2,3. Hii Qur'ani imeteremshwa kutokana na Mwenyezi Mungu, Mwenye
nguvu, Mwenye kushinda, Mwenye kuvizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake, naye
ni Mwenye kupokea toba ya wenye kutubia, na Mkali wa kuadhibu, Mwenye neema
nyingi; hapana wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa Yeye peke yake. Ni kwake
Yeye peke yake ndio marejeo na mafikio.
4. Hawazibishi Ishara za Mwenyezi Mungu zenye kuonyesha dalili zake
ila walio makafiri. Basi yasikukhadae huko kutanga tanga kwao katika nchi
ukadhani kuwa Mwenyezi Mungu kawasahilishia mambo yao juu ya ukafiri wao.
5. Kabla ya hawa walikufuru kaumu ya Nuhu, na makundi mengine yaliyo
jumuika kuwapinga Mitume baada ya kaumu yake Nuhu. Na hao wakawa na pupa
ya kumletea shari Mtume wao wamtie nguvuni, na wakawa wanajadiliana katika
upotovu usio kuwa na ukweli wowote, ili kwa upinzani wao wapate kuipindua
haki iliyo kwisha thibiti. Basi Mimi nikawashika, nikawatia katika adhabu
ya kuwang'olea mbali. Hebu angalia ilikuwaje adhabu yangu juu yao!
6. Na kila lilipo thibiti neno la adhabu juu ya mataifa yaliyo wakadhibisha
Manabii wao, basi kadhaalika lilithibiti neno la Mola wako Mlezi juu ya
hao wanao kukanusha wewe, ewe Muhammad, kwani hao ni watu wa Motoni, kwa
kuwa wamekhiari ukafiri kuliko Imani.
7. Malaika wanao beba A'rshi, na wenye kuizunguka, wanamtakasa Mwenye
kumiliki mambo yao na Mlezi wao, wanamtakasa kutokana na kila upungufu,
kwa mtakaso ulio lingana na sifa zake. Na wanamuamini, na wanamwomba maghfira
awaghufirie Waumini, huku wakisema: Ewe Mola wetu Mlezi! Rehema yako imeenea
kila kitu, na Ujuzi wako umezunguka kila kitu, basi yasamehe makosa ya
walio rejea kwako, na wakaifuata Njia yako, na waepushe na adhabu ya Motoni.
8. Na Malaika hawa husema: Ewe Mola wetu Mlezi! Waingize Waumini
katika Mabustani ya Milele ulio waahidi kwa ndimi za Mitume wako, na pia
waingize pamoja nao walio wema katika wazazi wao, na wake zao, na dhuriya
zao. Hakika wewe peke yako ndiye Mwenye kushinda, wala hushindiki; Mwenye
hikima usiye kosa.
9. Na husema katika dua zao: Waepushe Waumini malipo ya madhambi
yao, na unaye muepusha Wewe na malipo ya madhambi yake Siku ya Malipo basi
hakika ndio umemrehemu kwa fadhila yako. Kuepushwa na malipo ya madhambi
ndio ushindi ulio fikilia ukomo mkubwa mno.
10. Hakika walio kufuru watanadiwa waambiwe: Bila ya shaka chuki
ya Mwenyezi Mungu na bughdha yake kwenu ni kubwa kuliko chuki zenu wenyewe
zilizo kupelekeeni mkapata adhabu pale mlipo itiwa kwenda kwenye Imani
mara kwa mara nanyi mkakimbilia kwenye ukafiri.
11. Makafiri watasema: Mola wetu Mlezi! Umetufishe vifo viwili, kifo
kimoja katika uhai wetu wa duniani, na kifo kingine katika uhai wetu wa
Barzakh, (1) yaani kaburini. Na ukatuhuisha mara mbili, mara moja ndiyo
ya uhai wetu wa duniani, na mara ya pili ni wakati wa kufufuliwa kutoka
makaburini. Basi, hebu, ipo njia ya kutoka kwetu kwenye adhabu?
(1) Na huenda yakaonyesha uhai wa Barzakh, ambao ni uhai makhsusi
hatuujui hakika yake, aliyo yataja Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kauli
yake juu ya watu wa Firauni: "Moto wanadhihirishiwa asubuhi na jioni; na
siku itapo fika Saa ya Kiyama patanenwa: Waingizeni watu wa Firauni katika
adhabu kali kabisa." Na kauli yake Mtukufu: "Wala usiwadhanie wale walio
uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali ni wahai, wanaruzukiwa
kwa Mola wao Mlezi."
12. Hiyo ni adhabu mliyo nayo. Kwani mwendo wenu duniani ni kuwa
akitajwa Mwenyezi Mungu peke yake nyinyi mnakufuru, na pindi akishirikishwa
na mwenginewe ndio mnaamini. Na ikiwa huu ndio mwendo wenu basi mnastahiki
kweli malipo ya ushirikina wenu. Basi hukumu ni ya Mwenyezi Mungu Mtukufu
Mkuu ambaye humlipa aliye kufuru kwa anavyo stahiki.
13. Mwenyezi Mungu ambaye anakuonyesheni dalili za uweza wake, basi
anakuteremshieni kwa maslaha yenu maji kutoka mbinguni ambayo ni sababu
ya riziki zenu. Na hapana anaye waidhika kwa haya ila mwenye kurejea akazifikiria
Ishara za Mwenyezi Mungu.
14. Basi muabuduni Mwenyezi Mungu mkimsafia Yeye ibada, na hata walau
wakiichukia makafiri ibada yenu na ikhlasi yenu.
15,16. Mwenyezi Mungu, Mwenye vyeo vya juu, Mwenye A'rshi, huteremsha
Wahyi kwa hukumu yake na amri yake juu ya anaye mteuwa katika waja wake,
ili awaonye watu adhabu ya kwenda kinyume na Mitume Siku ya kukutana viumbe
vyote, Siku ya Hisabu watapo tokeza watu wazi, hapana lifichikanalo kwa
Mwenyezi Mungu, watakuwa wakijisikilizanisha wao kwa wao wito unao tisha:
Ufalme wa nani leo? Na jawabu ya kukata: Wa Mwenyezi Mungu, Mmoja, Mwenye
kutengeka kwa hikima, Aliye pita mipaka kwa nguvu zake!
17. Leo tunailipa kila nafsi kwa iliyo tenda. Hapana dhulma leo kwa
kupunguziwa ujira au kuzidishiwa mateso. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi
kuhisabu kwake, basi hachelewi na wakati wake.
18. Ewe Muhammad! Waonye, Siku ya Kiyama ipo karibu. Siku zitakapo
kuwa nyoyo zipo kooni kwa wingi wa khofu, zimejaa majonzi, haziwezi hata
kuyaelezea. Walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri hawatakuwa na jamaa wala
mwombezi wa kuwat'ii katika amri yao.
19. Na Yeye Subhanahu analijua jicho linalo khuni, na siri zilizo
fichikana vifuani.
20. Na Mwenyezi Mungu anahukumu kwa uadilifu, na hao miungu ya uwongo
wanayo iomba badala ya Mwenyezi Mungu haihukumu chochote, kwa kuwa haiwezi
kitu. Hakika Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kuvizunguka vyote vinavyo
sikia na vinavyo ona.
21. Kwani hao washirikina wamekaa kitako tu wala hawatembei katika
ardhi wakaiona vipi ilikuwa hali ya mataifa yaliyo kuwa kabla yao? Walikuwa
wana nguvu kuliko wao na walijenga zaidi kuliko hawa, nao Mwenyezi Mungu
aliwang'olea mbali kwa madhambi yao, wala hawakuwa na mlinzi wa kuwalinda
na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
22. Na adhabu hiyo iliwateremkia kwa sababu ilikuwa Watume wao wakiwajia
na dalili zilizo wazi, nao wakazikataa, basi Mwenyezi Mungu akafanya haraka
kuwapelekea adhabu ya kuwang'oa. Hakika Yeye ana nguvu kubwa mno, na amefikilia
ukomo katika kuadhibu.
23,24. Ninaapa kuwa tulimtuma Musa na miujiza yetu na ushahidi wenye
uthibitisho ulio wazi kumpelekea Firauni na Hamana na Qaruni, wakasema:
Huyu ni mchawi kwa hiyo anayo dai kuwa ni miujiza, na amepita mipaka kwa
uwongo katika madai yake kuwa yeye ni Mtume aliye toka kwa Mola wake Mlezi!
25. Musa alipo waletea Haki kutoka kwetu, Firauni na wafuasi wake
walio kuwa pamoja naye walisema: Wauweni watoto wa kiume wa hao walio amini
pamoja naye, na waachilieni wahai binti zao! Na vitimbi vya makafiri haiwi
ila kuondoka, na kuangamia, na kupotea.
26. Na Firauni akasema: Nachilieni nimuuwe Musa, naye naamwite huyo
Mola wake Mlezi amwokoe kwangu! Hakika mimi nakhofia asije huyu akaigeuza
dini yenu, enyi watu wangu, au akaeneza fitna katika nchi.
27. Na Musa akamwambia Firauni na watu wake: Hakika mimi nimejilinda
na Mwenye kumiliki mambo yangu ambaye ndiye aliye nilea, na ndiye Mwenye
kumiliki mambo yenu pia, na Mwenye kukuleeni nyinyi kwa neema zake na hisani
zake, nimejilinda na kila anaye jivuna na kutakabari, asiye iamini Siku
ya Hisabu.
28. Akasema mtu mmoja Muumini anaye ficha Imani yake katika watu
wa Firauni, akiwasemeza watu wake: Mnataka kumuuwa mtu kwa sababu anasema:
Mungu wangu ninaye muabudu ni Mwenyezi Mungu, naye amekuleteeni dalili
zilizo wazi zinazo tokana na Mwenye kumiliki mambo yenu na Mlezi wenu?
Na akiwa yeye mwongo, basi uwongo wake ni juu yake yeye peke yake, balaa
ya uwongo wake itamwangukia mwenyewe. Na akiwa ni mkweli baadhi ya adhabu
anazo tutahadharisha nazo zitakuteremkieni nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu
hamwafikishi njia ya uwokovu mwenye kupita mipaka, aliye mwongo mno.
29. Enyi watu wangu! Leo nyinyi mnao ufalme, na ni watu wa juu katika
nchi ya Misri, wala hapana mwenginewe. Lakini ni nani atakaye kukingeni
na adhabu ya Mwenyezi Mungu pindi ikitujia? Firauni akasema: Sikwambiini
rai ila ambayo mimi mwenyewe ninayo itakidi. Na sikuongozeni kwa rai hii
ila njia ya uwongofu.
30,31. Akasema yule mtu aliye amini katika watu wa Firauni: Enyi
watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni isikufikieni siku kama ile siku walipo
jikusanya watu makundi mbali mbali kuwapinga Mitume wao, mfano wa
ada ya kaumu Nuhu, na ya A'di, na ya Thamudi, na mataifa mengine yaliyo
kuja baada yao. Wala Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu waja wake.
32,33. Na enyi watu wangu! Mimi nakukhofieni siku viumbe watapo pigiana
makelele, siku mtapo kimbia kurudi nyuma, hapana wa kukukingeni na Mwenyezi
Mungu. Na mwenye kuachiliwa na Mwenyezi Mungu kupotea - kwa kuwa anamjua
kuwa amekhiari upotovu kuliko uwongofu - basi hatokuwa na mwongozi wa kumwongoa.
34. Ninaapa! Bila ya shaka alikwisha kujieni Yusuf na Ishara zilizo
wazi. Nanyi hamkuacha kuwa na shaka na hayo aliyo kuja nayo kwenu, mpaka
alipo kwisha kufa mkasema: Mwenyezi Mungu hatoleta tena Mtume mwengine
baada ya Yusuf. Mfano wa upotovu kama huu mbaya Mwenyezi Mungu humwacha
kupotea yule aliye pindukia mipaka, mwingi wa mashaka na wasiwasi.
35. Wanao bishana juu ya Ishara za Mwenyezi Mungu bila ushahidi wowote
ulio wajia, humkirihisha mno na kumchukiza Mwenyezi Mungu na Waumini kwa
yale majadiliano waliyo yatilia muhuri. Mfano wa muhuri huu Mwenyezi Mungu
anaupiga juu ya kila moyo ulio takabari juu ya viumbe wenzake, na ukataka
kuwatawala.
36,37. Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee jengo refu nifikilie
njia za mbinguni nipate kumwona huyo Mungu wa Musa. Na mimi nina hakika
huyu ni mwongo kwa anavyo jidai kuwa yeye ati ni Mtume. Mfano wa pumbao
la uwongo kama hivi Firauni alipambiwa uovu wa vitendo vyake, hata akaviona
mwenyewe kuwa ni vizuri, na akazuilika na njia ya haki kwa kukhiari mwenyewe
njia ya upotovu. Na havikuwa vitimbi vya Firauni ila katika upotovu tu.
38. Na akasema yule aliye amini katika watu wa Firauni: Enyi watu
wangu! Nifuateni mimi, nitakuongozeni njia njema!
39. Enyi watu wangu! Haya maisha ya duniani si chochote ila ni kama
starehe ya muda ya mwenye kupanda kipando, inakwisha upesi. Na makaazi
ya Akhera, hayo tu peke yake, ndiyo makaazi ya kudumu.
40. Mwenye kutenda uovu duniani hatolipwa kwa uovu huo huko Akhera
ila kwa mfano wake. Na mwenye kutenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke,
naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi watakapo ruzukiwa bila ya kipimo
cha kuhisabiwa na wenye kuhisabu.
41,42. Na enyi watu wangu! Kwani mimi nina nini? Mimi nakuiteni mfuate
njia za kuokoka, na nyinyi mnaniita niingie Motoni! Mnaniita nimkufuru
Mwenyezi Mungu kwa kumshirikisha Yeye na vitu nisivyo vijua, na hali mimi
nakuitieni mwende kwa Mwenye Nguvu asiye shindwa, Mwingi wa kusamehe madhambi!
43. Bila ya shaka yoyote huyo mungu mnaye niitia nimuabudu hana wito
wowote unao stahiki kuitikiwa la duniani wala Akhera. Na hakika marejeo
yetu sote ni kwa Mwenyezi Mungu, na wenye kupita mipaka ndio watu wa Motoni,
wala si Waumini walio kaa sawa.
44. Basi watakuja jua ukweli wa niliyo kuambieni, na mimi namtegemezea
mambo yangu Mwenyezi Mungu. Hakika jicho la Mwenyezi Mungu limewaenea waja
wake wote, na Yeye ni Mwenye kuwalipa kwa vitendo vyao.
45,46. Mwenyezi Mungu akamlinda yule Muumini katika watu wa Firauni
mateso ya vitimbi vyao, na ikawazunguka watu wa Firauni adhabu mbaya, nayo
ni Moto wanao uingia asubuhi na jioni. Haya ni ya duniani na wapo katika
ulimwengu wa Barzakh, kaburini. Na Siku ya Kiyama, atasema Mwenyezi Mungu:
Waingizeni watu wa Firauni kwenye adhabu iliyo kali kabisa!
47. Ewe Muhammad! Watajie pale wanapo zozana watu wa Motoni humo,
wakawa walio kuwa wanyonge, nao ni wafuasi, wakiwaambia wanao takabari,
nao ni maraisi: "Sisi tulikuwa duniani ni wafuasi wenu, basi je, hamtuchukulii
baadhi ya adhabu ya moto?"
48. Na walio takabari waseme: "Hakika sote sisi tumo humu, sisi na
nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu amehukumu kwa haki baina ya waja. Basi kila
mmoja wetu amepata adhabu aliyo hukumiwa juu yake."
49. Watasema walio Motoni, wanyonge na wakuu, kuwaambia walinzi wa
Jahannamu wakiwaomba msaada: Muombeni Mungu wenu atupunguzie japo siku
moja tupumzike na adhabu.
50. Walinzi wa Jahannamu watawaambia kwa kuwahizi: Kwani hamkunabihika
kwa yaliyo kuwa mkiteremshiwa, na hali walikuwa wakikujieni Mitume na ushahidi
ulio wazi? Na watasema watu wa Motoni: Kwani? Walitujia Mitume na sisi
tukawakadhibisha. Walinzi wakasema: Ikiwa mambo ni hivyo, basi waombeni
nyinyi! Lakini madua ya makafiri hayana ila kupotea bure.
51. Hakika Sisi bila ya shaka tunawanusuru Mitume wetu na Waumini
katika maisha ya duniani kwa kulipiza juu ya maadui wao, na kusimamisha
hoja juu yao; na Siku ya Kiyama watasimama Mashahidi washuhudie kwamba
Mitume wamefikisha Ujumbe wao, na washuhudie kwamba makafiri waliukadhibisha.
52. Siku ambayo madhaalimu hautawafaa udhuru wao kwa yale waliyo
yakosa kuyatenda duniani. Nao watapata laana, yaani watafukuzwa kwenye
rehema, na watapata makaazi maovu kabisa.
53,54. Naapa kwamba tulimpa Musa cha kuongoa kwendea Haki, na tukawarithisha
Wana wa Israili Taurati yenye kuongoa na yenye kuwakumbusha wenye akili
zilio nzima.
55. Ikiwa umejua tuliyo kusimulia, basi subiri, ewe Muhammad, kwa
maudhi yanayo kupata. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kukunusuru wewe
na kuwanusuru Waumini ni kweli isiyo geuka. Na taka maghfira kutoka kwa
Mola wako Mlezi kwa hayo ambayo kwa mnasaba wako wewe huhisabiwa
kuwa ni dhambi. Na mtakase Mola wako Mlezi na kila upungufu kwa mtakaso
unao ambatana na kumsifu jioni na asubuhi.
56. Hakika hao wanao jadili katika dalili za Mwenyezi Mungu bila
ya hoja iliyo tokana naye Yeye Mtukufu, hamna vifuani mwao ila kutaka uluwa,
ubora, wasiifuate Haki, wala huko kutaka kwao uluwa, ubora, hakuwafikishii
walitakalo. Basi wewe iombe Hifadhi kutokana na Mwenyezi Mungu; kwani Yeye
hakika ni Mwenye kuenea kila kitu kusikia kwake na kuona kwake.
57. Ninaapa: Bila ya shaka kuziumba mbingu na ardhi ni jambo kubwa
zaidi kuliko kuwaumba watu. Lakini wengi wa watu wameitupa ilimu, wakawa
hawaamini kufufuliwa juu ya kukubali kwao kwamba Yeye ndiye Muumba mbingu
na ardhi.
58. Na hawawi sawa, kipofu asiyo iona Haki, na mwenye kuijua. Wala
hawawi sawa wema wenye kuamini na wakatenda mema, na muovu wa itikadi na
vitendo. Ni kwa uchache, uchache mno, ndio mnakumbuka, enyi watu!
59. Hakika Kiyama kitakuja tu, hapana shaka yoyote. Na lakini wengi
wa watu hawasadiki.
60. Na anasema Muumba wenu na Mwenye kumiliki mambo yenu yote: Niombeni
nami nitakupeni! Hakika wale wanao takabari hata wakakataa kuniomba wataingia
Jahannamu nao ni madhalili wanyonge.
61. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye kujaalieni usiku mpate kutua
ndani yake mpumzike na kazi, na mchana wenye mwangaza mpate kufanya kazi
ndani yake. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye fadhila kuu juu
ya watu. Lakini watu wengi hawamshukuru juu ya neema zake.
62. Huyo Mwenye kukuneemesheni kwa neema hizi tukufu ndiye Mwenyezi
Mungu, Mwenye kumiliki mambo yenu, Muumba wa kila kitu, hapana wa kuabudiwa
kwa haki ila Yeye. Basi mtaelekea wapi kwa ibada mkimwacha Yeye?
63. Mfano wa kukengeuka huku kuiacha Haki kuendea upotovu, walikengeuka
walio kuwa kabla yenu. Wakazikanya Ishara za Mwenyezi Mungu na wakazikataa.
64. Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye kufanyieni ardhi iwe
ni pahala panapo silihi maisha yenu, na mbingu zikawa ni jengo lilio shikamana.
Na akakadiria kukuumbeni nyinyi, akazitengeneza sura zenu, na akakujaalieni
na umbo zuri lilio nyooka. Na akakuruzukuni katika vitu vya halali mnavyo
viona vitamu. Mneemesha huyo kwa neema hizi ndiye Mwenyezi Mungu
Mola wenu Mlezi. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mwenye kuumiliki ulimwengu
wote, na Mwenye kuulea.
65. Yeye pekee Mwenye uhai wa daima dawamu, hapana wa kuabudiwa kwa
Haki ila Yeye. Basi muelekeeni Yeye kwa kumuomba, mkimsafia ibada Yeye.
Sifa njema zote ni haki iliyo thibiti kwa Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa
viumbe vyote.
66. Ewe Mtume! Sema: Hakika mimi nimekatazwa kuiabudu miungu
mnayo iabudu nyinyi badala ya Mwenyezi Mungu, zilipo nijia hoja kutoka
kwa Mola wangu Mlezi, na nikaamrishwa nimfuate Mwenyezi Mungu Mola Mlezi
wa walimwengu wote katika mambo yangu yote.
67. Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye aliye kuumbeni, enyi wanaadamu,
kutokana na udongo, kisha akaugeuza udongo ukawa tone la manii, kisha akalifanya
tone la manii kuwa pande la damu iliyo gandana, kisha akakutoeni kwenye
matumbo ya mama zenu kuwa ni watoto wachanga. Kisha akaukuza umri wenu
mpaka mkakamilika nguvu zenu na akili, tena ukawa mrefu umri wenu mpaka
mkawa wazee. Na wako kati yenu wanao kufa kabla ya kufikia ujana au uzee.
Na Mwenyezi Mungu akakuumbeni kwa namna hii ili mfikilie wakati maalumu
kwake Yeye, nao ni wakati wa kufufuliwa; na kwa ajili mpate kupima na kufahamu
hikima na mazingatio katika mageuzi haya.
"Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii,
kisha kwa pande la damu..n.k."
Maoni juu ya "Tone la manii", "pande la damu" na "pande la nyama"
yamo katika Aya 7,8 na 9 Sura Assajda; Aya 12, 13 na 14 Sura Al-Muuminuna;
Aya 67 Sura Ghaafir; 5 Sura Al-Hajj. Neno Nut'fa katika lugha hutumika
kwa maana ya manii ya mwanamume.
Tukirejea kwenye Aya Tukufu (75.37) "Je! Hakuwa tone la manii lilio
shushiwa?" inadhihiri kuwa makusudi kwa "tone la manii" ni sehemu makhsusi
ya manii. Na ilimu ya sayansi imevumbua kuwa makusudi ya sehemu hiyo ni
kile kijidudu kinacho shushiwa, ambacho kinacho chukuliwa na maji yanayo
shushwa, na kidudu hicho "Sperm" ambacho kikiingia kwenye kijiyai (Buwaydha
Kiarabu au Ovum kwa Kizungu), cha mwanamke ndio huumbika mtoto.
Al-A'laqah katika maana zake kilugha ni damu iliyo ganda, au inayo
tiririka iliyo nyekundu mno. Na ki-sayansi maana yake ni Khalaya, au Cells
za Embryo (Mtoto ndani ya tumbo la mama) lilio gandamana (ta-a'llaqa) na
ukuta wa tumbo la uzazi baada ya kwisha ingiana kidudu cha ume na yai la
uke, na ikapatikana Khalaya moja ambayo ikagawika ikawa Khalaya kadhaa
wa kadhaa zinazo endea kwenye ukuta wa tumbo la uzazi, kwenda kujibandika
na huzua hapo kumwagika damu.
Al-mudhghah huyo ni mtoto katika mageuzi yake baada ya kutoka kuwa
Al-a'laqah, yaani baada ya kwisha shikamana na ukuta wa tumbo la uzazi
na kuviringana bila ya sura maalumu, na huzungukwa na vifuniko, na hubaki
katika hali hiyo wiki chache hivi mpaka yafanyike mafupa. Na Mudhghah ambayo
imefasiriwa kama pande la nyama ina khalaya zenye umbo maalumu, na hizo
ndizo zinakuwa mtoto, na khalaya zisio kuwa na umbo maalumu, na hizi
huzunguka sehemu ile iliyo timia umbo lake, na kazi yake ni kulinda na
kutoa chakula.
Mafupa: Ilimu ya mimba Gynaecology imethibitisha karibuni kuwa mafupa
yanadhihiri katika t'abaka ya katikati katika Khalaya za Mudhghah baada
ya kutoka kiwango cha kugawanyika Khalaya za viungo.
68. Mwenyezi Mungu ndiye anaye huisha na kufisha. Akitaka jambo lolote
kulidhihirisha katika kuwepo basi huliambia: Kuwa! Na huwa bila ya taakhira.
69. Je! Huwaangalii hao wanao zozana katika Ishara za Mwenyezi Mungu
zilio wazi, vipi walivyo geuzwa nadhari yao katika hizo, na wanaendelea
kushikilia ule ule upotovu wao walio nao?
70,71,72,73,74. Walio ikadhibisha Qur'ani na Ujumbe tulio watumia
Mitume wetu, Ufunuo wote, watakuja jua matokeo ya kukanusha kwao zitapo
kuwa pingu na minyororo zipo shingoni mwao, wakibururwa kwazo katika maji
yaliyo fikia ukomo wa moto, tena baadae watupwe Motoni waokwe kwenye joto
lake. Kisha waambiwe kwa kuwakejeli na kuwahizi: Wako wapi hao miungu yenu
mliyo kuwa mkiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema makafiri: Wametupotea.
Bali kwa hakika sisi hatukuwa hapo zamani duniani tukiabudu chochote. Katika
mfano wa upotovu mbaya kama huu ndio Mwenyezi Mungu anawawacha makafiri
waipotee Njia ya Haki kwa kujua kwake kwamba hao wamekhiari upotovu kuliko
uwongofu.
75,76. Makafiri wataambiwa: Adhabu hiyo ni kwa sababu ya mlivyo kuwa
katika dunia mkifurahi katika nchi kwa jambo lisilo stahiki kufurahikiwa,
na kwa sababu ya kufurahikia kwenu kwa maudhi yaliyo kuwa yakiwasibu Manabii
wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Basi ingieni kwenye milango ya
Jahannamu, ambako mmekadiriwa mkae daima dawamu. Pahala paovu kabisa pa
kukaa wenye kujivuna ni Jahannamu.
77. Subiri, ewe Muhammad! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu kwako ya
kwamba atawaadhibu maadui wako, ni kweli isiyo na shaka yoyote. Na adhabu
itawafikia tu, ama wakati wa uhai wako au wakati watapo rejea wao kwetu!
Wakiacha baadhi ya adhabu tunayo wahadharisha nayo katika uhai wako, basi.
Na ikiwa tutakufisha, basi watarejea kwetu. Nasi tutawahisabia waliyo kuwa
wakiyatenda.
78. Ninaapa: Bila ya shaka tuliwatuma Mitume wengi kabla yako wewe.
Wengine tumekuzungumzia khabari zao, na wengine hatukukuzungumzia khabari
zao. Wala haikuwa Mtume yeyote kuleta muujiza ila kwa apendavyo Mwenyezi
Mungu na kutaka kwake. Hawezi kuleta kwa nafsi yake tu, wala kwa watakavyo
watu wake. Na inapo kuja amri ya Mwenyezi Mungu ya kuleta adhabu duniani
au Akhera wanahukumiwa kwa uadilifu. Na wakati huo wapotovu huwa ndio wenye
kukhasiri.
79. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kudhalilishieni ngamia, mpate kuwapanda
wengine, na wengine muwale.
80. Na mnapata kwao manufaa mengi, mbali ya kuwapanda na kuwala;
na ili mpate kufikilia haja zenu mnazo zishughulikia nafsi zenu, kama kuburura
mizigo na kuibeba, na kadhaalika. Na juu ya ngamia, ambaye ni katika nyama
hoa, na juu ya marikebu, mnajipakia nyinyi wenyewe na mizigo yenu.
81. Mwenyezi Mungu anakuonyesheni dalili zake, basi hebu nambieni
dalili gani katika hizo mnazo zikataa? Na hizo dalili zenyewe ziwazi, hawezi
kuzikataa yeyote mwenye akili hata kidogo.
82. Je! Kwani hao watu wamekaa tu, hawazunguki ulimwenguni wakaona
ulikuwaje mwisho wa wale walio kuwa kabla yao, walivyo hilikishwa na wakaangamizwa?
Hao walio kabla yao walikuwa wengi kwa kuwahisabu kuliko wao, na walikuwa
na nguvu na waliathiri kwa majenzi na maendeleo kushinda wao. Hapana kilicho
wakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu katika hayo waliyo yachuma, si
mali wala nguvu, wala utawala.
83. Basi Mitume wao walipo wajia mataifa haya kwa sharia na miujiza
iliyo kuwa wazi, hayo mataifa yalifurahi na kujitapa kwa kuwa wao ati wana
ilimu za dunia, na wakawafanyia maskhara Mitume. Ikawateremkia adhabu waliyo
wakhubiria Mitume, na hali wao wakiwakejeli.
84. Mataifa haya yalipo ona adhabu imekuwa kali walisema: Tumemsadiki
Mwenyezi Mungu pekee, na tumewakataa miungu ambao kwa sababu yao tulikuwa
washirikina.
85. Imani yao haikuwafaa kitu wakati walipo kwisha ona ukali wa adhabu
yetu. Mwenyezi Mungu alikwenda mwendo ule ule aliyo kuwa akienda nao waja
wake, nao ni kutokukubali Imani wakati wa kuteremka adhabu. Na makafiri
ndio walio khasiri wakati wa kuteremka adhabu.