1. Walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakawazuilia
watu wasiingie katika Uislamu, Mwenyezi Mungu amevivunja vyote walivyo
vitenda.
2. Na walio amini, na wakatenda mema, na wakasadiki yaliyo teremshwa
kwa Muhammad, nayo ni Haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi, atawafutia makosa
yao, na atawatengenezea hali yao ya Dini na dunia.
3. Hayo ni kwa sababu walio kufuru wamefuata njia ya upotovu, na
kwamba walio amini wamefuata njia ya Haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi.
Kwa mfano kama huu wa kubainisha kwa uwazi ndio Mwenyezi Mungu anawaeleza
watu hali zao ili wapate kuzingatia.
4,5,6. Mtapo kutana na walio kufuru katika vita basi wapigeni kwenye
shingo zao, mpaka mtakapo wadhoofisha kwa wingi wa kuwauwa, basi tena wafungeni
mateka. Tena ama waachilieni wende zao kwa wema na ihsani, baada ya kwisha
vita, kwa kuwaachia bila ya fidia, au kwa fidia ya kutoa mali au kubadilishana
kwa mateka wa Kiislamu. Inakuwa mmewaachilia kwa badali. Huu ndio uwe mwendo
wenu na makafiri mpaka vita vimalizike kabisa. Mwenyezi Mungu anawahukumieni
hivyo. Na lau angeli taka bila ya shaka angeli washinda bila ya vita, lakini
haya ni ili awajaribu Waumini kwa makafiri kama mtihani ndio ameamrisha
Jihadi. Na walio uwawa katika njia ya Mwenyezi Mungu kabisa hatoacha vitendo
vyao vipotee. (1) Atawahidi, na azitengeneze nyoyo zao, na awatie
katika Pepo aliyo kwisha wajuulisha.
(1) Katika Aya hii tukufu zimetajwa "shingo" khasa, kwa sababu kuzipiga
hizo ndio njia inayo faa mno kummaliza upesi mwenye kupigwa bila ya kumuadhibu
na kumtesa. Kwani imethibiti kwa ilimu kuwa shingo ndiyo kiungo baina ya
kichwa na kiwiliwili kizima. Basi ukikatika mshipa wa uti wa mgongo wenye
kupeleka hisiya zote, basi viungo vyote muhimu vinapooza. Na ikikatika
mishipa ya damu, damu inasita kufika kwenye ubongo. Na zikikatika njia
za kupitisha hewa, basi pumzi husita. Na katika hali hizi zote uhai unakatika
mara moja.
7. Enyi mlio amini! Mkiinusuru Dini ya Mwenyezi Mungu, na Yeye atakunusuruni
muwashinde maadui zenu, na ayatilie nguvu mambo yenu.
8. Na walio kufuru Mwenyezi Mungu atawatia mashakani, na atawapotoa
vitendo vyao.
9. Mambo yao ni hivyo kwa sababu wao wanakereka na aliyo teremsha
Mwenyezi Mungu, yaani Qur'ani na amri zake. Basi Mwenyezi Mungu amevibat'ilisha
vitendo vyao.
10. Wameshindwa kutafuta ya kuwazindua, hata hawakutembea katika
ardhi wakaangalia hali gani ulikuwa mwisho wa walio wakadhibisha Mitume
kabla yao? Mwenyezi Mungu aliwateremshia hilaki katika kila kilicho khusiana
nao, nafsi zao, mali yao, na watoto wao. Na wenye kumkataa Mwenyezi Mungu
na Mitume wake ndio hupata mwisho mfano wa huo.
11. Malipo hayo ndio ushindi wa Waumini na kushindwa nguvu makafiri,
ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ni rafiki mlinzi wa walio amini na
ndiye Mwenye kuwanusuru; na makafiri hawana rafiki mlinzi wa kuwanusuru
wala kuwakinga na kuangamia.
12. Hakika Mwenyezi Mungu atawatia wenye kuamini na wakatenda mema
katika Pepo tukufu zenye kupitiwa ndani yake mito. Na makafiri wanastarehe
duniani kidogo, na wanakula kama walavyo wanyama, wamepigwa na mghafala
wala hawajifikirii mwisho wao. Hawanalo lao ila matamanio yao. Na kesho
Akhera nyumba yao ni Motoni.
13. Na wengi katika watu wa miji walio tangulia walio kuwa na nguvu
zaidi kushinda watu wa mji wako wa Makka ambao watu wake wamekufukuza,
ewe Muhammad, tuliwaangamiza kwa namna mbali mbali za adhabu. Na hakutokea
yeyote wa kuwanusuru nasi.
14. Je! Wanaweza kuwa sawa makundi mawili haya katika malipo? Mwenye
kuwa na ujuzi wazi kumjua Muumba wake na Mlezi wake, naye akawa anamt'ii,
atakuwa sawa na mwenye kuwa na vitendo vyake viovu naye akaviona ni vizuri,
na akafuata hayo ayatendayo na akaeneza pumbao lake la upotovu.
15. Sifa ya Pepo walio ahidiwa wachamngu ni kama hivi: ndani yake
imo mito ya maji yasiyo chafuka, na mito ya maziwa yasiyo haribika utamu
wake, na mito ya mvinyo yenye ladha kwa wanywao, na mito ya asali iliyo
safishwa na takataka zote. Na humo watakuwa na kila namna ya matunda, na
msamaha mkubwa kutokana na Mola wao Mlezi. Je! Sifa za Pepo ya hawa ni
kama sifa itayo kuwa ni malipo ya mwenye kudumu milele Motoni, na akanyweshwa
maji yaliyo tokota ya kukata matumbo?
Aya hii tukufu inataka tuzingatie kuwa maji yaliyo vunda, yaliyo
tuama, yenye kutaghayari, ni maji yenye madhara. Na Aya hii tukufu imesema
hayo kabla ya kuvumbuliwa darubini za kutazamia vijidudu (Microscope) kwa
makarne ya miaka, ndipo ilipo juulikana kuwa maji yaliyo tuama yaliyo taghayari
yanakuwamo ndani yake mamilioni ya vijidudu vyenye madhara ya kuwasibu
watu na wanyama kwa namna mbali mbali ya magonjwa.
16. Na miongoni mwa makafiri kipo kikundi cha watu wanao kusikiliza
wewe, Muhammad. Hawakuamini wewe, wala hawanafiiki na maneno yako. Mpaka
wakisha ondoka kwenye baraza yako husema kwa kejeli kuwaambia walio pewa
ujuzi: Kasema nini huyu Muhammad sasa hivi? Watu hao ndio Mwenyezi Mungu
amepiga muhuri wa ukafiri juu ya nyoyo zao. Ndio wameiacha kheri wakifuata
matamanio yao.
17. Na walio ongoka wakashika njia ya Haki, Mwenyezi Mungu huwazidishia
uwongofu, na akawapa kinga chao cha kujikingia na Moto.
18. Wanao kanusha hawawaidhiki na hali za walio tangulia. Basi je!
Wanangojea Saa (ya Kiyama) iwajie kwa ghafla? Kwa hakika alama zake zimekwisha
dhihiri, na wao hawajazingatia kuwa inakuja. Basi watakumbuka wapi itapo
wajia mara moja kwa ghafla?
19. Basi thibiti juu ya ujuzi ya kwamba hakika hapana wa kuabudiwa
kwa Haki ila Mwenyezi Mungu tu. Na muombe maghfira Mwenyezi Mungu kwa dhambi
yako na madhambi ya Waumini wanaume na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu
anajua kila lenu, la kupita na la kukaa.
20,21,22. Walio amini wanasema: Haiteremki Sura ya kututaka tupigane?
Na ikiteremka Sura ambayo haifasiriki vyenginevyo ila ni kulazimisha tu,
na ikataja ndani yake kuamrishwa vita, utawaona ambao katika nyoyo zao
mna unaafiki wanakuangalia kwa muangalio wa mwenye kuzimia kwa mauti, jinsi
ya kuviogopa na kuvichukia vita. Linalo wastahikia kulifanya ni kumt'ii
Mwenyezi Mungu na kusema neno linalo kubaliana na sharia. Na mambo yakawa
ni kweli, na ikawalazimu kupigana, basi lau kuwa ni kweli wana Imani ya
Mwenyezi Mungu na ut'iifu ingeli kuwa bora kwao kuliko huo unaafiki. Basi
ndio mnavyo tarajiwa, enyi wanaafiki, kuwa mkipata madaraka ndio mfisidi
katika nchi na mkate makhusiano yenu na jamaa zenu?
23. Hao ndio alio watenga mbali kabisa Mwenyezi Mungu na rehema yake,
na akawatia uziwi wasiisikie Haki, na akawatia upofu wa macho wasiione
Njia ya Uwongofu.
24. Wameingia upofu hata hawaufahamu uwongofu wa Qur'ani? Bali kwenye
nyoyo zao zipo kufuli zinawazuia wasiizingatie.
25. Hakika wale walio ritadi, wakarejea nyuma kwenye ukafiri na upotofu
walio kuwa nao baada ya kuwadhihirikia njia ya uwongofu, Shetani ndiye
aliye wapambia, na akawakunjulia matamanio ya uwongo.
26,27. Kurejea huko ukafirini ni kwa kuwa waliwaambia wenye kuchukia
aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu: Tutakut'iini katika baadhi ya mambo. Na
Mwenyezi Mungu anazijua siri za hawa wanaafiki. Hiyo ndiyo hali katika
maisha ya duniani, basi watakuwa katika hali gani Malaika watapo wafisha
huku wakiwapiga nyuso zao na migongo yao kwa kuwadhalilisha?
28. Kufishwa namna hiyo ya kutisha katika hali hiyo ni kwa kuwa hakika
wao waliufuata upotovu ulio mkasirisha Mwenyezi Mungu, na wakaichukia Haki
inayo mpendeza Mwenyezi Mungu. Basi akayabat'ilisha waliyo yatenda.
29. Hivyo wanadhani hawa wenye unaafiki katika nyoyo zao kwamba Mwenyezi
Mungu hatazifichua chuki zao wanazo mchukia Mtume wake na Waumini?
30. Tungeli penda bila ya shaka tungeli kuonyesha hao wanaafiki,
nawe ungeli wajua kwa alama zao, na ungeli wajua kwa namna yao wanavyo
sema. Na Mwenyezi Mungu anajua ukweli wa vitendo vyenu vyote.
31. Na ninaapa: Bila ya shaka tutakujaribuni kama kukufanyieni mtihani,
mpaka tuwajue Mujaahidina, wanao pigana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, katika
nyinyi, na wenye kuvumilia wakati wa shida na dhiki, na tuzijue khabari
zenu za ut'iifu na maasi katika Jihadi na penginepo.
32. Hakika walio kufuru na wakazuia njia ya Mwenyezi Mungu, na wakenda
kinyume na Mtume kwa inda na ukaidi, baada ya kwisha wadhihirikia uwongofu,
hao hawatamdhuru Mwenyezi Mungu kwa lolote. Na Yeye atayabat'ilisha yote
waliyo yatenda.
33. Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu katika aliyo kuamrisheni,
na mt'iini Mtume kwa hayo anayo kuitieni, wala msivipoteze vitendo vyenu.
34. Hakika walio kufuru na wakazuia watu wasiingie katika Uislamu,
kisha wakafa nao ni makafiri, basi Mwenyezi Mungu hatawasamehe.
35. Basi msijifanye wanyonge mbele ya maadui zenu mnapo kutana nao.
Wala msiwatake suluhu kwa kuwaogopa, na hali nyinyi ndio mko juu, na ni
wenye kushinda kwa nguvu za Imani. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi kwa
nusra yake; na wala hatakupunguzieni malipo ya vitendo vyenu.
36,37. Hakika uhai wa dunia ni upotovu na udanganyifu. Na nyinyi
mkiamini na mkaacha maasi, na mkafanya kheri, Mwenyezi Mungu atakupeni
thawabu ya hayo, wala hakutakini mali yenu. Akikutakeni na akakushikilieni
basi nyinyi mtafanya uchoyo, na chuki zenu zitaonekana kwa mnavyo yapenda
mali.
38. Hivi mnaitwa mtumie katika njia ya Mwenyezi Mungu aliyo iamrisha.
Kati yenu wapo wanao fanya ubakhili kutoa. Na mwenye kufanya ubakhili hamdhuru
mtu ila nafsi yake. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye tajiri, hana haja
ya mtu, na nyinyi ndio mafakiri wenye kumhitajia Yeye.
Na mkiacha kumt'ii Mwenyezi Mungu basi atakubadilisheni pahala penu
awalete watu wengine, tena hao hawatakuwa mfano wenu wa kuacha kumt'ii.