
huku mkitaraji Mwenyezi Mungu akurehemuni kwa uchamngu wenu.
11. Enyi mlio amini! Wanaume katika nyinyi wasiwadharau wanaume wenginewe,
huenda hao mbele ya Mwenyezi Mungu wakawa bora kuliko wao. Wala wanawake
Waumini wasiwadharau wanawake wenzao, huenda pengine wakawa hao ni bora
kwa Mwenyezi Mungu kuliko wao. Wala msifanye kuaibishana nyinyi kwa nyinyi,
wala mtu asimwite mwenzie kwa jina la kumuudhi. Ni uovu mno kwa Waumini
kutajwa kwa upotovu baada ya kwisha sifika kwa Imani. Na wasio rudi wakaacha
waliyo katazwa, basi hao peke yao ndio walio jidhulumu nafsi zao na wakawadhulumu
wengineo.
12. Enyi mlio amini, jitengeni mbali na wingi wa kudhania dhana mbovu
kwa watu wa kheri. Kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi zinazo stahiki
adhabu. Wala msiwe mkitafuta aibu za Waislamu. Wala msisengenyane, yaani
kumsema mtu nyuma yake kwa jambo linalo muudhi. Hebu yupo yeyote
kati yenu anaye penda kula nyama ya nduguye aliye kufa? Bila ya shaka
hayo yanakuchukizeni! Basi ichukieni pia tabia ya kusengenyana
na kusemana, kwani haya nayo ni mfano wa hayo. Na zikingeni nafsi zenu
na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri zake, na kuyaepuka ayakatazayo.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkubwa wa kukubali toba ya wenye kutubia, Mwenye
rehema kunjufu kwa walimwengu wote.
13. Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni nyinyi sawa sawa kutokana
na asli moja, ya Adamu na Hawa. Na tukakufanyeni mkawa wengi kwa mataifa
makubwa na makabila mengi, ili kutimie kujuana na kuawiniana baina yenu,
sio kubaguana. Na hakika mwenye cheo cha juu miongoni mwenu kwa Mwenyezi
Mungu duniani na Akhera ni yule anaye mcha Yeye zaidi. Hakika Mwenyezi
Mungu amevizunguka vitu vyote kwa kuvijua, ni Mwenye khabari za dogo na
kubwa la kila jambo.
14. Wakaazi wa majangwani wamesema kwa ndimi zao: Tumeamini. Ewe
Muhammad! Waambie: Bado hamjaamini; kwa sababu nyoyo zenu bado hazijasadiki
hayo mnayo yatamka. Lakini nyinyi semeni: Tumefuata dhaahiri ya Ujumbe
wako. Bado Imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimt'ii Mwenyezi Mungu
na Mtume wake kwa kweli, hato kunyimeni hata chembe katika malipo ya vitendo
vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkubwa wa kuwasamehe waja wake, ni Mwenye
rehema kunjufu kwa kila kitu.
15. Hakika Waumini wa kweli ni wale ambao wanamuamini Mwenyezi Mungu
na Mtume wake, kisha hapana shaka yoyote inayo ingia katika nyoyo zao kwa
hayo wanayo yaamini; tena wakapigana Jihadi kwa kutoa mali yao na roho
zao katika njia ya ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. Hao peke yao ndio walio wakweli
katika Imani yao.
16. Ewe Muhammad! Waambie kwa kuwakanusha ile kauli yao kuwa wameamini:
Ndio hivyo ati mnampa khabari Mwenyezi Mungu kuwa nyoyo zenu zimesadiki?
Na Mwenyezi Mungu peke yake anajua kila kiliomo katika mbingu na katika
ardhi. Na Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.
17. Wanaona kuwa kusilimu kwao ni kukuunga mkono wewe, Muhammad,
na hivyo inastahiki wewe uwashukuru. Sema: Msinisimbulie kusilimu kwenu;
kwani kheri yake mnaipata nyinyi. Bali ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye
aliye kufanyieni ihsani kwa kukuongoeni kwenye Imani, ikiwa nyinyi ni wakweli
katika hayo madai yenu.
18. Hakika Mwenyezi Mungu anajua kila lilio fichikana katika mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuona vyema yote myatendayo.