') //-->
1. Sura hii imeanzia kwa Aya hii ili kufahamisha kwamba Qur'ani imetungwa kwa hizi hizi harufi wanazo zitamka Waarabu kwa wepesi na kwa uwazi. Lakini wanao kanya wameshindwa kuleta mfano wake. Nazo vile vile zinawazindua watu wasikilize na wanyamaze, na ziwapelekee kuusadiki Utume wa Muhammad s.a.w.
Rudi kwenye Sura
2,3. Waajemi waliwashinda Warumi katika nchi ya karibu na Arabuni, nayo ni mipakani mwa Shamu. Nao Warumi baada ya kushindwa kwao watakuja washinda Waajemi...
Rudi kwenye Sura
4,5... kabla ya kupita miaka tisa. Na washirikina walifurahi kwa kushinda Waajemi, na wakawaambia Waislamu: Tutakushindeni kama Uajemi ilivyo ushinda Urumi ambayo ni katika Watu wa Kitabu. Lakini Mwenyezi Mungu alitimiza ahadi yake, Warumi wakawashinda Waajemi kwa muda ule ule alio utaja. Ikawa ile ni Ishara ya ukweli wa Muhammad s.a.w. katika wito wake, na ukweli wa aliyo yaleta. Ni ya Mwenyezi Mungu amri na hukumu kabla ya kila kitu na baada ya kila kitu. Na siku ya Warumi kuwashinda Waajemi watafurahi Waumini kwa ajili ya ushindi wa Mwenyezi Mungu anao mpa amtakaye. Na Yeye ndiye Mwenye kuwashinda maadui zake, Mwenye kuwarehemu vipenzi vyake.
Maoni ya wataalamu juu ya Aya 1-4:
Katika Aya hizi tukufu ipo ishara ya vituko viwili. Cha kwanza kilikwisha tokea khasa. Na cha pili kilikuwa bado hakijatokea, na hayo ni kutoa khabari ya ghaibu. (Na imetajwa kuwa yatatokea mnamo miaka michache, ambayo maana yake ni mitatu mpaka tisa.)
Na maelezo ya tukio la mwanzo ni kuwa Waajemi na Warumi walipambana kwa vita katika nchi ya Shamu katika enzi za Khasro Abrawiz, au Khasro wa Pili, Mfalme wa Uajemi, maarufu kwa Waarabu kwa jina la Kisra, na Heraklius Mdogo, Mfalme wa Wafalme wa Kirumi, ambaye kwa Waarabu ni maarufu kwa jina la Heraklu. Katika mwaka 614 Uajemi iliiteka Antiokia, mji mkubwa kabisa katika jimbo la Mashariki katika Ufalme wa Rumi, na baadae ikatekwa Dimishqi (Damask), na ukazingwa mji wa Baitul Muqaddas (Yerusalemu) mpaka ukasalimu amri. Wakauunguza, wakawaingilia wakaazi wake kuwachinja. Moto huo uliteketeza Kanisa la Kiyama. Wavamizi hao waliuchukua Msalaba wakaupeleka kwenye jiji lao. Nyoyo za Wakristo zilihuzunika sana kwa msiba huu wa kutisha. Ilivyo kuwa kushindwa huku kuliwaletea furaha washirikina wa Makka na wakawa wanawafanyia tashtiti Waislamu kwa kuwa Warumi ni Watu wa Kitabu kama watu wa Muhammad s.a.w., na Waajemi kama washirikina si Watu wa Kitabu, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu aliye tukuka alimteremshia Muhammad Aya hizi zilizo wazi ili ambashirie kuwa Watu wa Kitabu watakuja shinda, nao Waumini watafurahi. Na kushindwa kwa washirikina na uovu wa khatima yao kuliwekewa kiwango cha miaka michache.
Na ufafanuzi wa tukio la pili ni kuwa Heraklu, Kaisari wa Rumi, ambaye jeshi lake lilishindwa, hakukata tamaa kuwa atashinda. Akawa anajiandaa kwa ajili ya mpambano utakao futa ari ya kushindwa. Mpaka mwaka wa 622 wa kuzaliwa Nabii Isa a.s. , yaani mwaka wa kwanza wa Hijra Waajemi wakalazimika kuingia vita katika nchi ya Arminia. Huko Warumi wakashinda. Na ikawa hapo ndio chanzo cha ushindi mara nyingi wa Rumi kuishinda Uajemi. Ndio hivi Watu wa Kitabu wakawashinda washirikina, na ukweli wa bishara ya Qur'ani ukathibiti.
Na tena kituko cha tatu kinafahamika kwa maana kutokana na Aya hizi tukufu, nacho kikaleta furaha kwa Waislamu. Nacho ni kushinda kwao kuwashinda washirikina Makureshi katika Vita vya Badri vilivyo tokea siku ya Ijumaa, 17 Ramadhani mwaka wa pili wa Hijra, yaani mwaka 623 wa kuzaliwa Nabii Isa a.s.
Rudi kwenye Sura
6. Mwenyezi Mungu ameagana na Waumini kwa agano la kweli. Na Mwenyezi Mungu havunji agano lake. Lakini makafiri, wanao kataa, si ada yao kujua mambo hakika yalivyo.
Rudi kwenye Sura
7. Wanajua mambo na njia za kuamirisha na kustarehe na mapambo yake, na hali wao wamepita mpaka katika ujinga na kughafilika kujitengenezea Akhera yao.
Rudi kwenye Sura
8. Yamefutwa macho yao na nyoyo zao, na hivyo hawajifikirii mambo yaliyo khusiana na roho zao wakaujua mwisho wao. Mwenyezi Mungu hakuziumba mbingu na ardhi na nyota na vinginevyo viliomo baina yao ila kwa kweli kweli, si mchezo, na kwa wakati ulio wekewa kiwango chake maalumu kitakacho kwisha. Na hakika wengi wa watu wanakataa kuwa watakuja kukutana na Mwenyezi Mungu, na kwamba itakuwapo Saa ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
9. Wao wameshikilia kukaa katika nchi zao tu, wala hawendi kote kote duniani wapate kushuhudia ulikuwaje mwisho wa walio kufuru wa kabla yao. Hao walikuwa na nguvu zaidi kuliko hawa makafiri wa sasa, na wakaugeuza uso wa ardhi wapate kutoa humo viliomo ndani yake, kama maji, na maadeni, na makulima. Na wakaiamirisha ardhi zaidi kuliko walivyo amirisha hawa. Na Mitume wa Mwenyezi Mungu wakawajia na miujiza iliyo wazi, na wao wakaikataa. Mwenyezi Mungu akawatia mkononi, kwani Yeye hawalipi bila ya makosa, wala hawashiki kabla ya kuwakumbusha na kuwapa muhula. Lakini watu hawakuwa wanadhulumu ila nafsi zao tu.
Rudi kwenye Sura
10. Tena mwisho wa hao watu walio tenda hadi ya uovu ni kuzikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazidharau khasa.
Rudi kwenye Sura
11. Mwenyezi Mungu, aliye takasika na kutukuka, huanzisha uumbaji wa binaadamu tangu mwanzo. Kisha hurejea tena kuwaumba baada ya kwisha kufa kwao. Tena hao wote wanarejea kwake Yeye peke yake kwa ajili ya hisabu na malipo.
Rudi kwenye Sura
12. Na kikifika Kiyama makafiri watakata tamaa ya kuweza kujitetea nafsi zao.
Rudi kwenye Sura
13. Na wala hawapatikani waombezi kutokana na hao walio waabudu badala ya Mwenyezi Mungu na kwa sababu yao wakawa ni makafiri duniani.
Rudi kwenye Sura
14. Na itapo simama Saa, yaani Siku ya Kiyama, kila kikundi kitaendea kwenye ajali yake ya milele.
Rudi kwenye Sura
15. Ama walio amini, na wakaambatisha Imani yao na vitendo vyema, basi hao watakuwa katika Bustani yenye miti na mauwa, watafurahi na wataneemeka.
Rudi kwenye Sura
16. Ama wale walio kufuru, na wakazikataa Ishara zetu na mkutano wa kufufuliwa na kuhisabiwa, basi hao watakuwa wanaishi katika adhabu, wala hawatoki humo.
Rudi kwenye Sura
17. Basi mtakaseni Mwenyezi Mungu na kila ambacho hakimuelekei kwa utukufu wake na ukamilifu wake. Na muabuduni Yeye mnapo ingia jioni na mnapo ingia asubuhi.
Rudi kwenye Sura
18. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye kustahiki kuhimidiwa na kusifiwa na kushukuriwa na walioko katika mbingu na katika ardhi. Basi mhimidini na mumuabudu wakati wa alasiri na mnapo ingia adhuhuri.
Rudi kwenye Sura
19. Yeye hutoa kiumbe kihai kutokana na kitu kisicho kuwa na uhai. Na hukitoa kitu kisicho kuwa na uhai kutokana na kitu chenye uhai. Na huihuisha ardhi kwa mimea baada ya kuwa ni kavu tupu. Na mfano wa anavyo fanya hivi basi ndivyo hivyo Mwenyezi Mungu atakutoeni makaburini mwenu.
Rudi kwenye Sura
20. Na katika dalili za kuonyesha ukamilifu wa uweza wake ni kuwa ameumba asili yenu kutokana na udongo usio kuwa na uhai. Kisha nyinyi mmekuwa watu mlio tawanyika katika ardhi kwa ajili ya kutafuta kitacho kuleteeni kubaki kwenu.
Rudi kwenye Sura
21. Na katika dalili za rehema yake ni kuwa kakuumbieni, enyi wanaume, wake wa jinsi yenu mkae nao kwa uzuri na kituo. Na amekujaalieni baina yenu na wao mapenzi na kuoneana huruma. Hakika katika haya bila ya shaka zipo dalili kwa watu wanao ufikiria uumbaji wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Rudi kwenye Sura
22. Na katika dalili za kuonyesha uweza wake na hikima yake ni uumbaji wa mbingu na ardhi kwa mpango huu wa namna peke yake wenye kupendeza, na kukhitalifiana ndimi zenu katika lugha mbali mbali na lafdhi mbali mbali, na kutafautiana rangi zenu katika weusi na weupe na nyenginezo. Hakika katika haya bila ya shaka zipo dalili zinazo wanufaisha watu wenye ujuzi na kufahamu.
Rudi kwenye Sura
23. Na katika Ishara zake zenye kuonyesha ukamilifu wa uweza wake ni kuwa amekupeni sababu za mapumziko kwa kulala kwenu. na akakusahilishieni kutafuta riziki usiku na mchana kutokana na fadhila zake kunjufu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo dalili kwa watu wanao nafiika kwa wanayo yasikia.
Rudi kwenye Sura
24. Na katika Ishara zake ni kuwa anakuonyesheni umeme katika mawingu, muone khofu kwa radi na tamaa ya kupata mvua ya kuteremka kutoka mbinguni ili ardhi ihuike baada ya kuyabisika. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo dalili kwa watu wanao zingatia mambo wakayafahamu kama ifaavyo.
Rudi kwenye Sura
25. Na katika dalili za ukamilifu wa uweza wake, na hikima yake, na ukunjufu wa rehema yake, ni kuwa mbingu na ardhi zimesimama kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kama muonavyo, kwa mujibu wa hukumu za ufundi na ustadi wa kupanga. Kisha akikuiteni kwa ajili ya kukufufueni mtatoka makaburini mbio mbio kuitikia wito wake.
Rudi kwenye Sura
26. Na ni vyake Mwenyezi Mungu Subhanahu vyote viliomo katika mbingu na ardhi, kwa kuviumba, na kuvimiliki, na kunyenyekea. Vyote ni vyenye kumt'ii Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
27. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu aliye umba viumbe vyote bila ya ruwaza, kisha atavirudisha tena baada ya mauti. Na kurudisha kwake ni jambo jepesi zaidi kuliko kuvizua mwanzo, kwa mujibu wa nadhari ya vipimo vyenu na itikadi yenu, kwamba kukirudisha kitu ni sahala kuliko kukizua. Na Mwenyezi Mungu ana sifa ya kutangulia ya shani ya namna ya pekee katika uweza ulio kamilika, na hikima iliyo timia, katika mbingu na ardhi. Na Yeye ni Mwenye kushinda katika ufalme wake, Mwenye hikima katika vitendo vyake na kukadiria kwake.
Rudi kwenye Sura
28. Mwenyezi Mungu amekupigieni mfano unao tokana na nafsi zenu - na Mwenyezi Mungu Mtukufu Mwenye kutukuka amempigia mfano huo huyo aliye wafanya viumbe ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Mfano wenyewe ni: Kwani nyinyi mnawafanya watumwa wenu washirika katika mali na vyenginevyo tulivyo kupeni? Basi, je! Nyinyi na wao ni sawasawa katika hayo, mnawaogopa hao watumwa wenu, na hamfanyi kitu kwa mnavyo miliki bila ya ruhusa yao, kama wanavyo ogopana waungwana wao kwa wao? Ikiwa nyinyi hamyatii akilini haya wala hamyafanyi, basi imekuwaje hata mnavifanya baadhi ya alivyo vimiliki Mwenyezi Mungu kuwa ni washirika wake? Kwa ufafanuzi kama huu tunawabainishia Aya watu ambao wanazingatia mifano inayo pigwa.
Rudi kwenye Sura
29. Bali walio kufuru wanafuata pumbao zao bila ya kujua matokeo ya kufuru zao. Basi hapana yeyote aliye achiliwa na Mwenyezi Mungu kupotoka, atakaye ongoka. Wala hapana ataye waombea, na akawalinda na adhabu.
Rudi kwenye Sura
30. Basi elekeza uso wako, na uelekee kwenye Dini mbali na upotovu wao. Na shikamana na maumbile ya Mwenyezi Mungu aliyo waumbia watu. Nayo ni kuwa wao ni wenye kuikubali Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, wala si wenye kuikataa. Na haitakikani kuigeuza khulka hii. Huko ndio kuumbwa juu ya Tawhidi, nayo ndiyo Dini Iliyo Nyooka sawasawa. Lakini washirikina hawaujui ukweli huo.
Rudi kwenye Sura
31. Kuweni wenye kurejea kwake kwa kutubu! Na tendeni aliyo kuamrisheni, na acheni aliyo kukatazeni. Na hifadhini Sala, wala msiwe katika wenye kumuabudu mwenginewe pamoja na Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
32. Katika walio igawanya dini yao, wakawa makundi mbali mbali, kila kikundi kinawania upande wake, na kila fungu miongoni mwao linafurahia kwa waliyo nayo, wanajidhania kuwa wao tu ndio wako katika haki.
Rudi kwenye Sura
33. Na watu yakiwapata madhara, ya ugonjwa au shida yoyote, humkimbilia Mwenyezi Mungu, na wakamwomba nao wamerejea kwake, wakitaka waondolewe hiyo shida. Kisha akiwaonjesha kuondokewa na hiyo shida, na akawapa sehemu ya fadhila yake, baadhi yao hukimbilia mbio kwendea kumshirikisha Mola wao Mlezi.
Rudi kwenye Sura
34. Upate kuwa mwisho wa mambo yao kuzikanya neema za Mwenyezi Mungu alizo wapa. Basi enyi makafiri mnao kataa! Stareheni kama mpendavyo. Mtakuja ujua mwisho wenu.
Rudi kwenye Sura
35. Kwani tuliwaacha katika upotovu wao, wala hatukuwazindua na ndoto zao, bali tukawateremshia hoja ya kushuhudia kwa yale walio kuwa wakiyashirikisha na Mwenyezi Mungu?
Rudi kwenye Sura
36. Na tukiwaonjesha watu neema huifurahia kwa furaha ya kuwatia kiburi. Na ikiwapata shida kwa madhambi waliyo yachuma wenyewe huwa wepesi wa kukata tamaa na Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema.
Rudi kwenye Sura
37. Je! Wameingiwa na ujinga hata hawajui nini kinacho fikisha kwenye Imani? Wala hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humdhikisha amtakaye, kwa mujibu inavyo wafikiana na hikima yake? Hakika katika hayo zipo dalili wazi kwa watu wanao iamini Haki.
Rudi kwenye Sura
38. Na ilivyo kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye anaye kunjua riziki na akaidhikisha, basi mpe aliye jamaa haki yake kwa ajili ya hisani na kuunga udugu. Na mhitaji na aliye katikiwa safari yake wape pia haki zao kutokana na Zaka na Sadaka. Hayo ndiyo ya kheri kwa wenye kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, na wanataka thawabu zake. Na hao ndio wenye kufuzu kuipata neema ya milele.
Rudi kwenye Sura
39. Na mnacho toa, enyi wala riba, katika mali ili yakuzidieni kutokana na mali yao, basi kwa Mwenyezi Mungu hakizidi wala hakiingii baraka. Na mnacho toa sadaka kwa kutafuta wajihi wa Mwenyezi Mungu, bila ya riya, kujionyesha tu, wala tamaa ya kulipwa - basi hao ndio watakao pewa malipo mema marudufu.
Rudi kwenye Sura
40. Mwenyezi Mungu, Subhanahu, Aliye takasika, ndiye aliye kuumbeni. Kisha akakupeni cha kukupeni maisha. Kisha ndiye anaye kufisheni; na kisha atakufufueni kutoka makaburini kwenu. Je! Yupo yeyote katika hao miungu wa kishirikina mnao dai, na mkawaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, mwenye kutenda hayo, ya kuumba, na kuruzuku, na kufisha, na kufufua, au kitendo chochote? Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wanayo mshirikisha naye.
Rudi kwenye Sura
41. Kumetokea moto, na ukame, na kila maafa, na kuharibika biashara, na mafuriko, kwa sababu ya uovu na madhambi, ili Mwenyezi Mungu awaadhibu watu duniani kwa baadhi ya vitendo vyao, huenda labda wakatubia maasi yao.
Rudi kwenye Sura
42. Ewe Nabii! Waambie washirikina: Nendeni pande mbali mbali za dunia, muangalie vipi waliishia walio kutangulieni? Mtaona kuwa Mwenyezi Mungu aliwaangamiza na akayaharibu majumba yao, kwa sababu wengi walikuwa washirikina kama nyinyi.
Rudi kwenye Sura
43. Na uelekeze sawa sawa uso wako kwenye Dini iliyo kamilika kunyooka kwake, kabla haijafika Siku ambayo hapana mtu atakaye weza kuirejesha kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu watagawanyika, na hali zao zitakhitalifiana.
Rudi kwenye Sura
44. Mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu, basi itampata mwenyewe laana ya ukafiri wake. Na wenye kuamini na wakatenda mema basi ni kwa ajili ya nafsi zao tu, wanajitengenezea njia nzuri iliyo nyooka.
Rudi kwenye Sura
45. Kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu huwalipa walio amini na wakatenda mema kwa yale waliyo yatanguliza. Na tena huwazidishia malipo yao kwa kuwafadhili. Kwani Yeye anawapenda hao na anawachukia walio kufuru na wakazikanya neema zake.
Rudi kwenye Sura
46. Na katika dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu na rehema yake ni kuwa Yeye huzipeleka pepo za kubashiria mvua kwa sababu ya kumwagia mashambani na kunyweshea wanyama na watu. Na ili akupeni katika kukumimieni hisani zake manufaa yanayo tokana na mvua, na ili zipate kwenda marikebu za majini kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kudra yake, na ili mtafute riziki kwa fadhila yake kwa biashara na kutumia viliomo nchi kavu na baharini, na ili mpate kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ut'iifu wenu na kumuabudu Yeye tu.
Rudi kwenye Sura
47. Na kabla yako hakika tulikwisha watuma Mitume kwa kaumu zao. Na kila Mtume alikuja na hoja zilizo wazi, zenye kuonyesha ukweli wake. Kaumu yake ikamkadhibisha. Nasi, basi, tukawaangamiza wale walio fanya madhambi na wakaasi. Na Mwenyezi Mungu amejilazimisha nafsi yake kuwanusuru waja wake Waumini.
Rudi kwenye Sura
48. Mwenyezi Mungu, Subhanahu Wataa'la, Aliye takasika na akatukuka, ndiye anaye zituma pepo ambazo kwa nguvu zake zikayasukuma mawingu. Na Mwenyezi Mungu akayatandaza mbinguni kama atakavyo hapa na kule, kwa uchache au wingi. Na akayafanya mapande mapande. Basi nawe ndio unaona mvua inatoka kwenye mawingu. Na Mwenyezi Mungu anapo iteremsha mvua kwa waja wake awatakao, hao huwa wepesi kukunjuka roho na kufurahi.
Rejea kwenye maelezo ya Aya ya 43 ya Sura An-Nur.
Rudi kwenye Sura
49. Nao hakika kabla ya kunyweshewa na mvua hiyo walikuwa wamekwisha kata tamaa na wamedawaa.
Rudi kwenye Sura
50. Basi iangalie mvua, muangalio wa kufikiri na kuzingatia, vipi Mwenyezi Mungu anavyo ihuisha ardhi baada ya kuwa imetulia kama maiti. Hakika aliye ihuisha ardhi baada ya kufa kwake bila ya shaka ni Muweza wa kuwahuisha watu. Na Yeye ni mtimilivu wa uweza, hashindwi na kitu.
Rudi kwenye Sura
51. Nami ninaapa! Lau kuwa tukiwapelekea upepo wa kudhuru mimea, nao wakauona umekuwa manjano kwa sababu yake, hapana shaka wataendelea hata baada ya kuwa manjano, wakizikanya neema, na wakimkataa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
52. Basi wewe usihuzunike kwa inadi yao na kuto kukuitikia. Kwani wewe huwezi kuwafanya maiti wausikie wito wako; wala kuwafanya viziwi wakusikie unapo wanadia, wakizidi uziwi wao kwa wanavyo kukimbia kwa mapuuza.
Rudi kwenye Sura
53. Na watu hawa ni kama vipofu, kwa vile nyoyo zao zimefungika hawafuati uwongofu. Na wewe huwezi kuwaongoa vipofu, na ukawazuia wasifanye ukafiri wao. Ama hakika wewe unaweza kuwafanya wakusikie msikio wa kufahamu na kukubali wale ambao nyoyo zao zimejitayarisha kupokea Imani. Basi hao wanaifuata Haki inapo dhihiri.
Rudi kwenye Sura
54. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na tone la manii, mkawa dhaifu, hamna nguvu. Kisha akakujaalieni baada ya unyonge huo mkawa na nguvu. Akakukuzeni hata mkawa watu wazima. Kisha akakufanyeni baada ya nguvu hizi mkawa na udhaifu wa uzee na ukongwe. Yeye huumba atakavyo. Na Yeye ndiye Mjuzi wa kupanga uumbaji wake, Muweza wa kuleta atakacho.
Rudi kwenye Sura
55. Na Siku itapo fika Saa ya Kiyama makafiri wataapa kwamba hawakukaa duniani au makaburini mwao isipo kuwa kwa muda wa saa moja tu. Na mfano wa mwendo kama huo ndivyo Mashetani walikuwa wakiwaendesha duniani, kuwaachisha Haki na kuwapeleka kwenye upotovu.
Rudi kwenye Sura
56. Na walio pewa ujuzi na Mwenyezi Mungu, nao ni Manabii, na Malaika, na Waumini, watasema: Bila ya shaka nyinyi mlikwisha kaa katika hukumu ya Mwenyezi Mungu na amri yake mpaka Siku ya kufufuliwa. Basi hii ndiyo Siku ya kufufuliwa mlio ikanya. Na lakini nyinyi duniani mlikuwa hamjui kama hii ni Haki, kwa ujinga wenu na mapuuza yenu.
Rudi kwenye Sura
57. Basi Siku hiyo watafufuliwa watu. Hakutowafaa kitu makafiri kutoa udhuru wao kwa kukanya kwao na kuwakadhibisha kwao Mitume wao. Wala hatawataka mtu yeyote wafanye jambo la kumridhi Mwenyezi Mungu. Kwa kuwa wao wamekwisha dharaulika mbele yake, na wamefukuzwa kutokana na rehema yake.
Rudi kwenye Sura
58. Na kwa ajili ya uwongofu wa watu, tumebainisha katika Qur'ani hii kila mfano wa kuwaongoza kwenye Njia ya Uwongofu. Na wewe ukiwaletea kila muujiza bila ya shaka makafiri, kwa kupita hadi inda yao na ugumu wa nyoyo zao, watasema: Wewe na hao wanao kufuata si chochote ila ni waongo tu katika huo wito wenu.
Rudi kwenye Sura
59. Na muhuri kama huu umepigwa juu ya nyoyo za hao wasio ijua Tawhidi miongoni mwa majaahili.
Rudi kwenye Sura
60. Ewe Nabii, yavumilie maudhi yao. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu kukupa ushindi juu ya maadui wako, na kushinda kwa Uislamu juu ya dini zote, ni kweli isiyo geuka kabisa. Wala wasio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wasikuletee dhiki na ukaiacha subira.
Rudi kwenye Sura