2. Mwenyezi Mungu ni Mmoja, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Na kila kiliomo ulimwenguni kinashuhudia hayo kwa namna ya kilivyo umbika na kushikamana, katika umbo na kazi, na viumbe vyenginevyo. Na Yeye Mwenyezi Mungu ni Yuhai, hafi. Ni Mwenye kusimamia na kuendesha mambo yote ya ulimwengu. Yeye ndiye Mwenye kuyadabiri na kuyasarifu.
3. Umeteremshiwa wewe, Muhammad, hii Qur'ani yenye kukusanya ukweli wa misingi yote ya Sharia ya Mbinguni iliomo katika Vitabu vilivyo tangulia. Na hakika kabla ya Qur'ani Mwenyezi Mungu alikwisha teremsha Taurati kwa Musa, na Injili kwa Isa.
4. Ameziteremsha hizo kabla ya Qur'ani ili kuwaongoa watu. Walipo kengeuka akaiteremsha Qur'ani ipambanue baina ya Haki na baat'ili, baina ya kweli na uwongo, baina ya uwongofu na upotovu. Basi hii Qur'ani ni Kitabu cha kweli, chenye kudumu milele. Na kila mwenye kuacha aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu na akazikanya Aya zake, Ishara zake, atapata adhabu iliyo kali. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza, hashindwi na kitu, na Mwenye kuwalipa wanao stahiki kulipwa.
5. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. Kwa hivyo hapana kinacho fichika kwake katika ardhi na hata katika mbingu, kikiwa kidogo au kikubwa, kinacho onekana na kisicho onekana.
6. Ni Yeye, Mwenyezi Mungu, ndiye anakuundeni, anakupeni Sura na hali nyinyi mmo matumboni mwa mama zenu, kwa Sura na umbo mbali mbali kama apendavyo Yeye. Hapana mungu ila Yeye Mwenye nguvu katika ufalme wake, Mwenye hikima katika kuunda kwake.
7. Na Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuteremshia wewe, Muhammad, hii Qur'ani. Na ni katika hikima yake kufanya ndani yake mna Aya zilizo wazi, maana yake na makusudio yake yanajuulikana wepesi. Hizi ndio msingi, ndio asli. Marejeo yote yawe juu ya hizi. Na zipo Aya nyengine za mifano, za mshabaha, zenye kutatanisha. Wengi hawawezi kuzielewa. Na wale ambao hawakubobea, hawakuzama katika ilimu, huwababaisha. Na zimeteremka hizi Aya za mifano ili wanazuoni wachungue kutafuta ilimu ndani yake, na wazingatie, na wazidi kufikiri katika jitihadi, na kufanya uchunguzi katika Dini. Lakini mtindo wa walio iacha Haki ni kutaka kuzifuata hizo Aya za mifano ili kutaka kuchochea fitna, na huzifasiri kwa kufuata matamanio yao. Na hapana anaye jua maana ya Aya hizi kwa hakika ila Mwenyezi Mungu, na wale walio thibiti kweli katika ilimu. Na hao walio thibiti husema: "Sisi tuna yakini kuwa hayo yanatokana na Mwenyezi Mungu. Sisi hatufarikishi katika kuiamini Qur'ani baina ya sehemu zilizo wazi (Muhkam) na zile za mifano (Mutashaabih). Na hawazingatii ila watu wenye akili iliyo nzima, ambayo haifuati pumbao na matamanio.
8. Hao wanazuoni wenye akili husema: Mola wetu Mlezi! Usizifanye nyoyo zetu zikaacha Haki baada ya Wewe kwisha tuongoza kuiendea hiyo Haki. Ewe Mola wetu Mlezi! Tupe rehema kutoka kwako kwa kutuwezesha na kututhibitisha. Hakika Wewe ndiwe Mwenye kunyima na ndiwe Mpaji.
9. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ndiwe utao wakusanya watu Siku hiyo isiyo na shaka, ili kumlipa kila mmojapo kwa alilo litenda. Kwani Wewe umeahidi hayo, na Wewe hukhalifu miadi yako.
10. Katika Siku hiyo makafiri hawatokingwa na mali yao na yangawa mengi vipi, wala na watoto wao na wangawa wengi vipi. Hayo yote yatakuwa ndio kuni za Moto za kuwateketeza wenyewe.
11. Na hali ya hao ni kama hali ya kaumu ya Firauni walio kuwa na inda kabla yao. Walizikadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu juu ya kuwa zilikuwa ziwazi kabisa. Basi Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa sababu ya madhambi waliyo yatenda. Na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
12. Ewe Nabii! Waambie hawa walio kufuru: Bila ya shaka nyinyi mtashindwa hapa duniani, na kesho Akhera mtaadhibiwa. Na Jahannamu ndio itakuwa tandiko lenu la kulalia; na ovu lilioje tandiko hilo!
13. Ilikuwa Ishara wazi na mazingatio yaliyo dhaahiri katika makundi mawili ya wapiganaji walipo pambana siku ya Badri. Kundi moja, hilo la Waumini, likipigana kwa ajili ya kutukuza Neno la Mwenyezi Mungu na kueneza Haki. Na kundi la pili, hilo la makafiri, likipigania pumbao na matamanio. Ikawa, basi, Mwenyezi Mungu katika kuwaunga mkono Waumini aliwafanya wale makafiri wawaone Waumini idadi yao mara mbili kuliko walivyo. Kwa hivyo makafiri wakaingiwa na khofu nyoyoni mwao wakaemewa. Na Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Katika haya, hakika, pana mazingatio kwa wenye nadhari iliyo ongoka isiyo kengeuka na kuiacha Haki.
14. Wanaadamu wameumbwa kuwa wanapenda matamanio ya vitu kama wanawake, wana, na wingi wa madhahabu na fedha, na farasi wazuri wazuri walio fundishika, na mifugo kama ngamia, ng'ombe, mbuzi, kondoo, na kadhaalika mashamba makubwa. Lakini yote hayo ni starehe na kwa matumizi ya uhai huu wa duniani wenye kupita na kuondoka. Na hayo si chochote si lolote ukilinganisha na hisani anayo wafanyia Mwenyezi Mungu waja wake wanao pigania jihadi katika Njia yake watakapo rejea kwake Yeye Akhera.
15. Ewe Nabii! Sema: Nikwambieni yaliyo bora kuliko hayo yote mliyo pambiwa duniani? Kwa wale wachamngu wamewekewa malipo ya dhamana kwa Mola wao Mlezi, nayo ni Bustani zipitazo mito chini ya vivuli vya miti. Humo watastarehe kwa maisha mazuri wala hawatoingiliwa na khofu ya kuwa neema hiyo itaondoka, kwani wamekwisha katibiwa kuwa humo watabaki daima milele. Watakuwamo humo wake walio t'ahirika, wamesafika na kila ila ya wanawake wa kidunia. Na juu ya yote hayo, watapata Radhi ya Mwenyezi Mungu ambayo wataihisi chini ya kivuli chake kuwa ndiyo Neema kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali za waja wake; hapana jambo linalo fichikana kwake, hawana siri asiyo ijua Yeye.
16. Malipo haya watayapata wale ambao nyoyo zao zimejaa Imani, na wakatangaza kwa ndimi zao wakisema kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu: Mola Mlezi wetu! Hakika sisi tumeamini kwa kuitikia wito wako. Basi tusamehe dhambi zetu, na utuhifadhi na adhabu ya Moto.
17. Na malipo haya huyapata wanao stahamili mashaka kwa ajili ya ut'iifu wao, na kujitenga na maasi, na kuvumilia dhiki, watu ambao ni wakweli katika kauli zao na vitendo vyao, na niya zao, wenye kudumu katika ut'iifu kwa kunyenyekea, wenye kutoa wawezacho bilhali walmali na vyenginevyo kwa sababu ya mambo ya kheri, ambao kwamba wanamtaka msamaha Mwenyezi Mungu mwishoni mwa usiku, kabla ya alfajiri, zinapo safika roho na hutengenea kuzingatia na kutafakari katika utukufu wa Muumbaji.
18. Mwenyezi Mungu amebainisha wazi katika maumbaji yake dalili na Ishara ambazo hawezi kuzipinga mwenye akili, ya kwamba Yeye ni Mmoja, wala hana mshirika wake, na kwamba Yeye ndiye Mwenye kusimamia mambo ya viumbe vyote kwa uadilifu. Na kwa haya pia wamekiri Malaika walio t'ahirika, na wameyajua watu wa ilimu kwa yakini, na kwamba Yeye ilio tukuka shani yake ni Mpweke katika Ungu, wala hana wa kumshinda katika jambo, na hikima yake imeenea kila kitu.
19. Hakika Dini ya Haki aliyo iridhi Mwenyezi Mungu ni Dini ya Tawhidi, ya Mungu Mmoja, na kumnyenyekea Yeye kwa usafi wa moyo. Mayahudi na Wakristo wamekhitalifiana na Dini hii, wakazua na wakabadilisha. Na wala kukhalifu kwao hakukuwa kwa kudanganyikiwa au kwa ujinga ilipo wajia ilimu, bali yalikuwa hayo kwa uhasidi na ushindani tu. Na mwenye kupinga Ishara za Mwenyezi Mungu, basi na angojee hisabu ya Mwenyezi Mungu, nayo yenda kasi mno.
20. Na hawa makafiri wakijadiliana nawe katika Dini hii baada ya wewe kuwapa hoja zote, huna haja kupigizana nao kelele kwa majadiliano. Waambie tu: Mimi na Waumini walio nifuata tumemsafia Mwenyezi Mungu peke yake ibada yetu. Na waambie Mayahudi na Wakristo na washirikina wa Kiarabu: Dalili zimekwisha bainika kwenu, basi silimuni. Wakisilimu inakuwa wameijua njia ya uwongofu na wameifuata. Na wakikataa huna lawama wewe kwa kukataa kwao. Waajibu wako ni kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu tu. Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema waja wake. Hapana lolote lao, hali yao na vitendo vyao, linalo fichikana kwake.
21. Hakika wale wanao zipinga Ishara za Mwenyezi Mungu katika uumbaji na hizi zilizo teremka, na wakawauwa Manabii alio watuma Mwenyezi Mungu waje kuwaongoa - bila ya haki kabisa, na hiyo ni dhulma kubwa mno - na wakawauwa wale wanao waita watu wafanye haki na uadilifu, watu hao wanastahiki adhabu kali. Basi wabashirie adhabu hiyo!
22. Watu wenye sifa kama hizo, a'mali zao zimebat'ilika ijapo kuwa baadhi yake ni njema, na hazina matunda. Kwa hivyo haziwafai duniani, na mwisho wake ni hizaya na adhabu huko Akhera. Na wala hawana wa kuwaokoa na khasara na adhabu watayo ipata.
23. Je! Huijui hali ya wale walio pewa sehemu ya Kitabu na ilimu (nao ni Mayahudi na Wakristo) wanaitwa wende kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu, nacho ni Qur'ani ili kiwapambanulie baina ya Kweli na uwongo, Haki na baat'ili, katika khitilafu zilizo zuka baina yao, na wala hawafanyi haraka ya kumuitikia anaye waita. Bali baadhi yao wanamkataa; shani yao ni kuukataa wito wa kheri.
24. Hao wanao kataa miongoni mwa Mayahudi wamedanganyika kwa kukataa kwao na matumaini ya uwongo wanao jitamanisha nafsi zao ya kuwa Moto hautawagusa ila siku chache tu. Na kudanganyika huko na matamanio hayo yamewapelekea kuendelea kuzua katika dini yao kunako endelea.
25. Basi itakuwaje hali yao wakati atapo wakusanya Mwenyezi Mungu Siku ya Akhera, ambayo hapana shaka kuwapo kwake, na kuwa kutakuwapo kuhisabiwa. Basi kila nafsi itapewa malipo yake ya kutosha. Na wao wanastahili kupata hiyo adhabu ya Jahannamu watakayo ipata.
26. Ewe Nabii! Sema kwa unyenyekevu na kuukiri utukufu wake Mwenyezi Mungu: Ewe Mola Mlezi! Ni Wewe peke yako ndiye Mwenye kumiliki kutasarafu katika mambo yote. Unampa kuhukumu na utawala umtakaye, na unamnyima umtakaye. Unampa utukufu umpendaye kati ya waja wako kwa kumwezesha kuzishika sababu za kuufikia huo utukufu. Na unampiga madhila na unyonge umtakaye. Basi Wewe peke yako unamiliki kheri yote. Hushindwi na kitu katika kutimiza muradi wako na yanayo kupelekea hikima yako kuyakatia shauri katika mipango ya uumbaji wako.
27. Na Wewe kwa ulivyo umba na ukawekea sababu na nyendo, unauingiza usiku katika mchana kwa unavyo zidi mchana urefu wake, na unauingiza mchana katika usiku kwa unavyo zidi usiku urefu wake. Na unatoa chenye sifa za kuonekana kihai katika kisicho kuwa na sifa za uhai, kama unavyo toa chenye kukosa uhai kutokana na kilicho hai, chenye kutamakani na sababu za uhai. Unampa neema zako kubwa umtakaye kwa mujibu wa mipango ya hikima zako. Hapana mchunguzi wa kukuhisabu Wewe. Huyo Mwenye shani hii haemewi na kumjaalia Mtume wake na awapendao, ubwana, na utawala, na utajiri, na wasaa, kama alivyo waahidi.
28. Ikiwa basi ni Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la ndiye Yeye peke yake Mmiliki wa mamlaka, anatukuza na kuangusha, na katika mikono yake pekee ipo kheri, na uumbaji, na riziki, basi haifai kwa Waumini kuwafanya wasio kuwa Waumini wawe na utawala juu yao, wakauwacha msaada wa Waumini wenzao. Kwani wakifanya haya inakuwa wanaivunja Dini, na wanawaletea maudhi wenye Dini, na ni kuudhoofisha utawala na udugu wa Kiislamu. Na mwenye kufuata njia hii basi kwa Mwenyezi Mungu Mmiliki wa mamlaka yote hana lake jambo. Wala haimfalii Muumini kuridhia kuwapa utawala na ulinzi makafiri ila awe hana hila. Hapo basi anaweza kujikinga na madhara yao kwa kuonyesha ut'iifu kwao. Ni juu ya Waumini wawe daima katika ulinzi wa Kiislamu, kwani huo ndio ulinzi wa Mwenyezi Mungu. Na watahadhari wasitoke kwenye ulinzi wa Mwenyezi Mungu kuuendea ulinzi mwenginewe asije akawaadhibu kwa kuwaletea madhila baada ya utukufu. Na kwake Yeye ndio marejeo, wala hapana pa kukimbilia kutokana na madaraka yake duniani wala Akhera.
29. Sema, ewe Nabii!: Mkiyaficha yaliyomo vifuani mwenu au mkiyadhihirisha katika vitendo vyenu na kauli zenu ni sawa, kwani Mwenyezi Mungu anayajua yote, na anayajua yote yaliymo mbinguni na yaliyomo duniani, yanayo onekana na yanayo fichikana. Uwezo wake unapenya katika viumbe vyake vyote.
30. Basi na watahadhari wale wanao ikhalifu amri yake na Siku ambayo kila mtu atakuta vitendo vyake vya kheri hata kilicho kichache kimeletwa hadharani; na pia uovu wake alio utenda ambao angetamani lau kuwa uko mbali, mwisho wa umbali, hata asiuone kwa kuuchukia na kukhofu kutumbukia katika adhabu zake. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni na adhabu zake pindi mkitokana na ulinzi wake na utawala wake, ambao ni upole na rehema kwa waja wake.
31. Sema: Ikiwa nyinyi ni wakweli katika madai yenu, kuwa mnampenda Mwenyezi Mungu na mnataka Mwenyezi Mungu akupendeni, basi nifuateni mimi kwa ninayo kuamrisheni na ninayo kukatazeni. Kwani mimi nimetumwa na Mwenyezi Mungu. Basi Mwenyezi Mungu atakupendeni kwa hivyo, na atakulipeni kwa kukufanyieni hisani na kusamehe makosa yenu. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kuwasamehe na kuwarehemu waja wake.
32. Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na wakikukataa basi hao ni makafiri, wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri.
33. Kama Mwenyezi Mungu alivyo mteua Muhammad afikishe ujumbe wake, na akajaalia kumfuata Muhammad ni njia ya kufikia mapenzi ya Mwenyezi Mungu na kupata maghfira na rehema yake, kadhaalika ametaja Mwenyezi Mungu kuwa Yeye alimteua Adam na akamjaalia ni katika wateule wa walimwengu. Pia alimteua Nuhu kwa kumpa ujumbe, na akamteua Ibrahim na ukoo wake, nao ni Ismail na Is-haq na Manabii wengine kutokana na wana wao hao. Miongoni mwao ni Musa a.s. Akawakhitari ukoo wa Imran, na miongoni mwao akamkhitari Isa na mama yake. Alimfanya Isa awe ni Mtume kwa Wana wa Israili, na Maryam akamfanya awe ni mama wa Isa bila ya baba.
34. Amewakhitari hao ukoo ulio safi, wakirithiana usafi na fadhila na kheri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maneno ya waja wake kwa vitendo vyao na vinavyo fichwa vifuani mwao.
35. Ewe Nabii! Taja hali ya mke wa Imran alipo weka nadhiri wakati alipo kuwa na mimba, kuwa mwana aliomo tumboni mwake awe ni wa kumtumikia Mwenyezi Mungu tu na kukhudumia nyumba yake. Alisema: Ewe Mola! Hakika mimi nimekuwekea nadhiri huyu aliyomo tumboni mwangu awe ni wa kukhudumia nyumba yako, basi nikubalie haya. Hakika Wewe ni Mwenye kusikia kila kauli, na Mwenye kujua kila hali.
36. Alipo jifungua mimba akasema kwa kujiudhuru kumwambia Mola wake Mlezi: Niliye mzaa ni mwanamke - na Mwenyezi Mungu anajua vilivyo alicho kizaa, na kuwa mwana wenyewe ni mwanamke ni bora kuliko alivyo taka mama kuwa awe mwanamume. Akasema yule mama: Mimi nimemwita Maryamu, na mimi nakuomba umlinde yeye na ukoo wake na uharibifu wa Shetani maluuni.
37. Mwenyezi Mungu alimpokea Maryamu kuwa ni nadhiri aliyo iweka mama yake, akamwitikia maombi yake, akamkuza makuzo mema, na akamlea katika kheri yake, Mola Mlezi, huku akimruzuku na kumshughulikia kwa malezi mazuri ya kumpa nguvu mwili wake na roho yake. Mwenyezi Mungu akamkabidhi Zakariya a.s. awe mlezi wake. Zakariya kila akiingia chumbani, alipo kuwa Maryamu anaabudu, akikuta chakula wasicho kizowea wakati ule. Zakariya akasema kwa kustaajabu: Ewe Maryamu! Umepata wapi riziki hii? Naye akamjibu: Hichi ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu. Ni shani yake kumruzuku mja wake amtakaye riziki nyingi bila ya hisabu au kipimo.
38. Zakariya a.s. alipo iona neema ya Mwenyezi Mungu kwa Maryamu alimwelekea Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu akimwomba kwa fadhila yake na ukarimu wake na uwezo wake, naye ampe mtoto mwanamume. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maombi ya mwenye kuomba kwake kwa unyenyekevu. Naye ni Muweza wa kuitikia maombi na hata zinge kuwapo pingamizi za kikawaida kama ukongwe na utasa.
39. Mwenyezi Mungu aliitikia dua yake. Malaika akamnadia naye kasimama pahala pake pa ibada akimwelekea Mola wake Mlezi kumbashiria mtoto mwanamume jina lake Yahya, atakaye muamini Isa a.s. ambaye atazaliwa kwa kauli ya Mwenyezi Mungu kwa njia isiyo ya dasturi. Na Yahya atawahimiza kaumu yake kushika ilimu na kusali, na atakataza mambo ya pumbao na matamanio, na atamfanya awe miongoni mwa Manabii na watu wema.
40. Basi Zakariya alipo pewa bishara hii, ya kupata mwana, alimwelekea Mola Mlezi wake kwa shauku ya kutaka kujua vipi yatakuwa hayo, ya kuwa na mwana na ilhali yeye hanazo njia zijuulikanazo, kwa kuwa yeye mwenyewe kesha konga, na mkewe ni tasa. Mwenyezi Mungu akamjibu kuwa Yeye anapo taka jambo ama huzileta njia au huumba bila ya njia zinazo juulikana. Kwani Yeye hutenda apendavyo.
41. Zakariya akamwomba Mola wake Mlezi amfanyie alama ya kuhakikisha bishara hii. Mwenyezi Mungu akamjibu: Alama yako ni kuwa hutaweza kusema na watu muda wa siku tatu, isipo kuwa utatumia ishara tu kuashiria utakacho. Na shikamana na dhikri ya Mwenyezi Mungu ukimtakasa na kumtukuza jioni na asubuhi.
42. Na kumbuka ewe Nabii, pale Malaika walipo mwambia Maryamu ya kwamba Mwenyezi Mungu amekukhitari uwe ni mama wa Nabii wake, na amekusafisha na kila uchafu, na amekuteuwa wewe uwe mama wa Isa kuliko wanawake wote wengineo.
43. Na kwa haya ewe Maryamu, yanakuwajibikia wewe umshukuru Mola wako Mlezi. Basi jilazimishe ut'iifu kwake, na uwe mwenye kushika Sala, na shirikiana na wengine wanao muabudu Mwenyezi Mungu na wanasali kwa ajili yake.
44. Haya unayo simuliwa wewe Muhammad na Qur'ani ni katika khabari tukufu za wale alio wateuwa Mwenyezi Mungu, nazo ni khabari za ghaibu ambazo Mwenyezi Mungu anakufunulia. Na wala wewe hukuwapo wakati walipo kuwa wakipiga kura kwa mishale, ili waweze kukata shauri juu ya Maryamu. Na wala wewe hukuwapo walipo gombana kuwania nani wa kupata cheo hicho kitukufu.
45. Kumbuka na utaje ewe Nabii, pale Malaika walipo mbashiria Maryamu kuwa atamzaa mwana kwa neno lake tu Mwenyezi Mungu kinyume na ada wanavyo zaliwa watu. Jina lake mwana huyo ni Masihi Isa bin Maryamu. Na Mwenyezi Mungu amemjaalia hapa duniani kuwa atakuwa na cheo kwa unabii wake na kuepukana na aibu zote, na kesho Akhera kuwa atakuwa na cheo cha juu pamoja na kundi la walio takasika, wakawa wenye kuwa karibu mno na Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii walio imara baraabara.
46. Na Mwenyezi Mungu alimjaalia Nabii Isa na uwezo wa kusema na watu na ilhali yungali mtoto maneno ya kufahamika yenye hikima, kama alivyo sema nao utuuzimani mwake, bila ya tafauti katika hali hizo mbili. Na akawa katika miongoni walio jaaliwa kuwa ni watu wema.
47. Maryamu alisema kwa kustaajabu kupata mwana kwa njia isiyo ya kawaida: Vipi nitapata mwana na ilhali hapana mwanamume aliyenigusa? (yaani aliye lala nami). Mwenyezi Mungu Mtukufu akakumbusha kuwa Yeye huumba atakacho kwa kudra yake bila ya shuruti za sababu zilizo zowewa. Kwani Yeye akitaka jambo hulileta tu kwa taathira ya uwezo wake katika atakalo bila ya kutafuta kinginecho cha kutimiza matakwa yake.
48. Na Mwenyezi Mungu atamfunza mtoto huyu aliye zaliwa kuandika, na ilimu njema yenye manufaa, na Taurati, Kitabu cha Musa a.s., na Injili atayo mfunulia yeye.
49. Na atamtuma awe Mtume wake kwa Wana wa Israili, (Katika Injili ya Mathayo 15.24 Yesu anasema: Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.- Tazama pia Mathayo 10.5-6 na Mathayo 19.28 na Yohana 17.9) mwenye kutumia hoja za ukweli wa Utume wake kwa miujiza kutokana na Mwenyezi Mungu. Miujiza yenyewe ni kama kufanya kwa udongo Sura ya ndege, kisha akipulizia vitaingia uhai na kutaharaki mithili ya ndege kwa atakavyo Mwenyezi Mungu. Pia ataponyesha, kwa kudra ya Mwenyezi Mungu, walio zaliwa vipofu na wataona, na wenye maradhi ya ukoma waondokewe na ukoma, na walio onekana wamekwisha kufa wafufuke. Na yote hayo ni kwa idhini na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Pia atawatajia wanacho weka akiba majumbani mwao, vyakula na vyenginevyo. Naye Nabii Isa awaambie: Ishara zote hizi Mwenyezi Mungu amezionyesha kwangu ili iwe hoja kuwa Utume wangu ni wa haki, ikiwa nyinyi ni katika watu wanao t'ii na kusadiki.(Katika Injili ya Yohana 5.30 Yesu anasema: Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe.)
50. Na mimi nimetumwa kwenu nisadikishe sharia ya Taurati aliyo teremshiwa Musa, na nikuhalalishieni, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, baadhi ya mliyo harimishiwa zamani. Na mimi nimekuja na ishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuthibitisha ukweli wa ujumbe wangu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi.(Katika Injili ya Mathayo 5.17 Yesu anasema: Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua torati au manabii, la, sikuja kutangua, bali kutimiza.)
51. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ametumiminia mimi na nyinyi kila namna ya wema, amenilea mimi na nyinyi, ni Mola Mlezi wenu na wangu mimi. Basi muabuduni Yeye tu. Na hii ndio njia isiyo kwenda ovyo.
52. Basi alipo kuja Isa a.s. akawaita watu wake wafuate Njia Iliyo Nyooka, wengi wao walikataa. Alipo yajua hayo aliwaelekea na kuwaambia: Ni nani atakaye nisaidia katika kazi hii niifanyayo ya kuitia kwenye Haki? Wakamjibu baadhi ya Waumini wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na yeye: Sisi tunakuunga mkono, na tutakusaidia, kwa sababu wewe ni Mwitaji, unaita watu wende kwa Mwenyezi Mungu. Na shuhudia kuwa sisi tumemsafia Mwenyezi Mungu na ni wenye kufuata amri zake.
53. Na sisi tunasema: Ewe Mola Mlezi wetu! Tumekisadiki Kitabu chako ulicho mteremshia Nabii wako, na tunaifuata amri ya Mtume wako, Isa a.s. Basi tuthibitishe kuwa miongoni mwa wenye kumshuhudia Mtume wako katika kufikisha ujumbe, na kuwashuhudia Wana wa Israili katika ukafiri wao na upinzani wao.
54. Ama hao makafiri wapinzani walipanga njama za chini kwa chini kuupiga vita wito (Da'wa) wa Isa. Mwenyezi Mungu alizibat'ilisha njama zao, wasifanikiwe kuyapata waliyo yakusudia. Na Mwenyezi Mungu kwa hikima yake anawashinda watu wote wafanyao hila.
55. Taja ewe Nabii, pale Mwenyezi Mungu alipo sema: Ewe Isa Mimi nitakutimizia ajali yako,(yaani nitakufisha kifo cha kawaida kama alivyo sema Ibn Abbas r.a. Taz. Ibn Kathir) wala sitamwezesha mtu yeyote kukuuwa. Nami nitakunyanyua pahala pa utukufu wangu, na nitakuepusha na maadui wako wanao kusudia kukuuwa, na nitawafanya wanao kufuata wasio kengeuka na dini yako, wawe na nguvu na utawala juu ya wale wasio fuata uwongofu wako, mpaka Siku ya Kiyama. Kisha marejeo yenu ni Akhera. Hapo nitawahukumu katika hayo mlio kuwa mkizozana kwayo katika mambo ya dini.
56. Ama wale wanao kataa kwa ukafiri nitawaonjesha adhabu ya hizaya na mateso kwa kuwasalitisha mataifa mengine juu yao katika dunia, na hakika adhabu ya Akhera ni kali zaidi na ina hizaya zaidi. Na wala hawana wa kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
57. Na ama walio ongoka kwa uwongofu wa Mwenyezi Mungu, wakatenda vitendo vya kufuata mwendo wa kheri, Mwenyezi Mungu atawapa malipo ya kutosha kwa hizo a'mali zao. Na ndiyo shani yake Mwenyezi Mungu kuwa hawalipi thawabu zake wale wanao pindukia mipaka ya Mwenyezi Mungu wakafanya jeuri ya kutoitikia wito wake na kumtendea wema. Wala hawanyanyulii cheo chao.
58. Hayo tuliyo kusimulia ni miongoni ya hoja zenye kuonyesha ukweli wa ujumbe wako, nayo ni katika Qur'ani Tukufu yenye kukumbusha, na yenye kukusanya ilimu ya manufaa.
59. Baadhi ya watu wamepotea katika kadhiya ya Isa, wakadai ati kuwa yeye ni Mwana wa Mwenyezi Mungu kwa kuwa kazaliwa bila ya baba. Mwenyezi Mungu anawaambia: Hakika shani ya Isa katika kuumbwa kwake bila ya baba ni kama shani ya Adam alivyo umbwa kwa udongo bila ya baba wala mama. Mwenyezi Mungu alimfanya na akataka awe, akawa mtu sawasawa.
60. Bayana hii katika kuumbwa Isa ndiyo ukweli wenyewe ambao unabainisha hakika yaliyo tokea katika khabari za Mola Mlezi wa viumbe vyote. Basi wewe dumu katika yakini yako wala usiwe katika wenye kutia shaka.
61. Basi wenye kujadiliana nawe, ewe Nabii, katika shani ya Isa baada ya kukujia wewe khabari iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu na ambayo haina ubabaifu ndani yake, basi waambie kauli itakayo dhihirisha ujuzi wako wa yakini na upotovu wao wa uwongo: Njooni! Kila mmoja wetu na wenu awaite watoto wake, na wakeze na wenyewe nafsi zao. Kisha tumnyenyekee Mwenyezi Mungu kumtaka ateremshe ghadhabu yake na nakama yake juu ya aliye mwongo katika hili jambo la Isa kuzaliwa bila ya baba na kuwa yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu wala si Mwana wa Mungu.
62. Hiyo ndiyo kweli isiyo na shaka yoyote. Kwani hapanapo mungu ila Mwenyezi Mungu aliye umba kila kitu, na Yeye ni pekee katika utukufu wa Ufalme wake na hikima katika uumbaji wake.
63. Wakiikataa Haki baada ya kwisha wadhihirikia, na wasiache upotovu wao, basi hao ndio waharibifu. Na Mwenyezi Mungu anawajua.
64. Sema, ewe Nabii! Enyi Watu wa Kitabu! (Biblia, yaani Mayahudi na Wakristo) njooni kwenye neno moja la uadilifu lenye kutukusanya sote na tunalo litaja, nalo ni kuwa hatumuabudu ila Mwenyezi Mungu tu, wala tusimwekee washirika katika ibada. Na wala tusiwe tunawat'ii baadhi yetu tukiwafuata katika kuhalalisha na kuharimisha, tukaachilia mbali hukumu ya Mwenyezi Mungu katika mambo ya halali na haramu. Wakiukataa wito huu wa haki waambie: Shuhudieni kuwa sisi ni Waislamu, yaani tunafuata hukumu za Mwenyezi Mungu, na Yeye tu tumemsafia Dini, wala hatumwombi mwengineyo. (Taurati:Kutoka 20.3:Usiwe na miungu mingine ila Mimi. Injili ya Marko 12.29 : Yesu akamjibu, [amri] Ya kwanza ndiyo hii, Sikia Israel, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja.)
65. Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnazozana na kujadiliana kwa mambo ya Ibrahim, kila mmoja wenu akidai kuwa yeye ndiye anaishika dini yake, na ilhali Ibrahim alikuwako kabla ya Taurati na Injili akifuata sharia mbali. Hizo Taurati na Injili hazikuja ila baadae. Basi atakuwaje yeye afuate sharia za vitabu hivyo? Hamna akili ya kutambua jambo hili lilio wazi?
66. Watu nyinyi mlikuwa mkijadili mambo yalio wakhusu Musa na Isa mnayo yajua kama mnavyo dai wenyewe. Imekuwaje basi hivi sasa kudai kuwa Ibrahim alikuwa Yahudi au Mkristo - jambo ambalo nyinyi hamlijui! Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujua hakika ya hayo mnayo gombania, na nyinyi hamjui kitu.
67. Hakika Ibrahim a.s. hakufuata dini ya Kiyahudi wala dini ya Kikristo, lakini ameachana na dini zote za upotovu na akashika Dini ya Haki, ya Uislamu, yaani kumwelekea Mwenyezi Mungu, na kumtakasia Yeye kwa ut'iifu, na wala hakuwa miongoni wa hao wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu katika kuabudu.
68. Hakika wenye haki kabisa kunasibiana na Ibrahim na Dini yake ni wale walio mwitikia wito wake na wakaongoka kufuata uwongofu wake katika zama zake, na vile vile Muhammad s.a.w. na walioamini pamoja naye. Kwani hao ni watu wa Tawhidi safi ya kweli, kumwamini Mwenyezi Mungu mmoja bila ya walakini. Hiyo ndiyo Dini ya Ibrahim. Mwenyezi Mungu anawapenda Waumini, na Yeye atawanusuru, kwani wao ni vipenzi vyake, na atawalipa kwa mema na ziada.
69. Kipo kikundi katika Watu wa Kitabu wanao tamani kuwapotoa Waumini na kuwafitini waache Dini yao, kwa kuwatilia mikorogo ya kudhoofisha itikadi. Lakini katika kazi yao hii hawatampotoa mtu ila nafsi zao wenyewe kwa kuendelea katika upotovu, ambao utakuja kuwagubika wao wenyewe tu, na wala hawajui kuwa matokeo ya juhudi yao ovu yatawapata wenyewe, wala hayatawadhuru Waumini.
70. Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnakanusha Aya na Ishara za Mwenyezi Mungu zilizo teremka kuthibitisha Unabii wa Muhammad, s.a.w. na hali nyinyi mnaijua haki?
71. Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mkachukua Haki waliyo kuja nayo Manabii, na ikateremshiwa Vitabu, mkaichanganya na mambo ya udanganyifu ya kubuni na mkaleta tafsiri potovu, na msieneze Haki safi iliyo wazi isiyo kuwa na mchanganyiko? Na nyinyi mwajua vyema kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kitendo kama hichi ni kubwa.
72. Katika mtindo wao wa kutaka kuwapotoa Waumini, hawa Watu wa Kitabu wakiwaambia wenzao: Jitieni kuiamini Qur'ani aliyo teremshiwa Muhammad asubuhi, na ikifika jioni ikataeni. Huenda kwa hivyo mkawafitini hawa kwa kuwaingiza shaka katika nyoyo zao, wakaiacha dini yao.
73. Aidha wao husema: Msiwakubalie ila aliye fuata dini yenu, asije yeyote kati yao akadai kuwa nao wamepewa kama mlio pewa nyinyi, au akachukulia hoja mbele ya Mola wenu Mlezi kwa kuwakubalia kwenu. Ewe Nabii! Waambie: Hakika uwongofu wote unateremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye anaye mmiminia na kumteua amtakaye. Na ewe Nabii! Waambie: Hakika fadhila ziko kwa Mwenyezi Mungu humpa amtakaye katika waja wake, na Yeye ni Mkunjufu wa fadhila, Mjuzi wa anaye stahiki hayo na anaye teremkiwa na hayo.
74. Yeye Mwenyezi Mungu humpa amtakaye Unabii na Utume, na anaye mkhusisha kwa kumpa hayo ni katika fadhila yake tu. Na Mwenyezi Mungu ana fadhila kubwa kubwa kabisa, na wala hapana anaye muingilia yeyote, wala hapana anaye mzuia katika kutoa kwake.
75. Huo ndio mwendo wao Watu wa Biblia katika itikadi, ama mwendo wao katika mambo ya mali utaona: Kati yao kuna ambaye ukimpa amana ya chungu ya dhahabu au fedha atakurejeshea sawa sawa bila ya kupunguka chochote. Na mwengine kati yao ukimpa amana ya dinari moja tu hakurudushii, ila ikiwa utamshikilia mpaka aitoe. Haya ni kwa sababu wapo baadhi yao wanawaona watu wa mataifa mengine, si watu wa Biblia basi haiwalazimu wao kuwatendea haki, na wanadai kuwa hiyo ni hukumu ya Mwenyezi Mungu. Na wao wanajua vyema kuwa hayo ni kumzulia uwongo Mwenyezi Mungu. (Tazama katika Agano la Kale: Kumbukumbu la Torati, 23.19-20 inaruhusu kumnyonya riba mtu mbali asiyekuwa Yahudi. Kumbukumbu 12.21 inaruhusu kumlisha nyamafu mgeni na kumuuzia pia. Uzushi kama huu unakashifiwa na Aya 78 ifuatayo kuwa haya hayakutokana na Mwenyezi Mungu, bali wamepachika wao tu katika vitabu vyao.)
76. Hakika ni kweli wamemzulia uwongo Mwenyezi Mungu. Kwani mwenye kumrejeshea mwenyewe haki yake na akamtimizia kwa wakati wake kama alivyo ahidi, na akamwogopa Mwenyezi Mungu, wala asipunguze kitu wala asiakhirishe, huyo basi atapata mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa sababu amemcha Yeye.
77. Wanao iacha ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo fungamana nao ya kuwa watazitimiza haki na watasimamia yaliyo waajibu, wala hawatoacha viapo vyao walivyo apa kuwa watatimiza - kwa thamani ndogo ya faida ya dunia, na ingawa kuu katika maoni yao, hao hawatakuwa na sehemu yoyote katika raha za Akhera. Mola wao Mlezi atawapuuza, wala hatowaangalia kwa jicho la rehema Siku ya Kiyama, wala hatowafutia dhambi zao, na watapata adhabu chungu ya kuendelea.
78. Katika Watu wa Kitabu wapo ambao huzipindua ndimi zao kutamka maneno yasiyo kuwamo katika Kitabu kwa lafdhi ya Kitabu, watu wadhanie kuwa ni maneno yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu, na wala hayamo katika ufunuo wa Mwenyezi Mungu. Wanamzulia Mwenyezi Mungu nao ndani ya nafsi zao wanajua kuwa wanasema uwongo.
79. Si akili wala haimfalii mwanaadamu aliye teremshiwa Kitabu na Mwenyezi Mungu na akapewa ilimu ya manufaa na kuweza kuzungumza mambo yanayo tokana na Mwenyezi Mungu, tena awatake watu wamuabudu yeye badala ya kumuabudu Mwenyezi Mungu. Lakini linalo ingia akilini, na lifaalo, ni kuwa yeye awatake watu wamsafie ibada Mola wao Mlezi aliye waumba kwa mujibu alivyo wafunza kutokana na ilimu ya Kitabu na kwa mujibu ya wanayo soma.
80. Wala hayumkini akuamrisheni kuwafanya Malaika au Manabii kuwa ndio miungu badala ya Mwenyezi Mungu. Ni ukafiri usio ingia akilini kukuamrisheni hayo baada ya kuwa mmekwisha kuwa Waislamu mlio muelekezea nyuso Mwenyezi Mungu. (Nabii Isa a.s. hakujidaia Ungu hata katika Injili hizi zilizo korogwa, wala hakumfanya Roho Mtakatifu, ambaye ni Malaika, kuwa ni Mungu.)
81. Ewe Nabii! Watajie kuwa Mwenyezi Mungu aliahidiana na akaagana na kila Nabii aliye teremshiwa Kitabu na akapewa ilimu ya manufaa, ya kwamba akija Mtume ambaye wito wake unakubaliana na wito wao basi ni waajibu wao wamuamini na wamsaidie. Na Manabii wote walikiri kuitimiza ahadi hiyo, na wakakiri na wakashuhudia kwa nafsi zao, na Mwenyezi Mungu akawashuhudia hayo. Tena wao wakayafikisha hayo kwa kaumu zao. Ahadi hiyo imewapasia wao imani na wamnusuru wakimwahi. Kama hawakumwahi basi ni waajibu wa kaumu zao wamuamini na wamnusuru kwa kutimiza na kufuata yaliyo walazimu Manabii wao.(Tazama katika Biblia: Kumbukumbu 18.17-19, Injili ya Yohana 16.7-14)
82. Anaye kataa kumuamini Nabii huyu baada ya ahadi hii madhubuti ni mpotovu aliye toka kwenye sharia ya Mwenyezi Mungu, ni kafiri mwenye kuwakataa Manabii wote wa mwanzo mpaka wa mwisho.
83. Je, wanataka dini isiyo kuwa Dini ya Muhammad, na hiyo ndiyo Dini ya Manabii wote? Dini hii ndiyo pekee Dini ya Mwenyezi Mungu anaye nyenyekewa na kila kilichomo mbinguni na duniani kwa ut'iifu, kwa kupenda na khiari, au kwa lazima kwa kufuata tabia na maumbile. Na kwake Yeye ndio viumbe vyote vinarejea.
84. Mwenyezi Mungu ametilia mkazo kuwa Yeye ni Mmoja, na Ujumbe wake ni mmoja. Amemuamrisha Nabii wake na walio pamoja naye wasema: Tumesadiki kuwa Mwenyezi Mungu ndiye peke yake anaye faa kuabudiwa, na ndiye anaye watuma Mitume wake. Na tumeiamini Qur'ani na Sharia aliyo tuteremshia Mwenyezi Mungu, na pia tumeamini Vitabu na Sharia alizo wateremshia Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na watoto wao thinaashara, na aliyo teremsha Mwenyezi Mungu kwa Musa, nayo ni Taurati, na kwa Isa, nayo ni Injili, na walio teremshiwa Manabii wote walio baki. Hapana khitilafu katika kuamini baina ya yeyote katika wao. Na sisi kwa hivyo tumeuelekeza uso wetu kwa Mwenyezi Mungu.
85. Baada ya kupata utume Muhammad s.a.w. akitaka mtu dini na sharia zisio kuwa Dini ya Islamu na Sharia yake, Mwenyezi Mungu hatamkubalia. Na malipo ya mtu huyo Siku ya Malipo ni kuwa miongoni mwa walio zikhasiri nafsi zao, ikawajibikia adhabu chungu.
86. Mwenyezi Mungu hakubaliani na watu walio kwisha shuhudia kuwa Mtume ni wa haki, na zikawajia dalili za kuonyesha hayo, kisha baada ya yote hayo wakamkataa, na wakakataa miujiza yake. Huo basi ni udhaalimu wao, na Mwenyezi Mungu hakubaliani na madhaalimu.
87. Adhabu ya watu hao wataipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama wanavyo stahiki kukasirika kwake juu yao, na laana yake, na laana ya bora ya viumbe vyake miongoni mwa Malaika na wanaadamu.
88. Laana hiyo haitowabanduka, wala hawatapunguziwa adhabu, wala hawapewi muhula.
89. Lakini wale ambao wamejing'oa na madhambi yao, wakaingia kati ya watu wema, wakayaondoa waliyo yaharibu, basi hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu atawafutia madhambi yao, kwani maghfira na rehema ni miongoni mwa sifa za dhati yake Tukufu.
90. Kukubaliwa toba na kupata rehema ya maghfira kunashurutishwa mtu adumu juu ya Imani. Wanao ipinga Haki baada ya ut'iifu na kusadiki, na wakazidisha upinzani na ufisadi na kuwaudhi Waumini, Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la hatokubali toba yao. Haiwezi kuwa toba yao hiyo ni kweli na safi na hali wanaendelea na vitendo vyao, wapo mbali na Haki na wanaigeuzia nyuso zao.
91. Wale wanao ipinga Haki wala hawaifuati, na wanaendelea na uwovu wao mpaka wakafa nao ni wapinzani tu, basi yeyote miongoni mwao hawezi kujitolea fidia ya kujiepusha na adhabu ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, hata ikawa anacho kitoa kuwa fidia ni dhahabu ya kujaza dunia nzima kama angeweza. Na adhabu yao ina uchungu mkali.
92. Enyi Waumini! Hamtoipata kheri kaamili mnayo itaka na itakayo mridhisha Mwenyezi Mungu ila mkitoa katika vitu mnavyo vipenda na mkatoa katika Sabili Llahi, Njia ya Mwenyezi Mungu, kwa namna mbali mbali. Na chochote mnacho kitoa, kidogo na kikubwa, kilio bora au chenginecho, Mwenyezi Mungu anakijua. Kwani Yeye ni Mwenye Kujua, hapana kitu kilioko mbinguni au duniani kinacho fichikana naye.
93. Mayahudi waliwatoa kombo Waislamu kwa kuhalalisha baadhi ya vyakula kama nyama ya ngamia na maziwa yake. Wakadai kuwa hayo yaliharimishwa na sharia ya Ibrahim. Mwenyezi Mungu Subhanahu aliwarudi madai yao hayo kwa kubainisha kuwa vyakula vyote vilikuwa halali kwa Wana wa Yaakub (ndiye Israil) kabla ya kuteremka Taurati, ila alicho jizuia Yaakub mwenyewe kwa sababu zilizo mkhusu yeye tu, basi na wao wakijiharimishia nafsi zao. Mwenyezi Mungu akamuamrisha Nabii wake awatake walete uthibitisho wa Taurati kuwa sharia ya Ibrahim imeharimisha hayo kama wao wanasema kweli. Wakashindwa, wakanywea.
94. Ilipo thibiti kuwa wameemewa basi wenye kumsingizia uwongo Mwenyezi Mungu baada ya hoja hizo, hao ndio walio selelea na udhaalimu wao, na wanastahiki kuitwa Madhaalimu.
95. Baada ya kushindwa kwao Mwenyezi Mungu amemuamrisha Nabii wake awabainishie kuwa ukweli wa Mwenyezi Mungu umethibiti katika ayasemayo. Basi ifuateni Sharia ya Ibrahim anayo kutakeni muifuate, na nyinyi mnaikanusha. Hii ni mbali kabisa na hizo dini za uwongo, kwani Ibrahim hakuwa miongoni mwa washirikina.
96. Katika kufuata mila ya Ibrahim ni kuelekea wakati wa Sala Nyumba aliyo ijenga, na kwenda kuhiji huko. Mwenyezi Mungu amebainisha hayo kwa kusema: Hakika Nyumba ya awali kwa ukongwe na utukufu aliyo ijaalia Mwenyezi Mungu iwe ni ya ibada kwa watu ni hiyo iliyoko Makka (au Bakka kama pia inavyoitwa). Nayo ina kheri nyingi na manufaa, na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la ameijaalia iwe na baraka. Nayo Nyumba hiyo ni pahali pa uwongofu kwa watu kwa kuhiji na kuelekea wakati wa Sala.
97. Zipo dalili wazi za kuonyesha utakatifu wake huo Msikiti wa Makka na kuzidi fadhila zake. Miongoni mwa hizo ni hapo alipo kuwa akisimama Nabii Ibrahim a.s. kwa kusali. Na pia kuwa anaye ingia humo huwa amesalimika halimpati ovu. Na kuhiji Makka ni waajibu wa kila mtu awezae kwenda. Na mwenye kukataa, akaiasi amri ya Mwenyezi Mungu, na akaipinga Dini yake, basi khasara itamuangukia mwenyewe, na Mwenyezi Mungu anajitosha, hawahitajii watu wote.
98. Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la amemuamrisha Mtume wake awahizi Watu wa Kitabu kwa kuendelea kwao kukufuru na kupotoka na kupotosha, akasema: Enyi Watu wa Kitabu! Huo ukafiri wenu hauna Sura wala maana. Kwa sababu gani mnakanusha dalili, na hoja za Mwenyezi Mungu zenye kuthibitisha Unabii na Ukweli wa Muhammad? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvijua vitendo vyenu na atakulipeni malipo yake.
99. Enyi Watu wa Kitabu! Vipi mnajaribu kumgeuza mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kuifuata Haki aache Njia Iliyo Nyooka ya Mwenyezi Mungu wa Kweli, na mnajaribu kuikosoa Njia hiyo, na nyinyi mnajua kuwa hiyo ndiyo Haki? Wala Mwenyezi Mungu hakughafilika na vitendo vyenu, naye atakulipeni kwavyo.
100. Mwenyezi Mungu anawahadharisha Waumini na vitimbi vya baadhi ya Watu wa Kitabu,(Mayahudi na Wakristo), vya uchochezi wao wa udanganyifu kwa kusema: Mkiwat'ii baadhi ya Watu wa Kitabu katika yale wanayo yaeneza ya kutilisha shaka katika Dini yenu, itakuwa mnarajea tena kwenye upotovu baada ya uwongofu, na wakurejezeni muwe makafiri baada ya kuwa ni Waumini.
101. Hebu izangitieni hali yenu ya ajabu, kuwa mnapotoka na mnakufuru baada ya Imani, na hali mnasomewa Qur'ani, na Mtume mnaye, anakubainishieni na anakukingeni na upotovu katika Dini yenu. Na mwenye kumkimbilia Mola wake Mlezi, na akashikamana na Dini yake, basi huyo amefanya vyema. Mola wake Mlezi amemwongoa kwenye Njia ya kufuzu na kufaulu.
102. Hakika mlango wa shari uwazi ikiwa hamumchi Mwenyezi Mungu. Basi enyi mlio amini! Mkhofuni Mwenyezi Mungu kwa khofu inayopasa, kwa kutenda anayo amrisha, na kuyaepuka anayo yakataza. Na dumuni juu ya Uislamu mpaka mtakapo kutana na Mwenyezi Mungu.
103. Nyote nyinyi shikamaneni na Dini ya Mwenyezi Mungu, wala msifanye jambo litalo leta mfarakano baina yenu. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlivyo kuwa wakati wa ujahili nyinyi kwa nyinyi maadui. Mwenyezi Mungu akaziunganisha nyoyo zenu kwa Uislamu, mkawa mnapendana, na ilhali kwa sababu ya ukafiri wenu na kufarikiana kwenu mlikuwa juu ya ukingo wa Moto, akakuokoeni kwa Uislamu. Kwa mfano wa bayana kama hii ya pekee Mwenyezi Mungu anakubainishieni daima njia za kheri, ili mdumu katika uwongofu.
104. Hakika njia ya kuungana kuliko kamilika juu ya Haki katika kivuli cha Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kivuli cha Mtume wake, ni kuwa muwe nyinyi Umma unao lingania (unao itia) watu waje wafuate mwendo utao waletea maslaha ya Dini na dunia, uamrishe ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu, ukataze maasia. Na hapo ndipo mtakuwa mlio fuzu, kufuzu kulio kamilika.
105. Wala msiwe kwa kupuuza kwenu kuamrisha mema na kukataza maovu--mambo ambayo ndiyo yanayo kukusanyeni katika kheri na Dini ya Haki--kama wale walio puuza kuamrisha mema na kukataza maovu,wakagawika mapande mbali mbali, wakakhitalifiana katika dini yao baada ya kuwafikilia hoja zilizo wazi, zenye kubainisha Haki. Na hao walio farikiana wakakhitalifiana, watapata adhabu kuu.
106. Adhabu kuu hiyo itakuwa Siku zitapo nawiri nyuso za Waumini kwa furaha, na kusawijika kwa masikitiko na huzuni nyuso za makafiri. Wataambiwa kwa kuwatahayarisha: Je, mmekufuru baada ya kuwa mlikulia juu ya Imani na ut'iifu wa haki, na mkaletewa hoja zilizo wazi? Basi onjeni adhabu kwa sababu ya ukafiri wenu!
107. Ama wale nyuso zao zimekuwa nyeupe, yaani zimenawiri, kwa kufurahi, hao watakuwa katika Pepo ambayo Mwenyezi Mungu amewapa kwa rehema yake, wadumu humo milele.
108. Na hizo Aya zilizo kuja za kueleza kuwa mwema na mwovu watalipwa tunakusomea, nazo zimekusanya haki na uadilifu. Na Mwenyezi Mungu hataki kumdhulumu yeyote kati ya watu na majini.
109. Na vyote viliomo mbinguni na ardhini ni vya Mwenyezi Mungu peke yake, ni vyake kwa kuviumba, na kuvimiliki, na kuvisarifu. Na marejeo ya mambo yao ni kwake Yeye. Kwa hivyo humlipa kila mmoja kama anavyo stahiki.
110. Nyinyi Umma wa Muhammad ni bora ya umati alio umba Mwenyezi Mungu kwa manufaa ya watu, maadamu mtaamrisha ut'iifu na mtakataza maasi, na mtakuwa ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu kwa Imani safi na ya kweli. Na lau kuwa Watu wa Kitabu wangeli kuwa ni wakweli katika imani yao kama nyinyi, basi ingeli kuwa ni bora kwao kuliko walivyo. Walakini baadhi yao ni Waumini, na wengi wao wameikiuka mipaka ya Imani na yanayo pasa.
111. Hao wapotovu hawawezi kukudhuruni nyinyi kama walivyo kuandalieni, wala hawakuathirini. Ijapo kuwa mtapata maudhi kwao, lakini athari yake haiselelei. Na hata wakipigana nanyi wataingia kiwewe wakimbie wasipambane nanyi, na hapo mwishoe hawatopata ushindi juu yenu maadamu nyinyi mtashikamana na kuamrisha mema na kukataza maovu.
112. Na Mwenyewe Subhana ameeleza kuwa lazima watapata madhila popote watapo kutikana, ila wakifungamana kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu na ahadi ya Waislamu. Na wao wamestahiki wapate ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na pia Mwenyezi Mungu amewajaalia lazima uwafikie unyonge na unyenyekevu kwa wengineo. Na hayo ni kwa sababu ya kukataa kwao Ishara zote za Mwenyezi Mungu zinazo onyesha Unabii wa Muhammad s.a.w. na vile kuridhi kwao hapo zamani kuuliwa Manabii ambako hakuwezi kuwa ni kwa haki, bali ni kwa uasi wao na uadui wao.
113. Watu wa Kitabu si wote sawa sawa. Miongoni mwao wapo walio simama msimamo mwema, wa uadilifu, wanakisoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu nyakati za usiku wakisali.
114. Wanaamini kweli kuwepo Mwenyezi Mungu, na kuwa Yeye ni Mmoja tu. Wanaamini Mitume wote, hawamuabudu ila Mwenyezi Mungu. Na wanaamini kuwa itafika Siku ya Kiyama; wanaamrisha ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu, na wanakataza maasi, na wanawania kutenda mambo ya kheri. Hawa kwa Mwenyezi Mungu huhisabiwa miongoni mwa watenda wema.
115. Kheri yoyote wanayo ifanya watu hao hawatonyimwa thawabu zake. Na Mwenyezi Mungu amezizunguka kwa kuzijua na kuziweza hali zao na malipo yao.
116. Wale walio kufuru, mali yao na wangayatoa kuwa ni fidia hayatowafaa kitu, wala watoto wao na wangawataka msaada hawatoweza kuwasaidia hata chembe kuwakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu katika Akhera. Na hawa ndio walio lazimika kuingia Motoni na waselelee humo.
117. Hakika hali ya wanacho kitoa makafiri duniani kuwa ni sadaka au cha kuwakaribisha mbele ya Mwenyezi Mungu Akhera mfano wake, kwa kuwa ni kazi bure katika ujira wa vitendo, ni kama hali ya shamba la watu walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na maasi. Shamba hilo likakumbwa na upepo wenye baridi kali ya barafu, likateketea shamba lote kuwa ni malipo yao. Wala Mwenyezi Mungu siye aliye wadhulumu ujira wa kazi yao, lakini ni wao wenyewe ndio walio jidhulumu nafsi zao kwa kufanya yaliyo sabibisha hayo. Nayo ni kuzipinga dalili na ushahidi wa Imani na kumkufuru Mwenyezi Mungu.
118. Enyi mlio amini! Msitafute kuwafanya marafiki wa ndani watu wasio wa Dini yenu mkatumai msaada kwao, na mkawa mkiwapa siri zenu. Hao hawatoacha kuyafisidi mambo yenu, kwani wao wanapenda mno kukutieni taabuni na kukudhuruni kwa madhara makubwa. Zimekwisha dhihiri ishara za bughdha yao kukuchukieni nyinyi katika kuropokwa ndimi zao. Na yaliyo ficha nyoyo zao ni makubwa zaidi. Tumekwisha kuonyesheni alama za kumtambua rafiki na adui kama nyinyi ni watu wa akili na utambuzi wa kweli.
119. Enyi nyinyi Waumini! Mnawapenda hawa makafiri na wanaafiki kwa ajili ya ujamaa, au urafiki au mapenzi tu. Na wao, lakini, hawakupendeni kwa sababu ya kuing'ang'anilia dini yao. Na nyinyi mnaamini Vitabu vyote vilivyo teremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanapo kutana nanyi hujitia imani ili kukudanganyeni. Na wakisha kuacheni huziuma ncha za vidole vyao kwa chuki na kukasirika. Ewe Nabii! Waambie: Endeleeni na hiyo chuki yenu mpaka mfe! Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyajua yanayo fichikana vifuani, na atakulipeni kwavyo.
120. Nyinyi mkipata neema, kama vile kushinda vitani na ngawira, wao husikitika. Mkipata msiba kama ukame na kushindwa, wao hufurahia msiba wenu. Lakini nyinyi mkisubiri juu ya maudhi yao, na mkajizuilia na kule kuwafanya urafiki mliko katazwa, basi maudhi yao na uadui wao hautakudhuruni kitu. Kwani Yeye Aliye tukuka anavijua vyema vitimbi wanavyo vifanya, wala Yeye hashindwi kukulindeni nao.
121. Na hebu taja Ewe Nabii! Pale ulipo toka asubuhi mapema ukaacha ahali zako, watu wako wa nyumbani, ukenda mpaka Uhud kwa makusudi ya kuwaweka Waumini katika makao yao kwa ajili ya vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia kauli zenu, ni Mwenye kuzijua niya zenu.
122. Ilipo tokea kuwa vikundi viwili vya Waumini kuingiwa na khofu ya kushindwa na wakataka kurejea nyuma, Mwenyezi Mungu aliwalinda akawapa moyo wa kuthibiti, wakasonga mbele katika vita. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye utawala katika mambo yao mawili, na ndiye wa kuwalinda na kuwawezesha kwa kuwapa tawfiqi. Basi Waumini nawachukue funzo kutokana na haya, na wamtegemee Yeye ili awanusuru.
123. Mwenyezi Mungu amewakumbusha Waumini ile
neema ya nuSura aliyo wapa katika vita vya Badri (1) waliposubiri.
Akawahakikishia kuwa Yeye ndiye aliye wapa ushindi katika vita vile na
ingawa walikuwa wachache na wapungufu wa silaha; akawataka wamt'ii kuwa
ni shukrani kwa neema hiyo.
(1) Badri ipo mwendo wa kiasi ya maili 120 kusini magharibi ya Madina.
Mpambano hapo baina ya Waislamu na Makureshi ulikuwa siku ya Jumaane 17
Ramadhani mwaka wa pili wa Hijra (13 Machi 624 B.K.). Mtume s.a.w. na Masahaba
wake walitoka Madina taarikh 8-9 ya Ramadhani mwaka wa pili wa Hijra (5
Machi 624 B.K.) Idadi ya wapiganaji wa Kiislamu katika vita hivi ilikuwa
kiasi watu mia tatu au zaidi kidogo, na Washirikina walizidi mara tatu
kuliko hao. Mwenyezi Mungu alitimiza ahadi yake katika vita hivi, Waumini
wakashinda juu ya kuwa ni wachache, kwa kuwa Imani yao juu ya haki na uadilifu
ilikuwa kubwa. Na kuungwa mkono na Mwenyezi Mungu pamoja na kuwa na moyo
wenyewe kulikuwa ni sababu za ushindi kuliko wingi wa watu na ubora wa
silaha. Ushindi huu ulio dhaahiri ukawa ndio sababu ya kuenea Neno la Imani
na kutukuka likawa juu. Na hichi ni chanzo cha yaliyo kuja baadae, na kivuli
cha Uislamu kikatanda Arabuni kote, na kisha kwengineko ulimwenguni.
124. Ushindi ulipatikana Mtume alipo waambia Waumini: Haitatosha kukutulizeni nafsi zenu Mola wenu Mlezi akikusaidieni kwa Malaika elfu tatu watakao letwa ili kukutieni nguvu?
125. Ndio! Msaada huo unakutosheni. Na pindi mkivumilia vita, na mkashikilia uchamngu, na hata maadui zenu wakikutokeeni kwa ghafla, Mola wenu Mlezi atawaongeza hao Malaika mpaka wafike elfu tano ili kukupeni nguvu.
126. Na wala Mwenyezi Mungu hakujaalia huko kukuleteeni msaada wa Malaika ila iwe ni bishara tu kwenu ya ushindi, na zipate kutulia nyoyo zenu. Na hapana ushindi ila unao tokana na Mwenyezi Mungu Mwenye Kushinda wote, ambaye anapanga kila kitu kwa pahala pake, na anaye wapangia mambo waja wake Waumini.
127. Naye Mwenyezi Mungu amekupeni ushindi ili wateketee baadhi ya wale walio kufuru kwa kuuwawa, au wadhalilike na awakasirishe kwa kushindwa na aibu na hizaya, wapate kurejea nao wameemewa.
128. Huna lako katika ninayo wafanyia waja wangu, kwani mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Ama atawasamehe kwa Imani, au atawaadhibu kwa kuuwawa na hizaya na mateso ya Siku ya Kiyama, kwani hao ni madhaalimu.
129. Bila ya shaka vitu vyote vilioko katika mbingu na katika ardhi ni vya Mwenyezi Mungu peke yake, kwa kuviumba na kuvimiliki. Na Yeye ndiye Mwenye uwezo juu ya kila kitu, kila kitu kimo mikononi mwake. Yeye humsamehe ampendaye na akamuadhibu amtakaye. Lakini kusamehe kwake ndiko kulio karibu zaidi, na rehema yake ni ya kutarajiwa sana zaidi. Kwani Yeye hakika ni mwingi wa kusamehe na kurehemu.
130. Enyi mlio amini! Mkikopesha msichukue katika deni ila rasilmali yenu tu. Msifanye kuzidisha juu ya deni faida ya kuzidi mwaka kwa mwaka ikawa kuzidi juu kwa juu. Msiyale mali ya watu kwa upotovu. Hakika nyinyi mtaongokewa na mtafuzu pindi mkiepukana na riba, ikiwa ndogo au kubwa.
131. Tahadharini na Moto ulio andaliwa kwa ajili ya makafiri kwa kujiepusha kutafuta kuihalalisha riba.
132. Na mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume katika kila wanacho amrisha na kila wanacho kikataza ili mpate kurehemeka duniani na Akhera.
133. Na kuweni wa mbele katika kutenda mema ili mpate kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye kumiliki mambo yenu yote, maghfira makubwa ya kufutiwa dhambi zenu, na Pepo yenye wasaa, na upana wake ni kama upana wa mbingu zote na ardhi. Hayo wametengenezewa wale wanao mcha Mwenyezi Mungu na wakaiogopa adhabu yake.
134. Hao wachamngu ndio wale wanao toa mali yao kwa kumridhi Mwenyezi Mungu wanapo kuwa na neema na wasaa, na pia wanapo kuwa na shida na dhiki na uzito, na wanazuia ghadhabu zao wanapo kasirishwa wasiwaadhibu wale wanao wakosa, bali wanawasamehe walio watendea mabaya. Hao kwa haya huhisabiwa kuwa ndio watenda mema. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu huwalipa mema hao watenda mema na huwa radhi nao.
135. Watu hao nao pindi wakifanya makosa makubwa au dhambi ndogo tu, mara humkumbuka Mwenyezi Mungu na Utukufu wake, na adhabu zake na malipo yake mema, na rehema yake na ghadhabu zake. Tena hapo hujuta kwa waliyo tenda na wakaomba msamaha wake, na hapana anaye samehe madhambi ila Mwenyezi Mungu. Na hao wachamngu hawabaki kuendelea juu ya jambo baya na ilhali wanajua ubaya wake.
136. Basi hao wenye kusifika kwa sifa hizi ujira wao ni maghfira makubwa kutokana na Mola wao Mlezi, Mwenye kumiliki mambo yao yote, na Bustani zipitazo mito kati ya miti yake, na humo watadumu daima. Na hayo ni malipo ya neema kubwa ilioje kwa watendao amri za Mwenyezi Mungu.
137. Enyi Waumini, kabla yenu shani ya Mwenyezi Mungu imewapitia kaumu zilizo kadhibisha kwa mapuuza yao. Mwenyezi Mungu akawashika kwa madhambi yao. Basi zingatieni vipi yalikuwa matokeo ya vitendo vya walio kadhibisha.
138. Kwa kutajwa sifa za Waumini na kueleza shani ya Mwenyezi Mungu iliyo pita kwa walio kwisha tangulia lipo Bayana na Uwongozi kwa watu wafuate njia ya kheri, na kuwaachisha njia ya shari.
139. Wala nyinyi msilegelege mkadhoofika katika Jihadi Fi Sabili Llahi kwa yanayo kupateni, na wala msihuzunike kwa wanao uliwa miongoni mwenu, kwani nyinyi kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na Imani yenu na nguvu za Haki mnayo ipigania mko juu. Ushindi ni wenu ikiwa Imani yenu ni ya kweli, na maadamu mtadumu nayo.
140. Ingawa katika vita vya Uhud wameuwawa au kujuruhiwa vibaya baadhi yenu na kwa hayo mkaathirika nafsi zenu, lakini msilegee na kuhuzunika. Kwani hao makhasimu zenu yaliwapata kama hayo katika vita vya Badri. Nyakati za ushindi huendeshwa na Mwenyezi Mungu kwa watu kama apendavyo, pengine hawa hushinda, na pengine hawa, ili awatie mtihani na kuwajaribu Waumini, awateuwe wenye kusimama imara juu ya Imani yao, na apate kuwatukuza baadhi yao kwa kuwafisha mashahidi katika Sabili Llahi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi washirikina wenye kudhulumu na wangashinda kwa kusaidiwa na wengineo.
141. Kwa huku kushindwa kwa muda, Mwenyezi Mungu anawasafisha jamaa Waumini, na anawat'ahirisha kutokana na wale wenye nyoyo mbaya na imani dhaifu, na wenye kueneza moyo wa kushindwa na wasiwasi; na kwa hivyo ndio anaung'olea mbali ukafiri na makafiri wenyewe pia.
142. Enyi Waumini! Msidhani kuwa mtaingia Peponi bila ya kubainika kati yenu wepi Mujahidiina, Wapigania Haki, wenye kusubiri na kuvumilia ambao wanat'ahirishwa na misukusuko na shida.
143. Nyinyi mlikuwa mkitaka kufa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kabla hamjayaona mauti na mkajua kitisho chake. Sasa basi nyinyi mmekwisha yaona mauti walipo uliwa ndugu zenu mbele yenu nanyi mnaangalia.
144. Katika vita vya Badri ulitoka uvumi kuwa ati Mtume Muhammad s.a.w. kauwawa. Baadhi ya Waislamu walidahadari wakaingiwa kiwewe wakataka kurtadi, kuuacha Uislamu. Mwenyezi Mungu aliwakaripia kwa kuwaambia: Muhammad si chochote ila ni Mtume tu, na kabla yake wamekufa Mitume mfano wake yeye. Naye atakufa kama walivyo kufa wao, na atapita kama wao walivyo pita. Je, akifa au akauliwa ndio mtarejea nyuma kwenye ukafiri wenu? Na mwenye kurejea kwenye ukafiri baada ya kwisha amini, basi hatomdhuru kitu Mwenyezi Mungu, ila atakuwa anajidhuru nafsi yake kwa kujipeleka kwenye mateso. Na Mwenyezi Mungu atawalipa malipo mema wale wenye kusimama imara juu ya Uislamu, wenye kuishukuru neema yake.
145. Hayumkini mtu kufa ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Naye amekwisha viandikia viumbe ajali yao. Na atakaye starehe ya dunia Mwenyezi Mungu atampa, na atakaye malipo ya Akhera atayapata. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanao shukuru neema yake wakamt'ii kwa aliyo waamrisha ikiwa ni kupigana Jihadi au mengineyo.
146. Na Manabii wangapi wamepigana vita na pamoja nao Waumini wengi wenye ikhlasi kwa Mola wao Mlezi! Nyoyo zao hazikuingia woga, wala azma zao hazikudahadari, wala hawakuwanyenyekea maadui zao kwa sababu ya masaibu yaliyo wapata katika Sabili Llahi, Njia ya Mwenyezi Mungu. Haya ni kwa sababu wamo katika ut'iifu wake, na Mwenyezi Mungu huwalipa wanao vumilia ikiwafika balaa.
147. Na kauli yao vilipo kuwa vita vikali haikuwa ila kusema: Mola wetu Mlezi! Tusamehe dhambi zetu kubwa na ndogo. Na tusimamishe imara katika midani za vita, na utunusuru na hawa maadui wa Dini yako, wenye kukukanya Wewe na ujumbe wa Mtume wako.
148. Mwenyezi Mungu akawapa ushindi na tawfiqi katika dunia, na akawadhaminia malipo mema kwa Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwalipa wale wafanyao vitendo vyema.
149. Enyi mlio amini! Mkiwat'ii maadui zenu makafiri, walio tangaza ukafiri wao au wakauficha, kwa hayo wanayo kuitieni kwa maneno au vitendo, watakuja kugeuzeni muingie ukafirini. Na hapo tena itakuwa mmekhasiri dunia na Akhera.
150. Mwenyezi Mungu ndiye wa kukunusuruni, basi msiwaogope hao binaadamu wenzenu, kwani Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kunusuru.
151. Yasikutieni unyonge yaliyo kupateni siku ya Uhud. Sisi tutaingiza khofu na vitisho katika nyoyo za maadui zenu kwa kuwa wao wamemshirikisha Mwenyezi Mungu na miungu mengine ambayo Mwenyezi Mungu hakuwateremshia hoja yoyote. Kwani Miungu hiyo hainafiishi wala haidhurishi kitu. Na makao yao yatakuwa Motoni Akhera, na maovu mno hayo makao ya madhaalimu.
152. NuSura ya Mwenyezi Mungu ni jambo la hakika ya kweli. Mwenyezi Mungu ametimiza miadi yake kuwa alikupeni ushindi pale mara ya kwanza mlipo wauwa maadui wengi kwa radhi yake; mpaka yalipo dhoofika maoni yenu katika vita na mkakhitalifiana kuifahamu amri ya Nabii aliyo kupeni msiondoke kwenye vituo vyenu. Baadhi yenu mkaacha vituo vyenu mlipo ona mnashinda, na wengine wakabaki mpaka mwisho. Kikundi kimoja kikaasi amri ya Mtume kikenda kuwania ngawira baada ya kwisha kuonyeshwa mkipendacho, nao ni ushindi. Mkawa makundi mawili, wanao taka raha ya dunia, na wanao taka malipo ya Akhera. Ilivyo kuwa hivyo Mwenyezi Mungu akaondoa kwenu nuSura yake, mkashindwa, ili akujaribuni, atambulikane mwenye ikhlasi na asiye kuwa nayo. Lakini sasa amekusameheni kwa kuwa mmejuta. Na Mwenyezi Mungu ana fadhila kwenu kwa kukusameheni na kukubali toba yenu.
153. Enyi Waumini! Hebu ikumbukeni hali yenu wakati ule mlipo kuwa mkitoka mbio wala hamumsikii mtu kwa shida ya kukimbia; na Mtume anakuiteni nyuma yenu mrejee. Mwenyezi Mungu akakujazini huzuni ya kufudikiza kama wingu lilio funika nafsi zenu, ili msisikitike kwa ngawira mlizo zikosa wala kushindwa kuliko kusibuni. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema makusudio yenu na vitendo vyenu.
154. Kisha Mwenyezi Mungu baada ya dhiki akakupeni neema ya utulivu, ambao ulidhihiri kwa usingizi ulio wafunika wale walio wa kweli katika Imani yao na kumtegemea kwao Mwenyezi Mungu. Ama kile kikundi kingine, hamu yao ni juu ya nafsi zao tu hawana jenginelo; kwa hivyo wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbovu za kijahiliya, wakisema kwa kuchukiwa: Tumepata ushindi wowote sisi huo tulio ahidiwa? Sema ewe Nabii: Mambo yote ya kushinda na kushindwa yako kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye mwenye kuyaendesha mambo kwa waja wake pindi wao wakichukua khatua za ushindi, au wakifanya mambo ya kusabibisha kushindwa. Na wao wanapo sema hayo wana jambo wanalo lificha katika nafsi zao, wala hawalidhihirishi. Kwani wao husema: Ingeli kuwa sisi tuna khiari yetu tusingeli toka, basi tusingeli shindwa. Waambie: Hata mngeli kuwa ndani ya majumba yenu na kama wapo walio andikiwa kuuliwa basi hapana shaka wangeli toka mpaka pahala pao pa kufa wakauliwa. Na Mwenyezi Mungu amefanya aliyo yafanya hapo Uhud kwa maslaha makubwa, ili apate kutoa ndani yenu ikhlasi, na azitahirishe nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua vilivyo yaliyo fichika ndani ya nyoyo zenu.
155. Enyi jamaa wa Kiislamu! Wale miongoni mwenu walio acha kusimama imara pale pahali pao walipo wekwa wasimame hakika ni Shetani ndiye aliye wavuta kwenye utelezi na kukosea kwa sababu ya makosa yao kumkhaalifu Mtume. Lakini Mwenyezi Mungu amekwisha wasamehe, kwani Yeye ni mwingi wa maghfira, na mwingi wa upole.
156. Enyi mlio amini! Msiwe kama walio kufuru wakasema, kwa mintarafu ya wenzao wanapo ondoka kwenda safarini kutafuta maisha wakafa, au wakenda vitani wakauwawa: Lau wangeli bakia nasi hapa wasingeli kufa, na wasingeli uwawa. Mwenyezi Mungu amejaalia kauli yao hiyo na dhana yao iwe ni majuto ya nyoyoni mwao. Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuhuisha na Mwenye kufisha, na kudra ya kila kitu imo mikononi mwake. Yeye anayajua yote myatendayo, ya kheri na shari. Na Yeye ndiye wa kukulipeni.
157. Na mkiuwawa katika Jihadi au mkafa wakati huo, basi hayo hakika ni kupata maghfira ya Mwenyezi Mungu kufutiwa dhambi zenu, na kupata rehema itokayo kwake. Hayo ni bora kuliko starehe za dunia ambazo mnge zikusanya lau mngeli bakia.
158. Na lau mtakufa au mtauliwa katika Jihadi hazitopotea bure a'mali zenu, kwani mtakusanywa kwa Mwenyezi Mungu akulipeni kwa Jihadi yenu na ikhlasi yenu.
159. Ilikuwa ni rehema ya Mwenyezi Mungu kwako wewe (Muhammad) na kwao (Waumini) kwa kuwa wewe umekuwa laini kwao wala hukuwatolea neno la ukali kwa kukosea kwao. Na lau kuwa wewe ungeli kuwa unawachukulia kwa ukavu, na moyo mgumu wangeli kukimbia. Basi nawe yapuuze makosa yao, na waombee msamaha, na ushauriane nao katika mambo ili upate maoni yao katika mambo ambayo siyo ulio teremshiwa ufunuo, Wahyi. Ukisha funga azimio lako juu ya jambo baada ya kushauriana, basi endelea nalo na huku ukimtegemea Mwenyezi Mungu. Kwani Mwenyezi Mungu humpenda anaye mwakilisha mambo yake Yeye.
160. Mwenyezi Mungu akikuungeni mkono kwa nuSura yake, kama ilivyo tokea siku ya Badri, hatokushindeni yeyote. Na akikuacheni mkono kwa kuwa nyinyi hamkuchukua khatua zifaazo za ushindi, kama yaliyo pita siku ya Uhud, basi hamtakuwa na wa kukunusuruni mwenginewe. Na ni juu ya Mwenyezi Mungu peke yake ndio yawapasa Waumini wategemeze mambo yao yote.
161. Haisihi kuwa Nabii yeyote kukhuni katika ngawira kama walivyo eneza kwa uzushi wanaafiki waongo. Kwani khiyana ni kinyume na Unabii. Basi isikupitikieni dhana hiyo. Na mwenye kukhuni atakuja Siku ya Kiyama na mzigo wa dhambi wa khiyana yake, tena kila nafsi italipwa ilicho tenda, kwa ukamilifu. Na wala hawatadhulumiwa kwa kupunguzwa thawabu zao wala kuzidishiwa adhabu yao.
162. Hawawezi kuwa sawa, anaye piga mbio kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu kwa vitendo na ut'iifu, na yule anaye stahiki ghadhabu kuu ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ya uasi wake. Na mwenye kuasi ataishia Jahannamu, na kuovu kulioje huko!
163. Makundi mawili hayo hayawi sawa, bali yametafautiana mbele ya Mwenyezi Mungu kwa daraja mbali mbali. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zao na daraja zao, na atawalipa kwa mujibu wake.
164. Mwenyezi Mungu amewafadhili Waumini wale wa mwanzo walio kuwa na Nabii s.a.w. kwa kuwapelekea Mtume aliye tokana na wao wenyewe, akiwasomea Aya za Kitabu, na akiwat'ahirisha na itikadi mbovu, akiwafundisha Qur'ani na Sunna za Mtume, na ilhali kabla ya kuletwa Mtume, walikuwa katika ujinga na ubabaishi na upotovu.
165. Hivyo mnapigwa na mshangao na kuemewa pale yalipo kupateni siku ya Uhud masaibu ambayo nyinyi mlikwisha wapa maadui mara mbili mfano wa hayo katika siku ya Badri, hata mnasema kwa mastaajabu: Yamekuwaje mauwaji haya na kushindwa huku, na sisi ni Waislamu na Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko nasi? Sema: Yaliyo kupateni yametokana na nafsi zenu kwa vile mlivyo mkhalifu Mtume. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, naye amekulipeni kwa mujibu wa mlivyo tenda.
166. Enyi Waumini! Yaliyo kusibuni lilipo pambana jeshi lenu na jeshi la Washirikina katika Uhud yametokana kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu, na ili awadhihirishie watu Imani ya Waumini ya kweli aliyo ifunza.
167. Na hayo ili pia udhihiri unaafiki wa wanaafiki. Nao hawa ni wale walipo kuwa wanaondoka wanaacha vita wakaambiwa: Njooni mpigane kwa kumt'ii Mwenyezi Mungu, au kwa ajili ya kujilinda nafsi zenu. Wakasema: Lau kuwa tunajua kuwa mtakutana na vita, tungeli kwenda nanyi. Na wao walipo sema kauli hiyo walikuwa karibu zaidi na ukafiri kuliko Imani. Wanasema kwa midomo yao: Huko hakuna vita. Na hali wanaitakidi ndani ya nyoyo zao kuwa vita kweli vitakuwepo. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema unaafiki wanao uficha, kwani Yeye anajua matokeo ya siri zao.
168. Na hao ndio walio baki nyuma wesende vitani wakakwepa, na wakasema kwa mintarafu ya ndugu zao walio toka wakauliwa: Lau wangeli tufuata sisi wakakaa nyuma kama tulivyo kaa sisi wangeli okoka kama tulivyo okoka. Waambie: Zizuieni nafsi zenu basi zisife, kama mnasema kweli kuwa hadhari inazuia kadari.
169. Wala usidhani kabisa kuwa walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni maiti, bali hao wahai kwa uhai anao ujua Mwenyewe Mwenyezi Mungu, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi, riziki njema anayo ijua Yeye.
170. Nyuso zao zinameremeta kwa furaha na bishara kwa fadhila ya pekee aliyo wapa Mwenyezi Mungu, na wanawafurahia ndugu zao ambao walio waacha duniani wangali wahai, wanashika mwendo wa Imani na Jihadi, na ya kwamba hapana khofu juu yao kupata lolote la karaha wala si wenye kuhuzunika kwa kumkosa mpendwa.
171. Nyuso za Mashahidi zinameremeta kwa neema ya kufa shahidi na neema ya Pepo, na ubora wa karama, na ya kwamba haupotei ujira wa Waumini.
172. Waumini hao ni wale ambao wameitikia wito wa Mtume wa kuanza upya Jihadi baada ya pigo kubwa walilo lipata katika vita vya Uhud. Kwa hivyo basi wakawa ni wenye kutenda wema, na wakajilinda na kuasi amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi wakastahiki ujira mkubwa katika Nyumba ya Malipo na Neema.
173. Hao ndio walio tiwa khofu na watu kwa kuwaambia: Maadui zenu wamekusanya jeshi kubwa kukupigeni, basi waogopeni. Na wao hawakudhoofika wala hawakulegea, bali walizidi Imani ya Mwenyezi Mungu na wakawa na moyo kuwa atawanusuru. Jawabu yao ikawa: Mwenyezi Mungu anatutosheleza. Yeye ndiye aliye tawala mambo yetu. Na Yeye ndiye anaye tegemezwa mambo yote.
174. Kisha wakatoka kwenda kwenye Jihadi na kupambana na hilo jeshi kubwa, lakini washirikina wakaingiwa na woga wakakimbia. Wakarejea Waumini kuwa wameshinda kwa neema ya salama ilhali wao wana hamu ya Jihadi, na wana malipo na thawabu na fadhila ya Mwenyezi Mungu kwao kwa vile kutia kitisho katika nyoyo za maadui zao, na wao wasipatikane na maudhi yoyote. Waliitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu, na wao wakaistahiki fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.
175. Mwenyezi Mungu Aliye takasika anawabainishia Waumini kwamba hao wanao kutieni khofu kuogopa kupambana na maadui zenu si lolote ila ni vibaraka wa Shetani anaye watia khofu wafwasi wake awafanye woga. Na nyinyi si katika hao. Basi msiridhie kutishwa, bali mkhofuni Mwenyezi Mungu peke yake kama nyinyi mna Imani ya kweli, na mnasimamia kutimiza yanayo lazimishwa na Imani hiyo.
176. Ewe Nabii! Usihuzunike ukiwaona wale ambao wanazidi ukafiri, na wanawania kuzidisha maovu. Hao hawamletei Mwenyezi Mungu madhara yoyote, kwani Yeye ni Mwenye nguvu juu ya waja wake. Bali Mwenyezi Mungu anataka wasiwe na sehemu yoyote katika thawabu za Akhera, na juu ya kukosa kwao thawabu hizo njema watapata adhabu kubwa.
177. Hakika watu hao walio khiari ukafiri badala ya Imani, wakatafuta ukafiri na wakaacha Imani, hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu, na watapata Akhera adhabu kali ya kutia uchungu mkubwa.
178. Wasidhani hao makafiri kuwa vile kuwapururia tunapo wakunjulia umri wao, na tukawapa njia za starehe katika maisha yao ya duniani, kuwa ndio kheri yao. Kwani kuwaongezea umri na kuwakunjulia riziki huwapelekea kudumu na kuchuma madhambi na kuzidi kustahiki adhabu ya kuwafedhehesha aliyo waandalia Mwenyezi Mungu.
179. Haiwi kuwa Mwenyezi Mungu akuacheni enyi jamaa Waumini katika hali hii hii mliyo nayo ya mchanganyiko wa Muumini na mnaafiki, mpaka awatenganishe baina yenu kwa misukosuko na taabu ili mumwone mnaafiki khabithi na Muumini mwema. Wala sio mwendo wa Mwenyezi Mungu kumjuulisha yeyote katika viumbe vyake khabari za ghaibu. Walakini Mwenyezi Mungu humteua katika Mitume yake ampendaye akamjuvya anacho kitaka katika mambo yake ya ghaibu. Na nyinyi mkiamini na mkamcha Mola wenu Mlezi kwa kujilazimisha kumt'ii atakutieni katika Pepo iwe ndio malipo. Na hayo ndio malipo yaliyo bora na makubwa kabisa.
180. Wasidhani wanao fanya ubakhili kwa mali aliyo waneemesha Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake, na hawayatoi katika yaliyo waajibu na njia za kheri, kuwa ubakhili huo ni kheri yao. Bali hiyo ni shari yenye matokeo mabaya juu yao. Watalipwa malipo maovu kabisa Siku ya Kiyama, na adhabu itawaganda kama kongwa au mnyororo aliyo fungwa nayo mfungwa shingoni mwake. Kila kiumbe kinamnyenyekea Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, naye ndiye Mmiliki wao, na Yeye Aliye takasika anajua kila mnacho kitenda, na atakulipeni kwacho.
181. Juu ya kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kumiliki kila kiliomo mbinguni na ardhini na Yeye ndiye mrithi wa vyote, wamesema baadhi ya Mayahudi kwa kejeli: Mwenyezi Mungu ni fakiri, ndiyo akatutaka tutoe, na sisi ni matajiri tukitoa au tusitoe. Mwenyezi Mungu amekwisha isikia kauli yao hiyo, na ameisajili dhidi yao, kama alivyo sajili kuwauwa kwao Manabii kwa dhulma na ukhalifu na uadui. Naye atawaambia Siku ya Kiyama: Onjeni adhabu ya Moto unao waka!
182. Na hiyo adhabu ni kwa dhambi zao walizo zitenda wenyewe, na malipo ya Mwenyezi Mungu hayawi ila ni kwa uadilifu, wala Yeye kabisa hawadhulumu waja wake.
183. Hao ndio walio sema: Mwenyezi Mungu ametuamrisha katika Taurati tusimfuate Mtume yeyote ila akileta dalili ya ukweli wake kwa kutuletea kitu cha kumkurubisha kwenye radhi ya Mwenyezi Mungu, na uteremke moto kutoka mbinguni ukile hicho kitu. Ewe Nabii! Waambie: Hakika Mitume kutoka kwa Mwenyezi Mungu wamekwisha kukujieni kabla yangu, wakaja na dalili zilizo wazi, na wakaja na hayo mnayo yasema. Na juu ya hayo mliwakadhibisha na mkawauwa. Kwa nini mkafanya hayo kama nyinyi ni wasema kweli katika ahadi yenu ya Imani yanapo timia mnayo yataka?
184. Ikiwa watakukadhibisha, Ewe Nabii, wewe usisikitike. Kabla yako wamekutangulia wengi walio kadhibishwa na watu wao kwa chuki na inda, juu ya kuwa walikuja na dalili zilizo nyooka, na Vitabu vya mbinguni vyenye kuthibitisha ukweli wa Ujumbe wao.
185. Hapana hivi wala hivi, kila nafsi lazima ionje kufa. Na ikiwa hapa duniani mtapata machungu basi Siku ya Kiyama mtalipwa thawabu kwa ukamilifu. Na mwenye kuukaribia Moto akaepushwa nao basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe yenye kupita, haina dawamu.
186. Kuweni na yakini, enyi Waumini, kuwa mtapata mitihani na majaribio katika mali yenu, kwa kupungua, kutoa au kunyang'anywa, na katika nafsi zenu kwa Jihadi au kuuwawa au kwa maradhi na machungu. Na kadhaalika mtasikia kutokana na Mayahudi na Wakristo na mapagani, washirikina, matusi na uchokozi wa kukuudhini. Na mkiyakaabili hayo kwa kuvumilia na kumcha Mwenyezi Mungu basi itakuwa ni katika mambo mema yanayo wajibika kuazimia kuyatimiliza.
187. Ewe Nabii! Kumbuka na utaje pale Mwenyezi Mungu alipo chukua ahadi madhbuti kwa Watu wa Kitabu, kuwa wayaeleze wazi maana ya Kitabu chao, na wala wasiwafiche watu chochote, na wao wakakitupilia mbali nyuma ya migongo yao, na badala yake wakatafuta starehe za dunia. Na starehe za dunia kama zitakavyo kuwa ni kitu chenye thamani duni kabisa kulinganisha na uwongofu na uwongozi. Ama wamejua kutenda uovu! (Hayo yalikuwa zamani na bado yanaendelea. Kuficha na kugeuza na kupotosha Biblia hakusiti. Vipo vitabu vyao vinavyo itwa "Apokrifa", maana yake "Vilivyo fichwa", kwa kuwa hivyo ni marfuku visisomwe ila na mapadri tu, na vingine vimeteketezwa. Miongoni mwa hivyo ni Injili ya Barnaba.)
188. Usiwadhanie kabisa kuwa wataepuka adhabu wale wanao tenda maovu, na wakapenda kusifiwa kwa wasilo lifanya. Shani yao hao ni kujifungia mlango wa Imani na Haki, kama Mayahudi. Nao watapata adhabu chungu Siku ya Kiyama.
189. Mwenyezi Mungu pekee ndiye Mwenye mamlaka ya kila jambo la mbinguni na duniani. Naye ni Muweza wa kila kitu. Atawashika wenye dhambi kwa dhambi zao, na atawalipa thawabu watendao mema kwa wema wao.
190. Hakika katika kuumbwa
mbingu na ardhi na viliomo ndani yao kwa vile vilivyo umbwa tangu mwanzo
na mipango yake, na kukhitalifiana usiku na mchana kwa
mwangaza na giza, kwa urefu wake na ufupi, zipo dalili na ishara zilizo
wazi kwa watu wenye akili na kutambua za kuthibitisha Umoja wa Mwenyezi
Mungu na Uwezo wake.
"Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku
na mchana ziko ishara kwa wenye akili" -
Aya hii ina ukweli unao onyeshea taadhima ya Muumba. Mbingu ni moja
katika Ishara za Mwenyezi Mungu inayo tubainikia kwetu kwa miale ya jua
inayo piga juu ya anga linalo izunguka dunia. Miale hii inapo angukia chembe
chembe na vumbi vumbi jembamba liliopo angani humulika mianga hiyo na kutawanyika
kila upande. Huu mwanga mweupe kwa hakika ni mkusanyiko wa rangi zote zionekanazo.
Hizi chembe chembe za angani huzimeza baadhi ya hizo rangi.
Imedhihiri kuwa rangi yenye kuenea zaidi ni rangi ya kibuluu. Na
hii inazidi kuzagaa linapo kuwa jua liko utosini, na ubuluu wake unapungua
kidogo kidogo mpaka jua linapo kuwa upeo wa macho wakati wa magharibi au
alfajiri. Wakati huo ile miale ya jua inakwenda masafa makubwa zaidi kabisa.
Kwa hivyo zile chembe chembe za angani huzimeza rangi zote isipo kuwa rangi
nyekundu.
Usafi wa maneno ni: mwangaza wa mchana unahitaji miale ya jua na
kuwepo vumbi la kutosha katika anga. Dalili ya hayo ni yale yaliyo tokea
mwaka 1944 mbingu ilipo ingia kiza ghafla kati ya mchana. Jinsi ya kiza
mchana ukawa kama usiku. Kwa wakati mfupi yakawa hayo, kisha mbingu ikawa
nyekundu, kisha kidogo kidogo ikawa rangi ya machungwa, na kisha ya manjano
mpaka mbingu ikarejea rangi yake ya tabia, baada ya saa au zaidi.
Baadae ilibainika kuwa mambo hayo yalitokana na mripuko mbinguni
likatokea jivu, likachukuliwa na upepo mbali mpaka Afrika ya kati na kaskazini,
na kufika magharibi ya Asia. Huko ndiko ikaonekana hali hiyo katika pande
za Syria. Maelezo yake ni kuwa vumbi lilioko hewani liliifunika nuru ya
jua. Lilipo pungua jivu ulidhihiri mwangaza mwekundu na baadae wa manjano
n.k.
Mwanaadamu akipaa angani katika chombo atapitia matabaka yanayo
khitalifiana sifa. Ataiona mbingu inazidi ubuluu mpaka akifika kwenye anga
la nje lisio kuwa na hayo mavumbi n.k. ataona mbingu yote ni kiza kitupu
kama kwamba ni usiku juu ya kuwa jua lipo juu. Kwa ufupi ni kuwa zipo mbingu
nyingi si moja ziliyo pandana tabaka kwa tabaka kama maqubba, zinazo khitalifiana
katika sifa zake na rangi zake.
Haya ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu Mtukufu Aliye takasika kuwa
vyote viliomo mbinguni na ardhini vinamtukuza Yeye. Ama kukhitalifiana
usiku na mchana, tumekwisha fahamu kuwa mwanga wa mchana unategemea miale
ya jua kuanguka juu ya hili funiko la anga, lenye chembe chembe za vumbi
kwa kiasi maalumu. Mwangaza huu ni mkali hata unaficha mwangaza unao toka
kwenye nyota n.k. Ama wakati wa usiku mwangaza wa jua unapo fichika, inakuwa
hapana katika anga isipo kuwa vumbi linalo tuzunguka na mianga dhaifu ya
nyota. Kupishana usiku na mchana ni kwa sababu ya kuzunguka dunia kwa nafsi
yake wenyewe, na tafauti ya misimu na kurefuka na kufupika usiku na mchana
ni kwa mzunguko wa hii dunia kulizunguka jua. Na katika hikima yake Mwenyezi
Mungu na uwezo wake ni kuwa kubadilika usiku na mchana, na kubadilika misimu
ya joto na baridi, ni kutengeneza hali ya hewa iwe wastani, yaani kati
na kati, kwa kusilihi maisha ya vilivyo hai.
191. Ni shani ya wenye akili kuwa kila pahali wao wanahudhurisha katika nafsi zao adhama na utukufu wa Mwenyezi Mungu, wakiwa wamesimama au wamekaa au wamejinyoosha kitandani, na wanazingatia uumbaji wa mbingu na ardhi pamoja na viliomo ndani yake, na huku wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuumba haya ila kwa hikima uliyo ikadiria. Na Wewe umetakasika na kila upungufu. Bali umeumba hivi vyote kuwa ni dalili ya kudra yako, na ishara ya upeo wa hikima yako. Utuhifadhi na adhabu ya Moto kwa kutuwezesha kukut'ii.
192. Ewe Muumba wetu, na Mwenye kutusimamia mambo yetu, na Mlinzi wetu! Hakika mwenye kustahiki Moto na ukamuingiza, basi umempa hizaya. Na mwenye kudhulumu akastahiki Moto hana wa kumnusuru nao.
193. Ewe Muumba wetu, na Mwenye kutusimamia mambo yetu, na Mlinzi wetu! Hakika sisi tumemsikia Mtume wako akiita watu wakuamini Wewe, nasi tukamt'ii na tukamuamini. Ewe Mola wetu Mlezi! Tughufirie madhambi yetu makubwa, na tufutie maovu yetu madogo madogo, na baada ya kufa kwetu tujaalie tuwe pamoja na waja wako walio bora.
194. Ewe Muumba wetu, na Mwenye kutusimamia mambo yetu, na Mlinzi wetu! Tupe uliyo tuahidi kwa ndimi za Mitume yako, nayo ni ushindi na kuungwa mkono duniani. Wala usituingize Motoni ukatuhizi Siku ya Kiyama. Shani yako ni kuwa huendi kinyume na miadi yako.
195. Mola wao Mlezi aliwaitikia dua yao, akiwabainishia kuwa Yeye hampotezei mtendaji thawabu za vitendo vyake, sawa sawa akiwa mwanamume au mwanamke, kwani mwanamke anatokana na mwanamume, na mwanamume anatokana na mwanamke. Basi wale walio hajiri, wakahama, wakagura, wanatafuta radhi ya Mwenyezi Mungu, na wakatolewa makwao, na wakapata mateso katika Sabili Llahi, Njia ya Mwenyezi Mungu, wakapigana vita, na wakakhatirisha kuuwawa, bali wakauliwa walio uliwa, Mwenyezi Mungu amejilazimisha Mwenyewe kuwasamehe madhambi yao, na kuwatia kwenye Mabustani yenye kupita kati yake mito, kuwa ni malipo matukufu yaliyo bora kutokana na Mwenyezi Mungu. Na kwa Mwenyezi Mungu peke yake, ndio yako malipo mazuri.
196. Usiathirike, ewe Nabii, kwa kuwaona makafiri wamo katika starehe za neema, na biashara na uchumi unawaendea, wakienda huku na huku katika nchi.
197. Hizo ni starehe za kupita njia, na kila kipitacho ni duni. Kisha marejeo ya daima watayo ishia ni Jahannamu. Na hapana makaazi maovu kama Jahannamu.
198. Hayo ndiyo malipo ya makafiri. Ama walio muamini Mwenyezi Mungu wakamwogopa Mola wao Mlezi watapata Mabustani yapitayo mito kati yake, watadumu humo daima, kuwa ni wageni walio pokewa kwa ukarimu na Mwenyezi Mungu, Subhanahu, Aliye takasika. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ndio mazuri kwa watu wema kuliko hayo wanayo starehea makafiri ambayo yataondoka, hayadumu.
199. Hakika baadhi ya Watu wa Kitabu, Mayahudi na Wakristo, wanamuamini Mwenyezi Mungu, na wanaamini aliyo teremshiwa Nabii Muhammad s.a.w. na walio teremshiwa Mitume walio kuwa kabla yake. Utawaona wanamnyenyekea Mwenyezi Mungu, na wanakuwa wanyonge kwake, wala hawabadilishi bayana zilizo dhaahiri kwa ajili ya kutafuta pato la duniani. Hilo nalingawa kubwa ni kitu duni. Hawa wana malipo ya ukamilifu kwa Mola wao Mlezi katika makaazi ya kuridhisha. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu, hashindwi kuzidhibiti 'amali zao zote na kuwahisabia. Yeye ni Muweza wa hayo na malipo yake yatawafika bila ya shaka.
200. Enyi mlio amini! Shikamaneni na subira,
na mwashinde maadui zenu katika kusubiri. Na kaeni macho kuilinda mipaka,
na mkhofini Mola Mlezi wenu. Katika haya yote ndio mtaraji kufanikiwa.
(Jee! Baada ya kuijua Qur'ani yamfalia Muislamu kusema kuwa dini ni
kitu mbali na siyasa? Vipi uamrishe mema, ukataze maovu, uhukumu, ukatibiane
mikataba na dola nyengine, ukusanye zaka na kuzigawa, upigane Jihadi, ulinde
mipaka n.k., n.k. na uiepuke siyasa?
Amesema Prof. Khurshid Ahmad: "Uislamu si dini kwa maana ya ovyo ovyo
kama lilivyo potoshwa neno hilo, yaani kuwa umemkhusu mtu maisha yake ya
binafsi tu. Ni mwendo kaamili wa maisha, unao angalia kila midani ya uhai
wa binaadamu. Uislamu ni uwongozi katika kila nyendo za maisha - za binafsi
na za jamii, za kimwili na kiroho, za uchumi na siyasa, za sharia na mila,
za taifa na za mataifa."--Uislamu, Maana na Ujumbe wake uk. 37)