1. H'a Mim. Hizi ni harufi mbili katika harufi za kutamkwa,
zimeanzia Sura hii kama ada ya Sura nyingi katika Qur'ani ambazo zimeanzia
kwa harufi kama hivi ili kuashiria kuwa washirikina wameshindwa kuleta
mfano wake, ijapo kuwa hii Qur'ani imeundwa kwa harufi hizi hizi wanazo
zitumia katika maneno yao.
2. Huu mteremsho wa Qur'ani umetokana na Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu,
Asiye shindika, Mwenye hikima katika kupanga kwake na kuendesha kwake.
3. Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi ni katika ufundi wa namna
ya pekee wa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka ni dalili zenye nguvu kabisa
katika Ungu wake na Upweke wake, ambao wanauamini wenye kumsadiki Mwenyezi
Mungu kwa maumbile yao yaliyo sawa.
4. Na vile Mwenyezi Mungu kukuumbeni nyinyi, enyi watu, kama mlivyo,
mna sura nzuri, na umbo la peke yenu, na mnavyo khitalifiana baina
ya wanaadamu na wanyama na mkaenezwa ulimwenguni, na manufaa mbali mbali,
bila ya shaka ni Ishara zenye nguvu na ziwazi kwa watu wanao tafuta yakini
ya mambo yao kwa kuzingatia na kufikiri.
5. Na katika kukhitalifiana usiku na mchana, kwa urefu na ufupi,
na mwangaza na giza, na kupeana zamu kwa nidhamu iliyo thibiti, na katika
mvua anayo iteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, akaihuisha ardhi kwa
mimea baada ya kufa kwake kwa ukame, na kuziendesha pepo pande mbali mbali
nazo zinakhitalifiana kwa ubaridi na joto, na nguvu na udhaifu, ni alama
zilizo wazi za kuonyesha ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa watu
wenye kufikiri kwa akili zao, wakafikilia yakini yao.
6. Hizo ni Aya za Mwenyezi Mungu zinazo eleza uumbaji alio ufanya
Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watu. Tunakusomea wewe katika Qur'ani kwa ulimi
wa Jibrili, nazo Aya hizo ni za haki. Ikiwa hao hawaziamini hizi
basi maneno gani watayasadiki baada ya maneno ya Mwenyezi Mungu, nayo ni
Qur'ani na Aya zake
7. Atapata maangamizo makubwa kila anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo
mbaya, na mwenye kukithiri madhambi yake kwa kitendo hicho!
8. Mzushi kama huyu husikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, nazo
zinasema haki tupu. Kisha yeye huendelea na ukafiri wake kwa kutakabari,
akaikataa Imani. Hali yake ni hali ya asiye pata kuzisikia Aya. Basi
ewe Nabii! Mbashirie, kwa kumkejeli, kuwa atapata adhabu chungu kwa huko
kushikilia kwake kitendo kitacho mletea adhabu hiyo.
9. Na huyu mwenye inda, akijua kitu kidogo katika Aya za Mwenyezi
Mungu huzifanya Aya zote za Mwenyezi Mungu ni kitu cha kufanyia maskhara
na mzaha. Wazushi hao wingi wa madhambi watapata adhabu ya kuwadhalilisha
kwa kiburi chao.
10. Nyuma yao ipo Jahannamu inawangojea, na walicho kichuma duniani
hakitawapunguzia hata chembe ya adhabu yake. Wala hiyo miungu ya uwongo
walio ifanya ndio ya kuwanusuru badala ya Mwenyezi Mungu, haitawakinga
na chochote katika adhabu yake. Na wao watapata mateso makubwa, kwa kitisho
chake na ukali wake.
11. Hii Qur'ani ni ushahidi kaamili wa Haki itokayo kwa Mwenyezi
Mungu. Na hao wanao zikataa hoja zilio kusanywa na Qur'ani zilizo toka
kwa Muumba wao na Mlezi wao watapata adhabu kali mno miongoni mwa namna
za adhabu.
12. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye kufanyieni ikutumikieni
bahari ili marikebu zipate kwenda juu yake kwa idhini yake, na uwezo
wake, zikikubebeni nyinyi na bidhaa zenu, na ili mtafute kutokana na fadhila
za Mwenyezi Mungu mali ya baharini kwa kupata manufaa ya ujuzi, na biashara,
na jihadi, na zawadi, na uvuvi, na kutoa vyombo, na ili mpate kushukuru
neema zake kwa kumsafia Dini Mwenyezi Mungu.
13. Na akakudhalilishieni vyote viliomo mbinguni, nyota zenye kung'ara
na sayari, na vyote viliomo kwenye ardhi, makulima, mifugo, maji,
moto, hewa, na jangwa, vyote hivyo vinatokana na Yeye Mtukufu, ili akuenezeeni
manufaa ya uhai. Hakika katika hizo neema zilizo tajwa zipo Ishara zenye
kuonyesha kudra yake kwa watu wenye kuzingatia Ishara.
14. Ewe Mtume! Waambie wanao msadiki Mwenyezi Mungu na wanakufuata
wewe, wasamehe maudhi yanayo wafikia kutokana na watu ambao hawataraji
kuja siku za Mwenyezi Mungu za kuwalipa watu kwa kheri na shari kwa mujibu
walivyo.
15. Mwenye kutenda mema atapata ujira wake na thawabu mwenyewe; na
mwenye kutenda uovu basi dhambi za kitendo chake zitamuangukia mwenyewe.
Kisha mtarudishwa kwa Muumba wenu kwa ajili ya malipo.
16. Ninaapa kwa hakika tumewapa Wana wa Israili Taurati, na hukumu
iliomo ndani yake, na Unabii ulio funuliwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na
tumewaruzuku kheri namna mbali mbali, na tumewafadhilisha wao katika neema
nyingi juu ya viumbe vyote.
17. Na tumewapa dalili wazi katika mambo ya Dini yao. Basi haikutokea
khitilafu baina yao ila baada ya kwisha wajia ujuzi wa hakika ya Dini na
hukumu zake. Na hayo ni kwa uadui na uhasidi tu ulio baina yao. Hakika
Mola wako Mlezi atapambanua baina ya hao wanao khitalifiana Siku ya Kiyama
katika mambo waliyo kuwa wamekhitalifiana.
18. Tena tukakujaalia wewe, ewe Muhammad, baada ya khitilafu za Watu
wa Kitabu (yaani Mayahudi na Wakristo), kuwa ni Mtume wa kwenda Njia iliyo
wazi katika mambo ya Dini tuliyo kuwekea wewe na walio kuwa kabla yako
miongoni mwa Mitume. Basi ifuate Sharia yako ya Haki, yenye kuthibiti imara
kwa hoja na dalili, wala usifuate matamanio ya watu wasio ijua Njia ya
Haki.
19. Hakika hao waongo wenye tamaa ya kuwa ati wewe utawafuata wao,
hawatoweza kukuondolea hata chembe ya adhabu pindi ukiwafuata. Na hakika
wenye kupindukia mipaka ya Mwenyezi Mungu husaidiana wao kwa wao katika
upotovu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuwasaidia wale wanao mcha, basi
hao haitawafikia dhulma ya wenye kudhulumu.
20. Hii Qur'ani ulio teremshiwa wewe ni dalili kwa watu kuwaonyesha
Dini ya Haki, na uwongofu wa kuwaongoza kwenye njia za kheri, na neema
kwa watu wenye kuyakinisha thawabu na adhabu za Mwenyezi Mungu.
21. Bali wanadhani hao walio chuma yanayo chusha katika ukafiri na
maasi kwamba tutawafanya kama walio muamini Mwenyezi Mungu na wakatenda
vitendo vyema, na hivyo tuwafanye sawa baina ya makundi mawili hayo katika
uhai na katika kufa? Hukumu yao ni mbaya mno, ikiwa wanahisi kuwa wao ni
sawa na Waumini.
22. Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa mujibu wa hikima
na nidhamu, ili zidhihiri dalili za Ungu wake na uwezo wake, na apate kulipwa
kila mtu kwa alilo tenda, ikiwa kheri au shari. Na wao hawatapunguziwa
chochote katika malipo yao.
23. Ewe Mtume! Umeangalia, ukamwona huyo mwenye kufanya matamanio
yake ndiye mungu wake wa kumuabudu, akamnyenyekea, na akamt'ii, na akaiacha
Njia ya Haki na hali anaijua, na akaziba masikio yake asisikie waadhi,
na moyo wake asiamini Haki, na akabandika vitanga vya macho asione ya kuzingatiwa?
Basi nani wa kumwongoa mtu huyu baada ya kwisha puuzwa na Mwenyezi Mungu?
Je! Mnaacha kutazama ili msipate kukumbuka?
24. Na walisema wenye kukanya kufufuliwa: Hapana uhai ila huu uhai
wa duniani tu tulio nao sasa. Tunaishi na tunakufa. Na hapana nyuma ya
hayo uhai baada ya kwisha kufa. Na hapana cha kututeketeza isipo kuwa kupita
dahari, yaani zama na wakati. Wala wao hawasemi hayo kwa ujuzi na kuwa
na yakini, bali ni kwa kudhania na kukisia tu.
25. Na ukiwasomea Aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi zenye kuonyesha
uwezo wake wa kufufua, huwa hawana hoja ila kusema - kwa kuikimbia haki
: Wafufueni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wasema kweli katika kudai kuwa kupo
kufufuliwa.
26. Ewe Muhammad! Waambie: Mwenyezi Mungu amekupeni uhai duniani
nanyi hamkuwa chochote, kisha anakufisheni unapo timia wakati wenu. Kisha
atakukusanyeni Siku ya Kiyama, na hapana shaka ya kukusanywa huko. Lakini
wengi wa watu hawaujui uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kufufua, kwa sababu ya
mapuuza yao kuzingatia dalili ziliopo. Na huyo Muweza wa hayo pia ni Muweza
wa kuwaleta baba zenu.
27. Na ni wa Mwenyezi Mungu pekee ufalme wa mbingu na ardhi, kwa
kuumba, kumiliki, na kupanga. Na itapo fika Saa ya Kiyama, siku hiyo watakhasiri
wenye kufuata upotovu.
28. Ewe unaye semezwa! Utawaona siku itapo fika Saa watu wa kila
dini wamekalia magoti kwa khofu waliyo nayo kungojea kuitikia wito. Kila
umma utaitwa kwenye daftari la vitendo vyao, na wataambiwa: Leo mtalipwa
sawa malipo ya mliyo kuwa mkiyatenda duniani.
29. Na wataambiwa: Hichi hapa kitabu chetu tulimo sajili vitendo
vyenu, nanyi mmekichukua kwa mikono yenu, kinataja juu yenu yale mliyo
yatenda kwa ushahidi wa kweli. Hakika Sisi tulikuwa tukiwataka Malaika
waandike, ili tupate kukuhasibieni yaliyo tokana nanyi.
30. Basi ama walio amini na wakatenda vitendo vyema, Mola wao Mlezi
atawatia katika Pepo yake. Malipo hayo ndio kufuzu kulio bainika, kulio
wazi.
31. Na ama walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake wataambiwa
kwa kuwahizi: Kwani hawakukujilieni Mitume wangu? Hamkusomewa Aya zangu,
nanyi mkajiona bora hamfai kuikubali haki, na mkawa kaumu ya makafiri?
32. Enyi mnao kanya kufufuliwa! Akikwambieni Mtume wa Mwenyezi Mungu
kwamba agano la Mwenyezi Mungu la kuwalipa ni haki yenye kuthibiti, na
Saa haina shaka itakuja, nyinyi mkisema: Sisi hatujui chochote khabari
ya hiyo Saa ya Kiyama, wala ukweli wake; na sisi ni dhana ya kudhania tu
kuwa hiyo Saa itakuja, wala hatuna yakini kuwa itatokea.
33. Na utawadhihirikia hawa makafiri ubaya wa vitendo vyao, na itawateremkia
jaza ya maskhara yao waliyo kuwa wakizifanyia Ishara za Mwenyezi Mungu.
34. Na wataambiwa hawa washirikina kwa kuwahizi: Leo hii tunakuacheni
katika adhabu kama nyinyi mlivyo acha kujitayarisha kukutana na Mola wenu
Mlezi katika siku hii kwa ut'iifu na vitendo vyema. Na pahala penu pa kukaa
ni Motoni, na wala hamna wa kukunusuruni akakuokoeni na adhabu yake.
35. Adhabu hiyo imekuteremkieni kwa sababu ya ukafiri wenu, na maskhara
yenu kuzifanyia Ishara za Mwenyezi Mungu, na mlivyo khadaika na maisha
ya dunia kwa mapambo yake. Basi leo hapana yeyote awezaye kuwatoa hawa
kwenye Moto, wala hawatakikani kumtaka radhi Mola wao Mlezi kwa kutafuta
udhuru.
36. Basi ni za Mwenyezi Mungu pekee sifa njema, Muumba mbingu na
ardhi, na Muumba wa viumbe vyote. Kwani hivi kuwa ni Mola Mlezi wa kila
kitu unawajibika uhimidiwe kwa neema zote.
37. Na ni wake Yeye, Subhanahu, utukufu na utawala katika mbingu
na ardhi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, asiye shindika, Mwenye hikima, asiye
kosea katika hikima yake.
Na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi kuliko wote.