1,2,3. Hakika Sisi tumekupa, ewe Muhammad, FAT-H'I,
Ushindi mkubwa unao onekana wazi kwa Haki kuishinda baat'ili, kweli kuushinda
uwongo, ili Mwenyezi Mungu akughufirie yaliyo tangulia katika yanayo hisabika
kwa mwenye cheo kama chako kuwa ni dhambi, na pia yanayo kuja baada yake.
Na ili atimize neema zake juu yako kwa kuenea wito wako, na akuthibitishe
kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu Iliyo Nyooka. Na Mwenyezi Mungu akunusuru
na maadui wa Utume wako kwa nusura yenye nguvu za kushinda
4. Yeye ndiye aliye teremsha utulivu katika nyoyo za Waumini ili
wazidi kuwa na yakini juu ya yakini yao. Na ni Mwenyezi Mungu peke yake
ndiye mwenye majeshi ya katika mbingu na ardhi. Huendesha mambo yake apendavyo.
Na Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake. Ana hikima isiyo
na ukomo katika kuendesha kila kitu.
5,6. Ili Mwenyezi Mungu awaingize Waumini wanaume na Waumini wanawake
katika Mabustani, yaani Pepo, zipitiwazo na mito ndani yake, wadumu humo
daima dawamu, na awafutie makosa yao. Na malipo hayo kwa Mwenyezi Mungu
ndio kufuzu kulio fika ukomo kwa utukufu wake. Na ili awatie adhabu wanaafiki
wanaume na wanaafiki wanawake, na wanaume wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu
na wengineo, na washirikina wa kike, wanao mdhania Mwenyezi Mungu dhana
mbovu, ya kuwa ati hatamnusuru Mtume wake. Ni juu yao peke yao ndio yatawaangukia
mageuko maovu, wala hawawezi kuyakimbia. Mwenyezi Mungu amewaghadhibikia,
na amewafukuza kwenye rehema yake, na amewatengenezea Jahannamu kwa ajili
ya kuwaadhibu, na huo ndio mwisho mbaya.
7. Na Mwenyezi Mungu anayo majeshi ya mbinguni na katika ardhi. Anaendesha
mambo yake kwa hikima yake kama atakavyo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda
kila kitu, Mwenye hikima isiyo na mwisho katika kupanga kila kitu.
8. Ewe Muhammad! Hakika Sisi tumekutuma uwe Shahidi juu ya umma wako
na pia juu ya kaumu zilizo tangulia, na uwe Mbashiri kuwapa khabari njema
wachamngu kuwa watapata malipo mema, na uwe Mwonyaji kwa watendao maasi
kuwa watapata adhabu mbaya.
9. Ili nyinyi, mlio tumiwa Mtume, mpate kumuamini Mwenyezi
Mungu na Mtume wake, na mumnusuru Mwenyezi Mungu kwa kuinusuru Dini yake,
na mumtukuze kwa taadhima na utukufu, na mumtakase na kila lisilo muelekea,
asubuhi na jioni.
10. Hakika wanao kuahidi kuwa watafanya kama wawezalo kukunusuru,
kwa hakika wanamuahidi Mwenyezi Mungu. Nguvu za Mwenyezi Mungu ziko pamoja
nawe juu ya nguvu zao. Basi atakaye vunja ahadi yake baada ya kwisha itoa,
basi madhara yake hayatarudia ila juu ya nafsi yake. Na mwenye kutimiza
ahadi aliyo muahidi Mwenyezi Mungu, kwa kutimiza kufungamana nawe, Mwenyezi
Mungu atamlipa thawabu za hadi ya mwisho wa ukubwa.
11. Watakwambia hao walio wekwa nyuma na unaafiki wao katika wakaazi
wa majangwani, utapo rejea kutoka safarini: Yametushughulisha mali yetu
na ahali zetu hata hatukuweza kutoka nawe. Basi tuombee maghfira. Wanasema
hayo kwa ndimi zao yasiyo kuwamo katika nyoyo zao. Sema kuwajibu: Nani
anaye weza kukufanyieni chochote kukulindeni na hukumu ya Mwenyezi Mungu,
pindi akitaka kukudhuruni, au akitaka kukufaeni? Bali Mwenyezi Mungu amevizunguka
vyote mtendavyo kwa ujuzi wake.
12. Bali nyinyi mlidhani kwamba Mtume na Waumini hawatarejea kabisa
kwa watu wao baada ya vita vyao. Ndio maana mkabaki nyuma, na mkadanganyika
na hiyo dhana katika nyoyo zenu. Na mkadhania dhana mbovu katika mambo
yenu yote. Na Mwenyezi Mungu alikwisha jua kuwa nyinyi ni watu walio angamia,
wenye kustahiki ghadhabu zake.
13. Na asiye muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi Sisi tumewatengenezea
makafiri Moto unao waka kwa nguvu.
14. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye ufalme wa mbinguni na
katika ardhi, anaupanga kwa mpango wa Mwenye uweza, Mwenye hikima. Humsamehe
madhambi amtakaye, na humuadhibu kwa hikima yake amtakaye. Na Mwenyezi
Mungu ni Mkuu wa kusamehe, Mkunjufu wa rehema.
15. Watasema hawa wakaazi wa majangwani walio wekwa nyuma na unaafiki
wasitoke nawe: Mkenda kuchukua ngawira, aliyo kuahidini Mwenyezi Mungu
kuzichukua, twacheni tukufuateni. Hao wanataka kuigeuza ile ahadi ya Mwenyezi
Mungu juu ya ngawira hizo aliyo wapa walio toka na Mtume kwenda Hudaibiya.
Ewe Muhammad! Waambie: Hamtatufuata. Hukumu kama hiyo ya kuzuia kufuata
Mwenyezi Mungu aliihukumia kabla ya hapo kwa mintarafu ya ngawira kwa walio
toka kwenda vitani pamoja na Mtume wake. Wao watasema: Mwenyezi Mungu hakukuamrisheni
hayo, bali nyinyi mnatuhusudu tu, hamtaki tushirikiane nanyi. Bali watu
hawa, kwa haya wayasemayo, hawafahamu sharia za Mwenyezi Mungu ila
kwa fahamu chache.
16. Waambie walio baki nyuma wasitoke katika watu wa majangwani:
Mtakuja takiwa kwenda pigana na watu wa kali wa vita. Ikiwa mtaitikia wito
huo basi hapo Mwenyezi Mungu atakupeni ngawira nyingi katika dunia, na
thawabu katika Akhera. Na mkikataa kama mlivyo kwisha kataa kabla, basi
Mwenyezi Mungu atakuadhibuni kwa adhabu ya mwisho wa uchungu.
17. Kipofu hapati dhambi kuacha kwenda pigana na makafiri, wala kiguru
hapati dhambi, wala mgonjwa hapati dhambi kadhaalika. Kwani hao hawajiwezi.
Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika kila anacho amrisha
na kukataza, atamtia katika Mabustani ya Peponi yenye wasaa, yapitayo mito
kati yake. Na mwenye kuacha kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi
Yeye atamuadhibu adhabu iliyo chungu hadi.
18,19. Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waumini walipo kuahidi kwa kujitolea
chini ya mti. Yeye alijua yaliomo katika nyoyo zao, ya ikhlasi na kuutimiliza
Ujumbe wako. Basi akawateremshia utulivu, na kwa ajili ya ukweli wao katika
kukuunga mkono na kutimiza sulhu aliwapa nguvu hapo hapo, na ngawira nyingi
alizo waahidi kuwa watazipata. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda kila
kitu, Mwenye hikima ya mwisho katika kila analo lihukumia.
20,21. Mwenyezi Mungu amekuahidini ngawira nyingi mtakazo chukua
katika wakati ulio kadiriwa kwa hayo. Basi akakuleteeni haraka haraka.
Na hayo ndiyo hizo ngawira alizo kuahidini. Na akakukingeni na madhara
ya watu juu yenu. Na ili hayo yawe ni Ishara kwa Waumini juu ya ukweli
wa ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao, na akuongozeni kwenye Njia Iliyo Nyooka,
kwa kumt'ii Yeye na kumfuata Mtume wake. Na ngawira nyengine ambazo mlikuwa
hamjazipata Mwenyezi Mungu amekupeni ushindi wa kuzipata. Na Mwenyezi Mungu
ana uwezo ulio timia juu ya kila kitu.
22. Na lau makafiri wa Makka wangeli pigana nanyi, na wasifanye ile
sulhu nanyi, basi wangeli toka mbio kwa kushindwa, kwa kukuogopeni, na
tena hapo wasinge pata mlinzi wowote wa kuwatawalia mambo yao, wala mtu
wa kuwanusuru.
23. Mwenyezi Mungu ameendesha mambo yake kwa mwendo kama alio uendesha
zamani kwa viumbe vyake - navyo ni kuwa khatima njema ni ya Mitume wake
na Waumini. Wala hutakuta mabadiliko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu.
24. Na huyo ni Mwenyezi Mungu pekee, ndiye aliye izuia mikono ya
makafiri isikudhuruni katika vita vyao kati ya Makka. Na baada yake akakupeni
uwezo wa kuwashinda. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote myatendayo.
25,26. Watu wa Makka ndio walio kufuru na wakakuzuilieni msiingie
katika Msikiti Mtakatifu, na wakawazuilia dhabihu wanyama wa kutoa mhanga
mlio wachunga na kuwafunga kwa ajili ya kutoa dhahiya, wasifike pahala
pao pa kuchinjiwa. Na lau kuwa si ubaya wa kuwasibu Waumini wanaume na
wanawake kati ya makafiri wa Makka, ambao hamwajui, mkawauwa bila ya kuwajua,
na mkapata a'ri na hizaya kwa ajili ya kuwauwa, basi tungeli kusalitisheni
nao mkapambana nao. Na kuzuiliwa huko ni kwa ajili ya kuwa Mwenyezi Mungu
apate kuwaingiza katika ulinzi wake Waumini walio baina yao, na walio silimu
miongoni mwa makafiri. Lau kuwa wanatambulikana Waumini basi tungeli waadhibu
walio shikilia ukafiri kati yao adhabu ya ukomo wa uchungu, pale wale walio
kufuru walipo fanya katika nyoyo zao dharau za kijahiliya basi Mwenyezi
Mungu akateremsha utulivu juu ya Mtume wake na juu ya Waumini, na akawalazimisha
neno la kujikinga na ushirikina na adhabu. Na wao walikuwa ni wenye kustahiki
na kuelekea hayo, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
27. Ameitimiza Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake ile ndoto
ya Mtume kwa kuingia Msikiti Mtakatifu kwa hakika. Ninaapa: Hapana shaka
mtaingia katika Msikiti Mtakatifu, Mwenyezi Mungu akipenda, nanyi mmesalimika
na maadui zenu, na huku ni wenye kunyoa na kupunguza nywele zenu, na bila
ya khofu. Mwenyezi Mungu Subhanahu anaijua kheri msiyo ijua kwa kukuchelewesheni
kuingia Msikiti Mtakatifu. Basi amekujaalieni kabla ya kuingia kwenu mpate
Ushindi karibuni.
28. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu aliye mtuma Mtume wake na uwongozi
ulio wazi, na Dini ya Kiislamu, ili itukuke juu ya dini zote. Na Mwenyezi
Mungu anatosha kuwa ni Shahidi wa hayo.
29. Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Masahaba wake walio pamoja
naye, ni wakali na wenye nguvu kwa makafiri, na wanarehemeana na kuoneana
huruma wenyewe kwa wenyewe. Unawaona wakirukuu na kusujudu sana, wakiomba
kwa hivyo thawabu kubwa kwa Mwenyezi Mungu, na radhi za kuenea. Alama yao
ni unyenyekevu wao katika nyuso zao kutokana na kuathirika kwa Sala nyingi.
Hiyo ndiyo sifa yao kubwa katika Taurati. Na sifa yao katika Injili ni
kama mmea ulio chipua ukapata nguvu, ukageuka kutokana na udhaifu ukawa
mgumu, ukasimama sawa sawa kwenye shina lake. Ukawafurahisha wakulima kwa
nguvu zake. Basi Waumini ni hali kadhaalika, ili Mwenyezi Mungu awakasirishe
makafiri kwa nguvu zao. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio amini na wakatenda
mema katika wao maghfira ya kuwafutia madhambi yao yote, na thawabu kubwa
mno. (Katika Injili ya Marko 4.26-28 imeandikwa: "Ufalme wa Mungu, mfano
wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka
usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi
huzaa wenyewe; kwanza jani, tena suke, tena ngano pevu katika suke." Katika
Hesabu 16.22 ambacho ni sehemu ya Taurati kwa mujibu wa Biblia imeandikwa
kuwa Musa na Haruni walisali kwa kusujudu. Humo inasemwa: "Nao wakapomoka
kifudifudi, wakasema, Ee Mungu..." Na katika Injili ya Mathayo 26.39 inatajwa
pia kuwa Yesu pia alisali kwa kusujudu: "Akaendelea mbele kidogo, akaanguka
kifulifuli, akaomba.." Hivyo ndivyo wasalivyo Waislamu.)