1. Qur'ani imeteremka kutokana na Mwenyezi Mungu, ambaye
hana wa kumshinda kwa atakayo; Mwenye hikima katika vitendo vyake na utungaji
wa sharia zake.
2. Hakika Sisi tumekuteremshia wewe, Muhammad, Qur'ani hii yenye
kuamrisha Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia ibada Yeye
tu peke yake.
3. Jueni na mtambue kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye
Dini isiyo kuwa na ila. Na washirikina walio wafanya wenginewe kuwa ni
wasaidizi wa kuwanusuru, wanasema: Sisi hatuwaabudu hawa kwa kuwa ni waumbaji,
bali tunawaabudu wapate kutukaribisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa mkaribisho
wa kutuombea sisi kwake Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina ya
hawa washirikina na Waumini wenye kumuabudu Mwenyezi Mungu Mmoja katika
yale wanayo khitalifiana katika matatizo ya shirki na Tawhidi. Hakika Mwenyezi
Mungu hamjaalii afikie Haki mtu ambaye mtindo wake ni uwongo na kukanya.
4. Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa na mwana, kama wasemavyo
Wakristo kwa Masihi, na washirikina kwa Malaika, basi angeli jichagulia
amtakaye katika viumbe vyake, la sio kama mtakavyo nyinyi. Mwenyezi Mungu
ametakasika na upungufu wa kuhitajia mwana. Yeye ni Mwenyezi Mungu asiye
kuwa na mfano kama Yeye. Mtenda kama apendavyo, ukomo wa kutenda.
5. Ameumba mbingu na ardhi kwa kushikamana na Haki na kuwa sawa kwa
kufuatana na sharia zilizo thibiti. Usiku unaufunika mchana, na mchana
unaufunika usiku kwa mfululizo. Na amedhalilisha jua na mwezi kwa mujibu
atakavyo na kwa mujibu wa maslaha ya waja wake. Kila kimojapo katika hivyo
vinakwenda katika njia yake mpaka ufike wakati aliyo uwekea Yeye, nao ni
Siku ya Kiyama. Jueni basi kuwa Yeye tu, si mwenginewe, ndiye Mwenye kushinda
kila kitu. Basi hapana kitu chochote kilicho tokana na atakavyo Yeye, ambaye
amefikilia ukomo wa kuwasamehe wenye kutenda madhambi katika waja wake.
Aya hii tukufu inaonyesha kuwa ardhi ina sura ya mviringo
kama mpira, na inazunguka wenyewe kwa wenyewe juu ya msumari-kati wake.
Kwani kule kutumiwa neno Yukawwiru katika Kiarabu na ikafasiriwa Hufunika,
maana yake ni kufunika kitu kwa kitu kwa namna ya kufuatana, kukariri,
mara kwa mara. Na lau kuwa ardhi haina sura ya mpira, kwa mfano kuwa batabata
tu, usiku ungeli enea kote kwa ghafla, au mchana ungeli angaza dunia nzima
kwa mara moja.
6. Enyi watu! Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na nafsi moja,
naye ni Adam, baba wa watu wote. Na amemuumba kutokana na nafsi hiyo mkewe,
Hawa. Na amekuteremshieni kwa ajili ya maslaha yenu namna nane za nyama
hoa, wanyama wa mifugo, madume na majike. Nao ni ngamia, na ng'ombe, na
kondoo, na mbuzi. Naye anakuumbeni matumboni mwa mama zenu kwa kukua na
kugeuka geuka, katika viza vitatu, navyo ni kiza cha tumbo, na tumbo la
uzazi, na zalio. Huyo aliye kuneemesheni kwa neema hizi ndiye Mwenyezi
Mungu, Mlezi wenu, Mwenye kumiliki mambo yenu yote. Ni Yeye tu, si mwenginewe,
ndiye Mwenye utawala wa pekee. Hapana wa kuabudiwa kwa Haki ila Yeye. Basi
yawaje hata wanaacha kumuabudu Yeye wakenda kuwaabudu wenginewe?
Huzuka yai katika mwahala pa kufanyika mayai kwa mwanamke, hata
likisha kuwa tayari hutumbukia katika mojapo ya paipu za Filopia likapita
humo mpaka kufikia kwenye tumbo la uzazi Rahimi (Womb). Halifiki
huko ila kupita siku kidogo, na huenda kijidudu cha manii (Sperm) ya mwanamume
kikaliingia hilo yai, na hapo huanza viwango vya kugeuka na kukua kwa mwanzo.
Na katika tumbo la uzazi hubaki mtoto muda wa mimba, na hujifanyia vifuniko
viwili, na sehemu ya funiko moja hufanyika zalio, placenta. Na funiko jingine
ndio humfunika yule mtoto khasa.
Yapo maoni mbali mbali juu ya hivyo "viza vitatu" kama ilivyo tajwa
katika Aya hii tukufu. Katika hayo ni
(1) Tumbo, na tumbo la uzazi, na zalio, yaani mfuko unao mfunika
mtoto.
(2) Tumbo la uzazi, na ile mifuniko miwili.
(3) Tumbo na mgongo na tumbo la uzazi.
(4) Panapo toka mayai (Mabiidh, au Ovaries), na paipu ya kupitia
mayai, Fillopian tube, na tumbo la uzazi (Rahimi au Womb).
Na dhaahiri ni kuwa hii ya mwisho ndiyo rai yenye nguvu zaidi, kwa
sababu ni mahala patatu mbali mbali. Ama zile rai nyengine zinaonyesha
kwa hakika kiza kimoja katika pahala pamoja palipo zungukwa na t'abaka
kadhaa. Na Muumbaji Mtukufu ameashiria katika Kitabu chake ukweli huu wa
kisayansi katika zama walipo kuwa watu hawajavumbua hayo mayai ya mwanamke
na mwendo wake katika mwili ulio kuwa hauwezi kuonekana kwa macho.
7. Enyi watu! Mkizikataa neema za Mwenyezi Mungu, basi Yeye hakika
si mhitaji wa imani yenu na shukrani zenu. Lakini Yeye hapendi waja wake
wakufuru, kwa sababu hayo yanawadhuru wenyewe. Na mkimshukuru kwa ajili
ya neema zake, Yeye huwa radhi nanyi kwa shukra hiyo. Wala mtu mwenye madhambi
hayabebi madhambi ya mwenginewe. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi,
na hapo atakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda duniani. Hakika Yeye anayajua
mnayo yaficha katika nyoyo zenu ziliomo vifuani.
Haya yaliomo katika Qur'ani Tukufu yanaweka wazi msingi wa kutoa
adhabu, kama ilivyo vile vile katika Surat Yusuf katika kauli yake Mtukufu:
"Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali sisi kumshika yeyote ila tuliye
yakuta mali yetu kwake; hivyo basi tutakuwa madhaalimu." Na haya katika
Qur'ani ni kusimamisha msingi ulio kwisha tajwa, nao ni msingi ambao haukuthibiti
katika kanuni (sharia) za kutungwa na binaadamu ila katika zama za karibuni.
(Haya ni kinyume cha ilivyo katika imani aliyo itumbukiza Paulo katika
Ukristo, kwamba wanaadamu wamerithi dhambi ya Adam, wanayo ita "Dhambi
ya asili", na kwamba Nabii Isa, Yesu, kafa msalabani kwa kubeba dhambi
za wanaadamu. Biblia yenyewe inapinga haya. Tazama: Jeremiah 31:29-30;
Ezekieli 18 Kwa nadhariya ya Paulo Mungu amedhulumu mara mbili:
1. Kutubandika wanaadamu wote dhambi za Adam,
2. Kumbebesha "mwanawe" Yesu dhambi za walimwengu wote!)
8. Na mtu akifikiwa na shida yoyote katika shida za dunia humwomba
Mola wake Mlezi, na hurejea kwake, baada ya kuwa akimpuuza. Kisha Mola
wake Mlezi akimpa neema kubwa husahau zile taabu alizo kuwa akimwombea
Mola wake Mlezi amwondolee na amfarijie kabla hajamneemesha kwa neema hizo.
Na humfanyia Mwenyezi Mungu miungu washirika walio sawa na Yeye kwa kuwaabudu.
Huyo mtu hufanya haya ili ajipoteze yeye na wenginewe waiache Njia ya Mwenyezi
Mungu. Ewe Muhammad! Mwambie huyo mwenye sifa hizi kwa kumwonya: Starehe
na huko kuzikanya kwako neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yako kwa muda
mchache. Kwani hakika wewe ni katika watu wa Motoni.
9. Je! Mwenye kumnyenyekea Mwenyezi Mungu nyakati za usiku anao upitisha
na hali yeye yumo kusujudu na kusimama, akiiogopa Akhera, naye anataraji
rehema ya Mola wake Mlezi, ni kama anaye mwomba Mola wake Mlezi wakati
wa shida na akamsahau wakati wa neema? Ewe Muhammad! Waambie: Ati wanakuwa
sawa wenye kujua haki za Mwenyezi Mungu wakamuabudu Yeye tu peke yake,
na wale wasio jua wakapuuza kuziangalia Ishara? Hakika wenye akili nzuri
ndio wanao waidhika.
10. Ewe Nabii! Sema kwa kufikisha Ujumbe unao toka kwa Mola wako
Mlezi: Enyi waja wangu mlio niamini! Jikingeni na ghadhabu za Mola wenu
Mlezi. Mwenye kutenda mema atalipwa mema, duniani kwa kusaidiwa, na Akhera
kwa Pepo. Wala msikae katika unyonge, kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu ina
wasaa. Na subirini kwa kufarikiana na nchi zenu na wapenzi wenu. Kwani
hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wenye kusubiri ujira wao mara zisio ingia
katika hisabu za wanao hisabu.
11. Sema: Mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafia
ibada yangu isiwe na shirki ndani yake wala riya ya kujionyesha kwa watu.
12. Na nimeamrishwa amri iliyo tokana naye Mtukufu, amri ya nguvu,
ya kwamba niwe wa mwanzo wa kufuata amri zake.
13. Sema: Mimi naogopa adhabu ya Siku Kubwa yenye vitisho ikiwa nitamuasi
Mola wangu Mlezi.
14,15. Ewe Muhammad! Waambie: Ninamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake,
na ibada yangu haina shirki wala riya. Na nyinyi ikiwa mnaijua Njia
yangu nanyi hamnit'ii, basi abuduni mpendacho badala yake Yeye. Waambie:
Hakika wenye kupata khasara ni wale walio jitupa kwa upotovu wao wenyewe,
na wakawatupa ahali zao kwa kuwapoteza wao Siku ya Kiyama. Ama hakika
kupotoka huko ndio khasara iliyo timia na iliyo dhaahiri.
16. Hawa walio khasirika watakuwa na mat'abaka ya Moto yalio rindikwa
juu yao, na chini yao hali kadhaalika. Kwa namna ya adhabu hiyo ndio Mwenyezi
Mungu anawahadharisha waja wake. Enyi waja wangu! Basi yaogopeni mateso
yangu.
17,18. Na wale wanao jitenga na masanamu na mashet'ani wasiyakurubie,
na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu katika mambo yao yote, wanayo bishara tukufu
katika mwahala mote. Basi Ewe Muhammad! Wape bishara nzuri waja wangu wanao
sikiliza kauli na wakaifuata iliyo bora na yenye kuwaongoa kwendea katika
Haki. Hao tu, si wenginewe, ndio Mwenyezi Mungu atao wafikisha kwenye Uwongofu.
Na hao tu, si wenginewe, ndio wenye akili zilizo nawirika.
19. Je! Unaweza kuniingilia katika Ufalme wangu? Iliyo kwisha pita
juu yake hukumu ya kumuadhibu, je, wewe unaweza kuizuia? Unayo nguvu hiyo
wewe? Je! Unaweza kuwaokoa na Moto baada ya kwisha wathibitikia?
20. Lakini wenye kumkhofu Mola wao Mlezi watapata vyeo vya juu Peponi
na majumba yake ya fakhari, yenye kupitiwa chini yake na mito. Hiyo ni
ahadi ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu haendi kinyume na ahadi yake.
21. Ewe usemezwaye! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji
kutoka mbinguni, akayapitisha kwenye mito na chemchem za katika ardhi,
kisha kwa maji hayo akaotesha mimea ya namna mbali mbali. Kisha baada ya
kustawi kwake hiyo mimea, ikayabisika ukaiona imekuwa rangi ya manjano
baada ya kustawi kwake. Kisha akaifanya imevurugika na kukatika vipande
vipande. Hakika kutoka kwenye hali moja na kuingia hali nyengine ni mazingatio
kwa wenye akili zilizo nawirika.
Huku kuzunguka maji katika maumbile kutoka mbinguni na kufika kwenye
ardhi na huko yakenda chini na kutimbuka katika chemchem, hakukuwa kunajuulikana
kabla ya katikati za karne ya nane tangu kuzaliwa Nabii Isa a.s.
Fikra iliyo zagaa kabla ya hapo ni kuwa maji ya chemchem na mito yanatimbuka
kutoka chini ya ardhi kutoka kwenye mashimo na visima katika vina vya bahari.
22. Kwani watu wote ni sawa? Mwenye kufunguliwa kifua chake na Mwenyezi
Mungu kwa Uislamu kwa kupokea mafunzo yake, na akawa na utambuzi unao tokana
na Mola wake Mlezi, huyo basi ni kama yule anaye kataa kuangalia Ishara
zake? Basi hao ambao nyoyo zao zimekuwa ngumu hata hawamkumbuki Mwenyezi
Mungu watapata adhabu kali! Hao wenye nyoyo ngumu wameitupa Haki iliyo
wazi.
23. Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, nayo ni Kitabu
ambacho zimeshabihiana maana zake na matamko yake kwa kufikilia ukomo wa
kuwashinda watu kuleta mfano wake, na hukumu zake. Mawaidha na hukumu
zinakaririwa, kama kunavyo kaririwa kusomwa kwake. Kinapo somwa Kitabu
hicho na kikasikiwa maonyo yake, ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi
hukunjika, na kisha hulainika ngozi zao na nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi
Mungu. Hicho Kitabu kilicho kusanya sifa hizi ni Nuru ya Mwenyezi Mungu
ambayo kwayo humwongoa amtakaye, ikamwezesha kufikilia kumuamini Yeye.
Na anaye achwa na Mwenyezi Mungu apotee kwa kumjua kuwa tangu hapo ataiacha
Haki, basi hapati mwongozi wa kumwokoa na upotofu wake.
24. Kwani watu wote ni sawa? Mwenye kuikinga adhabu ovu, kali,
kwa uso wake Siku ya Kiyama baada ya kuwa mikono yake imetiwa pingu, ni
kama anaye kuja kwa amani Siku ya Kiyama? Na wenye kudhulumu wataambiwa:
Onjeni laana ya vitendo vyenu!
25. Walikanusha walio kuja kabla ya washirikina hawa, ikawajia adhabu
kutoka upande wasio utaraji.
26. Mwenyezi Mungu akawaonjesha unyonge katika maisha ya duniani.
Ninaapa: Hakika adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi kuliko ya duniani, lau
kwamba walikuwa ni watu wa kujua na kuangalia!
27. Na bila ya shaka tulikwisha wabainishia watu katika hii Qur'ani
kwa kila mfano wa kuwakumbusha Haki, kwa kutaraji kuwa watakumbuka na watawaidhika.
28. Tumeiteremsha Qur'ani ya Kiarabu kwa ulimi wao, haina upungufu,
kwa kutaraji kuwa watamcha na watamwogopa Mola wao Mlezi.
29. Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mshirikina kama mtumwa aliye
milikiwa na watu kadhaa wenye kushirikiana, na wenye kumgombania. Na mfano
wa mwenye kuamini Mwenyezi Mungu Mmoja kama mtu ambaye amemilikiwa na mtu
mmoja tu. Je hao wanakuwa sawa? Alhamdulillahi kwa kusimama hoja mbele
ya watu. Lakini watu wengi hawaijui Haki.
30,31. Hakika wewe, Muhammad, na wao wote mtakufa. Kisha baada ya
kufa kwenu mtafufuliwa mbele ya Mwenyezi Mungu mkishitakiana nyinyi kwa
nyinyi.
32. Basi hapana aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye msingizia
Mwenyezi Mungu lisio kuwa lake, na akaikanusha Haki bila ya kufikiri wala
kuzingatia pale inapo mjia kwa ndimi za Mitume. Kwani katika Jahannamu
sio makaazi ya makafiri walio ghurika hata wakamfanyia jeuri Mwenyezi Mungu?
33. Na wale walio ileta Haki na wakaisadiki ilipo wajia, hao ndio
wachamngu kweli, wala si wengineo.
34. Wachamngu hao watapata kutoka kwa Mola wao Mlezi kila wakipendacho.
Fadhila hiyo ni malipo ya kila mwenye kufanya vizuri katika itikadi yake
na vitendo vyake.
35. Mwenyezi Mungu amewakirimu wachamngu kwa alivyo wakirimu, ili
awafutie vile vitendo vyao viovu kabisa, na awalipe ujira wao kwa bora
ya vitendo vyao walivyo vitenda duniani.
36. Mwenyezi Mungu, peke yake, ni Mwenye kuwatosheleza waja wake
kwa kila lilio wakhusu. Na ati hao makafiri wa Kikureshi wanakutisha, ewe
Muhammad, kwa miungu yao wanayo iomba badala ya Mwenyezi Mungu. Na hayo
ni katika upotovu wao. Na mwenye kupotozwa na Mwenyezi Mungu, kwa kumjua
kuwa huyo amekhiari upotovu kuliko uwongofu, basi hatakuwa na mwongozi
wa kumwongoza.
37. Na mwenye kuongozwa na Mwenyezi Mungu kuendea Haki, na
akamwezesha kuifikia, kwa kujua kwake kuwa huyo amekhiari uwongofu kuliko
upotovu, basi hatokuwapo wa kumpotoa akaiacha Njia ya Uwongofu. Kwani Mwenyezi
Mungu si ndio Yeye ambaye hashindiki kwa kila upande, ambaye ni Mwenye
kulipiza kwa ukali? Na kwa hivyo huwalinda vipenzi vyake na maadui wake?
38. Na ninaapa, lau ungeli wauliza, wewe Muhammad, hawa washirikina:
Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka wangeli sema: Mwenyezi
Mungu ndiye aliye ziumba. Ewe Muhammad, waambie: Mmezingatia mkawaona hao
miungu mnao washirikisha na Mwenyezi Mungu, wanaweza kuniondolea madhara
ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kunidhuru? Au wanaweza kunizuilia rehema yake
akitaka inifikie? Ewe Muhammad! Waambie: Anaye nitosheleza kwa kila
kitu ni Yeyey peke yake, si mwenginewe, ndiye Yeye wanaye mtegemea
wote wanao tegemea na kumwachilia kila kitu.
39,40. Waambie, kwa kuwapa ahadi: Enyi watu! Ishikilieni hiyo hiyo
njia yenu ya ukafiri na kukadhibisha, na mimi hakika ninashikilia aliyo
niamrisha Mola wangu Mlezi. Mtakuja ona nani katika sisi atakaye fikiwa
na adhabu ya kumdhalilisha, na atakaye teremkiwa na adhabu ya daima isiyo
mwondokea?
41. Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekuteremshia Qur'ani Tukufu hii kwa
watu wote, nayo imekusanya Haki iliyo thibiti. Basi mwenye kuongoka kwa
sababu yake basi manufaa hayo ni kwa nafsi yake, na mwenye kuipotea njia
yake basi balaa ya upotofu wake itamrejea mwenyewe. Wala wewe, Muhammad,
si mwenye kuwakilishwa uwongofu wao. Jukumu lako ni kufikisha ujumbe, nao
umeufikisha.
42. Mwenyezi Mungu huzitakabadhi roho zinapo kufa. Na huzipokea roho
zisio kufa zinapo lala. Basi huzizuia zilizo kwisha hukumiwa kufa, zisirudi
kwenye miili yao, na huzirudisha nyenginezo ambazo hazijafikilia bado ajali
yao, wakati wa kuamka, mpaka itakapo fika ajali yao ilio wekewa. Hakika
katika hayo bila ya shaka zipo Ishara wazi kwa watu wanao zingatia.
43. Bali washirikina wakawafanya wengineo badala ya Mwenyezi Mungu
kuwa ni waombezi wao wa kuwakurubisha kwake. Waambie, ewe Muhammad: Mnafanya
haya ijapo kuwa hawa mnao wafanya "waombezi" hawanacho wanacho kimiliki,
wala hawana wanacho kifahamu?
44. Ewe Muhammad! Waambie: Uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu peke
yake! Hapana anaye upata ila aridhie Yeye. Ufalme wa mbingu na ardhi ni
wake Yeye tu. Na kisha mtarejeshwa kwake, akuhisabieni vitendo vyenu.
45. Na pindi akitajwa Mwenyezi Mungu peke yake, bila ya kutajwa miungu
yao, nyoyo za wasio yaamini maisha ya Akhera hukunjana na kukasirika. Na
wakitajwa miungu yao wanayo iabudu badala ya Mwenyezi Mungu wao huwa wepesi
kufurahi na kustarehe.
46. Ewe Muhammad! Sema, nawe umemwelekea Mola wako: Ewe Mwenyezi
Mungu! Ewe Muumba mbingu na ardhi bila ya mithali! Ewe Mjuzi wa siri na
dhaahiri! Wewe peke yako, ndiye wa kuhukumu baina ya waja wako katika hayo
wanayo khitalifiana katika mambo ya dunia na Akhera. Basi hukumu baina
yangu na hawa washirikina!
47. Na lau kuwa hao walio jidhulumu nafsi zao kwa ushirikina wanamiliki
vyote viliomo duniani na mara mbili kama hivyo, bila ya shaka wangeli
vitoa kuwa ni fidia ya kujigombolea nafsi zao na adhabu waliyo andaliwa
Siku ya Kiyama. Nao watakuja iona adhabu itokayo kwa Mwenyezi Mungu ambayo
haikupata kuwapitikia katika mawazo yao.
48. Na katika Siku hii ya leo utawadhihirikia uovu wa vitendo vyao,
na itawazunguka adhabu ya yale waliyo kuwa wakiyafanyia maskhaara duniani.
49. Na mtu yakimpata madhara hutuomba kwa unyenyekevu; kisha
tukimpa neema kwa kumfadhili, mtu huyo huyo husema: Sikupewa
neema hizi mimi ila kwa ujuzi wangu nilio nao wa kujua kuchuma. Naye mtu
huyu kasahau kuwa mambo si hivyo kama asemavyo, bali neema hizo alizo mneemesha
Mwenyezi Mungu ni kama majaribio tu, ni mtihani, ili amdhihirishe nani
mwenye kut'ii na nani mwenye kua'si. Lakini wengi wa watu hawatambui kama
hayo ni majaribio na fitna.
50. Maneno kama haya waliyasema walio kuwa kabla ya washirikina hawa,
na hayakuwalinda na adhabu hayo mali na starehe waliyo yachuma.
51. Yakawasibu makafiri walio tangulia malipo ya madhambi ya vitendo
vyao, na madhaalimu miongoni mwa hawa wanao semezwa hivi sasa yatawapata
vile vile malipo ya madhambi ya vitendo vyao. Wala hawa hawataiepuka adhabu.
52. Je! Hawa wanasema wayasemayo, wala hawajui kwamba Mwenyezi Mungu
humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na humpa kwa kadiri atakacho
kwa mujibu wa hikima yake? Hakika katika haya bila ya shaka ni mazingatio
kwa watu wanao amini.
53. Ewe Muhammad! Sema kwa kufikisha kutokana na Mola wako Mlezi:
Enyi waja wangu walio jizidishia juu ya nafsi zao maasi, msikate tamaa
na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huyafuta madhambi yote.
Hakika Yeye, peke yake, ndiye Mkuu katika kusamehe kwake na kurehemu kwake.
54. Enyi mlio jidhulumu nafsi zenu, rejeeni kwa Mwenye kuyamiliki
mambo yenu yote, na Mlezi wenu. Na mfuateni Yeye kabla haijakujieni
adhabu, tena hapo hapatakuwepo wa kukunusuruni na Mwenyezi Mungu
na kukulindeni na adhabu yake.
55. Na fuateni yaliyo bora kabisa katika mliyo teremshiwa kutokana
na Mola wenu Mlezi, nayo ni Qur'ani Tukufu, kabla ya kukujieni adhabu kwa
ghafla, na bila ya kujitayarisha, na hali nyinyi hamjui kuja kwake.
56. Rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na Msilimu kwake, na mfuate mafunzo
yake, ili nafsi yenye dhambi isisema itapo iona adhabu: Ee msiba wangu
kwa niliyo yawacha upande wa Mwenyezi Mungu na katika haki zake,
na kwamba mimi nilikuwa duniani miongoni mwa walio kuwa wakiifanyia maskhara
Dini yake.
57. Au iseme ile nafsi yenye dhambi, kutafuta udhuru: Lau kuwa Mwenyezi
Mungu angeli niwezesha kufuata uwongofu bila ya shaka ningeli kuwa duniani
katika wale walio jilinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa Imani na vitendo
vyema.
58. Au iseme nafsi ile yenye dhambi itapo ona adhabu: Laiti ningeli
rejeshwa duniani, nikawa katika wanao tengeneza imani yao na vitendo vyao!
59. Utayapata wapi, ewe mwenye majuto! Mafunzo yangu yalikujia
katika ndimi za Mitume, nawe ukayakanusha, na ukajiona bora, ukakataa
kuyafuata, na ukawa katika dunia yako miongoni mwa wenye kushikilia ukafiri.
60. Na Siku ya Kiyama utawaona walio mzulia uwongo Mwenyezi Mungu,
wakamkhusisha yasiyo kuwa yake, nyuso zao zimesawjika kwa huzuni na majonzi.
Hakika Jahannamu ndio makaazi ya wenye kiburi wakaikataa Haki.
61. Na Mwenyezi Mungu atawaokoa alio wajaalia ulinzi isiwapate adhabu
ya Mwenyezi Mungu, kwa vile alivyo kwisha wajua kuwa wamefuzu, kwa walivyo
ukhiari uwongofu kuliko upotofu. Na siku hii basi uovu hautawagusa,
wala hawatahuzunika kwa kuzikosa neema walizo kuwa wakizitaraji.
62. Mwenyezi Mungu Muumba kila kitu - naye peke yake - ndiye Mlinzi
wa kila kitu. Anaendesha mambo yake kwa mujibu wa hikima yake.
63. Maendesho ya mambo ya katika mbingu na ardhi yako kwa Mwenyezi
Mungu. Hayaendeshi hayo isipo kuwa Yeye. Na makafiri kwa hoja za Mwenyezi
Mungu na ushahidi wake ndio wao, peke yao, ndio wenye kukhasiri,
mwisho wa kukhasiri!
(Injili ya Mathayo 16:16-20 imedai kuwa Yesu kampa funguo za mbingu
na ardhi Petro, na hivyo ndiyo Papa wa Roma amerithi funguo hizo na kuanzisha
Kanisa la Kikatoliki, na uwezo wa kufutia watu dhambi na kuwaangamiza Motoni.
Marcello Craveri, mtaalamu wa Biblia wa Kitaliana ameandika katika kitabu
chake Maisha ya Yesu (sahifa 227-28 Panther Edn.) kuwa Mathayo 16:16-20
imeongezwa na ametoa hoja 7 kwa wazo hilo. Licha ya kuwa Yesu hakumpa Petro
hizo funguo za mbingu na ardhi, yeye mwenyewe Yesu hakuwa nazo.)
64. Ewe Muhammad! Sema: Je! Baada ya kuweka wazi Ishara zote kuwepo
Mwenyezi Mungu Mmoja wa kuabudiwa, mnaniamrisha nimuabudu mwenginewe, enyi
wajinga, majaahili?
65. Na ninaapa: Bila ya shaka, umepewa Wahyi, wewe, Muhammad na Mitume
walio kuwa kabla yako, kwamba bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu
na chochote kile basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atazibat'ilisha a'mali
zako, na utakuwa katika watu walio khasirika ukomo wa kukhasiri.
66. Ewe Mtume! Usiwakubalie kwa hayo wanayo kutaka, bali muabudu
Mwenyezi Mungu peke yake, na uwe katika wanao mshukuru Yeye kwa neema zake.
67. Washirikina hawakumtukuza Mwenyezi Mungu kama anavyo stahiki
utukufu wake, wala hawakumjua kama anavyo stahiki kujuulikana, kwa kuwa
wamemshirikisha pamoja naye wenginewe, na wakamtaka Mtume naye aingie katika
ushirikina, na hali ardhi yote ni milki yake Siku ya Kiyama, na mbingu
zitakuwa zimekunjwa, kama zinavyo kunjwa nguo, katika mkono wake wa kulia.
Mwenyezi Mungu ametakasika na kila upungufu, na ametukuka vikubwa mno na
vyote hivyo wanavyo mshirikisha naye.
68. Na litapulizwa barugumu kwa yakini (1), na watakufa walioko mbinguni
na katika ardhi ila anaye mtaka Mwenyezi Mungu kumuakhirisha mpaka wakati
mwengine. Kisha litapulizwa mara nyengine, na hapo wote watainuka kutoka
makaburini mwao, wakingojea watafanywa nini?
(1) Hilo barugumu (S'ur) kilugha, ni tarumbeta, mbiu, siwa, parapanda.
Barugumu inalo tusimulia Qur'ani ni katika mambo ya ulimwengu usio onekana,
hatujui lilivyo na hakika yake.
69. Na ardhi itang'ara siku hiyo kwa nuru ya Muumba wake na Mmiliki
wake. Na kitatayarishwa Kitabu kilicho sajiliwa ndani yake vitendo vyao,
na watahudhurishwa Manabii na mashahidi wapate kuwashuhudia viumbe vyote,
na wapambanuliwe baina ya viumbe kwa uadilifu, na wala hawatadhulumiwa
kwa kupunguziwa thawabu wala kuzidishiwa adhabu.
70. Na kila nafsi itapewa malipo ya a'mali yake, na Mwenyezi Mungu
ni mbora wa kujua vitendo vyao.
71. Na makafiri watahimizwa kwenda kwa nguvu kuendea Jahannamu kwa
makundi makundi. Na hata watapo fika milango yake itafunguliwa, na walinzi
wake watawaambia kwa kuwakebehi: Kwani hawakuja kwenu Wajumbe kutoka
kwa Mwenyezi Mungu wa jinsi yenu, wakikusomeeni Aya za Mola wenu Mlezi,
na wakakuhadharisheni na mkutano wenu huu? Makafiri watasema kwa kukiri:
Kwani! Walitujia Mitume. Lakini neno la adhabu limekwisha wajibikia juu
ya makafiri, kwa kuwa wao wamekhiari ukafiri kuliko Imani.
72. Wataambiwa: Iingieni milango ya Jahannamu mliyo jaaliwa mkae
humo milele. Jahannamu ni pahala paovu mno pa kukaa wenye kutakabari na
wakakataa kuikubali Haki.
73. Na wachamngu watahimizwa kwenda Peponi kwa hishima makundi makundi,
mpaka wakifika kwenye milango yake, wataambiwa na walinzi wake: Amani kubwa
juu yenu! Mmet'ahirika duniani na uchafu wa maasi, na mmet'ahirika Akhera
katika nafsi zenu kwa neema mlizo zipata. Basi ingieni Peponi mliko jaaliwa
kukaa milele. Kwani nyinyi mna neema zisio pita akilini.
74. Na wachamngu watasema: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu peke
yake, ambaye ametutimizia aliyo tuahidi kwa ndimi za Mitume wake, na akatumilikisha
ardhi ya Peponi tunashukia tutakapo humo. Ama hakika bora ya ujira wa wenye
kutenda mema ni Pepo.
75. Na utaona, ewe mwenye kuona, Malaika wakiizunguka A'rshi, wakimtakasa
Mwenyezi Mungu na kila upungufu, kwa utakaso unao fuatana na kumhimidi
Muumba wao na Mlezi wao, na akapambanua baina ya viumbe vyote kwa uadilifu,
na ulimwengu wote ukatamka kwa kusema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu,
Mola Mlezi wa viumbe vyote.