2. Kitabu hichi ni mteremsho wa namna ya peke yake, kutokana na Mneemeshaji
wa neema kubwa na neema ndogo.
3. Kitabu hichi ni namna ya peke yake kwa uzuri wake kwa matamshi
na ibara yake ya utungaji, na kwa maana inavyo pambanua baina Haki na baat'ili,
na bishara na onyo, na kuzitengeneza nafsi, na kupiga mifano, na kubainisha
hukumu. Nacho kinasomwa kwa ulimi wa Kiarabu, chepesi kukifahamu kwa watu
wanao jua.
4. Chenye kuwapa khabari njema Waumini wenye kutenda kuwa watapata
neema iliyo andaliwa kwa ajili yao, na kuwakhofisha wanao kanusha kuwa
watapata adhabu chungu iliyo andaliwa kwa ajili yao. Lakini wengi walikitupilia
mbali, wala wasinafiike nacho, kama kwamba hawakusikia.
5. Na makafiri wakamwambia Mtume s.a.w.: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko
vizito kwa hayo unayo tuitia yaliyo khusu Tawhidi (Upweke) wa Mwenyezi
Mungu. Na masikioni mwetu mna uziwi, basi hayasikii hayo unayo tulingania.
Na baina yetu na wewe lipo pazia nene linalo tuzuia kukubali hayo uliyo
tuletea. Basi fanya utakalo, na sisi tunafanya tutakalo.
6,7. Ewe Mtume! Waambie: Hakika mimi si chochote ila ni mtu mfano
wenu nyinyi, napata Wahyi (Ufunuo) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwamba wa
kuabudiwa kwa haki na nyinyi ni Mungu Mmoja tu. Basi fuateni Njia Iliyo
Nyooka ya kwendea kwake! Na mtake kwake msamaha kwa madhambi yenu. Na washirikina
wasio toa Zaka kuwapa wanao stahiki watapata adhabu kali. Na wao tu, si
wenginewe, ndio wanao kataa kuwa upo uhai wa Akhera.
8. Hakika Waumini wanao tenda mema watapata malipo mazuri yasiyo
katika.
9. Ewe Mtume! Waambie hawa washirikina: Ama nyinyi mnastaajabisha!
Mnamkataa Mwenyezi Mungu aliye iumba ardhi kwa siku mbili,
na huku juu ya hayo, mnamfanyia washirika wa kushirikiana naye huyo Muumba
ardhi, Mmiliki wa walimwengu wote na Mlezi wao?
Zimetajwa Siku moja au Siku nyingi katika Sura nyengine. Katika
Surat Al-Hajj, Aya 47 Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na kwa hakika siku
moja kwa Mola wako Mlezi ni kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi."
Na katika Surat Assajdah, Aya 5 amesema Mtukufu: "Anapitisha mambo yote
yaliyo baina ya mbingu na ardhi, kisha yanapanda kwake kwa siku moja tu
ambayo kipimo chake ni miaka elfu mnayo hisabu." Na katika Surat Al-Ma'arij
Mtukufu amesema: "Malaika na Roho hupanda kwake katika siku iliyo kadiri
yake ni miaka elfu khamsini."
Maoni ya kitaalamu: Vipimo vya wakati wanavyo vitumia watu vimefungamana
na dunia na inavyo zunguka juu ya msumari-kati wake na kulizunguka jua.
Mtu akitoka kwenye ardhi (dunia) akenda kwenye sayari nyengine za mbinguni
vipimo hivyo vya nyakati vinabadilika kwa kuzidi au kwa kupungua. Na hizi
Aya tukufu zinaonyesha ishara ya ukweli huu wa ki-ilimu, na ya kwamba zama
au nyakati ni jambo la mlinganisho tu.
Na bila ya shaka ipo miaka ya ki-ilimu ya Falaki ya kulinganisha
yenye kumkinika kuifarikisha baina yao. Mwaka wa ki-jua wa duniani huhisabiwa
kwa kupimwa wakati ambao dunia inachukua kulizunguka jua kwa ukamilifu
mnamo siku 365, na ilhali sayari zilio karibu na jua kama U't'aarid (Mercury)
humaliza safari yake ya kulizunguka jua mnamo siku 88, na upande mwengine
sayari ya Blutu (Pluto) ambayo ndiyo sayari iliyo mbali mno na jua, na
ndiyo inazunguka taratibu mno inachukua kuzunguka kwake mnamo miaka 250
kwa mujibu wa miaka yetu sisi.
10. Naye Mwenyezi Mungu amesimamisha juu ya ardhi milima iliyo simama
imara ili isiyumbe nanyi; na akakithirisha humo kheri nyingi, na akakadiria
humo riziki kwa watu wake, kwa mujibu wa hikima yake, mnamo siku nne. Na
nyinyi, juu ya haya, mnakwenda kumwekea washirika? Na Yeye amekadiria
kila kitu bila ya upungufu wala kuzidi. Kufafanua huku katika uumbaji wa
ardhi na vilio juu yake ni maelezo kwa hao wanao uliza.
11. Kisha amekhusisha uweza wake na kuumba mbingu, nazo zilikuwa
kama moshi, basi zikawapo. Na kuumba kwake mbingu na ardhi kwa mujibu wa
mapendo yake ni jambo jepesi kwake, ni kama kukiambia kitu: Njoo ukipenda
usipenda, nacho kikat'ii.
12. Na akatimiza kuumba mbingu saba mnamo siku mbili nyengine. Na
akaweka katika kila mbingu alicho kiandalia na ilivyo pelekea hikima yake.
Na akaipamba mbingu ya karibu na dunia kwa nyota zinazo ng'ara kama taa,
kwa ajili ya uwongofu wasisikilize mashetani khabari za walio juu. Kuumba
huko vilivyo ni mpango wa Mwenyezi Mungu asiye shindika, Mwenye kuzunguka
kila kitu.
13. Basi washirikina wakipuuza Imani baada ya kuwekewa wazi dalili
zake, wewe, Mtume, waambie: Nimekuonyeni msije kupatilizwa kwa adhabu
kali kama iliyo wateketeza kina A'di na Thamudi.
14. Walijiwa A'di na Thamudi na hiyo adhabu walipo watokelea Mitume
pande zote. Hawakuacha njia ya kuwaongoza ila waliipitia, na wakawaambia:
Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu. Wao wakasema: Lau Mwenyezi Mungu angeli
taka kumtuma Mtume basi angeli tuteremshia Malaika. Basi sisi hakika tunakataa
hayo ya Tawhidi na mengineyo mliyo kuja nayo nyinyi.
15. Ama kina A'di walipandwa na kiburi katika nchi bila ya haki ya
kuwa na kiburi hicho. Na walisema kwa kughurika na nafsi zao: Nani huyo
anaye tushinda sisi kwa nguvu? Ama ajabu watu hawa! Wanasema hayo na wao
hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ana nguvu zaidi kuwashinda wao?
Na wao walikuwa wakizikanya Ishara zetu!
16. Tukawapelekea upepo wenye sauti kali katika siku korofi, ili
tuwaonjeshe adhabu ya kuwafanya wawe madhalili wanyonge katika maisha ya
duniani. Na ninaapa kuwa bila ya shaka adhabu ya Akhera itakuwa ya hizaya
zaidi, wala wao siku hiyo hawatapata wa kuwasaidia.
17. Na ama kina Thamudi tuliwabainishia njia ya kheri na njia ya
shari. Lakini wao walikhiari upotovu kuliko uwongofu, ikawatwaa radi
iliyo waunguza kwa madhila na unyonge, kwa sababu ya madhambi waliyo yachuma.
18. Na tukawaokoa kutokana na adhabu hii wale walio amini, na wakawa
wanamcha Mwenyezi Mungu na wanaiogopa adhabu yake.
19. Ewe Nabii! Siku watakapo kusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kupelekwa
Motoni, wakawa wa mwanzo wao wanakutana na wa mwisho wao, ili ipate hoja
ilazimike juu ya wote,
20. Mpaka watakapo ufikilia Moto na wakaulizwa juu ya madhambi
waliyo yatenda duniani, na wao wakakataa, yakawashuhudilia masikio yao,
na macho yao, na ngozi zao kwa waliyo yatenda wao,
21. Na hao maadui wa Mwenyezi Mungu wakaziambia ngozi zao: Kwa nini
mmetushuhudilia? Na ngozi zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu aliye
tamkisha kila kitu. Na Yeye ndiye aliye kuumbeni hapo mwanzo kabla hamjawa
chochote. Na kwake Yeye, peke yake, ndio mtarejea baada ya kufufuliwa,
akuhisabieni mliyo kwisha yatanguliza katika vitendo.
22. Wala nyinyi hamkuwa mkiweza kuficha vitendo vyenu viovu hata
viungo vyenu visivione na ikawa macho yenu, na masikio yenu na ngozi zenu,
vyote hivyo vikakushuhudilieni. Lakini nyinyi mlikuwa mkidhani kuwa Mwenyezi
Mungu hajui mengi katika vitendo vyenu, kwa sababu mkivifanya kwa uficho.
23. Lakini dhana mbovu mliyo kuwa mkimdhania Mola wenu Mlezi imekuhilikini,
na kwa hivyo mmekuwa Siku ya Kiyama katika wenye kukhasiri vibaya mno.
24. Basi hata wakijizuia machungu yao, Moto ndio mwisho wao,
na makaazi yao ya daima. Na wakitaka kumridhi Mwenyezi Mungu sasa hawakubaliwi
hayo matakwa yao.
25. Nasi tumewaandalia duniani marafiki waharibifu, na wao wakawazainishia
mbele yao mambo ya Akhera, basi wakawaghuri kwamba ati hakuna kufufuliwa
wala kuhisabiwa, na wakawapambia pia mambo ya duniani ili wastarehe nayo.
Na neno la adhabu lilio wapata mataifa yaliyo kwisha pita miongoni
mwa majini na watu walio kuwa kama wao, likawathibitikia na wao kwa
sababu ya kukhiari kwao upotovu badala ya uwongofu. Hakika watu hao wote
walikuwa katika walio khasiri khasara iliyo timia.
26. Makafiri wakaambizana wenyewe kwa wenyewe: Msiisikilize hii Qur'ani,
na inapo somwa nyie leteni porojo lisio kuwa na maana, ili pasiwepo mtu
wa kuisikia wala kunafiika kwayo, asaa kwa hivyo mkamshinda Muhammad.
27. Tunaapa: Bila ya shaka tutawaonjesha walio kufuru adhabu kali
kwa vitendo vyao, na khasa kwa hivi kuipiga vita Qur'ani. Na bila ya shaka
tutawalipa malipo maovu kabisa kwa vitendo vyao.
28. Hizo adhabu zilizo tajwa ni malipo wanayo stahiki maadui wa Mwenyezi
Mungu - Moto walio andaliwa katika makaazi ya kuishi milele, kuwa ni malipo
kwa kule kuzikataa mfululizo Ishara za Mwenyezi Mungu na hoja zake.
29. Na makafiri watasema, nao wamo Motoni: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe
hayo makundi ya majini na watu walio tupoteza ili tuwaweke chini ya nyayo
zetu, wawe katika watu wa chini kabisa.
30. Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, kwa kuukubali
Upweke wake, kisha wakasimama sawa sawa juu ya sharia zake, Malaika watawateremkia
mara kwa mara wakiwaambia: Msikhofu kukuteremkieni shari, wala msihuzunike
kuwa mtakosa kheri, na furahini kuwa mtapata Pepo mliyo ahidiwa kwa ndimi
za Manabii na Mitume.
31,32. Na Malaika watawaambia: Sisi ni wasaidizi wenu katika maisha
ya duniani kwa kukuungeni mkono, na Akhera kwa kukuombeeni shafaa na kukutukuzeni.
Na huko Akhera mtapata kila cha ladha na kizuri kinacho pendwa na nafsi
zenu, na mtapata kila mnacho kitamani kuwa ni takrima, na maamkio
yanayo toka kwa Mola Mlezi Mkunjufu wa maghfira na rehema.
33. Hapana mwenye kauli nzuri zaidi kuliko mwenye kulingania Tawhid
ya Mwenyezi Mungu na ut'iifu wake, na pamoja na hayo, akatenda vitendo
vyema, na akasema kwa kuungama itikadi yake: Hakika mimi ni miongoni mwa
Waislamu, yaani wenye kunyenyekea amri za Mwenyezi Mungu.
34. Haziwezi kuwa sawa tabia njema na tabia mbovu. Pinga uovu ukikujia
kutokana na adui kwa tabia iliyo bora kuliko yake. Hapo matokeo yake ni
huyo ambaye uliye kuwa na uadui naye atakuja kuwa kama mwenzio wa kukunusuru
mwenye moyo safi.
35. Na hawaruzukiwi tabia hii, ya kulipa wema kwa uovu, ila
wale wenye khulka ya kusubiri, na hawaruzukiwi hayo ila wenye fungu kubwa
la tabia ya wema na ukamilifu wa nafsi.
36. Na akitokea Shetani akakutia wasiwasi kukuachisha hayo uliyo
amrishwa, ewe unaye semezwa, basi jilinde naye kwa Mwenyezi Mungu. Hakika
Mwenyezi Mungu kusikia kwake na kujua kwake kumezunguka kila kitu. Na Yeye
atakulinda naye.
37. Na katika dalili za uweza wake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni huu
usiku na mchana, na jua na mwezi. Msilisujudie jua wala mwezi, kwani hivyo
ni katika Ishara zake tu. Bali msujudieni Yeye Mwenyezi Mungu peke yake,
aliye umba jua, na mwezi, na usiku, na mchana, ikiwa nyinyi kweli mnamuabudu
Yeye peke yake.
38. Ikiwa washirikina watajiona wakubwa hawafai kufuata amri yako,
basi wewe usiudhike. Kwani hao walio kwa Mola wako Mlezi kwenye utakatifu
wake, nao ni Malaika, wanamtakasa Yeye na kila upungufu katika kila wakati,
usiku na mchana, wakimsafia ibada Yeye tu, wala hawachoki kumsabihi.
39. Na katika dalili za uweza wake, Mtukufu, ni kwamba unaona, wewe
unaye weza kuona, ardhi kavu. Tukiiteremshia maji inatikisika kwa mimea,
na inaumuka na kuja juu. Hakika huyo aliye ihuisha ardhi iliyo kwisha kufa
ndiye aliye elekea kuhuisha wafu katika hayawani. Yeye ni mtimilivu wa
uweza juu ya kila kitu.
Aya hii inabainisha kwamba mawadi za mbolea ambazo ni chumvi chumvi
zisio na uhai, pindi zipatapo maji ya mvua, huyayuka, na kwa hivyo husahilika
kufikilia kwenye mbegu za mimea na mizizi yake. Hapo hugeuka kuingia
katika khalaya (Cells) na mifumo na viungo vilio hai. Na kwa hivyo vinaonekana
kuwa ni hai. Na ukubwa wake hukua na kuzidi kwa kuingiana na kukuzwa na
mimea.
40. Hakika hao wanao iacha Njia iliyo sawa kwa mintarafu ya Ishara
zetu na wakaitupilia mbali kwa kuikadhibisha, mambo yao hayatupotei Sisi
wala hayo wanayo yakusudia. Nasi tutawalipa kama wanavyo stahiki. Kwani
anaye tupwa katika Moto ni bora au yule anaye kuja naye hali katulia
Siku ya Kiyama kwa kuokoka kwake na kila ovu? Kabisa hao hawalingani. Waambie
kwa kuwaahidi: Fanyeni mtakavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzunguka
kila kitu kwa jicho lake, naye atamlipa kila mmoja kwa a'mali yake.
41,42. Hakika wanao ikataa Qur'ani Tukufu inapo wajia bila ya kuzingatia,
watapata adhabu ambayo hapana mtu anaye weza kuikadiria. Wao wameipinga
Qur'ani nacho hakika ni Kitabu kisicho kuwa na mfano, kinamshinda kila
mwenye kukipinga, hakiingiliwi na upotofu usio kuwa na asli kwake kwa upande
wowote ule, kimeteremka kwa kukufuatana kutokana na Mungu aliye takasika
na upuuzi, Msifiwa kwa wingi wa sifa kwa neema alizo zitoa.
43. Ewe Muhammad! Huambiwi wewe na maadui wako ila kama walivyo ambiwa
Mitume wa kabla yako na maadui wao, nayo ni matusi na kuambiwa mwongo.
Hakika Muumba wako na Mlezi wako ana msamaha mwingi, na ni Mwenye kuadhibu
kwa machungu makubwa. Basi Yeye humghufiria mwenye kutubu kwake, na humtesa
mwenye kushikilia na inda yake.
44. Na lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni, kama walivyo
pendekeza baadhi ya hao wanao kera, basi bila ya shaka wangeli sema: Lau
zingeli bainishwa Aya zake kwa ulimi tunao ufahamu! Kitabu hichi cha lugha
ya kigeni, na huyu mkhubiri wake ni Mwaarabu! Yawaje haya? Ewe Mtume! Waambie:
Hii Qur'ani ni hivyo hivyo kama walivyo teremshiwa Waumini, si wengineo,
kuwa ni Uwongofu na Poza kwa Waumini; kiwaokoe na ubabaishi, na kiwaponyeshe
na shaka shaka. Na wasio amini wamekuwa kama katika masikio yao pana kizuizi,
uziwi, nayo hii Qur'ani kwao wao ni upofu, hawaoni chochote ndani yake
ila fitna tu. Hao makafiri ni kama wanao itwa waiamini kwa umbali kabisa.
Hawausikii wito huo.
45. Ninaapa: Kwa hakika tulimpa Musa Taurati, na watu wake wakakhitalifiana
kwayo. Na lau ingeli kuwa hukumu ya Mola wako Mlezi haikuakhirishwa, ewe
Muhammad, mpaka muda maalumu kwake, basi hapana shaka pange amuliwa hukumu
baina yako na hao kwa kuwang'olea mbali wanao kanusha. Na hakika makafiri
katika kaumu yako wamo katika shaka na Qur'ani, na hiyo inawatia dhiki
na wasiwasi.
46. Mwenye kutenda vitendo vyema ujira wake ataupata mwenyewe, na
mwenye kutenda uovu madhambi yake yatakuwa juu yake. Na Mola wako Mlezi
si mwenye kuwadhulumu waja wake, hata amtese mtu kwa dhambi za mwengine.
47. Kwa Mwenyezi Mungu peke yake ndio unarejea ujuzi wa kusimama
Saa ya Kiyama. Matunda hayatoki kwenye vifuniko vyake, wala mwanamke hachukui
mimba wala hazai ila awe Yeye anajua. Na kumbuka siku ambayo Mwenyezi Mungu
atawaita washirikina, kwa kuwakebehi, awaambie: Wako wapi hao washirika
wangu mlio kuwa mkiwaomba badala yangu? Watasema kwa kutaadhari: Ewe Mwenyezi
Mungu! Tunakujuvya kuwa sisi hatuna wa kushuhudia kuwa wewe una mshirika
yeyote.
48. Na hao miungu ya ushirikina walio kuwa wakiwaabudu watawapotea,
na waliyakinika kuwa hawana pa kukimbilia.
49. Mwanaadamu hachoki kumwomba Mola wake Mlezi kwa kheri za kidunia.
Ikimpata shari basi huwa mwingi wa kuikatia tamaa kheri, na kuvunjika moyo
hadi, ya kwamba Mwenyezi Mungu hamwitikii dua yake.
50. Tunaapa: Tukimwonjesha mtu neema, kwa fadhila yetu, baada ya
dhara kubwa iliyo msibu bila ya shaka husema: Hii neema niliyo ipata ni
haki yangu mimi. Wala sidhani kuwa Kiyama kitakuja. Na ninaapa ikitokea
nikarejeshwa kwa Mola wangu Mlezi basi na huko kwake bila ya shaka nitapata
malipo mema. Lakini Sisi tunaapa: Hapana shaka tutawalipa walio kufuru,
Siku ya Kiyama, kwa vitendo vyao! Na hapana shaka tutawaonjesha adhabu
kali iliyo rindikwa juu kwa juu!
51. Na tukimneemesha mtu huacha kutushukuru, na akajitenga mbali
na Dini yetu. Na tukimwonjesha shari basi huwa mwingi wa kuomba madua.
52. Ewe Muhammad! Waambie: Hebu nambieni; ikiwa hii Qur'ani imetoka
kwa Mwenyezi Mungu nanyi mkawa mnaikataa, basi nani aliye kuwa mbali mno
na Ukweli kuliko huyo aliye kinyume na Haki?
53. Karibuni hivi tutawaonyesha hao wanao zikataa Ishara zetu zenye
kuonyesha ukweli wako katika pande za mbinguni na ardhi, na katika nafsi
zao wenyewe, mpaka yawadhihirikie ya kwamba uliyo waletea ni Haki tupu
si vinginevyo. Je! Wanakataa kuwa Sisi tunawaletea Ishara hizo? Je!
Haitoshi kuwa Mola wako Mlezi ni Mwenye kukizunguka kila kitu?
54. Ama hakika hawa makafiri wamo katika shaka kubwa kukutana na
Mola wao Mlezi, kwa sababu ya kuwa hawaamini kufufuliwa. Ama hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kukizunguka kila kitu kwa ujuzi wake na uweza wake.