') //-->
1. Harufi hizi zimeanzia baadhi ya Sura kuashiria kuwa Qur'ani ni muujiza ulio tungwa na harufi kama harufi wanazo zitumia Waarabu katika maneno yao. Na juu ya hayo wao wameshindwa kuleta mfano wake. Na pia ni kwa ajili ya kuzindua watu wasikilize na watege sikio. Na washirikina walikuwa wamewafikiana kuwa wawe wanaropokwa maneno ya upuuzi tu ikisomwa Qur'ani wala wasiisikilize.
Rudi kwenye Sura
2. Hizi Aya tukufu ni Aya za Qur'ani iliyo kusanya hikima na ukweli.
Rudi kwenye Sura
3. Hizi Aya ni Uwongofu ulio kamilika, na Rehema iliyo kusanya kwa wenye kutenda mema.
Rudi kwenye Sura
4. Hao ndio wanao timiza Sala kwa njia ya ukamilifu kabisa, na wanawapa Zaka wanao istahiki; na wao wanayaamini maisha ya Akhera kwa imani yenye nguvu kabisa.
Rudi kwenye Sura
5. Hao Waumini wanao tenda vyema vitendo vyao, wametua kwenye Uwongofu ulio wajia kutokana na Mola wao Mlezi. Na hao tu - si wengineo - ndio wenye kufuzu kikweli.
Rudi kwenye Sura
6. Na miongoni mwa watu wapo ambao hununua maneno ya uwongo wawasimulie watu wapate kuwatenga na Uislamu na Qur'ani kwa kutojua dhambi zilio juu yao, na wanaifanyia maskhara Dini ya Mwenyezi Mungu na Ufunuo wake. Watendayo hayo watapata adhabu ya kuwatia unyonge na kuwadhalilisha.
Rudi kwenye Sura
7. Na mpotovu kama huyu akisomewa Aya za Mwenyezi Mungu huzipuuza kwa kiburi. Hali yake kwa haya ni hali ya ambaye hasikii, kama kwamba ana uziwi katika masikio yake. Basi mwonye kuwa hakika Mwenyezi Mungu amemuandalia adhabu yenye machungu makali.
Rudi kwenye Sura
8. Hakika walio amini na wakatenda vitendo vyema watapata Bustani zenye neema.
Rudi kwenye Sura
9. Watabaki humo daima dawamu; Mwenyezi Mungu amewaahidi ahadi isiyo vunjika. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mshindi wa kila kitu, Mwenye hikima katika maneno yake na vitendo vyake.
Rudi kwenye Sura
10. Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu zisio na nguzo za nyinyi kuziona. Na juu ya ardhi ameweka milima iliyo simama imara, ili ardhi isikutingisheni. Na humo katika ardhi ametawanya kila namna ya wanyama wanao tambaa na kwenda. Na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha mimea ya kila namna nzuri yenye manufaa katika ardhi.
Rejea uangalie maelezo ya kisayansi juu ya Aya 2, Sura ya Ar-Raa'd.
Rudi kwenye Sura
11. Hivi viumbe vya Mwenyezi Mungu vipo mbele yenu, basi hebu nionyesheni walicho umba hao mnao wafanya ni miungu badala yake Yeye hata wawe ni washirika wake! Bali madhaalimu - kwa ushirikina wao - wamo katika upotovu ulio wazi.
Rudi kwenye Sura
12. Na hakika tulimpa Luqman hikima, na ilimu, na kauli ya kusibu. Tulimwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema aliyo kupa. Na mwenye kushukuru basi hakika huyo anaitafutia kheri nafsi yake. Na mwenye kuzikufuru neema, akazikataa, na asishukuru kwa ajili yake, basi kwa hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuihitaji shukra yake, na Yeye Mwenyezi Mungu ni Mwenye kustahiki sifa zote njema, na ingawa pasiwepo hata mmoja wa kumsifu.
Rudi kwenye Sura
13. Taja pale Luqman alipo mwambia mwanawe: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu na yeyote. Hakika kumshirikisha Mwenyezi Mungu ni dhulma kubwa, kuwaweka sawa Mwenye kustahiki na asiye stahiki.
Waarabu walikuwa wanawajua watu wawili kwa jina hili. Mmoja wapo ni Luqman bin A'adi. Nao walikuwa wakimtukuza cheo kwa werevu wake, uraisi, ujuzi, ufasihi na ujanja. Na walikithiri sana kumtaja na kumpigia mithali, kama inavyo onekana katika vitabu vya Kiarabu vingi.
Ama mwengine ni huyo anaye itwa Luqman Alhakim, (Mwenye hikima), aliye kuwa mashuhuri kwa hikima yake na mifano yake, na ambaye Sura hii ya Qur'ani imeitwa kwa jina lake. Na hikima zake zilikuwa zimeenea kwa Waarabu. Ibn Hisham amesimulia kwamba Suwaid bin Ass'amit alifika Makka. Naye alikuwa mtu mtukufu kwa watu wake. Mtume s.a.w. akamtaka asilimu. Suwaid akasema: Huenda labda uliyo nayo wewe ndiyo kama niliyo nayo mimi. Mtume s.a.w. akasema: Nini ulicho nacho? Akasema: Majalla ya Luqman. Mtume s.a.w. akasema: Nisomee. Akamsomea. Tena akasema: Hakika haya maneno mazuri. Na niliyo nayo mimi ni bora zaidi, nayo ni Qur'ani aliyo niteremshia Mwenyezi Mungu, nayo ni Uwongofu na Nuru. Mtume s.a.w. akamsomea Qur'ani na akamtaka asilimu.
Na pia Imam Malik ametaja kwa wingi hikima za Luqman katika kitabu chake, Al Muwatt'a. Na baadhi ya vitabu vya Tafsiri ya Qur'ani na Adab (maandishi ya ufasihi wa lugha) vimetaja namna mbali mbali katika hikima hizo.
Kisha baadae ikakusanywa mithali kwa visa katika kitabu chenye jina la Mithali za Luqman. Lakini kwa sababu ya udhaifu wa mpango wake, na wingi wa makosa ya nahau na sarfu, na kuwa kutopokewa kitabu cha jina hili katika vitabu vya Waarabu wa kale, yatilia nguvu kuwa hichi kimezuliwa tu katika zama za mwisho.
Na maoni yanayo gongana juu ya uhakika wa Luqman Al-hakim: ni kuwa yeye ni Mnubi katika watu wa Abla au Uhabeshi, au mtu mweusi wa Sudan ya Misri, au ni Muibrani. Na wengi walio mtaja wanakubaliana kuwa hakuwa Nabii. Wachache tu ndio wanasema kuwa alikuwa Nabii. Na tunalo weza kutambua katika yaliyo tajwa ni kuwa hakuwa Mwaarabu, kwa sababu wote wamewafikiana kwa hayo. Na kwamba alikuwa ni mtu mwenye hikima, na hakuwa Nabii, na kwamba ameingiza miongoni mwa Waarabu hikima mpya zikawa zinatajwa mara nyingi kama ilivyo onekana baadae katika vitabu.
Rudi kwenye Sura
14. Na tumemuamrisha mtu awafanyie wema wazazi wake, na mama yake ampe fungu kubwa zaidi. Kwani yeye alimbeba katika mimba kwa udhaifu unao zidi kila siku kidogo kidogo. Na tena kamnyonyesha muda wa miaka miwili ndipo alipo muachisha ziwa. Na tumemuusia: Mshukuru Mwenyezi Mungu na wazazi wako. Kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo kwa ajili ya hisabu na malipo.
Rudi kwenye Sura
15. Na ikiwa wazazi wako wakikushikilia kwa juhudi umshirikishe Mwenyezi Mungu na vitu usivyo vijua kuwa vinastahiki kuabudiwa, basi usiwakubalie. Lakini endelea na kusuhubiana nao duniani kwa wema na ihsani. Na fuata njia ya wanao rejea kwangu kwa Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, na Ikhlasi, usafi wa niya na vitendo. Kisha nyote mtarejea kwangu, na nitakupeni khabari ya mliyo kuwa mkiyatenda, ya kheri na shari, ili nipate kukulipeni kwayo.
Rudi kwenye Sura
16. Ewe mwanangu! Hakika wema au ubaya kwa mtu, hata ukiwa, mathalan, kwa udogo wake kama chembe ya khardali, iliyoko pahali palipo fichikana kabisa, kama ndani ya jabali, au ndani ya mbingu, au chini ya ardhi, Mwenyezi Mungu ataufichua na autolee hisabu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, hakifichikani kitu hata kidogo kwake, ni Mwenye khabari ya kujua hakika ya kila kitu.
Rudi kwenye Sura
17. Ewe mwanangu! Zihifadhi Sala, na amrisha kila wema, na kataza kila baya, na stahamili kwa shida zinazo kusibu. Hakika anayo usia Mwenyezi Mungu ni katika mambo ambayo yanahitajia kufanyiwa hima na kuyashikilia.
Rudi kwenye Sura
18. Wala usiwageuzie watu uso wako kwa takaburi, wala usitembee katika nchi kwa kujiona na majivuno. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kuringa na kujiona.
Rudi kwenye Sura
19. Na nenda mwendo wa wastani, si mbio mbio mno wala taratibu mno. Na teremsha sauti yako. Kwani hapana sauti mbaya kama sauti ya punda. Inaanzia kwa mngurumo unao ghasi, na inaishia kwa ukenje unao kera.
Rudi kwenye Sura
20. Mmeona kwamba Mwenyezi Mungu amekudhalilishieni viliomo mbinguni kama jua, na mwezi, na nyota na vyenginevyo; na viliomo katika ardhi, kama mito, na matunda, na wanyama. Naye amekutimizieni neema zake zilio dhaahiri na zilio sitirika, msizo ziona. Na miongoni mwa watu, wapo wanao jadiliana juu ya dhati ya Mwenyezi Mungu na sifa zake bila ya dalili wala uwongozi ulio pokewa kutokana na Nabii au Wahyi (ufunuo) wenye kumurika kwa mwangaza njia ya Haki.
Rudi kwenye Sura
21. Na pindi wakiambiwa: Fuateni Haki na Uwongofu alio uteremsha Mwenyezi Mungu, wao husema: Bali sisi tunafuata tuliyo wakuta nao baba zetu. Je! Wanawafuata hao, ijapo kuwa Shetani ndio anawaitia wende kwenye upotovu utakao waingizia Motoni?
Rudi kwenye Sura
22. Na mwenye kumuelekea Mwenyezi Mungu kwa moyo wake na uso wake, na akamwakilisha Yeye mambo yake yote, naye akawa ni mwenye kutenda vitendo vyema, basi amefungamana na sababu za nguvu kabisa za kumfikisha kwenye radhi ya Mwenyezi Mungu. Na kwake Yeye, Subhanahu, ndio marejeo ya mambo yote.
Rudi kwenye Sura
23. Na asiye mtakasia Mwenyezi Mungu dhati yake na nafsi yake, basi usikuhuzunishe upinzani wake na mapuuza yake. Kwetu Sisi peke yetu ndio marejeo yao Siku ya Kiyama. Hapo tutawaonyesha vitendo vyao. Kwani Sisi tumezunguka kwa kuvijua viliomo ndani ya nafsi zao, seuze vitendo vyao vya dhaahiri.
Rudi kwenye Sura
24. Tunawastarehesha kwa muda mchache katika dunia yao, kisha tutawalazimisha kwenda kwenye adhabu kali isiyo stahimilika.
Rudi kwenye Sura
25. Ewe Nabii! Nakuapia ya kuwa ukiwauliza: Nani aliye umba mbingu na ardhi? Hapana shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, aliye ziweka dalili za Upweke wake hata zikaubomoa ushirikina wao wa kumshirikisha na wenginewe katika ibada. Na lakini wengi wao hawajui ya kuwa kwa kukiri kwao huku, basi wamesimamisha hoja ya kuwapinga wenyewe kwa ubovu wa itikadi yao.
Rudi kwenye Sura
26. Viliomo katika mbingu na ardhi ni vya Mwenyezi Mungu, kwa kuviumba, na kuvikadiria, na kuvipanga. Basi vipi wao wanaacha kumuabudu Yeye? Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika si mhitaji wa viumbe vyake wala ibada yao. Yeye ni Msifiwa kwa dhati yake. Ni mwenye kustahiki kusifiwa na waja wake.
Rudi kwenye Sura
27. Na lau kuwa miti yote ya duniani ikageuka kalamu, na maji yote ya baharini kwa wingi wake yakageuka wino, kuandikia maneno ya Mwenyezi Mungu, basi zingeli kwisha kalamu na wino ukamalizika kabla ya kumalizika maneno ya Mwenyezi Mungu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, hashindwi na chochote, Mwenye hikima hakimfutu kitu katika ujuzi wake na hikima yake. Basi hayeshi maneno yake na hikima yake.
Rudi kwenye Sura
28. Kukuumbeni nyinyi hapo mwanzo na kukufufueni baada ya kufa, mbele ya uweza wa Mwenyezi Mungu si chochote ila ni kama kumuumba na kumfufua mtu mmoja tu. Hakika Mwenyezi Mungu anaisikia kauli ya washirikina wanapo sema ati: Hakuna kufufuliwa. Naye ni Mwenye kuviona vitendo vyao, naye atawalipa kwavyo.
Rudi kwenye Sura
29. Je! Huangalii, ewe mwenye jukumu, kwa maangalio ya mwenye kuzingatia, ya kwamba hakika Mwenyezi Mungu huupunguza wakati wa usiku kwa kadri ya anavyo uongeza mchana? Na anaupunguza mchana kwa kadri ya anavyo uzidisha usiku? Naye amedhalilisha jua na mwezi kwa ajili ya maslaha yenu, na amefanya hayo yafuate mpango wa peke yao. Basi kila moja katika hayo huenda katika njia maalumu ya mbinguni wala haigeuki. Na mwendo huo unaendelea mpaka Siku ya Kiyama. Na hakika Yeye, Subhanahu, anazo khabari za yote myatendayo, na ni Mwenye kukulipeni kwayo.
Rudi kwenye Sura
30. Hayo yaliyo tajwa ni katika ajabu za uundaji wa Mwenyezi Mungu na uweza wake, kwa sababu muundaji wake ni Mungu aliye thibiti Ungu wake, Mwenye kustahiki peke yake kuabudiwa, na kwamba miungu yote mnayo iabudu badala yake ni miungu ya uwongo. Na hakika Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye Mtukufu wa shani, Mkubwa wa utawala.
Rudi kwenye Sura
31. Ewe mtu! Huzitazami marikebu, vyombo vinavyo kwenda baharini kwa rehema ya Mwenyezi Mungu, vikichukua ndani yake bidhaa za kukupeni manufaa, ili Mwenyezi Mungu akuonyesheni baadhi ya maajabu ya uundaji wake, na dalili za uweza wake? Hakika katika hayo zimo Ishara kwa kila mwenye kuvumilia mitihani yake, mwenye kuzishukuru kwa neema zake.
Rudi kwenye Sura
32. Hawa makafiri wanao mkataa Mwenyezi Mungu wakipanda marikebu, na bahari ikawachafukia, na mawimbi yakaja juu mpaka wakaona yatawafunika, na wakawa yakini watazama bila ya muhali, humkimbilia Mwenyezi Mungu, wakimwomba kwa ikhlasi na unyenyekevu, awaokoe. Basi akisha waokoa wakafika nchi kavu wapo kati yao wachache wanao kumbuka ahadi yao, na wakenda mwendo wa sawa. Na wapo kati yao, nao ndio wengi, walio sahau fadhila za Mola wao Mlezi, na wakaendelea na kumkataa. Na wala hakatai fadhila za Mola wake Mlezi na hisani yake ila kila mtu aliye mwingi wa ukhaini, aliye pita mpaka kumkanya Mola wake Mlezi.
Rudi kwenye Sura
33. Enyi watu! Fanyeni aliyo kuamrisheni Mola wenu Mlezi, na wacheni aliyo kukatazeni. Na tahadharini na adhabu yake ya Siku ya Kiyama, Siku ambayo kwamba mzazi hatamfaa mwanawe kwa lolote, wala mwana hatamfaa mzazi wake kwa lolote. Hakika Siku hii ndiyo aliyo iahidi Mwenyezi Mungu. Na ahadi yake ni ya kweli, hayendi kinyume. Basi yasikupumbazeni mapambo ya dunia na uzuri wake, mkaacha kujitayarisha kwa ajili ya Siku hiyo. Wala msikhadaike na uchochezi wa Shetani, ukakuachisheni kumuelekea Mwenyezi Mungu na kumt'ii.
Rudi kwenye Sura
34. Hakika ujuzi wa Saa ya Kiyama uko kwa Mwenyezi Mungu umethibiti. Basi hapana anaye ijua isipo kuwa Yeye tu. Na Yeye huteremsha mvua kwa wakati wake alio uweka. Na anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi, kama wanaume, au wanawake, hivyo viliomo vimetimia au havikutimia mimba. Wala hapana mtu ajuaye, mwema na muovu, atapata nini kesho, kama kheri au shari. Wala hapana mtu ajuaye pahala gani duniani itamfika ajali yake ya kufa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye timia ujuzi wake na kuwa na khabari ya kila kitu. Wala hapana yeyote awezae kujua siri yake.
Rudi kwenye Sura