1. H'a Mim. Imeanzia Sura hii kwa baadhi ya harufi za
kutamkwa kama ilivyo ada ya Qur'ani katika kufungulia Sura nyingi kwa harufi
kama hizi.
2. Mwenyezi Mungu anaapa kwa Qur'ani yenye kuweka wazi Dini ya Haki,
yenye kuwabainishia watu yaliyo na maslaha ya dunia yao na Akhera yao,
ili kujuulisha utukufu wa cheo chake.
3. Hakika Sisi tumeanza kuiteremsha Qur'ani katika usiku ulio jaa
kheri, wenye baraka nyingi, kwani ni mwendo wetu kuonya kwa kuwatuma Mitume
na kuteremsha Vitabu.
4. Katika usiku huu wenye baraka hupambanuliwa baina ya mambo yote
yenye hikima, na Qur'ani ndio kilele cha hikima, na ndio pambanuo baina
ya kweli na uwongo. Na kwa hivyo ndio ikateremshwa katika usiku huo.
5. Nakusudia kwa jambo hili, yaani jambo kuu lenye kutoka kwetu kama
ilivyo kwisha pita hukumu ya mpango wetu. Kwani ni shani yetu kutuma Mitume
kwa Vitabu ili kuwafikishia waja wetu.
6. Kwa ajili ya rehema ya Mola wako Mlezi kwa waja wake, amewatuma
Mitume kwa watu wawafikishie uwongofu wake, kwani hakika Yeye peke yake,
ndiye Mwenye kusikia kila cha kusikiwa, Mwenye kujua kila cha kujuulikana.
7. Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi
mna yakini na haki, na mnaifuata, na mnaamini kuwa hakika ndio Yeye Mwenye
kuteremsha Qur'ani kuwa ni rehema na uwongofu.
8. Hapana Mungu isipo kuwa Yeye anaye stahiki kuabudiwa, Yeye peke
yake, Mwenye kuhuisha na kufisha. Na Yeye peke yake, ndiye aliye kuumbeni
nyinyi na kawaumba baba zenu wa mwanzo.
9. Lakini makafiri wana shaka na ukweli huu, wamo wakifuata pumbao
lao. Na huo ndio mtindo wa watu wa pumbao na michezo, sio mwendo wa watu
wa ilimu na yakini.
10. Basi ewe Mtume! Ngojea ukame utapo wateremkia, wakasibiwa na
kukonda na udhaifu wa kuona, ikawa mtu huwa anaona baina ya mbingu na ardhi
moshi dhaahiri shaahiri, akawa anasikia mvumo wake wala hauoni.
11. Moshi huu utawazunguka wale wanao kadhibisha walio sibiwa na
ukame, watasema kwa wingi wa kitisho: Hii ni adhabu kali na chungu!
12. Kama pia watavyo sema kwa kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu:
Hakika sisi tutaamini ukituondolea adhabu ya njaa na dhiki.
13. Watu hawa watawaidhika vipi, hata watimize hiyo Imani wanayo
iahidi wakiondolewa adhabu, na hali Mtume mwenye ujumbe ulio wazi kesha
wajia na miujiza yenye kuonyesha ukweli wake, na hayo ndiyo mawaidha makubwa
kabisa?
14. Kisha wakaacha kumsadiki Mtume aliye tiliwa nguvu na miujiza
iliyo wazi, na wakamwambia: Huo uwongo na uzushi! Mara nyengine wakimsingizia
kuwa amefunzwa hayo na mtu, na mara nyengine kuwa akili yake imekorogeka.
15. Mwenyezi Mungu anawarudi: Sisi hakika tutakuondoleeni adhabu
wakati wa duniani, nao ni wakati mchache, lakini nyinyi mtarejea tu, bila
ya shaka, yale yale mliyo kuwa mkiyatenda.
16. Ewe Mtume! Watajie ile siku tutapo washika kwa mshiko mkubwa,
wa nguvu. Nasi kwa mshiko huu ndio tunawatesa.
17. Na bila ya shaka tulikwisha wafanyia mtihani, kabla ya makafiri
wa Makka, kaumu ya Firauni kwa kuwaitia kwenye Imani, na akawajia Musa,
Mtume Mtukufu kwa Mwenyezi Mungu. Wakamkataa kwa inda tu. Na huo ndio mtindo
wa hawa washirikina.
18. Mtume Mtukufu aliwaambia: Nipeni enyi waja wa Mwenyezi Mungu
lilio waajibu juu yenu, nalo ni kuitikia wito wangu, kwani mimi ni Mtume
nimetumwa makhsusi kwenu, na ni muaminifu katika ujumbe wangu.
19. Wala msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu kwa kumkadhibisha Mtume
wake, kwani mimi nakuleteeni muujiza ulio wazi wa kubainisha ukweli wa
Unabii wangu na Utume wangu.
20. Na mimi najilinda na Mwenye kuniumba msiweze kuniuwa kwa kunipiga
mawe.
21. Na ikiwa hamnisadiki basi jitengeni nami, wala msiniudhi.
22. Musa akamwambia Mola wake Mlezi kwa kumshitakia watu wake alipo
kata tamaa nao kuwa hawaamini: Hakika watu hawa shauri yao imekwisha fika
ukomo katika ukafiri; basi Wewe wafanyie wanalo stahiki.
23. (Naye Musa akaambiwa:) Toka na Waumini usiku usiku kwa kificho,
wasije kukupateni, kwani Firauni na askari wake watakufuateni pindi wakijua,
wakukamateni.
24. Na iache bahari imetulia kama ilivyo baada ya kwisha pigwa
kwa fimbo, wapate kuingia hao wanao kanya; kwani wao watazama tu, hapana
hivi wala hivi.
25. Hao watu wa Firauni baada ya kuzama kwao waliacha mabustani mengi
yenye kunawiri, na chemchem zinazo tiririka maji yake,
26. Na makulima ya namna kwa namna, na makaazi mazuri mazuri,
27. Na maisha ya raha na starehe, waliyo kuwa wakiyaonea utamu.
28. Mfano wa adhabu hiyo Mwenyezi Mungu humuadhibu mwenye kwenda
kinyume na amri yake, na akatoka katika ut'iifu wake, na humwondolea neema
yule mwenye nayo akawapa watu wenginewe wasio kuwa na makhusiano nao yoyote,
la ya ujamaa wala dini.
29. Basi la mbingu wala ardhi hazikuwahuzunukia ilipo wanyakua adhabu,
jinsi ilivyo haribika hali yao; wala hawakungojewa watubu, wala hawakupewa
muhula wapate kudiriki taksiri yao, kwa jinsi walivyo dharauliwa!
30. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu aliwaokoa Wana wa Israili na adhabu
ya kuwadhalilisha.
31. Aliwaokoa kwa Firauni. Hakika Firauni alikuwa jeuri kwa watu
wake, amepita mipaka kwa shari na uasi.
32. Ninaapa: Tuliwakhiari Wana wa Israili kwa kuwa tuliwajua kwamba
wao wana stahiki kuteuliwa kuliko watu wengine wote wa zama zao. Kwa hivyo
tukawatuma miongoni mwao Manabii wengi kwa kuwa tulijua hali zao.
33. Na Mwenyezi Mungu akawaletea katika mkono wa Musa dalili kadhaa
wa kadhaa za kuwatia wao katika mitihani iliyo wazi.
34,35. Hakika hawa wanao kadhibisha kufufuliwa bila ya shaka wanasema:
Hapana kufa ila kwa haya haya mauti yetu ya kwanza ya duniani, wala sisi
hatutafufuliwa tena.
36. Na wao humwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu na Waumini: Ikiwa nyinyi
mnasema kweli katika madai yenu kwamba Mola wenu Mlezi anahuisha wafu kwa
ajili ya hisabu katika Akhera, basi upesi upesi tufufulieni baba zetu walio
kwisha kufa, kwa kumwomba huyo Mola wenu Mlezi!
37. Je! Makafiri wa Makka wanawashinda kaumu ya Tubbaa' na walio
watangulia kwa nguvu, na ulinzi, na utawala, na mambo yote ya kidunia?
Ewe Muhammad! Hao washirikina wa kaumu yako hawawashindi hao kwa nguvu,
na hao Sisi tuliwateketeza katika dunia kwa ukafiri wao na madhambi yao.
Basi nawawazingatie!
38. Na Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao
bila ya hikima.
39. Hatukuziumba hizo ila kwa umbo lilio ambatana na hikima, kwa
nidhamu iliyo thibiti yenye kuonyesha ushahidi wa kuwepo Mwenyezi Mungu
wa pekee, Mwenye uwezo. Lakini wengi wa hawa wameghafilika, wamo katika
upofu, hawazioni dalili hizi.
40. Hakika siku ya hukumu kupambanua baina ya mwenye haki na asiye
na haki, ni wakati walio ahidiwa wote.
41. Siku ambayo jamaa hawezi kumtetea jamaa yake, wala rafiki kumtetea
rafiki yake kwa lolote, hata kwa uchache wa adhabu. Wala wao hawatanusuriwa
nafsi zao mbele ya Mwenyezi Mungu.
42. Lakini wale ambao Mwenyezi Mungu amewarehemu, miongoni mwa Waumini,
Mwenyezi Mungu atawasamehe, na atawapa ruhusa ya uombezi waweze kuwaombea
wenginewe. Hakika Yeye ndiye Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kuwarehemu
waja wake Waumini.
43,44. Hakika mti wa Zaqqumu unao juulikana kwa ubaya wa sura yake,
na ukarihi kuula kwake, na harufu yake, ni chakula cha wakosefu wenye madhambi
mengi.
45,46. Utamu wake kama maadeni iliyo yayushwa kwa moto, inatokota
matumboni kama yanavyo tokota maji yanayo chemshwa.
47. Enyi Mazabania wa Jahannamu (Walinzi wa Motoni)! Mkamateni huyu
mkosefu, mwenye dhambi, mumtokomeze kwa nguvu na ukali mpaka katikati ya
Jahannamu!
48. Kisha mmiminieni juu ya kichwa chake maji ya moto makali kuzidi
kumuadhibu na kumtesa.
49. Ataambiwa kwa kejeli na maskhara: Onja hii adhabu kali, kwani
ati wewe si ndiye mtukufu mwenye nguvu katika kaumu yako, ndiye mheshimiwa
unavyo jiona mwenyewe!
50. Hapana shaka hii adhabu mnayo ipata ni kweli yenye kuwa, na ndiyo
mliyo kuwa mkiibisha duniani, na mkiitilia shaka kuwa haiwi.
51. Hakika hao ambao wamejikinga nafsi zao na maasi kwa kufuata ut'iifu
wa Mwenyezi Mungu wapo pahala patukufu ambapo ndani yake wao wanajipatia
amani kwa nafsi zao.
52. Katika mabustani watapo kuwa ndani yake wanastarehe, na chemchem
za maji yanayo pita chini yao, kwa sababu ya kuwakirimu wao kwa kutukuza
hizo neema zao.
53. Wakivaa humo hariri nyepesi na nzito kuzidi kuongeza mapambo
yao, nao wakielekeana katika majlisi zao, ili kutimiza starehe.
54. Na pamoja na malipo haya tutawaoza huko Peponi mahurulaini, ambao
huwezi kuwachanganyia jicho kwa hadi ya uzuri wao na ukubwa wa macho yao.
55. Nao huko Peponi watataka kila tunda wanalo litamani, kwa kujua
kuwa hayatawaletea vimbizi, wala hayatakwisha, wala hayataadimika.
56. Huko Peponi hawataonja mauti baada ya mauti ya kwanza waliyo
kwisha yaonja duniani ulipo kwisha muda wao wa kuishi, na Mola wao Mlezi
atawalinda na adhabu ya Motoni.
57. Kuhifadhiwa kwao na adhabu ni fadhila na hisani ya Muumba wako.
Kuhifadhiwa huko na adhabu na kuingizwa kwao Peponi ndio hadi ya mwisho
ya kufuzu kulio kukubwa.
58. Basi hakika Sisi tumekufanyia wepesi kuisoma Qur'ani na kuifikisha
kama ilivyo teremka kwa lugha yako, na lugha yao, ili wapate kuwaidhika,
na waiamini, na watende kwa mujibu yaliomo ndani yake.
59. Basi wewe yangojee hayo yatakayo wafika, na wao pia wanangojea yatakayo kufika wewe na huo wito wako, mambo yakibadilika.