1. Imeanzia Sura hii kwa baadhi ya harufi kama ilivyo
ada ya Qur'ani katika Sura kadhaa wa kadhaa.
2. Hii Qur'ani imeteremka kutokana na Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda
kila kitu, Mwenye hikima katika ayatendayo.
3. Hatukuziumba mbingu na ardhi na vyote vilio baina yake ila kufuatana
na sharia zilizo thibiti, kwa makusudio yanayo ambatana na hikima, na kwa
muda maalumu ambao baada yake utakwisha. Na wale wanao ukataa ukweli huu
wanapuuza yale waliyo onywa kwayo, ya kuumbwa kupya siku watakapo fufuliwa
watu kwa ajili ya malipo.
4. Waambie hao wanao muomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu: Hebu nambieni
hali ya hao mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu. Nijuvyeni wameumba nini
katika ardhi, au wana ushirika wowote katika mbingu? Nileteeni Kitabu
kitokacho kwa Mwenyezi Mungu, au mabaki yoyote kutokana na ilimu za watu
wa zamani ambayo mnayategemea kwa madai yenu, ikiwa mnasema kweli.
5. Na nani aliye zidi kupotea kuliko anaye muacha Mwenyezi Mungu
akaiomba miungu mingine ambayo haitamjibu kitu mpaka mwisho wa dunia, na
ambao hao hata hawana khabari ya maombi yao.
6. Na watu wakikusanywa kwa ajili ya hisabu Siku ya Kiyama hawa wanao
abudiwa kwa upotovu watakuwa ndio maadui wa walio kuwa wakiabudu, na watajitenga
nao, na kuwakadhibisha kwa madai yao kwamba wao wanastahiki kuabudiwa.
(Katika Injili ya Mathayo inasimuliwa wazi vipi Nabii Isa a.s. atavyo wakataa
Wakristo wanao muabudu yeye. Tazama Mathayo 7.22-23. Yesu anasema: "Wengi
wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na
kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo
nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao
maovu.")
7. Na washirikina wakisomewa Aya zetu zilizo wazi wao husema,
kwa ule ukafiri wao na inadi yao, bila ya kuzingatia, kuzisema hizo Aya:
Huu ni uchawi dhaahiri!
8. Bali wanasema hawa makafiri: Muhammad ameizua hii na akamsingizia
Mwenyezi Mungu! Sema kuwajibu: Ikiwa mimi nimeizua hii Mwenyezi Mungu atanipatiliza
upesi upesi, wala nyinyi hamwezi kunilinda hata kwa chembe ya adhabu. Yeye
peke yake ndiye Mwenye kujua kabisa hayo mnayo ropokwa katika kuzitia kombo
Aya zake. Na Yeye anatosha kunishuhudia ukweli wangu, na kukushuhudilieni
nyinyi kuwa mnanikadhibisha. Na Yeye pekee, ndiye Mkunjufu wa msamaha kwa
mwenye kutubu, Mkubwa wa rehema, kwa kuwapa muhula wenye kuasi ili wadiriki
kurejea.
9. Waambie: Mimi sikuwa Mtume wa mwanzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu,
hata ndio muukatae ujumbe wangu. Wala mimi sijui Mwenyezi Mungu atanifanya
nini na atakufanyeni nini nyinyi. Mimi sifuati ninayo sema au kutenda ila
anayo nifunulia Mwenyezi Mungu. Wala mimi si chochote ila ni mwonyaji miongoni
mwa waonyaji.
10. Sema: Hebu nambieni, ikiwa hii Qur'ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu
na nyinyi mkaikataa, na hali ameshuhudia shahidi katika Wana wa Israili
kuwa imeshuka mfano wa hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu, akawa yeye kaamini
na nyinyi mkatakabari, basi hapo nyinyi si mtakuwa ni wenye kupotea na
wenye kujidhulumu wenyewe kuliko watu wote? Hakika Mwenyezi Mungu hamsaidii
kuongoka mwenye kujidhulumu mwenyewe na akapanda kiburi kuikataa Haki.
11. Na walio kufuru walisema kuwakhusu walio amini, kwa kejeli na
majivuno juu yao: Ingeli kuwa aliyo kuja nayo Muhammad ni ya kheri, basi
wasingeli tutangulia hawa katika kuyaamini. Kwani sisi ndio twenye ubwana,
na akili bora! Na ilivyo kuwa hawakuyafuata basi wakaangukia kuyatoa kombo,
wakisema: Huu ni uwongo wa zamani unatokana na hadithi za watu wa kale!
12. Na kabla ya Qur'ani Mwenyezi Mungu aliteremsha Taurati kuwa ni
uwongozi na rehema kwa wenye kuitenda. Na hii Qur'ani wanayo ikadhibisha
inasadikisha Vitabu vilivyo kwisha tangulia. Mwenyezi Mungu ameiteremsha
kwa lugha ya Kiarabu iwe ni onyo jipya kwa wenye kudhulumu, na bishara
kwa wenye kusimama sawa juu ya Njia.
13. Hakika wanao sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu peke yake,
kisha wakatengenea kwa kufanya vitendo vizuri, watu hao hawana khofu ya
kushukiwa la karaha, na wala hawatahuzunika kwa kuyakosa wayatakayo.
14. Hao wanao sifika kwa kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, na kusimama
sawa, ndio walio khusika kuingia Peponi wakikaa humo milele. Mwenyezi Mungu
amewapa hayo kuwa ni jaza yao kwa mema waliyo kuwa wakiyatenda.
15. Na tumemuusia mwanaadamu kwa wazazi wake awafanyie wema mkubwa.
Kwani mama yake amechukua mimba yake kwa mashaka, na akamzaa kwa mashaka.
Na muda wa kuchukuliwa mimba mpaka kuachishwa ziwa ni miezi thalathini.
Muda wote huo mama kapitikiwa na kila namna ya machungu. Mpaka huyo mtu
alipo fikilia ukamilifu wa nguvu zake na akili yake, na akafikia miaka
arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Nijaalie niishukuru neema yako uliyo
nineemesha mimi na wazazi wangu, na nijaalie nitende vitendo vyema utavyo
viridhi Wewe, na ujaalie huo wema wapate pia dhuriya zangu. Hakika mimi
nimetubu kwako kwa kila dhambi, na mimi ni miongoni wa Waislamu, yaani
walio zisalimisha nafsi zao kwako.
Uchache wa mimba ni miezi sita, kwa kauli yake Mtukufu: " Na kuchukua
mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini." Na kauli yake Mtukufu:
"Na kumwachisha ziwa kwake ni miaka miwili", na kauli yake Mtukufu: "Na
wazazi wa kike huwanyonyesha wana wao miaka miwili kaamili, kwa mwenye
kutaka kutimiza kunyonyesha." Basi ukitoa muda wa kuachisha ziwa
kutokana na muda wa mimba na kunyonyesha inabakia muda wa mimba ni miezi
sita. Na haya yanawafikiana na iliyo thibiti kwa ilimu za sayansi kwamba
mtoto mchanga akizaliwa baada ya mimba ya miezi 6 anaweza kuishi.
16. Hao walio sifika kwa sifa hizo ndio tutakao wapokelea a'mali
zao njema, na tutawasamehe maovu yao miongoni mwa watu wa Peponi. Itawathibitikia
miadi ya kweli walio kuwa wakiahidiwa duniani.
17. Na waliwafyonya wazazi wao kwa kuchukia na kuchoka nao, walipo
wataka waamini kufufuliwa, na wakawaambia: Mnaniambia tutatoka makaburini
na mataifa mangapi yamepita kabla yangu na hapana hata mmoja aliye fufuliwa
kutoka makaburini? Na hao wazazi wake wanaomba msaada kwa Mwenyezi Mungu
jinsi ya kuona ni makuu makosa ya mwana wao, wakisema kwa kumshikilia aamini:
Utaangamia wewe kama hukuamini. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kufufua
ni kweli. Naye bado amekakamia kukadhibisha kwa kusema: Hayo mnayo yasema
si chochote ila ni hadithi za uwongo za watu wa kale!
18. Hao wasemao hayo ndio iliyo wathibitikia kuwashukia adhabu sawa
sawa na mataifa yaliyo kuwa kabla yao miongoni mwa majini na watu, kwa
sababu hakika hao walikuwa ni wenye kukhasiri.
19. Na wote, Waislamu na makafiri, wana vyeo vyao vinavyo lingana
na vitendo vyao walivyo vitenda, ili uadilifu wa Mwenyezi Mungu upate kuonekana
kati yao, na ili awalipe jaza ya 'amali zao, nao hawatadhulumiwa, kwa sababu
wanastahiki hayo wanayo lipwa.
20. Na siku watakapo simamishwa walio kufuru kwenye Moto waambiwe:
Mmekwisha chukua fungu lenu la vitu vizuri katika maisha yenu ya duniani,
na mkavionea raha. Basi leo ndio mnalipwa adhabu ya kufedhehesha kwa mliyo
kuwa nayo duniani, ya kujivuna katika nchi bila ya haki, na kutoka kwenye
ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
21. Mtaje Hud, mwenzao kabila ya A'di, alipo wahadharisha watu wake
wanao kaa Ah'qaaf, kwenye vilima vya mchanga. Na Mitume kadhaa walikuja
kabla yake na baada yake kwa maonyo kama yake ya kusema: Msimuabudu ila
Mwenyezi Mungu. Mimi nakukhofieni isikupateni adhabu yenye vitisho vikuu.
Maskani ya kabila hii ilikuwa huko Ah'qaaf, kwenye vilima vya mchanga.
Na wapi hapo Ah'qaaf? Zipo khitilafu. Baadhi ya wanazuoni wa taarikh (historia)
wanasema kuwa hapo ni baina ya Yaman na Oman mpaka Hadhramaut na Shihr,
yaani mashariki ya kusini ya Bara Arabu. Na baadhi ya wachunguzi wa zama
za karibu wanaona ni mashariki ya A'qaba, wakitegemea maandishi ya Nabat'ia
waliyo yakuta katika magofu ya hekalu walilo livumbua katika mlima wa Arim.
Walikuta pembezoni mwa mlima huo mabaki ya siku za Jahiliya za zamani.
Wakasahihisha kuwa hapo ndipo ilipo Arim iliyo tajwa katika Qur'ani tukufu.
Kisha kabila hiyo ikatoka hapo kabla ya Uislamu, na hapana kilicho baki
chao isipo kuwa chemchem ya maji ambayo wafanyi biashara na watu wa misafara
wakishukia hapo katika njia yao kwendea Shamu.
22. Kaumu ya Hud walisema kwa kumkanya: Hivyo ndio umetujia ili utuachishe
kuwaabudu miungu yetu? Basi tuletee hiyo adhabu ikiwa wewe hakika ni mwenye
kusema kweli kwa ahadi hiyo.
23. Hud akasema: Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kujua wakati
wa kuileta adhabu yenu. Mimi nafikisha ujumbe tu nilio tumwa. Lakini naona
kuwa nyinyi hamjui chochote katika mambo wanayo tumwa Mitume.
24,25. Ikawajia adhabu kwa sura ya wingu. Walipo liona limetanda
kote juu linaelekea mabondeni kwao, walisema kwa furaha: Wingu hili
linatuletea mvua na kheri. Wakaambiwa: Bali hilo ni hayo mliyo yahimiza,
nayo ni upepo wenye adhabu kali na chungu, itakayo teketeza kila
kitu kwa amri ya Muumbaji wake. Nao ukawaangamiza, yasionekane mabaki yao
isipo kuwa nyumba zao. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila mwenye kutenda kama
makosa yao.
26. Na tuliwaweka kabila la A'di kwa nafasi na nguvu sio kama tulivyo
kuwekeni nyinyi watu wa Makka. Na tuliwajaalia masikio, na macho, na nyoyo,
lau wangeli taka kunafiika kwayo. Lakini hayakuwafaa hata kitu kidogo masikio
yao, wala macho yao, wala nyoyo zao, kwa sababu walikuwa wakizikanusha
Ishara za Mwenyezi Mungu. Basi hayo yakapinga baina yao na kunafiika kwa
waliyo letewa. Na ile ile adhabu waliyo kuwa wakiifanyia maskhara ikawazunguka.
27. Enyi watu wa Makka! Tumeiangamiza miji iliyo jirani zenu. Na
Sisi tuliwawekea wazi dalili namna mbali mbali, ili wapate kurejea waache
ukafiri. Hawakurejea.
28. Basi kwani hao walio wafanya miungu badala ya Mwenyezi Mungu
ili iwakaribishe kwa Mwenyezi Mtukufu imeweza kuwakinga na maangamizo?
Hasha! Bali miungu hiyo iliwakimbia, na hali wao ndio wana haja nayo mno
iwanusuru. Na hayo yaliyo wafika, ya kutupwa na miungu yao, na kuwapotea
ndio matokeo ya uwongo wao na uzushi wao.
29. Ewe Muhammad! Taja tulipo kuletea kikundi cha majini waje sikiliza
Qur'ani. Walipo hudhiria ilipo kuwa ikisomwa, baadhi yao wakawaambia wenzao:
Sikilizeni! Ilipo kwisha timia kusomwa wakarudi kwa haraka kwa wenzao,
kuwahadharisha na ukafiri, wakiwataka waamini.
30. Walisema: Enyi watu wetu! Hakika sisi tumekisikia Kitabu chenye
shani kubwa. Kimeteremshwa baada ya Musa, na kinasadikisha Vitabu vya Mwenyezi
Mungu vilivyo tangulia, kinaongoza kwenye itikadi ya haki, na sharia ya
vitendo iliyo simama sawa.
31. Enyi watu wetu! Muitikieni mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu anaye
ongoza kwenye Haki na kwenye Njia Iliyo Nyooka. Na msadikini Mwenyezi Mungu
akusameheni madhambi yenu yaliyo tangulia, na akulindeni na adhabu kali
iliyo chungu.
32. Na asiye muitikia Mwenyezi Mungu basi hawezi kumshinda Mwenyezi
Mungu asimtie mkononi hata akikimbia vipi katika ardhi. Na wala hana isipo
kuwa Mwenyezi Mungu wa kumnusuru na kumkinga na adhabu yake. Hao wanao
puuza wasimwitikie mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu wamo katika ubabaishi
na dhaahiri wako mbali na Haki.
33. Wameghafilika wala hawajui kwamba Mwenyezi Mungu aliye ziumba
mbingu na ardhi, na wala hakushindwa kuziumba, ni Muweza wa kuwafufua maiti?
Bali Yeye ni Muweza wa hayo, kwani Yeye Mtukufu ana uweza kaamili juu ya
kila kitu.
34. Na siku watakapo simamishwa walio kufuru Motoni wataambiwa kwa
kukemewa: Adhabu hii si jambo la kweli linakubaliana na tuliyo kuonyeni
nayo duniani? Na wao watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu Mlezi, haya
ni haki kweli. Atasema: Onjeni kila namna ya adhabu kali kwa kushikilia
kwenu ukafiri na ukanushi.
35. Ewe Muhammad! Wastahamilie makafiri kama walivyo stahamili Mitume wengine wenye nguvu na imara wakati wa shida. Wala usiwahimizie adhabu. Kwani hiyo itawafika tu, hapana hivi wala hivi, hata ikichukua muda mrefu. Siku watapo kiona kitisho chake watadhani kuwa hawakukaa kabla yake ila saa moja tu ya mchana. Haya uliyo watolea waadhi yatosha. Hawataangamizwa kwa adhabu isipo kuwa walio toka kwenye ut'iifu.