1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana
na nafsi moja, na kutokana na nafsi hiyo akamuumba mkewe, na kutokana na
hao wawili, wakaenea wanaume na wanawake wengi. Basi nyote mnatokana na
nafsi moja. Mcheni Mwenyezi Mungu mnaye mtaka msaada kwa kila mnacho kihitajia,
na kwa jina lake ndio mnaombana nyinyi kwa nyinyi katika mambo yenu.
Pia tahadharini na kuacha kuwasaidia jamaa zenu, wa karibu na wa mbali.
Kwani Mwenyezi Mungu daima anakuangalieni. Hapana chochote katika mambo
yenu kinacho fichikana kwake. Na Yeye ndiye Mwenye kukulipeni.
2. Na wapeni mayatima mali yao wanayo stahiki, na yalindeni mali
yao vizuri, wala msiwape kilio duni mkawanyima kizuri. Wala msichukue mali
yao mkaongezea kwenye mali yenu. Hakika kitendo hicho ni dhambi kubwa.
3. Ilivyo kuwa mnakhofu kuwadhulumu mayatima kwa kuwa hiyo ni dhambi
kubwa, basi kadhaalika khofuni machungu ya wake zenu kwa kuacha kuwafanyia
uadilifu baina yao, na kuzidisha juu ya wane. Basi mnaweza kuoa wawili,
au watatu, au wane, ikiwa mna imani kuwa mtaweza kufanya uadilifu. Mkiogopa
kuwa hamtaweza kufanya uadilifu basi oeni mmoja tu, au jitoshelezeni na
wajakazi walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hayo ni afadhali kuliko
kwenda kuingia katika dhulma na ujeuri (1). Na ni afadhali msije mkawa
na watoto wengi bila ya kiasi hata mshindwe kuwatazama.(Wafasiri wengi
wamependelea kufasiri "Alla Tau'luu" kuwa "Kutofanya jeuri au dhulma."
Lakini hii AL MUNTAKHAB imekhiari tafsiri hii ya "msikithirishe wana",
ambayo ndiyo aliyo ifuata Imam Shaafii r.a., naye alitanguliwa na Maimamu
wanazuoni wa Kiislamu, Zayd bin Aslam r.a.na Jabir bin Zayd r.a. kama alivyo
simulia Daar Qut'ni, na imetajwa katika Tafsir ya Qurt'uby juzuu ya 5 sahifa
22.)
(1) Sharia ya Kiislamu si peke yake inayo ruhusu kuoa wake wengi,
miongoni mwa sharia za dini za mbinguni. Sharia ya Taurati inamruhusu mwanamume
kuoa idadi ya wanawake atakao. Na imetaja kuwa Manabii walikuwa wakioa
wake kwa makumi na makumi. Na Taurati ni katika Agano la Kale la Biblia
ambalo linafuatwa pia na Wakristo katika mambo ambayo hayakukatazwa katika
Injili au Barua za Mitume. Na hakika iliopo ni kuwa hapana popote katika
Agano Jipya panapo pinga sharia hiyo ya kuruhusu kuoa wake zaidi ya mmoja.
Kanisa katika Karne za Kati liliruhusu hayo, na
wafalme wa Ulaya wa Kikristo walio kuwa na wake wengi ni maarufu katika
taarikh (historia).
Khitilafu iliyopo ni kuwa Uislamu ndiyo dini ya kwanza kuweka idadi
maalumu, isipindukiwe. Imeweka kiwango kwa mambo matatu.
* (Kwanza) wasipindukie hao wake kuliko wane.
* (Pili) asidhulumike mmoja katika hao wake,
* (Tatu) awe mtu anaweza kuwakimu hao wake.
Shuruti mbili za mwisho zimelazimu kila ndoa, ijapokuwa ni ya kwanza.
Wanazuoni wa Kiislamu wa sharia na wanga khitalifiana
wanakubaliana pamoja kuwa mume ambaye anajua kuwa hawezi kuwafanyia uadilifu
wakeze ni haramu kwake kidini kuongeza wake. Ila uharamu huu ni wa kidini,
watawala na mahakimu hawawezi kumuingilia. Kwani uadilifu ni jambo la nafsi
yake mtu, na dhamiri yake, na uwezo wa kutazama ni jambo la mnasaba halifungamani
na mizani mojapo. Ni yeye mwenyewe atakaye pata adhabu Siku ya Kiyama akikhalifu
amri hiyo. Dhulma au kutokuweza kukimu kunategemea hali ya siku zijazo,
na mikataba haifungamani na mambo ambayo huenda yakawa au yasiwe, bali
ni juu ya yaliyoko, na ilivyo kuwa dhaalimu huenda akawa muadilifu, na
asiye weza sasa hueza akaweza baadae, kwani mali huja na kuondoka, juu
ya hivyo Uislamu unasema mwanamume akimdhulumu mkewe au akashindwa kumkimu,
basi mwanamke anaweza kutaka kufarikishwa na mume huyo, lakini hazuiliki
na kuandikiana mkataba akifanya hayo kwa radhi yake na khiari yake.
Na Uislamu kwa kufungua mlango wa kuoa wake zaidi ya mmoja lakini
kwa mikazo kama hivyo ilivyo elezwa imekuwa umepiga vita magonjwa ya kijamii:
* Kwanza - Huenda ikawa idadi ya wanaume wanao faa kuoa ikawa chini
kuliko wanawake wanao faa kuoelewa. Khasa huwa hayo baada ya vita. Imeonakana
katika baadhi ya nchi za Ulaya imewahi kufika idadi ya wanawake kuwazidi
wanaume baada ya vita kwa mara saba! Kwa hivyo ni hishima ya mwanamke katika
hali kama hizo kuwa mke-mwenza kuliko kuwa akibahashika kama malaya, bila
ya mume.
* Pili - Huenda kutokea baina ya mwanamume na mwanamke hali inayo
walazimisha ama waingiane kiharamu au waoane kisharia. Ni maslaha
kwa umma yawe hayo kwa mujibu wa sharia. Na ni bora kwa mwanamke
kuwa mke kuliko kuwa hawara wa mwanamume huyu baada ya huyu. Ikiwa hii
ni sura mbaya ya kuoa wake wengi, basi juu ya hivyo ni afadhali kuliko
kuwa na mke mmoja. Kwani kuoa wake zaidi ya mmoja kama itavyo kuwa vibaya
kunakinga shari kubwa zaidi kwa umma, nayo ni umalaya na maovu yanayo pandana
nayo.
* Tatu - Mwanamke hakubali kuolewa na mume mwenye mke ila ikiwa
ni kwa dharura iliyo kweli. Ikiwa mke wa kwanza atapata madhara kwa uke-wenza,
basi huyu mwenzie atapata madhara makubwa zaidi kwa kuharimishwa mume kabisa,
kwa kuwa ama ufe uke wake au apotee kwa wanaume majiani. Madhara makubwa
hukingwa kwa madhara yaliyo akali.
* Nne - Imeonakana kuwa vijana wengi hawapendi kuoa, hata inakisiwa
kuwa vijana wanao oa kwa kulinganisha na wafaao kuoa hawazidi kuliko 60%.
Na haya yanazidi kila mwaka. Kupinga khatari hii hapana ila kuruhusu kuoa
wake wengi.
* Tano - Huenda mke akapata maradhi ambayo hayamruhusu kulala na
mumewe, au huenda akawa tasa. Ni maslaha ya umma na maslaha ya binafsi
kuoa mke mwengine. (Wakati huo huo ikawa kumpa talaka huyo mke ni madhara
makubwa zaidi kwa mke na ukatili kwa mume kufanya.)
Kwa sababu kama hizi na nyenginezo Uislamu umeufungua mlango kwa
shida na dhiki, na haukuufunga kabisa. Hivi sasa tunamwona Askofu Mkuu
katika Uingereza anaona kuwa dawa ya pekee ya kuondoa uharibifu ulio uingilia
ukoo wa Kiingereza ni kufungua mlango wa kuoa wake zaidi ya mmoja. Hakika
Uislamu ni Sharia ya Mwenyezi Mungu ambaye anajua kila kitu. Kwani Yeye
ndiye Mjuzi Mwenye hikima. (Haya tukijua kuwa dini ya Kikristo haikatazi
kuoa wake wengi. Ni sharia zilizo tungwa na makanisa ya Kizungu tu kwa
kufuata mila zao ndizo zinazo lazimisha kuoa mke mmoja. Basi hiyo ni mila
ya Wazungu, wala si sharia ya dini yoyote duniani. Bali Uislamu ndiyo Dini
pekee katika dini zote iliyo wekea kiwango, na kudhibiti idadi ya wanawake
kuoa, kwa maslaha ya Umma.)
4. Wapeni wanawake mahari yao kuwa ni kipawa, tunza iliyo safi. Na
nyinyi hamna haki yoyote katika hayo mahari. Ikiwa hao wanawake kwa radhi
ya nafsi zao wenyewe wakakubali kusamehe sehemu yoyote ya mahari mliyo
kwisha ahadiana, basi hapo mnayo ruhusa kuchukua na mkatumia kwa kheri
na salama.
5.Wala msiwape wasio na akili ya kutosha kuendesha mambo yao mali
yao, nayo ni mali yenu vile vile. Kwani mali ya yatima na ya mchache wa
akili yamekulazimuni myatazame yasiharibike. Mwenyezi Mungu ameyajaalia
mali hayo ya kukimu maisha. Wapeni kutokana na pato lake sehemu
kama wanavyo hitajia kwa kula, na wavisheni na muwatendee vyema, na mseme
nao maneno ya kuwaridhisha sio ya kuwaudhi au kuwadhili.
6. Na kabla ya hao mayatima kufika umri wa kubaalighi wajaribuni,
mpate kujua akili zao na hali zao na maarifa yao katika kuendesha mambo.
Hata wakifika wakati wa kusilihi kuoa na mkauona uwekevu wao, na matayarisho
kuchukua jukumu, basi hapo wapeni mali yao wenyewe. Wala nyinyi msiyale
mali yao kwa fujo, mkifanya haraka mpatilize kabla hawajabaalighi wakawa
watu wazima ikabidi haki yao kurudi. Na akiwa katika mawasii anajitosha
kwa utajiri, basi ajizuie asichukue chochote kuwa ni ujira kutazama mali
ya mayatima. Na akiwa fakiri muhitaji basi ajitosheleze kuchukua ujira
wa uangalizi kwa kadri ya ada ilivyo. Na mnapo wakabidhi mayatima mali
yao wekeni mashahidi wa kushuhudia. Na mjue kuwa Mwenyezi Mungu daima yupo
nyuma yenu, na Yeye ndiye Mhasibu, na Yeye ndiye Muangalizi. Na Yeye anatosha
kuwa Mhasibu na Muangalizi.
7. Wanaume wanalo fungu lao katika mali waliyo yaacha kurithiwa wazazi
wawili na jamaa walio karibia. Na wanawake, aidha, wana fungu lao,
bila ya kunyimwa au kupunjwa. Na mafungu hayo yamethibiti, na yamefaridhiwa,
na yamekadiriwa, yakiwa mali yenyewe kidogo au mengi.
8. Na pindi ikiwa wamehudhuria wakati ule wa kugawanya urithi baadhi
ya jamaa ambao hawarithi, na ni mayatima na masikini, basi wakirimuni kwa
kuwapa chochote katika huo urithi ili kuzipoza nafsi zao, na kuondoa uhasidi
katika nyoyo zao. Na ni vizuri pia katika kuwapa kuleta maneno laini na
udhuru mwema.
9. Watu watahadhari na kuwadhulumu mayatima, na wawaogopee watoto
wao wanyonge wasije na wao wakadhulumiwa kwa watendavyo wazee kwa mayatima
wa watu wengine. Na wamwogope Mwenyezi Mungu katika kuwatendea mayatima.
Na waseme maneno yaliyo kaa sawa yanayo fuata haki, wala wasimdhulumu yeyote.
10. Hakika wanao wadhulumu mayatima kwa kuchukua mali yao bila ya
haki, hakika wanakula yatakayo wapelekea Motoni. Na Mwenyezi Mungu atawaadhibu
Siku ya Kiyama kwa moto mkali wenye kutia machungu.(Je, huwaje basi adhabu
ya mwenye kudhulumu mali ya Mwenyezi Mungu? Wakfu za misikiti, madrasa
n.k.? Na huwaje mwenye kuuwa ili apate kudhulumu mali ya mayatima wa hao
alio wauwa?)
11. Mwenyezi Mungu anakuamrisheni katika mambo ya kuwarithisha watoto
wenu na wazazi wenu, pindi mtakapo kufa, kwa njia inayo leta uadilifu
na maslaha. Nayo ni kuwa sehemu ya mwanamume ni sawa na sehemu ya
wanawake wawili, ikiwa watoto wanao rithi ni wanaume na wanawake. Ikiwa
watoto wote ni wanawake watupu, na idadi yao imezidi wawili, basi sehemu
yao ni thuluthi mbili za tirka, yaani mali yaliyo achwa na maiti. Inafahamika
katika madhumuni ya Aya kuwa fungu la binti wawili ni kama fungu la walio
zidi hapo. Na akiwa mtu amemuacha binti mmoja tu, basi fungu lake ni nusu
ya alicho kiacha. Na akiwa mtu amemuacha baba na mama, basi kila mmojapo
kati ya hao atapata sudusi, yaani sehemu moja katika sita, ikiwa huyo maiti
alikuwa na mtoto mmoja - mwanamume au mwanamke - pamoja na hao wazazi wake.
Akiwa hana mtoto na wakamrithi wazazi wake tu, basi mama sehemu yake ni
thuluthi, na kilicho baki ni cha baba. Na ikiwa huyo maiti alikuwa na ndugu,
basi mama yake atapata sudusi na kilicho baki ni cha baba, na wale ndugu
hawapati chochote. Mafungu hayo hupewa wanao stahiki baada ya kwisha lipwa
deni lilio kuwa juu ya maiti, na kutimiza yale aliyo yausia katika mipaka
aliyo ruhusu Mwenyezi Mungu. Hii ni hukumu ya Mwenyezi Mungu. Na huu ndio
uadilifu na ndio hikima. Na nyinyi hamjui ni nani kwenu mwenye manufaa
zaidi kwenu, baina ya wazazi na wana. Na kheri khasa ni aliyo yaamrisha
Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ndiye Mwenye kuyajua maslaha yenu, na ndiye
Mwenye hikima katika yale aliyo kulazimisheni.
12. Fungu la mume ni nusu ya alicho acha mke ikiwa huyo mke hakuacha
mtoto kutokana na mume huyo au mwenginewe. Akiwa huyo mke ana mtoto, basi
mumewe atapata robo baada ya kutolewa wasia aliye uusia huyo mwanamke au
kulipwa deni lake. Na fungu la mke au wake ni robo ya alicho acha mume
ikiwa hakuacha mtoto kwa wake hao au wenginewe. Akiwa anaye mwana kutokana
na hao au wake wenginewe basi mke huyu au wake hawa watapata thumni ya
tirka baada ya wasia alio usia au deni. Na mwana wa mwana, yaani mjukuu,
ni kama mwana katika haya yaliyo tangulia. Na akiwa maiti ni mwanamume
au mwanamke, naye hana mwana wala mzazi, na kamwacha ndugu mume kwa mama,
au ndugu wawili wa kike kwa mama, basi kila mmoja wao atapata sudusi, yaani
sehemu moja katika sita. Na wakiwa wengi kuliko hivyo watashirikiana katika
thuluthi, watagawana sawa sawa wanaume na wanawake kwa mujibu wa ushirika,
baada ya kulipa madeni yaliyo kuwa juu yake, na kutimiza wasia ambao haudhuru
urithi, nao ni wasia usio pindukia thuluthi iliyo baki baada ya kulipa
madeni. Basi, enyi Waumini! Jilazimisheni kufuata aliyo kuusieni Mwenyezi
Mungu; kwani Yeye hakika ni Mwenye kujua vyema nani miongoni mwenu anaye
dhulumu na nani anaye fanya uadilifu, Yeye ni Mpole hafanyi haraka kutoa
adhabu.
13. Hizo ni hukumu zilizo tajwa kueleza khabari ya mirathi
na mengine yaliyo tangulia ni Sharia za Mwenyezi Mungu aliye zipanga kwa
ajili ya waja wake wazijue wala wasizikiuke. Na Mwenye kumt'ii Mwenyezi
Mungu na Mtume wake katika alivyo hukumu Yeye malipwa yake yatakuwa ni
Pepo ipitayo mito kati yake, na atakaa humo daima dawamu. Na huko ndiko
kushinda kukubwa.
Mpango wa mirathi uliyo bainishwa na Qur'ani Tukufu ni mpango wa
uadilifu na haki kuliko kanuni zote za mirathi nyenginezo duniani. Na haya
wameyakiri wataalamu wa sharia wote wa Ulaya. Na huu ni mmoja katika
ushahidi wa kuwa Qur'ani inatokana na Mwenyezi Mungu, kwani haya au yaliyo
karibia haya hayakuwa yakijuulikana kwa Waajemi wala kwa Warumi wala katika
sharia zozote za kabla ya Uislamu. Na sharia hii ya Kiislamu imefuata mipango
hii ya uadilifu:
* Kwanza - Umefanywa urithi kwa mujibu apendavyo Mwenyezi Mungu,
sivyo apendavyo mwenye mali, bila ya kupuuza kabisa mapenzi yake huyo.
Amepewa huyo ruhusa ya kufanya wasia kwa thuluthi ya mali kwa ajili ya
mambo mema, kama kutimiza kasoro katika waajibu wake wa dini, kama Zaka
ambazo alikuwa hakuzitoa, au kuwajaalia kitu wahitaji alio khusiana nao
kwa ujamaa au mapenzi nao hawastahiki urithi. Na amezuiliwa kufanya wasia
ikiwa hayo yatapelekea maasi au yatachochea kuendelea maasia. Na thuluthi
mbili zilizo baki baada ya wasia, au mali yote ikiwa hapana wasia, Mwenyezi
Mungu Mtunga sharia, amejipa Yeye kuzigawa kwa haki.
* Pili - Katika kuchukua madaraka ya ugawaji tirka, Mwenyezi Mungu
Aliye takasika, amempa aliye karibu zaidi kuliko mwenginewe, bila ya kuzingatia
ukubwa au udogo. Kwa hivyo ndio ikawa watoto wana sehemu kubwa zaidi katika
mirathi, kwani wao ndio kiendelezo cha yule maiti, na pia kuwa wao aghlabu
ni wanyonge. Juu ya hivyo hawakukoseshwa, bali wameshirikiana nao, mama
na bibi, baba na babu, ijapokuwa wanachukua akalli kuliko watoto.
* Tatu - Yaonekana kuwa mirathi ni kwa kadri ya haja. Kwa hivyo
sehemu ya watoto ni kubwa kwa sababu haja yao ni kubwa zaidi, na wao ndio
wanayakabili maisha, na kina baba na mama wanayapa mgongo maisha. Ama zingatio
la haja ndilo lililo pelekea kuwa fungu la mwanamke liwe nusu ya fungu
la mwanamume katika aghlabu ya hali za mirathi. Haya ni kwa kuwa mwanamume
inambdi zaidi kukabili matumizi, kwa kuwa yeye anatakikana awalishe watoto
na awatazame, amtumilie mwanamke. Maumbile ya kibinaadamu yamemfanya mwanamke
ndiye asimamie kazi za nyumbani na kulea watoto, kuangalia raha zao, na
mwanmume awe ni wa kuhangaika nje kiuchumi alete fedha za kutumia nyumba
nzima. Kumpa kila mmoja kwa kadri ya haja ndio uadilifu. Kuweka sawa kwa
wenye haja mbali mbali ni udhalimu.
* Nne - Sharia ya Kiislamu katika kugawa kwake tirka ya maiti
inakusudia kugawa sio kurundika. Kwa hivyo haikufanya urithi
wende kwa mtoto mkubwa peke yake, wala haikuwapa wanaume tu na kuwachilia
mbali wanawake, wala watoto wakaachwa wazazi. Wala hawakukoseshwa wasio
kuwa katika uti wa nasaba, kama ndugu, na maami, na banu-ami n.k. Urithi
unaendelea mpaka kwa wanao karibia ukoo, lakini aliye karibu hufadhilika
zaidi. Na shida kutokea kuwa mrithi ni mmoja tu.
* Tano - Mwanamke hakoseshwi kurithi, kama ilivyo kuwa ada ya Waarabu.
Hivi ni kumhishimu mwanamke na kumpa haki yake. Na juu ya haya Uislamu
hauzuii kurithi ujamaa wa mwanamke, bali hurithi jamaa walio kuwa upande
wake, kama wanavyo rithi jamaa upande wa baba. Makaka na madada kwa upande
wa mama wanachukua pale wanapo chukua ndugu wa baba na mama, bali katika
hali nyengine wanachukua watoto wa kwa mama na kuchukua ndugu wanaume na
wanawake. Na haya bila ya shaka ni kuutukuza umama, na kuutambua ukaribu
wake. Haya hayakuwa yakijuulikana kabla yake, walakini hii ni Sharia ya
Mwenyezi Mungu aliye Mjuzi na Mwenye hikima.
14. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake na
akaikiuka mipaka aliyo iweka Mwenyezi Mungu, na huku akihalalisha
kukiuka huko basi mtu huyo atalipwa Moto, na humo atakaa milele, akiadhibiwa
mwili wake juu ya kuadhibiwa roho yake.
15. Na wale wanawake wanao zini wakishuhudiwa na mashahidi wanaume
wane walio waadilifu, basi wazuieni wasitoke nyumbani kwa ajili ya kuwalinda
na kuzuia usiendelee ufisadi na shari mpaka wafe, au Mwenyezi Mungu awafungulie
njia ya maisha yaliyo sawa kwa kuolewa na kutubu. (Wafasiri wengine wanasema
hukumu hii ni kwa wanawake wanao fanya mambo machafu wenyewe kwa wenyewe,
sio ya zina baina ya mwanamke na mwanamume. Kwa kuhifadhi heshima ya wanawake
inalazimu wapatikane mashahidi wane, badala ya wawili, walio ona kitendo
khasa, sio kuwatuhumu watu kwa jambo ovu kama hilo bila ya mashahidi wane
walio shuhudia kwa macho yao.)
16. Mwanamume na mwanamke walio zini, nao hawajaoa (au kuolewa),
wapewe adhabu maalumu, pindi ikithibiti hiyo zina kwa mashahidi wane waadilifu.
Wakitubu baada ya kupewa adhabu, basi msiwatajie hayo maasi waliyo yatenda,
wala msiwaaziri. Hakika Mwenyezi Mungu kwa rehema yake anakubali toba ya
wenye kutubu.
17. Hakika toba imedhaminiwa na Mwenyezi Mungu kwa watendao
maovu katika hali ya ujinga, na kupitikiwa na kutoangalia vyema, kisha
wakafanya haraka ya kutubu kabla ya kufikiwa na mauti. Hawa
basi MwenyeziMungu anaikubali toba yao, naye ni Mjuzi, haumfichikii ukweli
wa toba, ni Mwenye hikima, hakosei katika kupima.
18. Toba isiyo kubaliwa ni ya wanao fanya maasi kisha hawafanyi haraka
kuyajutia mpaka mmoja afikwapo na mauti. Tena hapo husema: Sasa mimi natangaza
majuto na toba. Kadhaalika toba haikubaliwi kutokana na wanao kufa katika
ukafiri. Mwenyezi Mungu ameyaandalia makundi mawili hayo adhabu ya kutia
uchungu huko kwenye nyumba ya malipo, Akhera.
19. Enyi mlio amini! Haikujuziini kuwafanya wanawake kama bidhaa,
mkiwarithi wake zenu bila ya mahari na bila ya ridhaa yao. Wala msiwadhulumu
kwa kuwadhikisha ili wapate kusamehe baadhi ya mahari mlio wapa. Wala msiwadhiki
ili wapate kukurejesheeni mali mlio wapa, ila ikiwa wakifanya kosa wazi
la kuwacha ut'iifu, au la tabia mbovu, au la ukahaba. Hapo mnaweza kuwadhikisha
au kuchukua baadhi ya mlicho wapa wakati wa kufarikiana nao. Na ni waajibu
wenu, enyi Waumini, kukaa na wake zenu kwa vizuri, kwa maneno mema na vitendo
vyema. Ikiwa mtawachukia kwa aibu fulani katika tabia au katika umbo au
mengineyo, basi juu ya hivyo subirini. Msifanye haraka kuwaacha, kwani
asaa Mwenyezi Mungu akajaalia kheri nyingi katika hicho hicho mkichukiacho.
Na ujuzi wa mambo yote uko kwa Mwenyezi Mungu tu.
20. Na pindi ikiwa mnataka kubadili mke pahala pa mke mwengine, na
ikawa mmempa mmoja wao mali mengi basi si halali kwenu kuchukua chochote
katika hayo. Jee mtachukua hayo kwa njia ya upotovu na kwa dhambi iliyo
wazi?
21. Na vipi ikufalieni nyinyi kutaka kurudishiwa mahari mliyo kwisha
yatoa, na hali mlikwisha changanyika nyinyi kwa nyinyi, na wao wanawake
wakafungamana nanyi kwa agano lenye nguvu ambalo kwalo Mwenyezi Mungu amewajibisha
muingiane nao kwa ndoa.
22. Wala nyinyi, watoto, msiwaoe wanawake walio wahi kuolewa na baba
zenu. Jambo hilo ni uchafu na linachusha, na linakirihiwa na Mwenyezi
Mungu na watu. Na hiyo ni njia ovu kabisa. Lakini Mwenyezi Mungu anasamehe
yaliyo kwisha tendeka katika zama za ujahili.
Waarabu katika zama za ujahili walikuwa na ada zisio mpa heshima
mwanamke, bali zikimdhulumu sana, na zikikata makhusiano mema katika ukoo.
Ilikuwa mtu akifa baba yake na akawa na wake wasio kuwa mama yake mzazi,
akilazimishwa kuwaoa, au akiwarithi wake za baba yake bila ya ndoa mpya.
Na ilikuwa mtu akimwacha mke basi humpokonya kwa dhulma na uadui mahari
yote aliyo mpa. Na walikuwapo walio kuwa wakimzuia huyo mt'laka asiolewe
na mtu mwengine, kwa jeuri na inda. Ukaja Uislamu, ukamlinda mwanamke na
dhulma hii iliyo wazi, ukakataza kurithiwa mke, na kumpokonya mahari yake
hata chembe, ijapo kuwa ni mali mengi, na ukakataza kumzuia mt'alaka asiolewe,
au kumkera ili apate kutaka yeye mke t'alaka kwa kutoa mali. Na katika
mtindo wao Waarabu wa jahiliya ilikuwa yafaa mtu kumwoa aliye kuwa mke
wa baba yake na akafarikiana naye kwa t'alaka au mfano wake. Uislamu ukakataza
hayo, na ukauwita mtindo huo ni uchafu, kwa sababu ni jambo baya
analo lichukia Mwenyezi Mungu na kila mwenye akili sawa. Huo ndio uadilifu
wa Mwenyezi Mungu.
23. Mwenyezi Mungu amekuharimishieni kuwaoa mama zenu,
na binti zenu, na dada zenu (ndugu wanawake) na shangazi zenu, na khaalati
zenu (mama wadogo) na binti wa ndugu, na binti wa dada, na mama walio kunyonyesheni,
na dada zenu kwa kunyonya, na mama wakwe. Na walio harimishwa bila ya kunasibiana
kwa damu ni: mama wa kunyonyesha, dada wa kunyonya (1), mama mkwe, binti
za wake kwa waume wengine ikiwa hao wake wameingiliwa, na wake wa watoto
mlio wazaa, na kuwaoa pamoja ndugu wawili. Yaliyo pita katika siku
za ujahili yamesamehewa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe
kwa yaliyo pita kabla ya mpango huu, na Mwenye kuwarehemu katika aliyo
kuwekeeni sharia.
(1) Ni Sharia ya Kiislamu pekee iliyo harimisha kwa sababu ya kunyonyesha.
Anaye nyonya anakula kutokana na mwili wa mnyonyeshaji kama anavyo kula
kutokana na mama yake ndani ya tumbo lake. Wote hao wawili wanakuwa ni
sehemu yake huyo mtoto. Hapana khitilafu baina ya kukua ndani ya chumba
na ndani ya tumbo. Na katika kuharimisha kwa kunyonyesha ni kumtukuza mnyonyeshaji,
kwani anakuwa kama mama. Na haya ni kuzidi kushajiisha kunyonyesha kimaumbile,
sio kwa chupa, kwa watoto wachanga.
24. Haramu kwenu kuoa wake za watu wote, waungwana na wasio waungwana,
ila mateka mlio wateka katika vita baina yenu na makafiri. Kwani ndoa zao
zilizo pita zinafutika kwa kutekwa. Wanakuwa halali kwenu baada ya kuhakikisha
hawana mimba. Basi shikeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu kuhishimu mlicho
katazwa. Isipo kuwa hao wanawake Waumini walio maharimu yenu, mwaweza kutafuta
wanawake mkawaoa kwa mali yenu, bila ya kuzini au kuweka kinyumba. Kila
mwanamke mliye starehe naye baada ya kumwoa mpeni mahari yake kama mlivyo
patana. Hapana ubaya kwenu ikiwa watakuridhieni kupunguza au kuongeza.
Mwenyezi Mungu daima anayaangalia mambo ya waja wake, na ni mwenye kuwapangia
hukumu zinazo wasilihi kwa maisha yao.
25. Asiye weza kati yenu kuwaoa wanawake Waumini wa kiungwana basi
na aowe anaye muweza katika wanawake Waumini walio milikiwa. Na Mwenyezi
Mungu anajua vyema ukweli wa Imani yenu na ikhlasi yenu. Wala msione uvunjifu
kuwaowa hao vijakazi, kwani nyinyi na wao ni sawa katika Dini. Basi
waoweni kwa idhini ya watu wao, na muwape mahari yao mliyo wakadiria kwa
mujibu ya ilivyo zowewa kati yenu kwa ajili ya kutendeana mema na kutimiza
haki. Na chagueni wanawake walio safi, msichague wazinifu kwa dhaahiri
wala mahawara wa kinyumba. Na hao wakija zini baada ya kuolewa basi adabu
yao ni nusu ya muungwana. Na huku kuhalalishiwa kuowa wajakazi mnapo kuwa
hamuwezi kunajuzu kwa anaye ogopa taabu zinazo pelekea zina. Na mkisubiri
kuto owa wajakazi na mkakaa safi ni bora kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi
wa maghfira, na Mkubwa wa kurehemu.
26. Mwenyezi Mungu anataka kukuwekeeni wazi njia yenye maslaha kabisa,
na akuongoeni kwenye nyendo njema za walio kuwa kabla yenu, na akurejesheni
kwenye njia ya ut'iifu wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua vyema
mambo yenu, ni Mwenye kupanga baraabara katika hukumu zake kwa yanayo silihi
mambo yenu.
27. Na Mwenyezi Mungu anataka mrejee katika ut'iifu wake, na wale
wanao fuata ladha zao, na matamanio yao machafu, miongoni mwa makafiri
na waasi, wanataka muwe mbali kabisa na njia ya haki.
28. Mwenyezi Mungu anataka kukufanyieni wepesi katika kutunga sharia
ambazo ndani yake zina sahala na takhfifu kwenu. Kwani hakika Mwenyezi
Mungu amemuumba mwanaadamu kiumbe dhaifu katika kupambana na matamanio
na maelekeo ya nafsi. Kwa hivyo yanayo mlazimu katika sharia yana wepesi
na wasaa. Na hayo kwa fadhila yake na taisiri yake Mwenyezi Mungu ndiyo
anayo walazimisha waja wake.
29. Enyi mlio amini! Msinyang'anyane mali nyinyi kwa nyinyi. Lakini
ipo ruhusa kufanya biashara kwa kuridhiana. Wala msijiteketeze kwa
kuacha amri za Mola wenu Mlezi. Wala mmoja wenu asimtende uwovu mwenziwe,
kwani nyote ni nafsi moja. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye rehema daima
kwenu.
30. Na mwenye kuyatenda aliyo yaharimisha Mwenyezi Mungu kwa uvamizi
na kupindukia haki yake, basi tutamtia Motoni ateketee huko. Na hayo ni
madogo na mepesi kabisa kwa Mwenyezi Mungu.
31. Mkiyaachilia mbali madhambi makubwa makubwa anayo kukatazeni
Mwenyezi Mungu, tutakusameheni makosa yaliyo duni ya hayo, maadamu mnafanya
ukomo wa juhudi yenu kwenda sawa; na tutakuwekeni duniani na Akhera mwahali
penye ihsani na hishima kwenu.
32. Wala haifai wanaume kutamani yale waliyo khusishwa nayo
wanawake, wala haiwafalii wanawake kutamani waliyo khusishwa nayo wanaume.
Kwani kila kikundi kina sehemu yake kwa mujibu wa tabia ya maumbile ya
kazi zinazo wawajibikia, na haki wanazo ongezewa. Basi kila mmoja ajielekeze
kutaraji ziada ya fadhila za Mwenyezi Mungu kwa kukuza vipawa alivyo pewa
yeye na kutafuta msaada juu ya waajibu ulio juu yake. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mjuzi timamu wa kila kitu, na mtu amepewa namna ya kila kitu kinacho
msilihi.
33. Na wote, wanaume na wanawake, tumewajaalia kuwa wanastahiki urithi
wao wa kuwarithi wazazi wawili, na jamaa, na wale ambao mfiliwa amefungamana
nao kwa agano ambalo matokeo yake ni kuwa amrithi ijapokuwa si jamaa, na
amsaidie pindi anahitajia msaada kuwa ni badala yake. Basi mpeni haki yake
kila mwenye haki, wala msipunguze kitu. Hakika Mwenyezi Mungu anakuangalieni
kwa kila kitu, na yuko pamoja nanyi, anashuhudia yote myafanyayo.
34. Wanaume wana haki ya kuwaangalia na kuwachunga wanawake, na kuwasimamia
katika mambo yao kwa vile Mwenyezi Mungu amewapa wao wanaume sifa za kuweza
kuisimamia haki hii, na kwa kuwa wao ndio wanao hangaika na kufanya juhudi
ya kutafuta mali ya kuutumilia ukoo mzima. Basi wanawake wema wanakuwa
ni wat'iifu kwa Mwenyezi Mungu na waume zao. Ni wenye kuhifadhi vyote ambavyo
waume zao hawavioni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameamrisha vihifadhiwe, na
kwa kuwapa wao tawfiki. Na wanawake wanao onyesha kuanza uasi wanasihini
kwa maneno yenye kuathiri. Kama hawakusikia tenganeni nao kitandani. Hawakusikia,
watieni adabu kwa pigo dogo, si la kuwajuruhi wala kuwadhalilisha. Wakirejea
kwenye ut'iifu wenu kwa njia mojapo katika hizi tatu basi msiwatafutie
kisababu cha kuwatesa zaidi kuliko haya. Hakika Mwenyezi Mungu yuko juu
yenu, naye atakupatilizeni pindi mkiwaudhi wake zenu au mkawafanyia jeuri.
35. Pindi pakitokea kukhitalifiana baina ya mke na mume, na mkakhofia
kutokea kufarikiana kutako leta t'alaka, chagueni waamuzi wawili. Mmoja
kutokana na upande wa mume na mwengine upande wa mke. Wakitaka kusuluhiana
Mwenyezi Mungu atawawafikisha wafikilie lilio kheri kwa wote wawili, nako
ama kukaa kwa wema au kuachana kwa ihsani. Hakika Mwenyezi Mungu anachungua
kila kitu cha waja wake, kilicho dhihiri na kilicho fichikana.
36. Nanyi muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake, wala msimfanyie washirika
katika Ungu na kuabudiwa. Na watendeeni wema wazazi wenu bila ya taksiri
yoyote, na pia jamaa zenu, na mayatima, na walio fakirika kwa sababu ya
kuemewa au kupata masaibu katika mali yao, na jirani mliye karibiana naye
kwa nasaba, na jirani mtu mbali, na mwenzio katika kazi au njia au majlisi,
na msafiri mhitaji asiye kuwa na kituo katika nchi maalumu, na watumwa
wenu wanaume na wanawake mlio wamiliki. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi
anaye jipa ubora juu ya watu wengine, na hawachukulii watu kwa huruma,
na anakithirisha kujisifu mwenyewe kwa kujifakhiri.
37. Hao ndio wanao ongeza juu ya takaburi na tafakhuri yao ila ya
kuwafanyia watu ubakhili kwa mali yao na juhudi yao. Tena ikawa wanawataka
watu wafanye ubakhili kama wao. Kazi yao ni kukhofia neema na fadhila ya
Mwenyezi Mungu isiwatoke. Kwa hivyo, basi, hawajifai wenyewe wala hawawafai
watu. Wapinzani kama hao tumekwisha waandalia adhabu ya kutia machungu
na ya kudhalilisha.
38. Na Mwenyezi Mungu hawapendi wanao toa mali
kwa ajili ya kuonekana na watu, wapate kuwasifu na kuwatukuza, na ilhali
wao si wenye kumuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Malipo. Kwani
hao wamemfuata Shetani naye amewapoteza. Na mwenye kuwa rafiki yake ni
Shetani basi ana rafiki mbaya kweli.
39. Ama wamelaanika watu hawa! Kingewadhuru nini wao lau kuwa wamemuamini
Mwenyezi Mungu na Siku ya Akhera, na wakatoa katika alicho wapa Mwenyezi
Mungu kwa kufuatana na Imani hii, na usafi wa niya, na kutaraji thawabu
kama ilivyo wajibikia? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kwa ujuzi kaamili
mambo yote yaliyo wazi na yaliyo fichikana ndani.
40. Hakika Mwenyezi Mungu hamdhulumu mtu hata kidogo. Basi hampunguzii
ujira wake mtu, wala adhabu yake hamzidishii kabisa. Bali humzidishia mtenda
mema thawabu zake mardufu hata zikiwa kidogo vipi. Na humpa kwa fadhila
yake malipo makubwa yasiyo lingana na hayo mema yake ambayo yamekwisha
zidishwa mardufu.
41. Vipi basi itakuwa hali ya hao mabakhili wanao pingana na aliyo
yaamrisha Mwenyezi Mungu, tutapo mleta Siku ya Kiyama kila Nabii awe ni
shahidi juu ya kaumu yake, na tukakuleta wewe, ewe Nabii Muhammad, kuwa
ni shahidi juu ya kaumu yako, na hali miongoni mwao wapo hao wanao zuia
mali yao na wanao pinga?
42. Yatapo tokea haya watatamani hao wapinzani wanao pinga lau kuwa
wangeli potea chini ya ardhi kama wanavyo potea maiti makaburini! Na wao
hawawezi kumficha Mwenyezi Mungu kitu chochote katika mambo yao, na hali
zao na vitendo vyao vitadhihiri.
43. Enyi mlioamini! Msende kusali misikitini nanyi mmo katika hali
ya ulevi mpaka muwe mnafahamu myasemayo. Wala msiingie misikitini nanyi
mna janaba, ila ikiwa ni kupita njia tu bila ya kusita, mpaka mtahirike
kwa kukoga. Na mkiwa ni wagonjwa hamuwezi kutumia maji kwa kuogopa maradhi
yasikuzidini au kuchelewa kupona, au mkiwa mmo safarini na ipo shida ya
kupata maji, basi tumieni mchanga ulio safi. Kadhaalika mmoja wenu akitoka
chooni, au mkawaingilia wanawake na mkawa hamkupata maji ya kujitahirishia
kwa kukosekana kwake, basi vile vile chukueni mchanga safi upigeni kwa
mikono yenu, na mpangusie nyuso zenu na mikono yenu. Hakika ni shani ya
Mwenyezi Mungu kuwa ni Mwenye kusamehe sana na Mwenye kufuta dhambi.
44. Hebu huyastaajabii mambo ya hawa walio pewa sehemu ya Vitabu
vilivyo tangulia wanavyo acha uwongofu na wakatafuta upotovu katika mambo
yaliyo wakhusu nafsi zao! Na wao tena wanakutakeni nyinyi mjitenge na Haki
ambayo ndiyo Njia ya Mwenyezi Mungu Iliyo Nyooka!
45. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi kuliko nyinyi kuwajua maadui
zenu wa kweli, na anatambua zaidi yaliyo ndani ya nafsi zao. Ulinzi wa
Mwenyezi Mungu unakulindeni, na unakuangalieni, na unakutosheni.
Basi msitafute ulinzi wa mwenginewe usio kuwa wake. Msaada na nusura yake
inakutoshelezeni; basi msiwe kutaka msaada wa mwenginewe.
46. Miongoni mwa Mayahudi kipo kikundi kazi
yao kugeuza geuza maana ya maneno. Wao husema kimoyomoyo
kumwambia Mtume s.a.w.: Tumesikia hayo maneno, na hatuifati hiyo amri.
Na pia husema: Sikia maneno yetu - hukusikia wito. Wakikusudia kwa hayo
kumuapiza Mtume. Na husema: Sikia bila ya kusikilizwa. Tamko hilo
wanalipindua maana. Muradi wao ni kumuapiza, na wanajidai kuwa muradi wao
ni kumwombea dua. Na husema: "Raai'na", wakipindua ndimi zao wakijitia
kuwa wanakusudia "Undhurna" yaani "Tuangalie". Wanaonyesha kuwa wanataka
uangalizi wake, na kumbe wanakusudia neno la Kiyahudi lenye maana ya "Mpumbavu"
ili kuibeza Dini ya Kiislamu.
Na lau kuwa wangeli nyooka sawa wakasema: "Tumesikia na tumet'ii"
badala ya hiyo kauli yao ya "Tumesikia na tumeasi", na wakasema:
"Sikia" na wasiseme "Bila ya kusikilizwa", na wakasema :"Undhurna" yaani
"Tuangalie", badala ya "Raa'ina", ingeli kuwa bora kwao kuliko hayo
wayasemayo, na ingeli kuwa ndiyo njia ya uadilifu zaidi. Lakini Mwenyezi
Mungu amewatoa katika rehema yake kwa ule upinzani wao. Kwa hivyo huwaoni
miongoni mwao wanao mwitikia mwenye kuwaitia Imani ila wachache tu.
47. Enyi mlio pewa Kitabu alicho teremsha Mwenyezi Mungu! Iaminini
Qur'ani tuliyo mteremshia Muhammad, inayo sadikisha mliyo nayo, kabla hatujawateremshia
adhabu ya kufutwa nyuso zenu zikawa kama visogo, hazina pua, wala macho,
wala nyusi. Au tukakutoeni katika rehema yetu kama tulivyo watoa wale walio
ikhalifu amri yetu wakatenda waliyo katazwa ya kuvua samaki siku ya mapumziko,(Sabt
au Sabato) siku ya Jumaamosi. Na hukumu ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutimizwa
tu, wala hapana cha kuipinga.
48. Hakika Mwenyezi Mungu hafuti dhambi za ushirikina, kumfanya Yeye
ana mshirika yeyote. Na husamehe dhambi zilio chini ya huo ushirikina kwa
amtakaye miongoni mwa waja wake. Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi
Mungu basi amemzulia Mwenyezi Mungu na ametenda dhambi kubwa mno isiyo
stahiki kusamehewa.
49. Hustaajabii hali ya hao makafiri wanao zua kwa vitendo vyao?
Vitendo vyao viovu wao wanaviona kuwa ni vizuri. Wanajisifu kuwa
kwa vitendo hivyo wao wametakasika. Na ni Mwenyezi Mungu tu peke yake ndiye
anaye jua jema na baya. Yeye ndiye wa kumtakasa amtakaye, na wala hamdhulumu
mtu yeyote kadiri yake hata chembe.
50. Vipi watu hawa wanavyo mzulia Mwenyezi Mungu uwongo kwa haya
na mengineyo mfano wa haya! Yatosha uwovu ulio wazi kwa huu uwongo wao
kuyakashifu maovu yao.
51. Hebu huwastaajabii hawa walio pewa sehemu ya ujuzi wa Kitabu
wanavyo ridhia ibada ya masanamu na Shetani, na wanavyo sema kuwa hao waabuduo
masanamu ni afadhali wameongoka kwenye Njia kuliko Waislamu wenye kuamini?
52. Hao ndio alio watupa Mwenyezi Mungu na akawafukuzilia mbali kutoka
kwenye rehema yake. Na mwenye kutupwa na Mwenyezi Mungu na akatolewa kwenye
rehema yake basi kabisa huyo hana wa kumnusuru na kumlinda na ghadhabu
ya Mola wake Mlezi.
53. Hao wamekoseshwa neema ya kuifuata haki, kama walivyo koseshwa
na utawala. Na lau wakipewa utawala hawanufaishi watu hata chembe.
54. Na vipi watu hawa wanavyo waonea maya Waarabu? Na wakaona
ni jambo kuu kuwa Mwenyezi Mungu alivyo wapa fadhila yake kwa kuwatolea
Nabii kutokana nao, na ilhali Mwenyezi Mungu alimpa Ibrahim na ukoo wake
- naye ni baba yenu (Mayahudi na Wakristo), na baba yao (Waislamu pia)
- Kitabu kilicho teremshwa kwa ufunuo, na Unabii na Utawala ulio mkubwa!
55. Miongoni mwa walio pelekewa Nabii Ibrahim na ukoo wake wapo wenye
kukiamini Kitabu kilicho teremshiwa kwao, na wapo walio kipa nyongo wakajitenga
nacho. Na jaza ya hawa wenye kujitenga na wito wa Haki ni Jahannamu yenye
moto wa kuteketeza.
56. Hakika wanao pinga hoja zetu zenye kubainisha wazi wazi, na wakawakanusha
Manabii, tutakuja watia kwenye Moto utakao babua ngozi zao. Na kila zikisita
kuhisi adhabu Mwenyezi Mungu atawabadilishia ngozi nyengine mpya ili machungu
ya adhabu yabaki yakiendelea. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ushindi katika
mambo yake, na Mwenye hikima katika vitendo vyake. Humuadhibu mwenye kumpinga
na akabaki na upinzani mpaka kufa kwake.
Qur'an Tukufu imeitangulia sayansi ya kisasa, ikathibitisha kuwa
katika ngozi mishipa ya kuhisi, Navo, imetanda kama wavu, na hiyo
hupokea mishipa yote ya kuhisi machungu, joto na baridi na mengineyo. Na
hayo hayakujuulikana ila hivi karibuni.
57. Na ambao walio yasadiki yaliyo wajia kutoka kwa Mola wao Mlezi,
na wakatenda vitendo vyema, tutawalipa kwa Imani yao na vitendo vyao na
tutawaingiza katika Mabustani ya Peponi yapitayo mito chini ya miti yake.
Uhai wao hauna kikomo kabisa. Nao humo watakuwa na wake walio t'ahirika
na kila la aibu na uchafu. Tutawapa uhai wa starehe chini ya vivuli vizuri
vya kudumu, waishi maisha mema yenye neema isiyo kwisha.
58. Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni nyinyi Waumini mrejeshe
vyote mlio pewa amana, kutokana na Mwenyezi Mungu au kutokana na watu,
kwa wenyewe kwa uadilifu. Basi msifanye jeuri katika kuhukumu. Haya
ni mawaidha yanayo toka kwa Mola wenu Mlezi. Basi yafanyieni pupa kuyafuata.
Bora ya mawaidha ni yanayo tokana naye Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu daima
ni Mwenye kusikia yasemwayo, ni Mwenye kuyaona yatendwayo. Basi anamjua
anaye rejesha amana, na anaye fanya khiana, na anaye hukumu kwa uadilifu,
na anaye fanya jeuri. Na kila mmoja atamlipa kwa atendalo.
59. Enyi mlio sadiki aliyo kuja nayo Muhammad! Mt'iini Mwenyezi Mungu,
na mt'iini Mtume, na wale wanao tawala mambo yenu miongoni mwa Waislamu
wanao simama juu ya haki na uadilifu, na wanatekeleza Sharia ya Mwenyezi
Mungu. Na mkizozana katika jambo baina yenu basi rejeeni kwenye Kitabu
cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake ili mpate kujua hukumu yake.
Kwani Yeye Mwenyezi Mungu amekuteremshieni Kitabu chake na Mtume wake amebainisha
hicho Kitabu. Na katika hayo ipo hukumu ya hayo mnayo khitalifiana kwayo.
Haya ni kwa mujibu wa Imani yenu kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.
Na haya ndio bora kwenu ili mpate kuongoka kwendea uadilifu katika mnayo
khitalifiana kwayo, na mwisho wake ndio mzuri zaidi. Kwani hivyo ndio kuzuia
zisitokee khilafu zinazo pelekea ugomvi na upotovu.
60. Ewe Nabii! Huwastaajabii hao wanao dai kuwa wanasadiki Kitabu
ulicho teremshiwa wewe na vilivyo teremshwa kabla yako wewe, wanataka wahukumiwe
katika ugomvi wao kwenye upotovu na uharibifu na hukumu isiyo kuwa ya Mwenyezi
Mungu? Na Mwenyezi Mungu amekwisha waamrisha wayapinge hayo, wala wasitake
kuhukumiwa kwa hayo. Na Shetani anataka awaachishe Njia ya Haki na Uwongofu,
awapotezelee mbali.
61. Na wakiambiwa: Njooni kwenye Qur'ani na Sharia aliyo iteremsha
Mwenyezi Mungu, na njooni kwa Mtume wake akubainishieni, utaona hao wanaafiki
wanajitenga nawe kabisa wanakukataa.
62. Itakuwaje hali basi yakiwateremkia masaibu kwa sababu ya uovu
wao na upotovu wa vitendo vyao, na wasipate pa kukimbilia ila kwako! Hapo
basi watakuapia Mungu mbele yako kuwa wao hawakukusudia kwa maneno yao
na vitendo vyao ila wema tu na kutaka mapatano.
63. Hao ndio wanao kula yamini kuwa hawakutaka ila wema na vitendo
vya muwafaka. Mwenyezi Mungu anayajua vyema yaliyomo katika nyoyo zao,
na anaujua uwongo wa hiyo kauli yao. Basi wewe usishughulike na maneno
yao. Waite kwenye haki kwa mawaidha yaliyo mema, na sema nao maneno yenye
hikima yenye kuathiri yanayo fika ndani ya nyoyo zao.
64. Na Sisi hatukumtuma Mtume yeyote ila jambo lake kuu ni kuwa at'iiwe,
na ut'iifu huo ni kwa ruhusa iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu. Na hakika
mwenye kwenda kinyume, au kukanusha, au kukhaalifu, anakuwa ni mwenye kujidhulumu
mwenyewe. Na lau kuwa hawa walio jidhulumu wakirejea kwenye uwongofu,
wakakujia wakiomba msamaha kutokana na Mwenyezi Mungu kwa yale waliyo yatenda,
na wewe ukawaombea msamaha kwa mujibu wa ujumbe wako na kwa ulivyo
ona ilivyo geuka hali yao, basi hapana shaka watamkuta Mwenyezi Mungu,
Aliye takasika na kutukuka, ni Mwingi wa kukubali toba, na Mwenye kuwarehemu
waja wake.
65. Naapa kwa jina la Mola wako Mlezi! Hawahisabiwi kuwa ni Waumini
wa Haki na wenye kuinyenyekea, mpaka watakapo kufanya wewe hakimu muamuzi
wa mizozo inayo tokea baina yao. Kisha nafsi zao zisione dhiki kwa utavyo
hukumu, na wakunyenyekee kama wanavyo nyenyekea Waumini wa kweli.
66. Na lau kuwa Sisi tumewalazimisha mashaka ya mwisho, kwa kuwaamrisha
wapigane Jihadi moja kwa moja, na wajitolee nafsi zao kutilifu, au watoke
nje waache majumba yao kwenda pigana Jihadi daima, wasinge kubali kut'ii
ila wachache tu. Lakini Mwenyezi Mungu, Aliye takasika na kutukuka, hakalifishi
ila linalo wezekana. Na lau kuwa wange fanya hayo na wakafuata haki yake
ingeli kuwa ni kheri yao ya duniani na Akhera. Na hivyo ndiyo inavyo pelekea
kuthibiti Imani, na kuingia imara, na kuleta utulivu.
67. Na lau kuwa wamesimama juu ya Haki aliyo ilazimisha Mwenyezi
Mungu kwa kadri ya uweza wao, Mwenyezi Mungu angeli wapa malipo makubwa
kwa fadhila yake.
68. Na kwa sababu ya kut'ii kwao kwa uweza wao inakuwa hakika Mwenyezi
Mungu amewaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka isio pindukia kiasi kwa kuzidi
au kupungua.
69. Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume kwa kuzifuata kwa unyenyekevu
amri zao na kuridhia hukumu yao, basi huyo yu pamoja na alio waneemesha
Mwenyezi Mungu kwa uwongofu na kuwawezesha duniani na Akhera. Na watu hao
ni Manabii wake, na wafuasi wao walio wasadiki na kuwakubali na wakafuata
nyendo zao, na Mashahidi walio kufa katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na watu
wema watendao mema kwa siri na dhaahiri. Na hapana la kushinda uzuri
kuliko kuwa pamoja na watu hawa - haingii mashakani mwenye kukaa nao, wala
hayachoshi mazungumzo yao.
70. Hayo ni makao matukufu kwa mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume
wake. Hiyo ni fadhila kubwa inayo tokana na Mwenyezi Mungu. Naye anavijua
sana vitendo vyenu, naye atakulipeni kwavyo. Yamtosha Muumini kuwa Mwenyezi
Mungu anamjua, naye lake ni kumt'ii Mola wake Mlezi na kutafuta radhi zake.
71. Enyi Mlio amini! Daima kuweni na hadhari na maadui wenu. Jizatitini
kupambana na vitimbi vyao. Na mkitoka kwenda vitani tokeni kwa vikosi vikosi,
au tokeni nyote pamoja.
72. Na wahadharisheni wanao kaa nyuma wasende
nanyi vitani. Miongoni mwa hao hao mnao ishi nao wakajizuia wasifuatane
nanyi kwenda kupigana, mkipatwa na shida na masaibu katika Jihadi, wao
wa kikundi hicho, kwa kufurahia yaliyo kusibuni, husema: Mwenyezi Mungu
katufanyia kheri kwa kuwa hatukwenda nao vitani.
73. Na mnapo pata fadhila ya ushindi kutokana na Mwenyezi Mungu,
mkapata ngawira za vita, kikundi hicho hicho, kwa kuona maya na kutamani,
husema: Laiti tungeli kuwa nao katika vita hivi, nasi tukapata mafanikio
ya ngawira nzuri. Na husema haya na hayo kama kwamba hapakuwepo mapenzi
yoyote yaliyo wafunga wao na nyinyi.
74. Ikiwa yupo kati yenu anaye bakia nyuma asende kupigana kutokana
na udhaifu wa Imani yake, au ulegevu wa azma yake, basi na wapigane, kuinua
Neno la Mwenyezi Mungu na kuwania Haki, wale walio uza uhai wao wa dunia
kutafuta uhai wa Akhera. Na mwenye kupigana vita kwa ajili ya kunyanyua
Neno la Mwenyezi Mungu na kuwania Haki, atapata moja ya mema mawili. Ama
atauliwa apate fadhila ya kufa shahidi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, au
atashinda, apate fadhila ya kufuzu katika dunia. Naye katika hali zote
mbili atapewa na Mwenyezi Mungu ujira mkubwa katika Akhera.
75. Vipi inakufalieni kuwa msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu
na hali wanyonge, wanaume na wanawake na watoto wao, wanayayatika kuomba
msaada wa kuwanusuru, huku wakimwomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu wakisema:
Ewe Mola Mlezi wetu! Tutoe kwenye utawala wa hawa madhaalimu, na
kwa nguvu zako na rehema yako tuwezeshe tuwe chini ya utawala wa Waumini;
na tujaalie kutoka kwako mgombozi wa kutunusuru!
76. Walio isadiki Haki na wakaifuata, hupigana kwa ajili ya kulitukuza
Neno la Mwenyezi Mungu, na uadilifu, na Haki. Na wale wanao pinga wakafanya
inadi hupigana kwa ajili ya dhulma na uharibifu. Kwa hivyo hawa wamekuwa
ni vipenzi vya Shetani. Basi enyi Waumini! Wapigeni vita hao, kwani wao
ni wenzake Shetani na wasaidizi wake. Na jueni kuwa nyinyi mtawashinda
tu kwa kuungwa mkono na Mwenyezi Mungu, kwani mpango wa Shetani, na ingawa
mkubwa vipi ufisadi wake, ni dhaifu, hauna nguvu. Na Haki ndiyo yenye ushindi.
77. Ewe Muhammad! Hebu huwaangalii ukawastaajabia wale walio taka
kupigana kabla ya kuja ruhusa, wakaambiwa: Bado haujafika wakati wa vita.
Basi izuieni mikono yenu msipigane. Bali shughulikieni kushika Sala, na
kutoa Zaka. Na Mwenyezi Mungu alipo waamrisha wapigane kikawa kikundi
kimoja kati yao kikawa kinawaogopa watu kama kumkhofu Mwenyezi Mungu, au
zaidi. Wakasema kwa kuona ni mageni hayo: Kwa nini ukatuamrisha kupigana?
Wao walidhani kuwa kuamrishwa vita kunahimiza ajali yao, na kwa hivyo wakasema:
Hebu lau ungeli tungojea muda kidogo tupate kustarehe na ulimwengu!
Waambie: Songeni mbele mkapigane hata ikiwa mtakufa mashahidi, kwani starehe
ya dunia, ingawa ni kubwa vipi, ni chache ukilinganisha na starehe ya Akhera.
Na Akhera ni bora na kubwa zaidi kwa mwenye kumcha Mwenyezi Mungu, na huko
mtakuja lipwa kwa vitendo vyenu vya duniani, wala hampunguziwi hata chembe
katika ujira wenu.
78. Hakika hayo mauti mnayo yakimbia yatakukuteni popote pale mlipo,
na hata mkikaa ndani ya ngome zilizo jengwa madhubuti imara. Na hao wenye
imani legevu na dhaifu husema pindi wapatapo ushindi na ngawira:
Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu. Na pindi wapatapo lawama
au kushindwa wao hukwambia wewe: Ewe Muhammad! Haya yanatokana na
wewe. Haya si lolote ila kukufanya kuwa wewe ni mkorofi, na kukutupia
lawama wewe badala ya nafsi zao. Basi waambie: Kila linalo kupateni,
mnalo lipenda na mnalo lichukia, linatokana na kudra ya Mwenyezi Mungu,
na linatokana na majaribio yake na mitihani yake. Wana nini watu hawa madhaifu
hata hawajakaribia kujua usawa wa maneno wanayo ambiwa?
79. Ewe Nabii! Kufanikiwa, na neema, na afya, na salama unayo ipata
inatokana na fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako. Yeye anafanya haya kukufadhili
kukufanyia hisani. Na inapo kusibu shida, na mashaka, na udhiya, na ya
karaha, basi yanatokana na nafsi yako mwenyewe kwa sababu ya upungufu fulani
au makosa uliyo yatenda. Haya anaambiwa Mtume s.a.w. ni kama mfano wa wanaadamu
wote ijapo kuwa halikutokea kwake la uovu. Kwani Mtume anaambiwa: Tumekutuma
kuwa Mtume kutoka kwetu kwa watu wote. Na Mwenyezi Mungu ni shahidi wa
kufikisha kwako huo ujumbe na juu ya kuitikia kwao hao watu. Na Yeye ni
Mjuzi wa kutosha.
80. Mwenye kumt'ii Mtume basi ndio amemt'ii Mwenyezi Mungu, kwani
yeye haamrishi ila alicho amrisha Mwenyezi Mungu. Wala hakatazi ila alicho
kataza Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo kumt'ii yeye (Mtume s.a.w.) ndio kutenda
na kuacha kwa ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kukataa kukut'ii wewe
basi, kwani Sisi hatukukupeleka wewe ila uwe ni mbashiri na mwonyaji tu,
sio uwe ni mlinzi wao na muangalizi wao, uwalindie vitendo vyao.
Hayo ni yetu Sisi sio yako.
81. Na kikundi hichi kinacho tapatapa husema: Amri yako tunait'ii.
Hatuna kwako ila kut'ii unayo amrisha na kukataza. Lakini wakisha
toka kwako wakawa mbali nawe, baadhi yao hupanga vijambo vyao usiku usiku,
kinyume na unavyo waambia ya kuwaamrisha na kuwakataza. Na Mwenyezi Mungu,
Subhanahu wa Taa'la, Aliye takasika na Kutukuka, anayadhibiti yote wanayo
yapanga kwa siri. Basi usiwashughulikie, na wapuuze, na mwachie mambo yao
Mwenyezi Mungu, na wewe mtegemee Yeye. Na Mwenyezi Mungu ni wa kutosha
kuwa ni Mtegemewa wako, na Mlinzi wako wa kumwachilia mambo yako yote.
82. Basi hao wanaafiki hawakizingatii Kitabu cha Mwenyezi Mungu wakajua
hoja za Mwenyezi Mungu zilio juu yao kuwa ni waajibu kut'ii na kufuata
amri yako? Na kwamba Kitabu hichi kinatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa yalivyo
shikamana maana yake na hukumu zake, na kinavyo fungamana wenyewe kwa wenyewe?
Hii ni dalili kuwa ni kweli kinatoka kwa Mwenyezi Mungu; kwani lau kuwa
kinatokana na mwenginewe basi maana yake yangeli gongana, na hukumu zake
zingeli khitalifiana sana.
83. Na hichi kikundi cha wanaafiki kikipata khabari zozote zilio
khusu nguvu au udhaifu wa Waislamu huzitangaza na kuzieneza nje, ili kuwababaisha
Waislamu au kuwatia khofu katika nyoyo zao, au ili zifike khabari zao kwa
maadui wao. Na lau kuwa hawa wanaafiki watangazao wamerudisha jambo
lilio khusu usalama au kitisho kwa Mtume na kwa wakuu wa mambo miongoni
mwa waongozi na Masahaba wakubwa, wakataka kwao kujua hakika, wangeli jua
hao wanao jitahidi kuchungua mambo na kuyatangaza, kuwa yaliyo kweli yanatokana
na Mtume na waongozi wengine. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi
Mungu juu yenu kwa alivyo zithibitisha nyoyo zenu juu ya Imani, na kuzuia
fitina, na rehema yake kwa kukupeni sababu na njia za ushindi, wengi wenu
wangeli fuata upotovu wa Shetani, na wasingeli okoka kutokana na upotovu
wake ila wachache tu.
84. Na kama wapo kati yenu mfano wa hawa wanaafiki basi wapuuzilie
mbali. Na wewe pigana kwa ajili ya Neno la Mwenyezi Mungu na kwa ajili
ya Haki. Wewe huna jukumu ila la nafsi yako tu. Kisha waite Waumini wende
vitani, na wahimize. Huenda Mwenyezi Mungu kwa kupitia kwako na kwao akazuia
hayo mashambulio ya makafiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukuungeni mkono,
na ni Mwenye kukunusuruni. Na Yeye ana nguvu kuliko wote, na mkali kuliko
wote katika kuwaadhibu makafiri.
85. Na hawa wanaafiki husaidia ufisadi, na watu wa Imani husaidia
Haki. Na mwenye kusaidia jambo jema ana fungu lake la thawabu. Na mwenye
kuwasaidia watu waovu naye ana mzigo wake wa dhambi katika malipo yake.
Na Mwenyezi Mungu ana uweza juu ya kila kitu, na Mwenye kujua kila kitu.
86. Akikuamkieni mtu yeyote kwa maamkio ya salamu, au dua, au ya
namna yoyote ya hishima, au namna nyengine yoyote ile, basi mjibuni kwa
maamkio yaliyo mazuri zaidi, au kwa uchache mjibuni kama alivyo kuamkieni
yeye. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kutia hisabuni kila kitu, kikubwa
na kidogo.
87. Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu ila Yeye, wala hapana mwenye
uweza ila Yeye, hapana shaka atakufufueni baada ya kufa kwenu, na atakukusanyeni
kwenye kituo cha kuhisabiwa kwa ajili ya malipo. Hayo hayana shaka. Yeye
anasema hayo, basi msiyatilie shaka maneno yake. Na kauli gani iliyo ya
kweli zaidi kuliko kauli ya Mwenyezi Mungu?
88. Haikufaliini, enyi Waumini, kukhitalifiana katika mas-ala yaliyo
khusu wanaafiki, ambao wanadhihirisha Uislamu na wanaficha ukafiri. Haikufaliini
kukhitalifiana kwa mas-ala yao, kuwa ati wao ni Waumini au makafiri? Wauwawe
au waachiliwe? Je, wameelekea kuongoka au hawatarajiwi uwongofu?
Fahamu zao zimegeuzwa kwa yaliyo chumwa na vitendo vyao. Shari imekuwa
ndio inayo wahukumu, basi usimtarajie kuongoka yule ambaye Mwenyezi Mungu
kwa ujuzi wake wa tangu na tangu kesha mkadiria asiongoke. Kwani
aliye andikwa katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu wa tangu azali kuwa ni mwenye
kupotea basi huna njia ya kumwongoa.
89. Hakika nyinyi mnapenda kuwaongoa hawa wanaafiki, na wao wanapenda
nyinyi mkufuru kama wao, ili muwe nyote sawa kwa ukafiri. Ilivyo
kuwa hivyo basi msitake wa kukuungeni mkono miongoni mwao. Wala msiwafanye
wenzenu, mpaka wakubali kutoka huko kwao kuwania Jihadi kwa ajili ya Uislamu.
Hivyo tu ndio itawatoka sifa ya unaafiki. Lakini wakiyakataa hayo, wakaungana
na maadui zenu, basi wauweni popote mtapo wapata, wala msiwaone kuwa
ni wenzenu, wala msiwachukulie kuwa ndio wasaidizi wenu.
90. Katika wanaafiki, wanao stahiki kuuliwa kwa fisadi yao kuwafisidi
umma wa Waumini, watoe wale ambao wamefungamana na kaumu ambao baina yao
na Waumini yapo mapatano ya kuzuia kuuliwa aliye fungamana na upande mmoja
wapo. Au vile vile ambao wametatizwa hawajui wapigane pamoja na watu wao,
ambao ni maadui wa Waislamu wasio na mkataba nao, au wapigane pamoja na
Waumini? Kwani hakika wale wa kwanza inakatazwa kuwauwa kwa ajili ya mkataba,
na wengine inakatazwa kuwauwa kwa kuwa hawajui moja wapo la kutenda.
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amependa angeli wajaalia hao wakupigeni
vita. Ilivyo kuwa wamekhiari kukaa tu wasikupigeni na wakaingiana nanyi
kwa salama na amani, basi haikufaliini nyinyi kuwauwa. Hapana ruhusa kufanya
hayo.
91. Mkiwashinda washirikina, hao wanaafiki huwa pamoja nanyi; na
washirikina wakiwashinda Waislamu, wao huwa pamoja na washirikina. Wao
hutaka wapate amani kwa Waislamu na wapate amani kwa jamaa zao washirikina.
Hawa wamo katika upotovu na unaafiki wa moja kwa moja. Ikiwa hawatoacha
kukupigeni vita na wakakutangazieni amani na salama, basi wauweni popote
muwapatapo. Kwani kwa kuto kujitenga na kukupigeni vita, basi inakuwa Waumini
wana haki kuwauwa. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa Waumini hoja iliyo
wazi kuwapiga vita.
92. Kuwagawa wanaafiki namna hii ni kwa ajili ya kutoka shakani,
ili Muumini asimuuwe Muumini mwenziwe kwa kumdhania kuwa ni mnaafiki. Na
haijuzu kumuuwa Muumini ila kwa kukosea, bila ya kukusudia. Na katika
hali ya kumuuwa Muumini kwa kukosea akiwa anaishi chini ya utawala wa dola
ya Kiislamu, basi atatoa muuwaji diya kuwapa walio fiwa kuwa ni fidia kwa
mtu waliye mkosa, na tena amkomboe mtumwa aliye Muumini iwe ni kuwafidia
umma wa Kiislamu kwa walicho kosa. Kwani kumkomboa Muumini ni kama kumhuisha
mtu kwa kumpatia uhuru. Inakuwa kwa kukomboa shingo ya Muumini ni kuulipa
umma wa Kiislamu kwa walicho kosa.(1)
Ikiwa aliye uliwa yumo katika watu ambao wana mapatano ya amani
na Waislamu, basi yapasa kumpa uhuru mtumwa na kuwalipa watu wa maiti diya,
kwani inakuwa hawaichukui hiyo diya kwa kuwaudhi Waislamu kwa sababu ya
mapatano yao. Na ikiwa mwenye kuuwa bila ya kukusudia hakupata mtumwa Muumini
wa kumkomboa, basi afunge miezi miwili mfululizo, asile mchana hata siku
moja. Hayo yawe ni kuitengeza nafsi na kujizoesha kuwa na hadhari zaidi.
Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika na Aliye tukuka anazijua sana nafsi za
watu na niya zao. Naye ni Mwenye hikima, anajua kuzipanga adhabu zake.
(1)"Kuulipa" kwa kuwa utumwa ni amana ya mtu, na kumkomboa
mtumwa ni kumhuisha mtu. Akiuliwa Muumini kwa kukosea, na mwenye kuuwa
akakomboa shingo ya Muumini basi huyo amehuisha na kuulipa umma.
93. Hakika mwenye kumuuwa Muumini kwa mauwaji ya kukusudia na kuona
ndio ndivyo mauwaji hayo, jaza yake inayo lingana na ukhalifu huo ni kuingizwa
Motoni milele, na kughadhibikiwa na Mwenyezi Mungu na afukuzwe kutokana
na rehema yake. Na Mwenyezi Mungu amemtengezea Akhera adhabu kubwa, kwani
kitendo hichi ndio ukhalifu mkubwa kabisa katika dunia.
94. Kutahadhari msije mkamuuwa Muumini ni waajibu katika wakati wa
kwenda vitani. Mkisafiri kwa ajili ya Jihadi ya Njia ya Mwenyezi Mungu
jijuvyeni hakika ya hao mnao pigana nao kabla ya kupambana. Je, hao wamesilimu
au bado ni washirikina. Wala msimwambie anaye kutoleeni salamu kuwa
ni ishara ya amani: Wewe si Muumini, kwa kuwa mnataka kumnyang'anya
mali yake na kondoo wake. Bali ipokeeni salamu yake, kwani kwa Mwenyezi
Mungu amekuahidini kupata ngawira nyingi nyenginezo. Na nyinyi, enyi Waumini!
Mlikuwa hivyo hivyo katika ukafiri kabla ya hayo, na Mwenyezi Mungu amekuhidini.
Basi hakikisheni mambo ya hao mnao wakuta. Na Mwenyezi Mungu anajua baraabara,
na hapana chochote kinacho fichikana kwake. Na Yeye hakika ni Mwenye kuhisabu
kwa mujibu wa ujuzi wake.
95. Na hakika Jihadi pamoja na kuchukua hadhari inayo takikana ina
fadhila kubwa sana. Basi hawawi sawa wanao kaa majumbani mwao wasende kupigana
Jihadi na wale Mujaahidiina, wanao pigana kwa mali yao na nafsi zao. Kwani
Mwenyezi Mungu amewanyanyua wale Mujaahidiina daraja, cheo cha juu kuwashinda
wale wanao kaa nyuma; ila ikiwa wale wanao kaa nyuma wana udhuru unao wazuia
kutoka kwenda vitani. Hapo inakuwa udhuru wao unawatoa lawamani, juu ya
kuwa wanao pigana wana fadhila na cheo makhsusi. Mwenyezi Mungu amewaahidi
makundi yote mawili mashukio mema, na matokeo mazuri.
96. Na cheo hichi walicho khusishwa nacho hao wanao pigana Jihadi
ni cheo kikubwa, cha juu, hata imekuwa ni kama cheo cha kutafautisha
sana baina yao na wengineo. Na kwa ajili ya cheo hichi watapata maghfira
makubwa na rehema kunjufu.
97. Na hakika ni waajibu wa Muislamu kuhamia kwenye dola ya Kiislamu
asiishi katika udhalili. Malaika watawauliza wakisha kufa: Mlikuwaje hata
mkaridhia maisha ya unyonge na kudharauliwa? Na wao watajibu: Tulikuwa
wanyonge katika nchi hiyo tukionewa. Malaika watawaambia: Kwani ardhi ya
Mwenyezi Mungu haikuwa kunjufu ina wasaa, mkaweza kuhama badala ya kuishi
katika uonevu? Watu hao wanao kubali uonevu, na wao wanaweza kuondoka,
makao yao yatakuwa ni Jahannamu. Na hayo ni mashukio maovu kabisa.
Basi Muislamu haimfalii kuishi katika udhalili, bali aishi na utukufu wake
na hishima yake.
98. Juu ya hivyo wanasameheka na adhabu hii wale wasio weza kusafiri
miongoni mwa wanaume, na wanawake, na watoto, wasio na nguvu, na hawana
hila, wala hawakupata njia ya kutoka.
99. Na hao wanatarajiwa kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu. Na ni shani
yake Mwenyezi Mungu kusamehe na kughufiria.
100. Anaye hama kutafuta njia za kuiwania Haki na kuiunga mkono,
atakuta duniani kwingi endako ambako maadui wa Haki wanahizika. Na atapata
wasaa wa uhuru, na makao ya hishima,na thawabu, na ujira mkubwa. Aliye
toka kwake kuhamia dola ya hishima, ambayo ndiyo dola ya Mwenyezi Mungu
na Mtumewe, kisha yakamdiriki mauti kabla hajafika endako, basi ujira wake
umethibiti. Mwenyezi Mungu amemkirimu kwa kujiwajibishia kumlipa ujira
wake, na kumghufiria na kumrehemu. Ni shani yake kughufiria na kurehemu.
101. Sala ni faridha isiyo epukika. Haiachiki Sala kwa ajili ya safari,
lakini hana dhambi anaye fupisha Sala safarini. Watokao kwenda safari wakikhofia
kuwa makafiri watawaletea ya kuwaudhi, wanaweza kufupisha Sala. Sala za
rakaa nne zisaliwe rakaa mbili. Kutahadhari na kuingiliwa na makafiri ni
waajibu, kwani wao ni maadui, na uadui wao uwazi.
102. Ewe Nabii Muaminifu, ukiwa nao na Sala ya Jamaa inasaliwa, msisahau
kutahadhari na maadui. Na hayo ni kuwagawa Waislamu makundi mawili. Moja
lianze kusali kwa kukufuata wewe, na wakati huo la pili lisimame kwa hadhari
na silaha likilinda vifaa. Ukisha nusu ya Sala, kundi lilio sali nawe lende
nyuma yako, na lije jengine lisali nawe Sala iliyo bakia. Kisha litimize
sehemu waliyo ikosa. Na lile la kwanza lisali baki ya Sala. Na hii huitwa
"Laahiqah", yaani iliyo kutwa (1) na nyengine inaitwa "Masbuuqah", yaani
iliyo tanguliwa ,kwa kuwa inasaliwa mwanzo wa Sala ya Jamaa; na "Laahiqah"
inasaliwa mwisho wa Sala ya Jamaa. Mpango huu ni kwa sababu isikosekane
Sala, na kutahadhari na makafiri ambao wanapenda mghafilike na silaha zenu
na vifaa vyenu wapate kukuvamieni kwa ghafla, na wakumalizeni nanyi mmo
katika Sala. Vita na washirikina ni waajibu, na havina ukomo. Lakini hapana
dhambi juu yenu kusita kwa ajili ya udhuru kama mvua au maradhi, juu ya
kuwa lazima muwe na hadhari ya kudumu. Na hii ni adhabu ya Mwenyezi Mungu
kwa makafiri hapa duniani, na Akhera amewaandalia adhabu ya fedheha na
udhalili.
(1) "Laahiq" ni anaye sali na Imam mwanzo wa Sala na akalazimika
kusali iliyo baki peke yake, na "Masbuuq" anaye iwahi sehemu ya mwisho
ya Sala ya Jamaa, kisha akatimiza sehemu aliyo ikosa peke yake.
103. Na mkisha Sala ya vita, inayo itwa Sala ya Khofu, msisahau kumkumbuka
Mwenyezi Mungu daima. Mkumbukeni nanyi mmesimama, mnapigana, mmekaa, na
mmelala. Kwani kumkumbuka Mwenyezi Mungu Mtukufu kunatia nguvu nyoyo, na
kuzituliza. Khofu ikiondoka pakawa na utulivu basi timizeni Sala kwa ukamilifu,
kwani Sala imefaridhiwa juu ya Waumini isaliwe kwa nyakati zake.
104. Msilegee kuwafukuzia makafiri walio kwisha kukutangazieni vita
na wanajaribu kukushambulieni kila pahala. Hakika vita havikosi maumivu.
Ikiwa nyinyi Waumini mmepata majaraha na mengineyo, na wao makafiri pia
wameyapata machungu. Khitilafu yenu ni kuwa wao hawapiganii Haki, wala
hawataraji kitu kwa Mwenyezi Mungu; na nyinyi mnataka Haki na mnataraji
radhi za Mwenyezi Mungu na neema za kudumu. Na Mwenyezi Mungu anavijua
vitendo vyenu na vyao, naye ni Mwenye hikima, anamlipa kila mtu kwa alitendalo.
105. Tumekuteremshia hii Qur'ani kwa haki na kwa kweli. Imekusanya
kila lilio la haki. Inabainisha haki mpaka Siku ya Kiyama, ili iwe ni taa
yako ya kukupa mwangaza kuwahukumu watu. Basi hukumu baina yao, wala usiwepiganie
walio makhaaini.
106. Na unapo hukumu baina ya watu muelekee Mwenyezi Mungu, na ukumbuke
utukufu wake, na uombe maghfira yake na rehema yake. Kwani kughufiria na
kurehemu ndio shani yake Subhanahu wa Taa'la.
107. Wala usiwatetee wale wanao fanya khiana, na wakaendelea mno
katika kuificha hiyo khiana katika nafsi zao. Kwani Mwenyezi Mungu hampendi
ambaye mtindo wake ni khiana na kufanya madhambi.
108. Wanajificha, na wanataka kujisitiri kwa watu wasiione khiana
yao. Wala hayumkini kuzificha khiana zao kwa Mwenyezi Mungu, na ilhali
Yeye daima yu pamoja nao. Na wao usiku usiku hukubaliana kwa maneno yasiyo
mridhi Mwenyezi Mungu ya kuwasingizia tuhuma watu wasio na makosa. Na Mwenyezi
Mungu Mtukufu anajua vyema, na hapana kitu kinacho weza kujificha na ujuzi
wake.
109. Ikiwa nyinyi mnawatetea hao wakosa wasipate adhabu ya duniani,
basi hatopatikana wa kuwatetea Siku ya Kiyama mbele ya Mwenyezi Mungu na
kukubali kuwa ni mlinzi wao wa kuwasaidia.
110. Mlango wa toba, hakika, uwazi. Anaye tenda kitendo kiovu cho
chote, au akajidhulumu nafsi yake kwa kufanya maasi, kisha akamtaka msamaha
Mwenyezi Mungu Mtukufu, atamkuta Mwenyezi Mungu yu tayari kukubali toba
yake, na kumghufiria madhambi yake. Kwani ndio mwendo wake Mwenyezi Mungu
kughufiria na kurehemu.
111. Hakika madhara ya madhambi ni juu ya yule yule ayatendayo. Mwenye
kuchuma madhambi basi anajidhuru mwenyewe. Na alitendalo linamuangukia
mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika na kutukuka anajua aliyo yatenda,
na atamchukulia kwa mujibu wa hikima yake. Atamuadhibu au atamsamehe kwa
mujibu wa hikima yake.
112. Na mwenye kutenda makosa na madhambi kisha akamsingizia mwenginewe
asiye na kosa alilo litenda - kama vile mwizi kaiba kitu kisha akamsingizia
wizi mtu mwengine - mtu huyo ana dhambi mbili. Moja ni uwongo na uzushi,
na la pili lile kosa lilio wazi la kwiba.
113. Lau kuwa Mwenyezi Mungu hakukufadhili kwa kukuteremshia Wahyi,
Ufunuo, na akakupa rehema ya kutambua na kufahamu hakika, kikundi cha wapotovu
kingependa kukupoteza. Lakini hawapotezi ila nafsi zao. Kwani Mwenyezi
Mungu ni muangalizi wako, na ndiye mwenye kukuonyesha haki. Hayakufikilii
madhara ya mipango yao na upotezi wao. Yeye Mwenyezi Mungu amekuteremshia
Qur'ani Tukufu ambayo hiyo ndiyo mizani ya haki, na ameutuza moyo wako
kwa hikima, na amekufundisha Sharia na hukumu ambazo ulikuwa hukuzijua
ila kwa kufunuliwa na Yeye. Hakika fadhila za Mwenyezi Mungu juu yako daima
ni kubwa.
114. Hakika wale wanao kaa wakipanga mambo yao kisirisiri, mambo
hayo hayana kheri, kwa sababu shari ndio huchipuka katika ufichoni.
Lakini ikiwa mazungumzo hayo ni kwa jambo la sadaka ya kuwapa watu, au
kufanya jambo lolote lisio baya, au kupanga mipango ya kusuluhisha baina
ya watu, hayo si mabaya. Kwani hayo ni mambo ya kheri. Na mwenye kufanya
hivyo kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataa'la, basi Mwenyezi
Mungu atampa malipo makubwa duniani na Akhera.
115. Na anaye mpinga Mtume s.a.w. baada ya kwisha itambua Njia ya
Haki na Uwongofu, na akaifuata njia isiyo kuwa ya Waumini, na akaingia
kwenye urafiki na maadui wa Waumini, basi huyo atakuwa na hao. Kwani amekhiari
kuwa hao ndio wawe marafiki zake na walinzi wake. Mwenyezi Mungu atakuja
mtia Motoni Siku ya Kiyama.
116. Hakika mwisho huu wa kuumiza ni wao hao vile vile, kwani hao
ni maadui wa Uislamu. Mfano wake ni mfano wa mwenye kumshirikisha Mwenyezi
Mungu. Hakika kila dhambi yaweza kughufiriwa, ila kumshirikisha Mwenyezi
Mungu, na kumuabudu mwenginewe asiye kuwa Yeye, na kumpinga Mtume katika
Haki. Ni shani ya Mwenyezi Mungu kusamehe madhambi, ila
dhambi ya kumshirikisha Yeye katika ibada. Kwa jenginelo lisilo kuwa hili
Yeye humsamehe amtakaye. Anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu katika ibada
na kumtegemea, basi huyo ameipotea Haki, na amekuwa mbali nayo mno; kwani
mtu huyo ameifisidi akili yake na nafsi yake pia.
117. Katika upotovu ulio wazi kabisa ambao uko mbali na Haki
ni ule wa mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Huyo anaabudu kitu ambacho
hakisikii wala hakioni, hakidhuru wala hakinafiishi. Na huita hiyo miungu
yake kwa majina ya kike, kama Laata na Uzza na Manaata na mengineyo ya
majina ya kike. Yeye hakika kwa hivyo anamuabudu Shetani.
118. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amekwisha mfukuza huyu
Shetani kutokana na kivuli cha rehema yake, na amemjaalia awe katika njia
ya upotovu. Na Shetani ameapa, na amejichukulia ahadi mwenyewe, kuwa atachota
miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu idadi maalumu awapumbaze kwa
upotovu wake na awatie wasiwasi kwa shari yake.
119. Hakika kiapo chake Shetani ni kuwa atawapoteza wale anao wapumbaza
kwa kuwatenga mbali na Haki, na kuchochea pumbao lao na matamanio yao,
mpaka wakawa wamepotea wanatanga tanga katika mawazo na tamaa za uwongo.
Wakisha kuwa katika kuzainiwa huku na tamaa hizo chini ya utawala wake
Shetani, tena huwatokomeza kwenye mambo yasiyo ingia akilini, na huwapelekea
hao wafikiri kufanya hayo ni ibada. Na ilhali haya yote ni mawazo
ya uwongo tu. Basi huwatia wasiwasi wakatenda mambo, kama kwa mfano kuwakata
masikio baadhi ya ngamia wao, wageuze khulka aliyo iumba Mwenyezi Mungu.
Wakafanya kuwa ngamia aliye katwa masikio yake hachinjwi, wala hafanyishwi
kazi, wala hazuiliwi kwenda machungani atakavyo. Yote haya ni kwa amri
yake Shetani kuwazaini. Tena huwatia wasiwasi mpaka wakaona kuwa hayo ni
katika dini. Na hakika wao inakuwa wanamfuata yeye Shetani, na wanamfanya
yeye ndiye wa kuwanusuru, na ndiye wa kumfuata badala ya Mwenyezi Mungu.
Na mwenye kumfanya Shetani ndiye msaidizi wake wa kumfuata, basi amekhasiri
khasara kubwa iliyo wazi. Kwani hapo anakuwa amepotea njia ya Haki, na
ameipumbaza akili yake, na utampata ufisadi duniani, na adhabu Akhera.
120. Shetani huwapambia shari, wakaiona nzuri, na huwaahidi manufaa
watayo pata pindi wakitenda kitendo fulani, na huwatia katika nafsi zao
matumaini ya kuyatumai. Na hapana lolote analo waahidi na analo wapambia
ila ni udanganyifu mtupu.
121. Hakika hao walio zipoteza akili zao na wakafuata wasiwasi wa
Shetani anao watia katika nafsi zao, mwisho wao ni kuendea Jahannamu, wala
hawatapata njia ya kutoka huko.
122. Huu ndio mwisho wa wafuasi wa Shetani. Ama mwisho wa wafuasi
wa Mwenyezi Mungu ni mzuri. Wao ndio walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume
wake, na wakatenda mema, wala hawazugwi na mawazo ya uwongo. Hakika Siku
ya Kiyama Mwenyezi Mungu Mtukufu atawatia katika mabustani yapitayo mito
kati yake, chini ya vivuli. Na hayo ni makubwa mno kuliko bustani hizi
za duniani. Na hayo ni yakini, kwani ahadi hizo ni ahadi za Mwenyezi Mungu,
na ahadi zake haziwi ila ni hakika isiyo geuka, wala haina udanganyifu.
Yeye ni mmiliki wa kila kitu. Wala haiwezi kufikirika kuwa yupo yeyote
yule aliye mkweli kwa neno lake na ahadi yake kuliko Mwenyezi Mungu.
123. Malipo siyo ayatamaniyo mtu na kuyaota bila ya vitendo vyema
vizaavyo matunda. Malipo siyo myatamaniyo nyinyi, Waislamu.
Wala siyo wayatamaniayo na kuyaota Ahlu-l-Kitabi, Watu wa Biblia, Mayahudi
na Wakristo. Bali malipo na kuepukana na adhabu ni kwa Imani na Vitendo
Vyema. Atendaye maovu atalipwa kwa vitendo vyake. Wala hampati mlinzi wala
wa kumnusuru ila Mwenyezi Mungu.
124. Watendao mema, kwa kadiri ya uwezo wao nao wanamuamini Mwenyezi
Mungu na Mtume wake, wataingia kwenye Pepo ya neema, wala hawatapunguziwa
hata chembe. Na hapana khitilafu baina ya malipo ya mwanamume na ya mwanamke,
kwani mwanamke naye ana waajibu wake, malipo ya vitendo vyema, na adhabu
kwa vitendo vibaya.
125. Msingi wa vitendo vyema ni itikadi iliyo sawa. Na bora
ya dini ni kumtakasikia niya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ukawa uso wako, na
akili yako, na nafsi yako, yote haitaki kitu isipo kuwa kumridhi Mwenyezi
Mungu Subhanahu. Kwa hivyo basi ndio fahamu zako zitanyooka sawa kuufahamu
ujumbe wa Mitume, na ndio utaweza kushika daima vitendo vilivyo bora, na
ukamfuata Baba wa Manabii, Ibrahim a.s. Kwani dini yake Ibrahim ndiyo Dini
ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo Dini inayo elekeza kutaka Haki daima. Na kwa
Ibrahim ndiyo umekutana umoja wa Dini, kwa Waislamu, na Mayahudi na Wakristo.
Basi ifuateni njia yake. Mwenyezi Mungu hakika amemkirimu Ibrahim, akamwita
"Rafiki Mwendani".
126. Hakika wa kumtakasia niya ni Mwenyezi Mungu, na ndio kwake Yeye
inapasa uusilimishe uso wako, yaani umuelekee na umnyenyekee. Huko ndiko
kumsafia niya Mwenyezi Mungu aliye umba ulimwengu wote, na ndiye mwenye
kuumiliki. Vitu vyote viliomo mbinguni na duniani - nyota, sayari, jua,
mwezi, milima, mabonde, majangwa, mashamba n.k. ni vya Mwenyezi Mungu.
Yeye ndiye Mwenye kubainikiwa na kila kitu, Mwenye kujua kwa ujuzi mkamilifu
wa kuvizunguka vitu vyote avitendavyo mwanaadamu. Na Yeye atamlipa
kheri akitenda kheri, na shari akitenda shari.
127. Watu walimtaka Mtume s.a.w. awambie nini hukumu ya sharia juu
ya wanawake. Na wanawake walikuwa, na wangali bado kuwa, ni watu wanyonge.
Basi Mwenyezi Mungu amembainishia Nabii wake ili naye abainishe hali ya
wanawake, na hali ya wanyonge wengine katika ukoo miongoni mwa watoto na
mayatima. Na akataja kuwa mayatima wanawake ambao wanaolewa wala hawachukui
mahari yao, na watoto, na mayatima, wote hao watendewe kwa uadilifu na
huruma na kuraiwa. Na kwamba kila kheri itendwayo basi hakika Mwenyezi
Mungu anaijua, na Yeye ndiye atakaye ilipa.
128. Na mwanamke akikhofia kuwa mumewe anapuuza mambo ya nyumbani
au anayatupa, hayajali, wala hayashughulikii, basi hapana dhambi kwa wote
hao wawili kutafuta njia za kusuluhiana kwa mapatano mema na kukurubiana.
Na mwenye akili kati yao ni yule anaye anza kutaka masikizano. Na suluhu
daima ina kheri, haina shari ndani yake. Linalo zuia masikizano ni kule
kuwa kila mmoja kung'ang'ania haki yake kwa ukamilifu, na ugumu na uchoyo
wa nafsi unapo wamiliki watu. Wala hapana njia ya kurejeza mapenzi ila
mmojapo kati ya wawili kulegeza kamba. Na huyo ndiye mwema, mchamngu, mwenye
kujihifadhi na dhulma. Na mwenye kutenda vitendo vyema na akamcha Mwenyezi
Mungu, basi Mwenyezi Mungu anayo khabari ya vitendo vyake, na atamlipa
kwavyo.
129. Kuwafanyia uadilifu wake kwa mapenzi ya daima yasiyo chafuliwa
na udanganyifu, na kutendeana usawa katika mapenzi ikawa nipe nikupe,
ni jambo lisilo wezekana kuwa. Kadhaalika haiwezi kuwepo usawa
katika kuwapenda wake, ikiwa kuna zaidi kuliko mke mmoja. Walakini mkijitahidi,
basi msimfanyie ujeuri mmoja wapo, mkamili upande mmoja, na mkamwacha mwengine
si mke si mt'alaka. Yapasa mjitengeneze, na muendeshe nyumba zenu kwa wema
si kwa ufisadi. Na mcheni Mwenyezi Mungu apate kughufirieni na akurehemuni.
Ni shani yake kughufiria na kurehemu.
130. Ikiwa suluhu haikumkinika na ikawa chuki (au karaha) imeshika
nguvu zaidi, basi inalazimika kufarikiana. Na wakifarikiana Mwenyezi
Mungu atawatosheleza kila mmoja wao kutokana na ukunjufu wa
rehema yake na fadhila yake. Na riziki ziko katika mikono ya Mwenyezi Mungu,
na Yeye ndiye Mwenye hikima, na hupanga mambo yote kwa mipango yake.
131. Kiini cha Dini ni kumnyenyekea Mwenye kuumba ulimwengu,
Mwenye utukufu na ukarimu, na kuukubali ufalme wake usio
na ukomo. Kwani ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni
na katika ardhi. Na kwa huu
Ufalme usio na ukomo amesema: Tumewausia watu wa dini zilizo toka
mbinguni, katika Watu wa Kitabu na nyinyi Waislamu, mumkhofu
Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na msiwe mnakufuru katika ibada
yake, maana Yeye ndiye Mwenye utawala mkubwa kushinda wote. Hapana kitu
kilicho toka nje ya utawala wake. Yeye ni Mkwasi, yaani mwenye kujitosha
wala hakuhitajiini nyinyi. Juu ya hivyo Yeye anakuhimidini kwa imani yenu,
kwani kwa kuwa Yeye ni Mwenye kujitosheleza mwenyewe, juu ya hivyo anasifu
na kushukuru vitendo vyema vya waja wake.
132. Kupanga kila kitu cha mbinguni na duniani ni kazi ya Mwenyezi
Mungu Aliye takasika na Aliye tukuka. Yeye ndiye Mwenye madaraka, Mwenye
kuendesha, Mwenye kupanga. Yatosha kuwa Yeye ndiye Mtawala aliye amrisha
ulimwengu ukajipanga ulivyo jipanga, na akawaamrisha watu wamuabudu, na
wamtegemezee Yeye mambo yao, na wamche Yeye.
133. Hakika nyinyi enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Mko chini ya ufalme
wa Mwenyezi Mungu Mwenye uweza na Mwenye nguvu. Akipenda atakufisheni
na alete wengine kabisa. Na Yeye Mwingi wa Utukufu ni Muweza
wa hayo, na Muweza wa kila kitu.
134. Na watu, pindi wakitafuta neema za dunia zilizo halali kwa njia
ya haki iliyo nyooka sawa, basi hakika Mwenyezi Mungu atawapa neema za
duniani na Akhera; kwani Yeye ndiye aliye miliki neema zote mbili.
135. Uadilifu ndio nidhamu ya maumbile. Na hiyo ndiyo sharia ambayo
haiwezi kuwapo ndani yake maoni ya kukhitalifiana. Basi enyi mlio mt'ii
Mwenyezi Mungu wa Haki, na wito wa Mitume wake, kuweni macho nafsi zenu
katika kuut'ii uadilifu, na kuweni macho kwa ajili ya watu. Mfanyieni insafu
aliye dhulumiwa, na msimame imara, si kwa ajili ya kumpendelea tajiri,
au kumwonea huruma masikini. Kwani Mwenyezi Mungu aliye waumba matajiri
na masikini anastahiki zaidi kuangalia hali ya tajiri au fakiri. Matamanio
ndiyo yanayo mpelekea mtu kumili nafsi yake, basi msiyafuate matamanio
mkaacha uadilifu. Na mkikengeuka mkaacha uadilifu, au mkapuuza kusimamisha
uadilifu, basi mjue Mwenyezi Mungu anayajua myatendayo, tena anayajua kwa
ujuzi wa ndani. Naye atakulipeni kwa mujibu wa a'mali yenu; ikiwa njema
mtalipwa wema, ikiwa ovu mtalipwa shari.
136. Kwa hakika Ujumbe wa mbinguni ni mmoja, kwa kuwa yule Mwenye
kutuma ni Mmoja, naye ni Mwenyezi Mungu. Basi enyi mlio amini! Mt'iini
Mwenyezi Mungu na mumsafie niya. Na msadikini Mtume wake Muhammad, na msadiki
yaliyo kuja katika Kitabu chake alicho mteremshia, na mtende yaliyo amrishwa
humo. Na sadikini Vitabu vilivyo teremshwa kabla yake kama alivyo
teremsha Mwenyezi Mungu bila ya mageuzo wala kusahau. Aminini yote hayo.
Kwani mwenye kumkanusha Mwenyezi Mungu, Muumba wa viumbe vyote, na Malaika,
na Mwenye kuyajua yaliyo fichikana, na Vitabu vya Mwenyezi Mungu na Mitume
wake, na akaikanusha Siku ya Mwisho, basi huyo ameipotea Njia Iliyo Nyooka,
na ametokomea mbali katika njia ya upotovu.
137. Hakika Imani ni kuit'ii Haki kusio kuwa na ukomo, na kunako
endelea daima. Basi wanao taradadi wakababaika si Waumini. Hao ambao wanaamini,
kisha wakakufuru, kisha wakaamini, kisha wakakufuru, na kwa hivyo wakazidi
ukafiri wao - Mwenyezi Mungu hatakuwa wa kuwaghufiria watu hao hivyo vitendo
vyao viovu, wala hatawaongoa kwenye Haki. Kwani kusamehe kwa Mwenyezi Mungu
kunahitajia toba, na kujing'oa na shari, na uwongofu wake ni kwa wale wanao
ielekea Haki na wanaitaka.
138. Ewe Mtume Mtukufu! Waonye wanaafiki kwamba Siku ya Kiyama watapata
adhabu chungu yenye kuumiza.
139. Hao wanaafiki huufanya utawala wa makafiri uwe juu yao, na wanawawacha
Waumini. Basi hebu hivyo wanataka wapate utukufu kwa hawa makafiri? Hakika
utukufu uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye huwapa waja wake wenye kuamini.
Na mwenye kutaka utukufu kwa Mwenyezi Mungu atatukuka, na mwenye kutaka
utukufu kwa mwenginewe atadhalilika.
140. Mwenyezi Mungu amekwisha kuteremshieni katika Qur'ani Tukufu
kwamba kila mkisikia Aya za Kitabu nyinyi mnaamini, na makafiri wanapinga
na wanakejeli. Na ikiwa hivyo ndiyo hali ya makafiri na wanaafiki, na mkasikia
kejeli zao, basi msikae nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine waache
dhihaki zao. Na nyinyi ikiwa hamtofanya hivyo, mkawa mnasikiliza kejeli
zao, basi mtakuwa nanyi kama wao katika kuifanyia maskhara Qur'ani. Mwisho
wa makafiri na wanaafiki ni muovu mno, kwani Mwenyezi Mungu atawakusanya
wote hao katika Moto wa Siku ya Kiyama.
141. Mtindo wa wanaafiki ni kukungojeeni kama anavyo
ngojea mwenye husda na maya anaye tamani mpate masaibu mnapo kuwa katika
vita na maadui. Mkishinda kwa nusra ya Mwenyezi Mungu, na mkafungukiwa
njia ya Haki, wao huwaambia Waumini - na hali wao ule ushindi walio pewa
wenye Imani na Mwenyezi Mungu umewashtusha : Sisi hatukuwa nanyi? Kwa maana
sisi ni jamaa zenu! Na ikiwa ni zamu ya makafiri kupata ushindi,
basi wao huwaendea na kuwaambia: Sisi hatukuyashughulikia mambo yenu hata
yakawa ni yetu? Na hatukukupeni mapenzi yetu, na tukakulindeni na hawa
Waumini? (yaani sisi ni wenzenu). Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la
atakuhukumuni baina yenu na hawa wanaafiki Siku ya Kiyama. Wala Mwenyezi
Mungu hatowapa makafiri njia kuwashinda Waumini maadamu Waumini watashikamana
na sifa ya Imani ya kweli na vitendo vyema.
142. Hakika wanaafiki, kwa ule unaafiki
wao, wanadhani kuwa wanamkhadaa Mwenyezi Mungu Mtukufu na wanamficha
hakika ya nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Yeye ndiye anaye
wakhadaa wao. Basi Yeye huwapururia kuwapa muhula, na anawawacha mpaka
wabobee katika maovu yao, kisha ndio awahisabu kwa waliyo yatenda. Na hawa
wanaafiki wana dhaahiri ya kuonekana, na ya ndani ya nafsi zao. Yale
ya kuonekana ni vile kuwa wakiinuka kwenda kusali huinuka kwa uvivu,
kwa unyong'onyo. Na sala yao ni riya tu, kuonyesha, si ya kweli. Na ya
ndani ni kuwa hawakumbuki kumtaja Mwenyezi Mungu ila kwa nadra, kwa tukizi.
Na lau kuwa wanamkumbuka vilivyo wangeli uacha unaafiki
143. Na hawa wanaafiki ni watu wanao taradadi, wanababaika. Kwenu
hawapo, na kwao makafiri hawapo katika kila hali. Na hayo ni kwa
sababu ya udhaifu wa imani, na udhaifu wa nafsi, na kwa sababu ya kupotoka
na Haki. Na mwenye kuandikiwa kupotoka na Mwenyezi Mungu tangu hapo azali,
basi huna njia wewe ya kumwongoa sawa.
144. Hakika katika sababu za unaafiki ni kuwa wanaafiki wamewafanya
watu wasio kuwa Waumini kuwa ndio walinzi wao, marafiki zao, watawala wao,
na ndio wa kuwanusuru. Enyi Waumini! Yaacheni haya, muepukane nayo. Wala
msiwafanye makafiri ndio wa kukunusuruni, wakukutawalini, mkawanyenyekea.
Na hapana shaka yoyote mkifanya hivyo mnampa Mwenyezi Mungu hoja iliyo
wazi ya kukuhojini. Mtakuja ingia pamoja na wanaafiki, na mtadhalilika.
Kwani inakuwa hamfanyi utukufu wenu utoke kwa Mwenyezi Mungu, na kwa haki,
na vitendo vyema.
145. Hakika wanaafiki kwa sababu ya unaafiki wao watakuwa katika
vina vya Jahannamu. Wao wako chini kabisa huko, na daraja ya mwisho kabisa.
Wala hutompata wa kuwanusuru, wa kuwatetea na adhabu hiyo.
146. Isipo kuwa wale katika wao walio tubia, na wakarejea kwa Mwenyezi
Mungu Mtukufu, na wakaungana naye Yeye peke yake, na wakajitakasa, na wakaelekeza
nyuso zao kwake, na wakatenda mema. Wakifanya haya basi ndio wanakuwa miongoni
mwa Waumini. Watapata malipo ya Waumini. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amekwisha
waahidi Waumini malipo makubwa duniani na Akhera.
147. Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hana alitakalo kwenu ila mumuamini
Yeye, na muishukuru neema yake. Mkiwa hivyo basi hampati adhabu, bali mtapata
malipo ya kheri na shukrani. Kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye
kushukuria waja wake kwa vitendo vyema, na ni Mjuzi, anajua hali zao zote
njema na mbaya.
148. Mwenyezi Mungu anawakataza waja wake wasiseme maneno maovu,
ila yule aliye patwa na dhulma. Ni halali kwake kumshitaki aliye mdhulumu,
na autaje uovu aliyo tendewa. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mwenye kusikia
vyema maneno ya aliye dhulumiwa. Na ni Mjuzi wa dhulma ya mwenye kudhulumu.
Na atamlipa kwa kitendo chake hicho.
149. Mkiyadhihirisha mema myatendayo, au mkayaficha, au mkamsamehe
anaye kufanyieni uovu, Mwenyezi Mungu atakulipeni kwa kufuata khulka yake
Mtukufu, ya kusamehe na hali ana uwezo kaamili. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu
ni mwingi mno wa kusamehe, Mwenye kukamilika uwezo wake.
150. Hakika wasio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wanao
taka kufanya ubaguzi katika imani ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na
wanasema: Tunawaamini baadhi ya Mitume, sio wote, hao wanawaamini wawapendao
na wanawakataa wasio wapenda. Na lilio waajibu ni kuwaamini wote, kwani
Imani haikubali kukatwa mapande mapande.
151. Hawa wote ndio walio ungama ukafiri wao ulio wazi. Na Mwenyezi
Mungu amekwisha waahidi wao na mifano ya hao adhabu kali yenye kudhalilisha.
152. Na ama wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, wala hawakumkanusha
hata mmoja wapo kati yao, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atawalipa malipo
makubwa kwa ajili ya Imani yao iliyo kamilika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi
wa maghfira kwa wenye kutubu, na ni Mwenye kuwarehemu waja wake.
153. Ewe Mtume! Watu wa Kitabu, yaani Mayahudi wapendao
kuudhi, wanakutaka ulete dalili ya ukweli wa unabii wako. Uwaletee kitabu
makhsusi kiwateremkie kutoka mbinguni kithibitishe ukweli wa utume wako,
na kiwatake wakuamini na kukut'ii! Ukiyaona makuu hayo wayatakayo, wewe
usifanye haraka. Kwani wenzao walio tangulia walifanya kero vile vile,
wakamtaka Musa makubwa kuliko hayo. Walimwambia: Tuonyeshe Mwenyezi Mungu
tumwone kwa macho. Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa lile kero lao na dhulma
yao kwa kuwapiga radi iliyo wateketeza!! Kisha watajie hawa watu
kosa kubwa zaidi na ovu zaidi, nalo ni pale walipo mfanya ndama kuwa ni
mungu wao, wakamwacha Mwenyezi Mungu aliye waumba. Haya baada ya kwisha
ona dalili zote alizo zionyesha Musa kwa Firauni na kaumu yake!! Kisha
juu ya hayo Mwenyezi Mungu akawakunjulia usamehevu wake kwao, na Mwenyezi
Mungu akampa nguvu Musa kwa hoja zilio wazi, na neno madhubuti.
154. Mwenyezi Mungu akaunyanyua mlima juu ya Wana wa Israili ili
kuwatisha kwa kule kuikataa kwao sharia ya Taurati, mpaka wakaikubali.
Akachukua kwao agano, na akawaamrisha waingie mjini hali wakimnyenyekea
Mwenyezi Mungu. Wala wasiyakiuke aliyo waamrisha kushika ibada katika siku
ya Sabato, yaani Jumaamosi.(Imeitwa "Sabt" Kiarabu, "Shabbath" Kiyahudi,
"Sabbath" Kiingereza, na "Sabato" Kiswahili, maana yake "Mapumziko" kwa
kuwa ni siku ya mapumziko kwa Mayahudi.) Na Mwenyezi Mungu alichukua kwao
ahadi ya nguvu.
155. Mwenyezi Mungu akawakasirikia kwa sababu ya kuvunja agano hili,
na kuzikataa ishara za Mwenyezi Mungu, na kwa kuwauwa Manabii kwa dhulma,
na kuendelea katika upotovu wao kwa kusema: Nyoyo zetu zimefungwa hazikubali
hayo unayo tuitia! Nao hawasemi kweli katika kauli yao hiyo, bali Mwenyezi
Mungu amezifuta nyoyo zao kwa ukafiri wao, basi ni wachache tu kati yao
wanao amini.
156. Na Mwenyezi Mungu amewaghadhibikia
Mayahudi kwa sababu ya kufru yao na kumzulia Maryam uzushi
mkubwa.
157. Na Mwenyezi Mungu pia amewaghadhibikia kwa kusema
kwao uwongo: Hakika sisi tumemuuwa Masihi Isa bin Maryamu, Mtume wa Mwenyezi
Mungu. Na kweli ya yakini ni kuwa hawakumuuwa kama wanavyo zua. Wala
hawakumsalibu kama wanavyo dai. Lakini walifananishiwa, nao wakadhani kuwa
wamemuuwa na wamemsalibu. Na hakika walimuuwa na kumsalibu aliye shabihiana
naye. Nao wakaja kukhitalifiana baada ya hayo, kuwa aliyeuwawa ni Isa au
mtu mwengine? Na wote hao, kwa hakika, wamo katika shaka tu juu ya jambo
hilo. Kweli iliyopo ni kuwa hawana ujuzi nayo mambo haya, ila ni dhana
dhana tu. Kabisa hawakumuuwa Isa. (Wataalamu wa Biblia mpaka hii leo wamo
kuzozana katika jambo hili. Mwenye kuzichungua Injili zinazo kubaliwa na
Wakristo ataona kuwa hazina uthibitisho kuwa aliye salibiwa ndiye Yesu,
au hata huyo naye alikufa msalabani au la.)
158. Bali Mwenyezi Mungu alimtukuza kwake, akamwokoa na maadui zake,
wasimsalibu na wasimuuwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda, hashindiki,
ni Mwenye hikima katika vitendo vyake. (Taaurati inayo kubaliwa na Mayahudi
na Wakristo imesema kuwa anaye kufa kwa kutundikwa msalabani amelaaniwa.
Ndio maana Mayahudi wakawa na hamu wamtundike Nabii Isa ili wathibitishe
kuwa huyo si chochote ila ni mlaanifu. Je, Mwenyezi Mungu Mtukufu vipi
aachilie jambo hilo liwe kwa Mtume wake?)
159. Na hapana mmojapo katika Watu wa Kitabu (Mayahudi na Wakristo)
ila atakuja tambua uhakika wa Isa (kuwa ni Nabii wa kweli wa Mwenyezi Mungu,
si mwana haramu, wala si mwana wa Mungu) kabla ya kufa kwake, na kuwa yeye
Isa ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na atakuja amini imani ambayo
haitomfaa kitu, kwa kuwa wakati wake umekwisha pita. Na Siku ya Kiyama
Isa atatoa ushahidi juu yao kuwa yeye alifikisha ujumbe, na kuwa yeye ni
mtumwa wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
160. Kwa sababu ya udhalimu wao Mayahudi Mwenyezi Mungu amewapa adabu
- amewakataza vyakula mbali mbali vilivyo vizuri, vimekuwa kwao haramu,
na ilhali kwanza vilikuwa halali kwao. Na kwa udhalimu wao wamewazuia watu
wengi wasiingie katika Dini ya Mwenyezi Mungu.
161. Na kwa sababu ya kupenda kula riba - na Mwenyezi Mungu alikwisha
wakataza hayo - na kuchukua mali ya watu kwa njia isiyo ya haki, ndio ikawa
adabu ya dini ni kuwazuilia na kula vyakula vilivyo vizuri. Na Mwenyezi
Mungu amewawekea hao walio kufuru adhabu yenye kutia machungu.
162. Lakini walio bobea katika ilimu, yaani wataalamu kweli kweli,
miongoni mwa Mayahudi, na Waumini katika umma wako, ewe Nabii, wanasadiki
wahyi ulio funuliwa wewe, na walio letewa Mitume wa kabla yako. Na wanao
shika Sala baraabara, na wanatoa Zaka, na wanamuamini Mwenyezi Mungu na
kufufuliwa na hisabu, hao Mwenyezi Mungu atawalipa malipo mema kabisa kwa
imani yao na ut'iifu wao.
163. Hakika Sisi tumekufunulia wewe, ewe Nabii! (tumekuteremshia
Wahyi), Qur'ani na Sharia, kama tulivyo wafunulia kabla yako Nuhu na Manabii
wa baada yake, na kama tulivyo wapa Wahyi Ibrahim, na Ismail, na Is-haq,
na Yaakub, na wajukuu zake, nao wale walio kuwa Manabii wa Mwenyezi Mungu
miongoni mwa dhuriya (wazao) wa Yaakub, na Isa, na Ayubu, na Yunus, na
Haarun, na Suleiman, na kama tulivyo mfunulia Daud tukamteremshia Kitabu
cha Zabur.
164. Kadhaalika tumewatuma Mitume wengi ambao tumekwisha taja khabari
zao kabla yake. Na Mitume wengine hatukukusimulia hadithi zao. Na njia
ya kumpa Wahyi Musa ilikuwa Mwenyezi Mungu akisema naye moja kwa moja nyuma
ya pazia, lakini bila ya kuwepo mwengine kati.
165. Tuliwapeleka Mitume hao kuwapa bishara njema ya thawabu wenye
kuamini, na kuwaonya adhabu wale walio kufuru, ili watu wasiwe na hoja
ya kumtafutia kisababu Mwenyezi Mungu baada ya kwisha wapeleka Mitume.
Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, ni Mshindi, wala hana yeyote
madaraka pamoja naye, na ni Mwenye hikima kwa atendayo.
166. Lakini ikiwa hao watu hawashuhudii kukusadikisha, basi Mwenyezi
Mungu Mwenyewe anashuhudia kuwa aliyo kuteremshia ni sahihi. Hakika Yeye
amekuteremshia hayo kwa hikima, na kwa mujibu wa ujuzi wake. Na Malaika
nao wanashuhudia hayo kadhaalika. Na ewe Mtume! Yakutosha wewe ushahidi
wa Mwenyezi Mungu, kuliko ushahidi wowote mwenginewe.
167. Hakika wale ambao wamekufuru wasikusadiki wewe, na wakawazuia
watu wasiingie katika Dini ya Mwenyezi Mungu, bila ya shaka wamekuwa mbali
mno na Haki.
168. Wale walio kufuru, na wakajidhulumu nafsi zao, na wakamdhulumu
Mtume kwa kuupinga ujumbe wake, na wakawadhulumu watu walipo wafichia Haki,
Mwenyezi Mungu hatowasamehe kamwe maadamu watabaki katika ukafiri wao.
Wala hatawapa uwongofu wa kuijua njia ya kuvuka. Sio mtindo wake Subhanahu
kuwasamehe watu kama hao nao wangali kubaki katika upotovu wao.
169. Lakini atawapeleka kwenye njia ya Motoni, na humo wabakie daima
dawamu. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jambo jepesi.
170. Enyi watu! Amekwisha kukujieni Mtume huyu, Muhammad, na Dini
ya Haki kutokana na Mola Mlezi wenu. Basi yaaminini aliyo kuja nayo; ndiyo
itakuwa kheri yenu. Na pindi mkikataa ila kukufuru tu, basi mjue kwamba
Mwenyezi Mungu ni Mkwasi na imani yenu, hana haja nayo. Yeye ndiye Mwenye
kukumilikini nyinyi. Kwani vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi
ni vyake Yeye, kwa kuvimiliki, kuviumba na kuviendesha atakavyo. Naye ni
Mwenye kuvijua vyema viumbe vyake, ni Mwenye hikima katika uendeshaji wake.
Haupotezi ujira wa mwema, wala hapuuzi kumlipa mwovu.
171. Enyi Watu wa Kitabu! Msipindukie haki,
mkazidisha kupita kiasi katika dini yenu, wala msimzulie uwongo Mwenyezi
Mungu, mkaukanya utume wa Isa, au mkamfanya kuwa ni Mungu pamoja na Mwenyezi
Mungu. Kwani Masihi ni Mtume kama walivyo Mitume wengine. Mwenyezi Mungu
amemuumba kwa uwezo wake na neno lake alilo mbashiria kwalo,
na Jibrili akampulizia Maryamu roho ya Mwenyezi Mungu. Hii ni siri katika
siri za uwezo wake Mwenyezi Mungu. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume
wake wote imani ya kweli. Wala msidai kuwa katika Ungu kuna Utatu!!
Tokeni katika upotovu huu, itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mungu mmoja tu, wala hana mshirika wake. Naye ametakasika na kuwa na mwana!
Na kila kilioko katika mbingu na ardhi ni chake. Na Yeye Mwenyewe anajitosha
peke yake kuwa ni Mwendeshaji wa Ufalme wake. (Kuitwa Nabii Isa Neno au
Roho iliyo toka kwa Mungu, hakumpi Ungu. Yeye ni neno kwa kuumbwa kwa amri
ya "Kun", "Kuwa" akawa. Haya ni kuwapinga Mayahudi walio dai kuwa yeye
ni mwanaharamu. Basi wanaambiwa kuwa ameumbwa kama vilivyo umbwa vitu vyote,
kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Naye ni Roho iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu
kama walivyo pewa Waumini wote (58.22) na alivyo puliziwa Adam (15.29)
na kwa hivyo wanaadamu wote (32.7-9). Hapana hata pahala pamoja katika
Injili ziliomo katika Biblia ambapo Yesu (Nabii Isa a.s.) alijiita mwenyewe
Mwana wa Mungu. Kila mara akijiita Mwana wa Adamu. Na alipo mwita Mungu
Baba, alikusudia ni Baba wa watu wote, kama alipo sema: "Ninapaa kwenda
kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu."
Injili ya Yohana 10.33-36.)
172. Masihi hakujiona bora hata akatae kuwa ni mtumwa wa Mwenyezi
Mungu, wala hawakujiona bora Malaika walio karibishwa. Na mwenye kutakabari
na kujiona mtu wa juu hataweza kuikimbia adhabu ya Mwenyezi Mungu
Siku atakayo wakusanya watu kwa ajili ya hisabu.
173. Ama walio amini wakatenda mema atawalipa thawabu za vitendo
vyao, na atawazidishia kwa fadhila yake, kwa kuwakirimu na kuwaneemesha.
Na ama wale walio kataa kumuabudu, na wakajiona bora wasimshukuru, hao
amewaandalia adhabu yenye machungu makali. Hapana msaidizi wa kuwakinga
nayo wala wa kuwanusuru.
174. Enyi watu wote! Zimekwisha kujieni dalili zilizo wazi za ukweli
wa Mtume Muhammad. Na tumekuteremshieni kwa ulimi wake Qur'ani iliyo wazi
kama mwangaza, unao angaza Njia, na inayo kuongozeni kwendea mafanikio.
175. Ama walio msadiki Mwenyezi Mungu na ujumbe wake alio leta, na
wakaifuata Dini yake, atawatia katika Bustani zake Akhera, na atawamiminia
rehema yake, na atawakusanya katika ukunjufu wa fadhila yake, na atawawezesha
hapa duniani kuthibiti katika Njia yake Iliyo Nyooka.
176. Ewe Nabii! Wanakuuliza vipi atarithiwa aliye kufa naye akawa
hana mwana, wala mzazi. Sema: Hakika hukumu ya Mwenyezi Mungu katika urithi
wa hawa ni kuwa, akiwa maiti ana ndugu wa kike basi atapata nusu ya tirka.
Na akiwa maiti ni mwanamke naye ana ndugu wa kiume basi atarithi mali yote.
Na ikiwa ameacha ndugu wawili wa kike, basi watapata hao thuluthi mbili
(1) ya urithi. Na ikiwa hao ndugu ni mchanganyiko wanaume na wanawake,
basi fungu la mwanamume ni sawa na mafungu mawili ya wanawake. Mwenyezi
Mungu anakubainishieni haya msije mkapotea katika kugawa mafungu ya urithi.
Na Mwenyezi Mungu ni Mkamilifu wa ujuzi wa a'mali zenu na vitendo vyenu
vyote. Na atakulipeni kwavyo. (Angalia: Urithi wa ndugu katika Aya hii
ni wa ndugu khalisa, yaani ndugu kwa baba na mama, au ndugu kwa baba. Ama
urithi wa ndugu kwa mama tu umekwisha tajwa katika Aya 12 ya Sura hii ya
Annisaa.)
(1) Na Sunna (Mafunzo ya Mtume) imebainisha kuwa wakizidi kuliko
ndugu wa kike wawili, pamoja na Aya ya mirathi iliyo tajwa, kuwa wakizidi
kuliko binti wawili, watachukua thuluthi mbili. Ni bora kuwa zaidi kuliko
ndugu wawili wa kike, kwa sababu mabinti ni karibu zaidi kwa maiti.
Tuzingatie kuwa kwa mujibu wa kanuni za Kizungu za kurithi, ambazo
zimetokana na kanuni ya Kirumi, ndugu wanaume wala wa kike wala watoto
wao hawarithi. Na juu ya hivyo mwenye mali anayo ruhusa kumkata yeyote
asipate urithi wake. Uislamu umekataza haya. Warithi lazima wapate urithi
wao, ila mtu anayo haki ya kuandika wasia kujihukumia kisicho zidi thuluthi
moja ya mali yake.(W.H. Ingrams katika kitabu chake Zanzibar Its History
and Its People ameandika: "Hakika Sharia Takatifu yaonekana kuwa ni ya
haki zaidi sana kuliko hata mpango wa Kiingereza wa kugawanya mali.
Katika Zanzibar [na bila ya shaka katika Waislamu wote] hapana mwendo wa
kuwa mtu "kukatwa urithi akabakishwa na shilingi moja tu"; vyo vyote vile,
ni sehemu ndogo tu ndiyo inaweza kuandikiwa wasia, na yaliyo baki lazima
yagawiwe kwa warithi kwa mujibu wa kiwango maalumu.")