') //-->
1. Sifa zote nzuri ni haki ya Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Mwenye kuumba, na Mwenye kumiliki, na Mwenye kupanga vyote vilioko mbinguni, na vilioko katika ardhi. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye sifa Akhera, kwa kutamalaki kwake kuliko enea. Naye ndiye Mwenye hikima asiye kosa, Mwenye khabari zote, hapana asicho kijua siri yake.
Rudi kwenye Sura
2. Anajua kila kinacho ingia katika sehemu za ardhi, kama maji, na khazina, na vilio zikwa, na sehemu za maiti; na kila kinacho toka, kama wanyama, na mimea, na maadeni, na maji ya visima, na chemchem. Na anajua vinavyo teremka kutoka mbinguni, kama Malaika, na Vitabu wanavyo vipokea Manabii, na mvua, na radi; na anajua vinavyo panda ndani yake na kwendea huko, kama Malaika, na a'mali za ibada, na roho. Na Yeye ni Mwingi wa rehema, Mkubwa wa kusamehe.
Rudi kwenye Sura
3. Na wenye kukufuru wakasema: Haitujii Saa iliyo ahidiwa kuwa ni ya kufufuliwa na kukusanywa watu. Waambie ewe Mtume! Hapana shaka itakujieni, nami naapa kwa Mola wangu Mlezi, Mwenye kujua ya siri, ambaye hapana chenye kughibu na ujuzi wake hata ingawa kiasi ya chembe tu, si katika mbingu wala katika ardhi. Wala kilicho kidogo kuliko chembe, wala kikubwa kuliko hivyo hakikosi kuandikwa katika Kitabu kilicho timia, chenye kubainisha kila kitu.
Dharra , tuliyo ifasiri "Chembe", na kisayansi ni Atom kwa hakika katika lugha ya Kiarabu ni kitu kidogo sana, kama sisimizi mdogo, au chembe ya vumbi. Na uzito wa Dharra maana yake ni uzani wake. Na Aya inaonyesha kuwa kipo kilicho kuwa ni kidogo kuliko Dharra. Na yafaa kutaja hapa kuwa sayansi za sasa zimethibitisha kuwa Dharra, yaani Atom, imegawika katika sehemu ndogo zaidi nazo ni Nucleus na Electrons. Na haya haya hayakuthibitika ila katika karne ya ishirini ya kuzaliwa Nabii Isa.
Rudi kwenye Sura
4. Ili Mwenyezi Mungu awathibitishe walio amini na wakatenda mema kwa ajili ya nafsi zao na kwa ajili ya watu wengine. Hao Waumini watendaji watapata kwa Mwenyezi Mungu msamaha wa kuwafutia madhambi yao, na riziki kunjufu isiyo na masimbulizi ndani yake.
Rudi kwenye Sura
5. Na hao walio zishughulisha nafsi zao kuipiga vita Qur'ani kutaka kuishinda amri ya Mwenyezi Mungu katika kumsaidia Mtume wake, hao watapata adhabu katika adhabu za mwisho wa ubaya na uchungu.
Rudi kwenye Sura
6. Na walio neemeshwa na Mwenyezi Mungu kwa kupewa ujuzi kuwa Qur'ani ulio teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi, yenye ndani yake mambo ya itikadi na uwongofu, ni Haki isiyo kuwa na shaka yoyote, wanajua kuwa hiyo ndiyo yenye kuwaongoa watu kwendea Njia ya Mwenyezi Mungu, Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kustahiki kila sifa njema.
Rudi kwenye Sura
7. Na makafiri waliambiana wenyewe kwa wenyewe, kwa kufanyia kejeli kufufuliwa: Je! Tukuonyesheni mtu ataye kuambieni kwamba mtapo kwisha kufa, na viwiliwili vyenu vikagawika mapande mapande kuwa ati mtafufuliwa tena kwa umbo jipya?
Rudi kwenye Sura
8. Mtu huyu amemzulia uwongo Mwenyezi Mungu kwa kumnasibishia kuwa atawafufua wafu, au mtu huyu ana wazimu ndio anasema asiyo yajua? Siyo hayo wayasemayo. Bali ukweli wa mambo ni kuwa hao wasio iamini Akhera wataingia katika adhabu na upotovu wa kupotelea mbali na Haki.
Rudi kwenye Sura
9. Je! Wamepofuka, hata hawaaoni yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao ya mbinguni na katika ardhi wakaujua uweza wetu wa kutenda tuyatakayo? Tukitaka ardhi iwameze, tutawazamisha. Au tungeli taka viwaangukie vipande vya mbingu tuwasage sage tungeli wateremshia. Hakika katika tuliyo yataja zipo dalili kwa kila mja mwenye kurejea kwa Mola wake Mlezi katika kila jambo lake.
Rudi kwenye Sura
10. Wallahi! Kwa hakika tulimpa Daudi fadhila kutoka kwetu kwa kumpa hikima na Kitabu. Na tulisema: Enyi milima! Karirini pamoja naye Tasbihi kumtakasa Mwenyezi Mungu, pale anapo sabihi yeye. Na Sisi tuliwafanya ndege pia wamtumikie, nao wawe wakikariri kumtakasa Mwenyezi Mungu. Na tukakifanya chuma kiwe laini kwake aunde kwa sura atakayo.
Daudi, a.s. ni mmoja wa Manabii wa Wana wa Israili, na mmoja wa wafalme wao. Aliishi katika zama za baina ya mwaka 1010 na 970 K.K. (yaani kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s.)
Rudi kwenye Sura
11. Tulimfunulia kumwambia aunde nguo za chuma pana za kujilinda katika vita na maadui. Naye azifume kwa hikima na ustadi katika kuviunga viungo vyake. Na tukamwambia yeye na watu wake: Tendeni yatakayo kuleteeni kheri na maslaha. Hakika Mimi nayaona vyema yote myatendayo, hapana kinacho niporonyoka nisikione.
Rudi kwenye Sura
12. Na Suleiman tukamfanyia upepo umtumikie. Mwendo wake wakati wa asubuhi mmoja ni sawa na safari ya dasturi inayo chukua mwezi mzima. Na mwendo wake wakati wa jioni moja ni kama safari ya kuchukua mwezi. Na tukamyayushia maadeni ya shaba ikawa inatiririka kwa wingi moja kwa moja. Na tukawafanya majini wawe wakimtumikia mbele yake kwa amri ya Mola wake Mlezi. Na yeyote katika majini aliye wacha kut'ii amri ya Suleiman basi tulimwonjesha adhabu ya Moto unao waka kwa nguvu.
Rudi kwenye Sura
13. Hao majini wakifanya atakacho Suleiman, kama misikiti kwa ajili ya ibada, na masanamu, na madeste au mabakuli makubwa kama mahodhi ya maji, na vyombo vya kupikia, yaani masufuria, makubwa yaliyo kaa pale pale penye mafya yake hayaondoki kwa kuwa ni makubwa mno. Na tukawaambia watu wa Daudi: Tendeni kazi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu vilivyo. Na ni wachache miongoni mwa waja wangu ambao wanakumbuka neema zangu wakawa wananishukuru kwa wingi.
Rudi kwenye Sura
14. Tulipo mhukumia Suleiman mauti, hapana aliye waonyesha majini kuwa kesha kufa ila kinyama cha ardhi kilicho ila fimbo yake aliyo kuwa akiiegemea. Alipo anguka majini wakajua kuwa lau kuwa wangeli jua ya ghaibu wasingeli endelea na ile adhabu ya mashaka ya kuwadhalilisha.
Rudi kwenye Sura
15. Ninaapa: Hakika katika watu wa Sabaa katika makaazi yao ya Yaman palikuwa na Ishara ya uweza wetu. Zilikuwako bustani mbili zilizo zunguka nchi yao, kulia na kushoto. Wakaambiwa: Kuleni katika riziki ya Mola wenu Mlezi, na mshukuru neema zake kwa kuzitumilia inavyo faa. Huu mji wenu ni mji mzuri, una vivuli na matunda. Na Mola wenu Mlezi ni Mwingi wa maghfira kwa anaye mshukuru.
Rudi kwenye Sura
16. Lakini wao waliacha kushukuru neema, na wakawa maisha yao ya kiburi. Tukawafungulia mafuriko ya nguvu yaliyo tokea baada ya kupasuka kuta za mahodhi, yakateketeza mabustani yao. Tukawabadilishia badala ya bustani zao mbili zile zenye matunda mazuri, zikawa nyengine mbili zenye matunda machungu, na miti isiyo kuwa na matunda, na mikunazi kidogo isiyo toa hamu.
Hili liitwalo "Hodhi" la maji ya mvua kubwa au "Hodhi la Ma`arib" ni kubwa kuliko mahodhi yote ya Yaman. Hodhi hili linaweza kubadilisha ardhi kavu ya kiasi ya maili 300 ya mraba ikawa yenye rutba na mashamba. Na dalili ya hayo ni hizo bustani mbili zilizo tajwa. Wanazuoni wa taarikh (historia) wanakhitalifiana katika ujenzi wa hilo hodhi kuu. Vile vile zipo kauli mbali mbali kukhusu kubomoka kwake.
Rudi kwenye Sura
17. Hayo ndiyo malipo tuliyo walipa kwa kufuru zao kuzikufuru neema na kuto zishukuru. Na kwani Sisi tunamuadhibu kwa adhabu hii kali yeyote yule ila aliye kuwa mwingi wa kumkufuru Mwenyezi Mungu na fadhila zake?
Rudi kwenye Sura
18. Na tulifanya baina ya maskani yao ya Yaman na baina ya miji mingine iliyo barikiwa miji mingineyo pia iliyo karibiana inaonana. Na tukafanya makhusiano baina yao ni kiasi maalumu cha mwendo usio kuwa wa taabu. Na tukawaambia: Nendeni humo usiku na mchana nanyi mko katika amani.
Rudi kwenye Sura
19. Kwa kutakabari kwa neema, na raha, na amani, walisema: Tuwekee mbali masafa ya safari zetu, tusisadifu kukuta miji iliyo amirishwa ya katikati mpaka tufike huko twendako! Mwenyezi Mungu akazifanya ziwe mbali hizo safari zao. Na wakawa wao wamejidhulumu nafsi zao kwa uasi wao. Tukawafanya hao ni masimulizi ya watu, na tukawatenganisha mtengano mkubwa. Hakika katika yaliyo wapata hao yapo mawaidha kwa kila mwenye kusubiri kwa balaa, mwenye kushukuru kwa apewacho.
Rudi kwenye Sura
20. Na bila ya shaka Iblisi amehakikisha dhana yake juu yao. Nao wakamfuata yeye isipo kuwa wachache miongoni mwa Waumini.
Rudi kwenye Sura
21. Na wala Iblisi hakuwa na nguvu za kuwafanya wamt'ii na kumnyenyekea; lakini Mwenyezi Mungu kawafanyia mtihani apate kuwadhihirisha wepi wanao isadiki Akhera, na wepi wana shaka nayo. Ewe Nabii! Mola wako Mlezi ni Mwenye kuchungua kila kitu, Mwenye kusimamia kila kitu.
Rudi kwenye Sura
22. Ewe Nabii! Waambie washirikina: Waombeni hao mnao dai kwa uwongo kwamba ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu, wakuleteeni manufaa au wakuondoleeni madhara. Hawakujibuni kitu. Kwani hao hawamiliki hata kiasi ya chembe ya kitu katika mbingu wala katika ardhi. Wala wao hawana ushirika wowote na Mwenyezi Mungu katika kuumba au kumiliki. Wala hapana yeyote katika hao miungu ya uwongo anaye msaidia Mwenyezi Mungu katika kupanga mambo ya viumbe vyake.
Rudi kwenye Sura
23. Wala maombezi kwa Mwenyezi Mungu hayawafai ila wenye kustahili makamo ya kuombewa. Mpaka itapo ondoka khofu katika nyoyo zao kwa kutolewa ruhusa ya kuombewa, hapo watakuwa wakiambiana kwa furaha: Mola wenu Mlezi kakwambieni nini? Na wengine watajibu kwamba alilo sema ni kauli ya haki, kwa kutoa ruhusa kuombewa aliye mridhi. Na Yeye peke yake, ndiye Mwenye Utukufu na Ukubwa. Na Yeye ndiye anaye ruhusu na kumkatalia amtakaye.
Rudi kwenye Sura
24. Ewe Nabii! Waambie washirikina: Nani anaye kuleteeni riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Watapo kuwa hawajibu kwa inda tu, waambie: Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anaye kuruzukuni kutoka kote kuwili. Je! Ni sisi Waumini au nyinyi washirikina ndio walio katika moja ya hali mbili, ya uwongofu au upotofu ulio wazi?
Rudi kwenye Sura
25. Ewe Nabii! Waambie: Nyinyi hamuulizwi khabari ya madhambi tuliyo yafanya sisi; wala sisi hatuulizwi khabari ya vitendo vyenu.
Rudi kwenye Sura
26. Waambie: Mola wetu Mlezi atatukusanya Siku ya Kiyama, kisha atatuhukumu kwa haki. Na Yeye Subhanahu ndiye Hakimu wa kila shauri, Mwenye kujua kwa hakika yetu sisi na yenu nyinyi.
Rudi kwenye Sura
27. Waambie: Nionyesheni hao mlio waunganisha na Mwenyezi Mungu kwa kustahiki kuabudiwa, mnao dai kuwa ni miungu wa shirika na Yeye. Yeye hana mshirika, bali Yeye ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima katika kupanga kwake na kuendesha kwake.
Rudi kwenye Sura
28. Na Sisi hatukukutuma ewe Muhammad, ila kwa watu wote. Uwe ni mwenye kuwabashiria Waumini kuwa watapata kheri, na mwenye kuwaonya makafiri kuwa watapata shari. Lakini aghlabu ya watu hawaujui ukweli wako, wala kuwa Utume wako ni wa kwa watu wote. (Haya ni kwa sababu hapana Mtume aliye kuja kwa watu wote ila huyu Nabii Muhammad s.a.w. Nabii Musa alikuja kwa Wana wa Israili kuwatoa Misri. Nabii Isa, Yesu Kristo, pia kaja kwa Wana wa Israili tu, kama isemavyo Qur'ani 3.49, na Injili ya Mathayo 10.5-6 Yesu alipo sema: "Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli." Na 15.24 alipo sema: "Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli." Na Injili ya Yohana 17.9)
Rudi kwenye Sura
29. Na makafiri wanasema kwa kuifanya haiwi hiyo Siku iliyo ahidiwa kwa ajili ya malipo: Lini itakuwa ahadi hii tuingie Motoni, na nyinyi muingie Peponi, kama nyinyi ni wakweli kwa hiyo ahadi yenu?
Rudi kwenye Sura
30. Ewe Nabii! Waambie: Miadi yenu ni Siku kubwa mno; ikifika hamto chelewa hata kwa saa moja, wala hamto tangulia.
Rudi kwenye Sura
31. Na walio kufuru wanasema: Hatuisadiki Qur'ani hii wala hivyo Vitabu vilivyo tangulia kabla yake kwa hayo vinavyo amrisha na kulingania. Na lau ungeli ona - ewe mwenye kuweza kuona - wakati wanapo simamishwa madhaalimu mbele ya Muumba wao, Mwenye kumiliki amri yao, ungeliona maajabu katika msimamo wao, pale wanapo jibizana maneno wao kwa wao. Walio wanyonge wakiwaambia walio tukuka juu yao: Ingeli kuwa si nyinyi, kwa kutusaliti na kutamalaki, hapana shaka tungeli kuwa Waumini.
Rudi kwenye Sura
32. Walio takabari na wakajiona ni wakubwa, watawaambia wanyonge, kwa kuyapinga maneno yao: Kwani sisi tulikuzuieni msiongoke ulipo kufikieni uwongofu? Tumekuzuieni sisi au nyinyi wenyewe ndio mmekhiari upotofu kuliko uwongofu.
Rudi kwenye Sura
33. Na wanyonge nao watawaambia walio takabari: Bali vitimbi vyenu na uchochezi wenu kutuchochea usiku na mchana ndio umetutumbukiza katika hilaki, pale mlipo kuwa mkitutaka tumkufuru Mwenyezi Mungu, na tumfanyie miungu mingine ya kumshirikisha. Na pande zote mbili zikaficha majuto yao walipo iona adhabu inawashukia. Wakajua kuwa hapana faida ya kuonyesha majuto. Na tukayaweka makongwa, (nira), juu ya shingo za wasio amini. Je! Watu hawa wanastahiki chochote ila malipo kwa yale waliyo kuwa wakiyatenda?
Rudi kwenye Sura
34. Na sisi hatukumtuma Mtume yeyote kwenda kwenye mji kuwaita watu wake wafuate Haki ila wale wanao jidekeza kwa starehe zao katika ule mji husema: Hakika sisi tunayakanusha hayo mliyo kuja nayo.
Rudi kwenye Sura
35. Na husema kwa kujipa: Sisi tuna mali mengi zaidi na watoto. Wala hatutaadhibiwa Akhera.
Rudi kwenye Sura
36. Ewe Nabii! Waambie: Hakika aliye niumba humkunjulia riziki amtakaye, katika wanao muasi na wanao mt'ii. Na humdhikisha amtakaye. Wala hiyo si dalili ya kuwa Yeye yuradhi na mtu au anamchukia. Lakini watu wengi hawajui haya.
Rudi kwenye Sura
37. Wala mali yenu wala watoto wenu sio jambo la kukurubisheni kwetu mkawa karibu. Lakini ambaye Imani yake imethibiti, na akawa anatenda mema, basi watu kama hao ndio watapata thawabu mara mbili kwa waliyo yatenda. Na Peponi watakuwa ni watu wa juu na wenye amani.
Rudi kwenye Sura
38. Na hao ambao wana fanya juhudi kuzipinga Ishara zetu, wakifanya kila hila kuzivunja na kuwazuia Manabii wetu wasifikishe Ujumbe wake, hao, basi watakuwa katika adhabu, wamehudhurishwa na wala hawataepuka.
Rudi kwenye Sura
39. Ewe Nabii! Sema: Hakika Mola wangu Mlezi anamkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na humdhikisha amtakaye. Na chochote mtacho kitoa Yeye atakilipa. Na Yeye Aliye takasika ni Mbora wa wenye kuruzuku.
Rudi kwenye Sura
40. Na taja, ewe Nabii, siku Mwenyezi Mungu atapo wakusanya wote, na kisha Subhanahu awaambie Malaika mbele ya wale walio kuwa wakiwaabudu: Je! Hawa walikuabuduni nyinyi khasa badala yangu mimi?
Rudi kwenye Sura
41. Malaika watasema: Sisi tunakutakasa kabisa na kuwa Wewe una mshirika wowote. Wewe ndiye tulio shikamana nawe kwa mapenzi na ut'iifu, sio wao. Hao wameghurika katika madai yao kuwa wanatuabudu sisi. Bali walikuwa wanafuata nyayo za mashetani walio wapambia ushirikina. Wengi wao wakiwasadiki hao.
Rudi kwenye Sura
42. Basi Siku ya Mkusanyo hapana atakaye weza kumletea mwenzie manufaa wala kumkinga na madhara. Na tutawaambia walio jidhulumu nafsi zao: Ionjeni adhabu ya Moto ambayo mlio kuwa duniani mkiikanusha.
Rudi kwenye Sura
43. Na makafiri walipo somewa Aya zetu zilio wazi dalili zake kuonyesha Haki, makafiri walisema: Huyu si chochote ila ni mtu anaye taka kukuzuilieni msiwaabudu walio kuwa wakiwaabudu baba zenu. Na pia walisema: Hii Qur'ani si chochote ila ni uwongo ulio tungwa tu. Na walio ikataa Qur'ani ilipo wajia walisema: Hii si chochote ila ni uchawi ulio wazi.
Rudi kwenye Sura
44. Na Mwenyezi Mungu hakuwateremshia Waarabu Vitabu vya mbinguni wavisome; wala hutukupata kuwapelekea Mwonyaji kabla yako wa kuwahadharisha na matokeo ya ukafiri wao.
Rudi kwenye Sura
45. Na kaumu zilizo tangulia ziliwakadhibisha Manabii wao. Na hawa washirikina wa kaumu yako hawajafikia hata sehemu moja katika kumi za nguvu na umadhubuti tulio wapa hao walio tangulia. Wakawakanusha Mitume wangu. Basi ilikuwaje ghadhabu yangu juu yao jinsi nilivyo wakasirikia!
Rudi kwenye Sura
46. Waambie: Mimi nakuamrisheni jambo moja tu - Msimame kwa ikhlasi ya kumtakasia Mwenyezi Mungu muache kufuata mitindo yenu ya zamani - katika kuchungua kwa kumsafia niya Mwenyezi Mungu, mkigawika wawili-wawili, au mmoja-mmoja, muangalie kwa uadilifu na insafu. Kisha mfikiri khabari ya huyu mwenzenu, Muhammad, ambaye mmeishi naye na mnajua kuwa akili yake ni timamu. Huyu hana wazimu kwa kuliingia jambo hili. Yeye huyu si chochote ila ni Mwonyaji kwenu, anakuhadharisheni msije mkapata adhabu kali inayo kukabilini mbele yenu.
Rudi kwenye Sura
47. Waambie makafiri: Ujira wowote nilio kutakeni juu ya kufikisha Ujumbe ni kwa maslaha yenu. (Yaani nyinyi mwongoke na mpate malipo kwa Mwenyezi Mungu.) Sina ujira ninao utaraji mimi ila kwa Mwenyezi Mungu. Naye ni Mwenye kuangalia na kuchungua kila kitu.
Rudi kwenye Sura
48. Waambie: Hakika Mola wangu Mlezi huitupa Haki juu ya baat'ili (uwongo) ikauondoa. Na Yeye ndiye Mwenye kuijua vyema ghaibu; hapana siri inayo fichikana kwake.
Rudi kwenye Sura
49. Waambie: Uislamu umedhihiri, wala uwongo hauwezi kuwa ndio njia ya kuipinga Haki. Na hizo mbinu za zamani hazirejei tena.
Rudi kwenye Sura
50. Waambie: Nikiiacha Haki basi madhara ya hayo yataniangukia mwenyewe. Na nikiongoka basi nimeongozwa na Mola wangu Mlezi. Yeye ni Mwenye kusikia kauli yangu na kauli yenu. Yupo karibu nami, na karibu yenu.
Rudi kwenye Sura
51. Na lau kuwa utaona, ewe mwenye kuona, pale watapo fazaika makafiri kweli itapo dhihiri, basi hawatakuwa na pa kukimbilia. Na watachukuliwa wapelekwe kwenye Moto kutoka pahala karibu.
Rudi kwenye Sura
52. Na watasema, watapo iona adhabu: Tunaiamini Haki! Na vipi wao waipate Imani kwa wepesi huo kutoka pahala mbali na dunia ambayo wakati wake umekwisha pita?
Rudi kwenye Sura
53. Na ilhali wao walikwisha ikataa Haki kabla ya Siku hii, na wakavurumiza kwa dhana ya uwongo kutoka mahala palipo mbali na ukweli.
Rudi kwenye Sura
54. Patawekewa kizuizi baina yao na hayo wanayo yatamani ya Imani ya kuwafaa, kama walivyo fanyiwa wenzao wa kabla yao walipo amini baada ya kwisha wakati wake. Kwa sababu wote hao wote walikuwa katika kuifanyia Haki shaka inayo pelekea kutuhumiwa.
Rudi kwenye Sura