1,2. H'a Mim, A'yn Sin Qaf: Sura imeanzia kwa harufi
hizi za kutamkwa kama ilivyo ada katika Sura nyingi katika Qur'ani.
3. Mfano wa yaliyomo katika Sura hii anakufunulia
wewe na Mitume walio kuwa kabla yako, Mwenyezi Mungu
Mwenye kushinda kwa nguvu zake, ambaye amepanga kila kitu kwa pahala
pake, kwa mujibu wa hikima katika vitendo vyake na mipango yake.
4. Ni vya Mwenyezi Mungu, peke yake, vyote viliomo katika mbingu
na ardhi, kwa kuviumba, kuvimilika, na kuviendesha. Naye ni peke yake aliye
tukuka kwa nafsi, na ukawa mkuu ufalme wake.
5. Mbingu, juu ya ukubwa wake na kushikamana kwake, zimekaribia kupasuka
kutoka huko juu kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu, na kuathirika kwa taadhima
yake na utukufu wake. Na Malaika wanamtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisilo
elekea naye, na humsifu kwa analo stahiki. Na humwomba Mwenyezi Mungu awasamehe
watu wa duniani. Na Yeye Subhanahu ananabihisha kwamba hakika ni Mwenyezi
Mungu tu, peke yake, ndiye Mwenye maghfira ya wote, na rehema iliyo kunjufu.
6. Na hao walio wafanya wengineo badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ndio
wa kuwanusuru, Mwenyezi Mungu anaangalia hayo wayatendayo. Wala wewe hukupewa
kazi hiyo ya kuwaangalia wao.
7. Na mfano wa ufunuo huo ulio wazi, tumekufunulia wewe hii Qur'ani
kwa lugha ya Kiarabu isiyo na ubabaishi, ili upate kuwaonya watu wa Makka
na walio pembezoni mwake katika Waarabu, na uwaonye watu adhabu ya siku
watakao kusanywa khalaiki wote kwa ajili ya hisabu. Hapana shaka yoyote
kuja siku hiyo. Watu siku hiyo watakuwa mafungu mawili - fungu moja litakuwa
Peponi. ma kundi jengine litakuwa Motoni.
8. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli penda kuwakusanya watu wote
katika dunia wakafuata njia moja angeli wakusanya hivyo. Lakini Yeye humtia
katika rehema yake amtakaye, kwa kuwa anajua kuwa hao wamekhiari uwongofu
kuliko upotofu. Na wenye kujidhulumu nafsi zao kwa ukafiri hawana mlinzi
badala ya Mwenyezi Mungu wa kudhamini kuwalinda, wala msaidizi wa
kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
9. Hawa wenye kudhulumu hawakumfanya Mwenyezi Mungu kuwa ni mlinzi
wao, bali wamewafanya wengineo kuwa ndio walinzi wao. Na wala haiwafalii
wao hayo. Kwani Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye Mwenye kustahiki kuwa
Mlinzi kama wao wanataka mlinzi. Yeye ndiye anaye fufua walio kufa kwa
ajili ya hisabu. Na Yeye ndiye Mwenye madaraka juu ya kila kitu kwa uweza
wake.
10. Na mliyo khitalifiana kwayo katika mambo yaliyo khusu Imani na
ukafiri, hukumu yake ya kukata iko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye amekwisha
ibainisha. Yeye huyo ndiye Hakimu wa kuhukumu mliyo khitalifiana, Mwenyezi
Mungu, Mwenye kumiliki mambo yangu yote. Mimi namtegemea Yeye kwa
mambo yangu. Na kwake Yeye peke yake ndio narejea ili kutafuta uwongozi.
11. Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akakuumbieni katika
jinsi yenu wanaume na wanawake, na akaumba katika mifugo yenu kadhaalika
madume na majike, na kwa mpango huu ndio wazidi kuwa wengi. Hapana kitu
chochote kama mfano wake Mwenyezi Mungu, basi hana kitu cha kuwa wa pili
yake. Na Yeye ndiye Mwenye kujua, kwa ujuzi wa kukamilika, kuvijua vyote
vinavyo sikilizana na kuonekana bila ya taathira ya hisiya.
12. Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi, kwa
kuzihifadhi na kuzitumia. Humkunjulia riziki amtakaye, na humdhikisha amtakaye.
Hakika Yeye, Mtukufu, ujuzi wake umezunguka kila kitu.
13. Amekufanyieni sharia itikadi kama alivyo agana na Nuhu, na tulizo
kufunulia wewe kwa Wahyi, na tulivyo agana na Ibrahim, na Musa, na Isa,
ya kwamba mzitie imara nguzo za Dini, kwa kuyafuata yaliyo letwa na Dini,
wala msikhitalifiane katika jambo hilo. Ni uzito kwa washirikina hayo unayo
waitia ya kusimamisha nguzo za Dini. Mwenyezi Mungu humteuwa kwa ajili
ya Ujumbe wake amtakaye, na humwezesha na kumsaidia katika Imani na kusimama
katika Dini mwenye kuacha inda na kumwelekea Yeye.
14. Wala hawakukhitalifiana katika Dini wafuasi wa Mitume walio tangulia
ila baada ya kuwafikia ujuzi wa kweli, na hayo ni kwa kutokana na uadui
na uhasidi ulio baina yao. Na lau kuwa si ahadi iliyo kwisha tangulia kutoka
kwa Mwenyezi Mungu ya kuakhirisha adhabu mpaka Siku ya Kiyama, basi bila
ya shaka walingeli teketezwa. Na kwa hakika wale walio rithishwa Kitabu
kutokana na walio kabla yao, na wakawahi zama zako, wana shaka na Kitabu
chao, tena shaka ya kuwatatanisha. Ndio maana hawaitikii wito wako. (Lau
kuwa Mayahudi wameamini kweli yaliyomo katika Taurati, wangeli muamini
Nabii Isa na Nabii Muhammad. Na lau kuwa Wakristo wameamini kweli yaliomo
katika Taurati na Injili basi hapana la kuwazuia wasimuamini Nabii Muhammad,
na kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, wala hana Utatu. Lakini hawana imani
ya yakini, na kwa hivyo wameunda mawazo yaliyo nje ya Taurati na nje ya
Injili.)
15. Basi kwa ajili ya umoja wa Dini, na kuondoa mtafaruku ndani yake,
waite waishike Dini, na shikilia Wito huo kama alivyo kuamrisha Mwenyezi
Mungu, wala usitafute kuyaridhi matamanio ya washirikina. Na sema: Mimi
naamini Vitabu vyote alivyo wateremshia Mwenyezi Mungu Mitume wake, na
Mwenyezi Mungu ameniamrisha nisimamishe uadilifu baina yenu. Na waambie:
Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wetu, na ndiye Muumba wenu. Vitendo vyetu
ni vyetu sisi, si vyenu. Na vitendo vyenu ni vyenu nyinyi, si vyetu. Hapana
la kubishana baina yetu na nyinyi, kwani haki iwazi. Mwenyezi Mungu atatukusanya
kwa kutuhukumu kwa uadilifu. Na kwake Yeye peke yake ndio marejeo ya kurejea.
16. Na hao wanao bisha katika mambo yaliyo khusu Dini ya Mwenyezi
Mungu, baada ya watu kwisha uitikia Wito ulio wazi, ubishani wa watu hawa
wenye shaka shaka ni baat'ili mbele ya Mola wao Mlezi. Na juu yao ipo ghadhabu
kali kwa ukafiri wao. Na adhabu chungu inawangojea.
17. Mwenyezi Mungu ndiye aliye teremsha Kitabu cha Muhammad na viliyo
kuwa kabla yake katika Vitabu vya Mitume, vyenye kukusanya Haki na uadilifu.
Na nini cha kukujuvya, pengine wakati wa Saa ya Kiyama ipo karibu na wewe
hujui.
18. Wanahimiza ije Saa ya Kiyama upesi upesi, kwa maskhara, hao wasio
iamini. Na wenye kuiamini wamo katika khofu isitokee. Hao hawaihimizi.
Na wanajua kuwa hiyo ni kweli iliyo thibiti, wala haina shaka. Naye Subhanahu
anazindua kwamba hao wanao bisha kuja kwake bila ya shaka wamo katika upotovu
ulio mbali na Haki.
19. Mwenyezi Mungu, ni mkuu wa kuwafanyia wema waja wake wote. Huwaruzuku
awatakao kama anavyo taka. Naye ni Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye nguvu
asiye shindika.
20. Mwenye kutaka kulipwa kwa a'mali yake thawabu za Akhera atalipwa
mara mbili ujira wake. Na mwenye kutaka kwa a'mali yake starehe ya dunia
tu, basi tutampa fungu lake hilo, na huko Akhera hatakuwa na fungu lolote
la thawabu.
21. Kwani wao wanao miungu walio watungia dini nyengine asiyo iamrisha
Mwenyezi Mungu? Hayakuwa hayo! Na lau halikwisha tangulia agano la kuakhirisha
hukumu mpaka Siku ya Kiyama, basi bila ya shaka pangeli hukumiwa
baina ya makafiri na Waumini hapa hapa duniani. Na hakika walio jidhulumu
nafsi zao kwa ukafiri watapata adhabu yenye machungu makali.
22. Ewe unaye semezwa! Utawaona Siku ya Kiyama hao walio jidhulumu
nafsi zao kwa ushirikina wamo katika khofu kuogopa malipo ya ushirikina
wao, nayo yatawateremkia tu hapana hivi wala hivi. Na utawaona wenye kuamini
na wakatenda mema wamestarehe katika mwahali mzuri kabisa katika Pepo.
Humo watapata neema wazitamaniazo kwa Mola wao Mlezi. Hayo ndiyo malipo
makubwa, na ndio fadhila kubwa ya kutarajiwa.
23. Hiyo fadhila kubwa ndiyo ambayo Mwenyezi Mungu amewabashiria
waja wake Waumini, wat'iifu. Ewe Mtume! Sema: Mimi sitaki kwenu ujira kwa
kufikisha huu Ujumbe, isipo kuwa mumpende Mwenyezi Mungu na Mtume wake
katika kujikurubisha kwenu kwake Yeye Subhanahu, kwa vitendo vyema. Na
mwenye kutenda ut'iifu Mwenyezi Mungu atampa ujira mara mbili. Hakika Mwenyezi
Mungu ni mkunjufu wa maghfira kwa wenye madhambi, ni Mwenye shukrani kwa
waja wake wenye vitendo vyema.
24. Je! makafiri wanasema Muhammad anamzulia uwongo Mwenyezi
Mungu? Mwenyezi Mungu akipenda atakufungia moyo wako usubiri maudhi
yao, na tuhuma yao kuwa unamzulia Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi
Mungu ataondoa na ataushinda ukafiri na ataupa nguvu Uislamu na ataudhihirisha
kwa wa'hyi alio mteremshia Mtume wake s.a.w., kwani - Yeye- Mwenyezi Mungu
anajua yote yaliomo ndani ya nyoyo zenu nyote.
25. Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kupokea toba kwa watu
wanao mt'ii hata kwa makosa yaliyo zaidi kuliko yale wanayo ombea toba.
Na Yeye ndiye anaye samehe madhambi yote isipo kuwa shirki, kwa kufadhili
na kurehemu; na anayajua myatendayo ikiwa ya kheri au shari.
26. Na huwaitikia Waumini kwa wanayo yaomba, na huwazidishia juu
ya hayo wanayo yaomba. Na makafiri watapata adhabu yenye kufikia ukomo
wa ukali na uchungu.
27. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wakunjulia waja wake wote,
kama watakavyo, basi bila ya shaka wangeli panda kiburi katika ardhi wakafanya
dhulma. Lakini Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humdhikisha
amtakaye, kwa mujibu wa hikima yake. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua vyema
mambo yote ya waja wake, ya siri na dhaahiri. Basi Yeye humkadiria kila
mmoja kwa linalo msilihi kwa mujibu wa hikima yake.
28. Na Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye anaye iteremsha mvua inayo
waokoa na ukame baada ya kwisha kata tamaa na kuzidi kiangazi, kuwa ni
rehema kwa waja wake. Na Yeye hueneza baraka za mvua katika mimea, na miti
ya matunda, na wanyama, na nyanda, na milima. Na Yeye, peke yake, ndiye
Mwenye madaraka ya kuyapanga mambo yote ya waja wake, na ndiye wa kuhimidiwa
kwa neema zake, na vitendo vyake vyote.
29. Na katika dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu kuumba atakacho ni
huku kuumba mbingu na ardhi kwa nidhamu iliyo pangwa; na kuumbwa vilivyo
tenganishwa humo na kuenezwa wanayama wanao onekana na wengineo. Na Mwenyezi
Mungu aliye hakikisha uweza wake kwa kuumba hivyo vilio tajwa ni Muweza
wa kuwakusanya wote katika wakati autakao kuwafufulia kwa ajili ya malipo.
30. Na msiba wowote unao kusibuni mnao uchukia ni kwa sababu ya maasi
yenu. Na anayo yasamehe Mwenyezi Mungu duniani au akayachukulia ahadi humo,
basi Mwenyezi Mungu ni Karimu; hatokuwa tena wa kuadhibu kwa hayo Akhera.
Na Kwa hivi ametakasika na dhulma, na amesifika kwa rehema kunjufu.
31. Wala nyinyi hamwezi kumshinda Mwenyezi Mungu na kumzuilia asilete
masaibu duniani kuwa ni adhabu kwa ajili ya maasi yenu, na hata mkikimbia
vipi. Na wala hamna asiye kuwa Mwenyezi Mungu wa kukurehemuni pindi ikikuteremkieni
balaa, wala hamna wa kukunusuruni nayo.
32. Na katika dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu, ni majahazi yaendayo
katika bahari kama vilima virefu kwa ukubwa wake.
33. Mwenyezi Mungu akipenda huutuliza upepo kukawa shuwari; basi
majahazi yaliyo thibiti juu ya bahari hutulia hayendi huko yendako. Hakika
huko kwenda kwao na kusimama kwao kwa amri ya Mwenyezi Mungu ni dalili
wazi juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu. Wanayazingatia hayo Waumini wenye
kusubiri wakati wa dhiki, na wenye kushukuru wakati wa furaha.
34. Au akayateketeza hayo majahazi kwa sababu ya madhambi ya walio
panda, kwa kuwapelekea upepo wa kimbunga. Na Mwenyezi Mungu akipenda anasamehe
mengi; kwa kuwa hawaadhibu kwa kuzuia upepo na kuleta shuwari, au kwa kuleta
kimbunga cha kuwazamisha.
35. Mwenyezi Mungu, Subhanahu, hufanya hayo ili Waumini wapate kuzingatia,
na wajue wale wanao zirudi Ishara zake kwa upotovu kwamba wao wamo katika
mkono wake, wala hawana pa kuikimbia adhabu yake.
36. Msidanganyike na starehe za dunia. Kwani enyi watu! Yote mliyo
pewa, mali, wana, na vyenginevyo, ni starehe zenu za maisha ya duniani.
Na aliyo yaandaa Mwenyezi Mungu katika neema za Peponi ni bora na zinadumu
zaidi kwa wenye kuamini, na kumtegemea Muumba wao na Mlezi wao wa pekee;
37. Na wanao jitenga mbali na kupanda madhambi makubwa makubwa aliyo
yakataza Mwenyezi Mungu, na madhambi yote yaliyo zidi ubaya, na pindi wakichochewa
kwa kufanyiwa mabaya katika mambo ya dunia yao, wao wenyewe wakawa mbele
kuanza kusamehe ili kuleta masikilizano;
38. Na wanao uitikia wito wa Muumba wao na Mlezi wao, na wakamuamini,
na wakazihifadhi Sala zao, na ukawa mwendo wao ni kushauriana katika mambo
yao ili upatikane uadilifu katika jamii zao, bila ya mtu mmojapo au kikundi
cha wachache kutaka kuwatumilia mabavu wenginewe, na wakawa wanatoa kwa
njia za kheri kutokana na neema alizo mneemesha Mwenyezi Mungu;
39. Na wale ambao anapo wavamia mwenye kudhulumu wao wanajitetea
nafsi zao kuupinga ule uvamizi wake.
40. Na malipo ya mwovu, ni kumtendea uovu kama wake, kwa kufuata
uadilifu. Lakini mwenye kusamehe uovu alio tendewa, naye anaweza kulipiza,
na akaleta masikilizano baina yake na yule khasimu yake, kwa kujenga mapenzi,
basi thawabu zake ziko kwa Mwenyezi Mungu. Hapana anaye zijua kadiri yake
isipo kuwa Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu hawarehemu wavamizi wanao fanya
uadui katika haki za watu, kwa kuzikiuka sharia za Mwenyezi Mungu.
41. Hakika wanao wapa adhabu wavamizi kama wanavyo fanya uadui wao,
hao hawaingiliwi wala hawalaumiwi.
42. Bali lawama na kushikwa haki ni juu ya wanao fanya uadui, wakadhulumu
watu, na wakafanya kiburi katika nchi, na wakafisidi humo bila ya haki.
Hao watapata adhabu yenye uchungu mkali.
43. Ninaapa: Bila ya shaka, mwenye kuvumilia kudhulumiwa, akamwachilia
aliye mdhulumu, wala asiitetee nafsi yake, pindi ikiwa huko kusamehe kwenyewe
hakuupalilii ufisadi ukapata nguvu katika nchi, hakika hayo ni katika mambo
ambayo yanatakikana mwenye akili ajilazimishe kuyatenda.
44. Na mwenye kuipotea Njia ya Uwongofu kwa kuwa hana ujuzi mwema,
basi hana wa kumnusuru isipo kuwa Mwenyezi Mungu, ndiye wa kumwongoa na
wa kumkinga na adhabu. Na, ewe unaye semezwa! Utaona Siku ya Kiyama wale
wenye kudhulumu watakapo iona adhabu ya Akhera wanamuuliza Mola wao Mlezi,
watumie mbinu gani wapate kurejea duniani, ili wapate kutenda mema, siyo
waliyo kuwa wakiyatenda kwanza?
45. Na kadhaalika, utawaona walio dhulumu, wakipelekwa Motoni, wamenywea
kwa sababu ya unyonge ulio tokana na hivyo vitisho walivyo vikuta, wakitupia
jicho kwa kificho kwenye huo Moto kwa kuukhofu vituko vyake. Na hapo Waumini
watasema: Hakika walio khasiri kweli ni hao walio dhulumu nafsi zao kwa
ukafiri wao, na wakawakhasiri wake zao na watoto wao na jamaa zao kwa mfarakano
walio usabibisha baina yao. Na Mwenyezi Mungu ananabihisha kwamba wenye
kudhulumu watakuwa katika adhabu ya milele.
46. Na wala hawatakuwa wa kuwanusuru kutokana na ile miungu ya uwongo
walio kuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, na walio kuwa wakiit'ii
katika kumuasi Mwenyezi Mungu, waje kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Na mwenye kupotea Njia ya Haki kwa kuto kuwa na ujuzi, basi hatokuwa
na njia ya kumwokoa na mwisho muovu.
47. Enyi watu! Kimbilieni kuitikia aliyo kuitieni Mtume wa Mwenyezi
Mungu aliye kuumbeni na akakuleeni, nayo ni Imani na Ut'iifu, kabla uhai
haujamaliza fursa ya kutenda vitendo, na ikafika Siku ya Hisabu ambayo
Mwenyezi Mungu hairudishi nyuma tena baada ya kwisha ihukumia. Siku hiyo
hamtakuwa na pa kukimbilia pa kukuhamini na adhabu, wala hapana cha kuzuia
kitakacho kufikieni.
48. Wakipuuza washirikina kukuitikia wewe, ewe Mtume, basi usihuzunike.
Kwani wewe si mwangalizi wao kwa hayo wanayo yatenda. Wewe umelazimishwa
kufikisha Ujumbe tu, na hayo umeyabainisha wazi. Na tabia ya watu tukiwapa
wasaa hupanda kiburi. Na ukiwasibu msiba kwa sababu ya maasi yao, mara
wanasahau neema, wanahuzunika kwa kuteremkiwa na balaa, na wanaingia katika
kufuru.
49. Ni wa Mwenyezi Mungu peke yake Ufalme wa mbingu na ardhi, kwa
kuumba, kuudabiri, na kuusarifu. Yeye anaumba atakacho. Humtunukia amtakaye
wana wa kike, na akamtunukia amtakaye wana wanaume bila ya wanawake.
50. Na Yeye Subhanahu humfadhili amtakaye kwa kumchanganyia wanaume
na wanawake, na akamfanya amtakaye bila ya mtoto yeyote. Hakika Mwenyezi
Mungu anajua vyema kila kitu. Ni Muweza wa kutenda kila akitakacho.
51. Wala haimfalii mtu kusemezwa na Mwenyezi Mungu ila iwe kwa Wahyi
(Ufunuo) kwa kumtilia ilhamu katika moyo wake, au usingizini, au
kwa kusikia maneno ya Kiungu bila ya kumwona Asemaye, au kwa kutumwa Malaika
akaonekana sura yake, na akasikilizana sauti, akamfunulia Nabii kwa idhini
ya Mwenyezi Mungu kama atakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtenda nguvu,
basi haziwiliki Mwenye kupita ukomo hikima yake katika kuendesha mambo
yake na kupanga kwake.
52. Na kama tulivyo wafunulia Mitume kabla yako, basi tumekufunulia
nawe, ewe Mtume, hii Qur'ani ili ihuishe nyoyo kwa amri yetu. Kabla ya
kuletewa wewe hii ulikuwa hujui nini Qur'ani, wala hujui Sharia za Imani.
Lakini tumeifanya Qur'ani kuwa ni Nuru Kubwa ya kuwaongoza wenye kukhiari
Uwongofu. Na wewe bila ya shaka utakuwa ukiwaitia watu kwa hii Qur'ani
kwenye Njia Iliyo Nyooka.
53. Njia ya Dini ya Mwenyezi Mungu ambaye ndiyo vyake Yeye tu peke
yake, vyote viliomo mbinguni na katika ardhi, kwa kuumba, na kupanga, na
kuendesha. Naye ananabihisha, Subhanahu, kwamba kwake Yeye peke yake ndio
yanarejea mambo yote.