1. T'aa Siin, (T' na S) harufi mbili za kutamkwa, ni harufi za alifbete, ndizo zimeanzia Sura hii, ili kunabihisha siri ya muujiza wa Qur'ani pamoja na kuashiria kuwa imeundwa kwa jinsi ya harufi hizi hizi mnazo zitumia katika kusema, na pia kuzindua akili ziisikilize hii Qur'ani inapo somwa.
Hizi Aya zilizo teremka kwa kusomwa, na ni Kitabu chenye kubainisha mambo yaliyo kuja ndani yake.
Rudi kwenye Sura

2. Na hii Qur'ani ni Uwongofu wa kuwaahidi Waumini waifuate njia ya kheri, na kufuzu duniani na Akhera, na inawabashiria kuwa watapata malipo mazuri.
Rudi kwenye Sura

3. Waumini hao ndio wanao ishika Sala kwa unyenyekevu na kutimiliza nguzo, na wanatoa Zaka kwa nyakati zake, nao wana yakini ya maisha ya baadaye Akhera, na yatayo kuwa huko ya adhabu na thawabu.
Rudi kwenye Sura

4. Hakika wale ambao hawaiamini Akhera, Sisi tumewapambia vitendo vyao kwa kuwaumbia matamanio ndani yake. Kwa hivyo wao wanababaika humo katika upotovu wao.
Rudi kwenye Sura

5. Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na Akhera ndio watakuwa khasarani kushinda wote.
Rudi kwenye Sura

6. Ewe Nabii! Wewe unapokea Qur'ani hii unayo teremshiwa kutokana na Yeye ambaye hapana anaye mkaribia kwa hikima yake, naye anajua kila kitu.
Rudi kwenye Sura

7. Kumbuka pale Musa alipo mwambia mkewe na walio pamoja naye na yeye ndio anarejea Misri: Mimi nimeona moto. Nitakwenda kuleteeni khabari ya njia, au nitapata kijinga cha moto, kitacho kufaeni kwa kuota moto kwa hii baridi.
Rudi kwenye Sura

8. Alipo fika huko paliitwa: Wamebarikiwa waliomo katika moto huu na walioko pembezoni mwake, yaani karibu yake. Nao ni Malaika na Musa. Na Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote ametakasika na kila kisicho kuwa laiki naye.
Rudi kwenye Sura

9. Ewe Musa! Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mwenye kustahiki kuabudiwa pekee, Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kuweka kila kitu pahala pake.
Rudi kwenye Sura

10. Na katika njia ya kufikisha wito wako, tupa fimbo yako na utaiona inatikisika kama kijoka jepesi kinakwenda mbio. Yeye akarudi nyuma, wala hakurejea baada ya kurudi nyuma. Mwenyezi Mungu Mtukufu akamtuza kwa kauli yake: Usiogope. Mbele yangu hawaogopi. Mitume ninapo sema nao.
 Kisa cha Musa kimetajwa zaidi ya mara moja katika Qur'ani. Pengine hutolewa yasiyo tajwa penginepo. Na kila sehemu ina mnasaba wake. Katika sehemu hii makusudio ni kuondoa yale mastaajabu ya kuwa Nabii Muhammad s.a.w. kapata Ufunuoa (Wahyi) vile vile.
Rudi kwenye Sura

11. Lakini mwenye kutenda asicho ruhusiwa, na kisha akaleta wema baada ya kuteleza kwake, basi Mimi ni Mwingi wa kusamehe, Mkubwa wa kurehemu.
Rudi kwenye Sura

12. Na utie mkono wako katika mfuko wa nguo zako, utatoka mweupe wala si kwa balanga. Hayo ni katika Ishara tisa (1) za kumpelekea Firauni na kaumu yake. Hakika hao walikuwa watu  walio tokana na amri ya Mwenyezi Mungu, ni makafiri.
(1) Hizo Ishara tisa ni:- Kupasuka bahari, T'ufani (Kimbunga), Nzige, Chawa, Vyura, Damu, Ukame, Fimbo, Kutoka mkono mweupe bila ya maradhi.
Rudi kwenye Sura

13. Ilipo kuja miujiza hii kwa uwazi na dhaahiri wakasema: Huu ni uchawi wazi!
Rudi kwenye Sura

14. Wakaikadhibisha miujiza wakikataa kuwa inaonyesha dalili ya Utume. Na hakika yakini ilikwisha waingia katika nyoyo zao, lakini hawakusalimu amri kwa kuwa walikwisha tangaza kufuata upotovu na kushika uasi. Basi ewe Nabii! Hebu angalia vipi yalikuwa matokeo ya walio shikilia ufisadi, wakaikanya miujiza nayo  iko wazi.
Rudi kwenye Sura

15. Hizo ndizo jeuri za Firauni kwa sababu ya ufalme wake. Hebu sasa angalia utawala muadilifu, utawala wa hukumu, utawala wa unabii wa Daudi na mwanawe, Sulaiman, Mwenyezi Mungu awape amani. Sisi tuliwapa ilimu nyingi za sharia na mazoezi ya kuhukumu. Wakasimamisha uadilifu, na wakamhimidi Mwenyezi Mungu aliye wapa fadhila kushinda wengi katika waja wake wenye kusadiki, na kuifuata Haki.
Rudi kwenye Sura

16. Ufalme na hukumu ukatoka kwa Daudi ukenda kwa mwanawe, Sulaiman; naye akasema: Enyi watu! Sisi tumefunzwa lugha ya ndege, na tumepewa mengi tunayo yahitajia katika utawala wetu. Hakika neema hizi ni fadhila iliyo wazi aliyo tukhusisha sisi Mwenyezi Mungu,
"Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhaahiri." Sulaiman a.s. ni mwana wa Daudi, naye ni Nabii na Mfalme kama yeye. Aliishi mnamo mwaka 974 mpaka 937 K.K. (yaani Kabla ya Kuzaliwa Nabii Isa). Mwenyezi Mungu alimjaalia kumjuvya kufahamu maneno ya ndege. Uchunguzi wa kisasa umeonyesha kwamba kila namna ya ndege wana njia zao za kufahamiana wao kwa wao. Katika njia hizo ni kwa kugusa, na sauti, na ishara.
Rudi kwenye Sura

17. Na Sulaiman alikusanya majeshi yake ya majini, watu, na ndege, kwenye uwanja mmoja. Na wao wakawa jeshi moja lenye nidhamu kwa vile kudhibitiwa wa mwanzo mpaka mwisho.
Rudi kwenye Sura

18. Hata walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, mdudu chungu mmoja akasema: Enyi wadudu chungu! Ingieni vishimoni mwenu, asije Sulaiman na askari wake wakakuuweni na wao wala hawahisi kuwa nyinyi mpo.
"Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, alisema mdudu chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu, asikupondeni Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua." Inafahamikana wazi katika Aya hii kuwa wadudu chungu wanaishi kwa makundi, yaani wana umoja, na moja katika sifa zao ni kuwa macho na kutahadhari. Na inajuulikana tangu zamani kuwa wadudu chungu wana sifa kadhaa wa kadhaa makhsusi ambazo zinaonyesha kuwa wana umoja wenye nidhamu madhubuti katika hukumu, na wana kiasi kikubwa cha akili, na werevu, na nguvu za kukumbuka, na kupenda kazi na kukakamia, na juhudi isiyo jua kunyong'onyea wala kukata tamaa. Kama wanavyo juulikana kuwa wana wingi wa hila za kuendesha kazi zao. Na dalili ya hayo ni kuwa jamaa wa wadudu chungu ni peke yao baada ya binaadamu  ndio wanao zika maiti wao. Na makundi mbali mbali yao yanashughulikia kukutana pahala pamoja kwa nyakati maalumu. Kwa ajili ya hayo zimewekwa siku makhsusi za kusimamisha soko wanapo kusanyika makundi yote kwa kubadilishana bidhaa na kujuana. Na makundi haya yanapo kutana hutokea mazungumzo kwa hima kubwa, na huulizana masuala yaliyo khusiana na mambo yao. Katika yanayo onekana yaliyo fungamana na mikusanyiko hiyo ni kuzuka mashauri yaliyo khusu umma wao, kama kutengeneza barabara ndefu, kwa subira na kukakamia kunako staajabisha. Wala makundi haya hayatosheki na kufanya kazi mchana tu, bali huendeleza kazi zao katika masiku ya mbaamwezi; ama masiku ya kiza hubaki mwahala mwao. Na jamaa wa makundi haya wana njia za pekee za kukusanya na kubeba na kuhifadhi vifaa vyao vya kula. Akishindwa mdudu kuchukua chakula alicho kikusanya kwa mdomo wake hukisukuma kwa miguu yake ya nyuma, na akakinyanyua kwa mikono yake. Na katika mtindo wao ni kuzing'ong'ona mbegu, na kuzipasua baadhi ya nafaka kabla ya kuzirindika ili zisije kuchipua. Na mbegu kubwa kubwa huzigawa vipande vipande ili iwe wepesi kuziingiza katika ghala zao. Na pindi zikiroana kwa mvua huzitoa zipate upepo na jua zikauke.
Rudi kwenye Sura

19. Sulaiman akatabasamu akicheka kwa ile kauli ya mdudu chungu yenye kushughulikia maslaha yao, na akahisi neema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyo juu yake. Akasema: Ewe Uliye niumba! Nijaalie niwe na shukrani kwako kwa neema ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na niwezeshe nitende vitendo vyema unavyo viridhia, na unitie kwenye rehema yako iliyo timia.
Rudi kwenye Sura

20. Akalikagua jeshi lake la ndege asimwone Hud-hud. Akastaajabu, akasema: Mbona simwoni Hud-hud! Yupo hapa na mimi simwoni, au ameghibu hayupo miongoni mwetu?
Rudi kwenye Sura

21. Wallahi! Nitampatisha adhabu kali ya kumshikisha adabu, au nitamchinja ikiwa kosa lake ni kubwa! Ila aniletee hoja madhubuti ya kumtoa makosani kwa kuto kuwepo mbele yangu.
Rudi kwenye Sura

22. Na Hud-hud alikuwa kakaa si pahala mbali kwa muda usio kuwa mrefu. Kisha akamjia Sulaiman, akamwambia: Nimejua jambo ulilo kuwa wewe hujalijua, na nimekujia kutoka nchi ya Sabai na khabari muhimu sana, nayo ni ya kweli kwa yakini.
"Basi hakukaa mbali, na akasema: Nimegundua usilo gundua wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na nakuletea khabari za yakini. Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa.Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na Shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa hivyo hawakuongoka." Hizi ndizo Aya khasa zilizo khusu Ufalme wa Sabai. Na hii Sabai ni moja katika falme za kusini ya Arabuni, inayo itwa Yaman, na ambayo zamani ilikuwa ni maarufu kwa jina la "Arabia Iliyo Neemeka".  Na jina hili la mwisho linaonyesha maendeleo yake na utajiri wake. Kwani kwa hakika ilikuwa nchi hiyo ina ustaarabu wa juu tangu miaka elfu mbili kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s. Ikitegemea makulima, kwa sababu ya rutuba ya ardhi yake, na uzuri wa hali yake ya hewa. Na pia ikitegemea biashara kwa kuwa ipo kati baina ya Bara Hindi, na Uhabeshi, na Somalia, na Sham, na Iraq. Na kwa hakika mahodhi yaliyo jengwa kuwekea maji na kuyatumia, na maarufu yao yote ni Hodhi Maa'rib (Tazama Aya 16 Surat Sabai) na miji iliyo jengewa ngome, na makasri, na mahekalu, yanashuhudia mpaka hii leo maendeleo ya kijamii ya utajiri ulio kuwako katika nchi hii.
Na hakika nakshi walizo zinakishi watawala wao, na baina ya nakshi hizo zipo kanuni za kuendesha mambo ya ujenzi na mengineyo, yanaonyesha kwa kila dalili ukomo wa ustaarabu ulio nawiri walio ufikilia. Na huu ufalme wa Sabai ambao ulifikilia kilele cha kustawi kwake katika siku za Sulaiman a.s. kiasi ya karne kumi kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s. ulikuwa ni ufalme kama wa kabla yake, yaani watoto wakiwarithi baba zao. Na kwa hivyo alikuwa akihukumu wakati wa Sulaiman a.s. Malkia. Wataalamu wa taarikhi wamekhitalifiana juu ya jina la Malkia huyo. Waarabu wakimwita Balqiis; akisaidiwa na wazee wahishimiwa kama ni Baraza la Mashauri lake. (Tazama Aya 28-33 katika Surat An-naml.) Wala haikuthibitisha taarikh (historia) kuwa Ufalme wa Sabai ulikuwa dola ya kuteka nchi, bali ulikuwa ufalme wa biashara, na misafara. Katika mabaki yake hatuoni kutajwa vita au kuteka nchi isipo kuwa kwa uchache. Na haya ni kuwa umuhimu wa majeshi yake ulikuwa ni kuhifadhi ngome zake na kuzihami, na kulinda misafara yake kwa aghlabu. Na wananchi wa Sabai walikuwa ni mapagani, makafiri, wakiliabudu jua, kama ilivyo kuja katika Aya tukufu nambari 24 katika Sura hii. Pia wakiabudu mwezi. Na hao ndio miungu yao muhimu kabisa. Na walikuwa wakiwatolea sadaka na wakifukiza ubani katika mahekalu yao.
Rudi kwenye Sura

23. Hakika mimi nimewaona watu wa Sabai wanatawaliwa na mwanamke, na amepewa kila kheri za kidunia, naye ana kiti cha enzi kikubwa kinacho onyesha dalili ya utukufu wa ufalme na nguvu za madaraka yake.
Rudi kwenye Sura

24. Nimemwona yeye na watu wake wanaabudu jua, wala hawamuabudu Mwenyezi Mungu. Na Shetani amewazainishia vitendo vyao na wenyewe wakaviona ni vizuri na hali ni viovu. Kwa hivyo amewapoteza Njia ya Haki, basi hawakuongoka.
Rudi kwenye Sura

25. Hawamsujudii Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye ndiye anayafichua yaliyo fichika katika mbingu na ardhi, na anajua mnayo fanya kwa siri na kwa dhaahiri.
Rudi kwenye Sura

26. Mwenyezi Mungu, ambaye hapana wa kuabudiwa kwa Haki isipo kuwa Yeye, ndiye Mwenye madaraka makuu yasio na ukomo juu ya kila kiumbe.
Rudi kwenye Sura

27. Sulaiman akasema kumwambia Hud-hud: Tutaichungua khabari yako hii tujue kwamba umesema kweli au wewe ni miongoni mwa waongo.
Rudi kwenye Sura

28. Nenda na barua yangu hii umfikishie yeye na kaumu yake. Kisha jitenge nao ujifiche pahali karibu, uangalie wanarejesheana maneno gani.
Rudi kwenye Sura

29. Barua ikamfikia yule Malkia, naye basi akawakusanya wahishimiwa wa kaumu yake, na halmashauri wake. Naye akasema: Enyi wahishimiwa! Mimi hakika imenifikilia barua yenye shani kuu.
Rudi kwenye Sura

30. Kisha akawasomea hiyo barua, nayo imeanzia kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu na neema zote, ambaye daima anawamiminia waja wake rehema zake.
Rudi kwenye Sura

31. Msifanye kiburi juu yangu, na nijieni nanyi mmet'ii na wanyenyekevu.
Rudi kwenye Sura

32. Akaiambia baraza ya washauri wake: Nibainishieni lifaalo katika haya mambo muhimu nilio wekewa mbele yangu. Kwani mimi sikati shauri juu ya jambo lolote mpaka muwe nyinyi mmehudhuria.
Rudi kwenye Sura

33. Wakamwambia nao wametua: Sisi ni watu wenye nguvu za mwili, na tuna moyo na mashujaa. Hatuogopi vita. Basi angalia wewe jambo unalo taka kutuamrisha nasi ni wenye kut'ii.
Rudi kwenye Sura

34. Akasema kwa taratibu na kupendelea salama: Hakika watawala wakiingia katika miji mikubwa pamoja na majeshi yao huifisidi, wakaondoa matengenezo yake, wakateketeza makulima na roho, na wakawafanya walio watukufu katika watu wa hiyo miji kuwa ndio madhalili, na huo ndio mtindo wao daima.
Rudi kwenye Sura

35. Na mimi kwa kupendelea salama na uzima nitampelekea zawadi Sulaiman na kaumu yake, na nitatazama wajumbe watarejea na nini - wataikubali zawadi au watairudisha?
Rudi kwenye Sura

36. Wajumbe walifika kwa Sayyidina Sulaiman na zawadi zao. Huku anazijua neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu zilio juu yake, Akawaambia naye ndio anamsemeza huyo Malkia na watu wake katika mkabala na wajumbe: Hivyo ndio mnanipa mimi mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ya Unabii, na ufalme, na neema, ni makubwa zaidi kuliko aliyo kupeni nyinyi. Bali nyinyi kwa hizi zawadi zenu na wingi wa mali yenu mnafurahi, sio kama mimi. Kwa sababu nyinyi hamjui ila yaliyo shikamana na dunia hii tu.
Rudi kwenye Sura

37. Akasema, akimsemeza yule msemaji kwa jina lao: Ewe mjumbe! Rejea kwao. Wallahi! tutawatokea kwa majeshi wasio yaweza kupambana nayo na kuyakabili. Na tutawatoa  kwenye nchi ya Sabai nao wamepoteza utukufu wao, wamefanywa watumwa.
Rudi kwenye Sura

38. Sulaiman akawaelekea binaadamu na majini aliyo dhalilishiwa na Mwenyezi Mungu kumtumikia, akawashitua kwa jambo geni. Akasema: Ni nani katika nyinyi anaweza kuniletea kiti chake cha enzi kikubwa kabla hawajanijia nao wamekwisha nyenyekea wanat'ii.
Rudi kwenye Sura

39. Mmoja pandikizi la kijini lilisema: Mimi nitakuletea, na wewe umekaa katika baraza yako hii, kabla hujaondoka. Na mimi hakika naweza hayo, na muaminifu katika maneno yangu na vitendo vyangu.
Rudi kwenye Sura

40. Akasema aliye pewa nguvu za kiroho, na ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea hicho kiti cha enzi kabla jicho lako halijapepesa. Na akatimiza aliyo yasema. Sulaiman alipo kiona kiti kile kimetua mbele yake bila ya mtingisiko, alisema: Haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu aliye niumba  na akanipa kheri zake ili anifanyie mtihani, nitashukuru kwa neema hizi au sitoi haki yake? Na mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu basi huyo hakika amejiondolea nafsi yake mzigo wa waajibu. Na mwenye kuacha kushukuru kwa neema basi hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi, si mwenye kuhitajia shukrani. Naye ni Karimu wa kuneemesha.
Rudi kwenye Sura

41. Sulaiman akawaambia watu wake: Kigeuzeni geuzeni hichi kiti cha enzi kwa baadhi ya mabadiliko ya nje, tupate kuona atakijua kwa kukiendea au hato kijua na kwa hivyo hato kiendea.
Rudi kwenye Sura

42. Alipo fika jicho lake lilipiga kwenye kiti chake cha enzi. Akaambiwa: Je! Kiti chako cha enzi ni mfano wa hiki? Akasema kwa vile kilivyo kamilika kufanana: Kama kwamba ndicho hichi. Na Sulaiman na walio pamoja naye wakasema: Sisi tulisha pewa ujuzi kumjua Mwenyezi Mungu na uwezo wake na ukweli wa yaliyo kuja kutoka kwake kama anavyo jua mwanamke huyu. Na sisi tangu hapo ni watu tulio mfuata Mwenyezi Mungu na tunamsafia Yeye ibada.
Rudi kwenye Sura

43. Na zile ibada za jua na mfano wake zilimzuia yule Malkia kumuabudu Mwenyezi Mungu. Kwani yeye alikuwa katika kaumu ya makafiri.
Rudi kwenye Sura

44. Baada ya hao akaambiwa: Ingia katika jumba la Sulaiman. Na uwanja wake wa ndani ulikuwa umesakafiwa kwa kiyoo, na chini yake maji, na samaki wakiogelea humo. Kupandisha nguo miundi yake ya miguu ikaonekana, kwa kuwa alidhania ni maji. Sulaiman akamwambia hicho ni kiyoo, basi yakamuathiri yale madhaahiri ya kilimwengu, na akaona kuwa ufalme wake yeye haufai chochote mbele ya ufalme wa Nabii Sulaiman. Akasema: Mola Mlezi! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu kwa kughurika na ufalme wangu na ukafiri wangu. Na sasa ninanyenyekea pamoja na Sulaiman kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenye kuumba walimwengu wote na kuwalea na kuwasimamia.
Rudi kwenye Sura

45. Na tuliwapelekea Thamud ndugu yao Saleh kuwafunza wamuamini Mwenyezi Mungu pekee. Wao wakakimbilia kugombana na kukhitalifiana. Wakawa makundi mawili. Moja lenye kuamini, na moja la kikafiri.
Rudi kwenye Sura

46. Saleh akasema nao kuwanasihi: Enyi watu! Mbona mnaihimiza adhabu mlio ahidiwa kabla ya kutubu? Kwa nini hamwombi msamaha kwa Mola wenu Mlezi, mkamuamini Yeye kwa kutaraji akurehemuni?
Rudi kwenye Sura

47. Wakasema: Sisi tunakuona wewe na hao walio nawe ni wakorofi, ndio tukapatilizwa na ukame. Yeye akasema: Sababu za kheri na shari zinazo kuteremkieni bila ya shaka yoyote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Bali nyinyi  ni watu mnao pewa mitihani ya neema na nakama, ili mpate kuamini.
Rudi kwenye Sura

48. Na waongozi wa shari kati yao walikuwa ni tisa, kazi yao ni kufisidi  katika nchi kwa maoni yao na madai yao. Wala haukuwa mtindo wao kutenda jema lolote.
Rudi kwenye Sura

49. Wale washirikina wakaambizana wenyewe kwa wenyewe: Apishaneni kwa jina la Mwenyezi Mungu, kwamba kwa yakini tutamshambulia yeye na ahali zake, na tutawauwa. Kisha tutamwambia jamaa yao wa damu kwamba sisi hatukayaona mauwaji yake wala ya ahali zake. Na hakika sisi ni wasema kweli kwa haya tuliyo yataja.
Rudi kwenye Sura

50. Walipanga kumuuwa Saleh na ahali zake, na Mwenyezi Mungu nyuma yao kapanga kumwokoa Nabii wake na ahali zake, na kuwateketeza wao, na hali wao hata hawatambui.
Rudi kwenye Sura

51. Ewe Nabii! Hebu tazama vipi yalikuwa matokeo ya mipango yao na mipango yetu. Sisi tuliwaangamiza wote hao wao na kaumu yao.
Rudi kwenye Sura

52. Na hebu yatazame mabaki yao. Utakuta nyumba zao zimeanguka, zimevurugika, kwa sababu ya udhalimu wao na kufru zao, na kumtakia shari Nabii wao. Hakika kwa walio fanyiwa kina Thamud ipo Ishara kwa watu wanao ujua uwezo wetu na wakawaidhika.
Rudi kwenye Sura

53. Na Sisi tukakiokoa kikundi kilicho muamini Saleh kutokana na hilaki hii, na wakawa wanao gopa kuziacha amri zake.
Rudi kwenye Sura

54. Ewe Nabii! Mtaje Lut'i na khabari zake pamoja na kaumu ya watendao uchafu, pale alipo waambia: Je! Mnafanya dhambi hizi ambazo zimepita hadi ya uchafu na kinyume na maumbile, na hali nyinyi mnaona na mnaangalia uovu wa haya mliyo yashikilia?
Rudi kwenye Sura

55. Hivyo inaelekea katika nadhari ya akili zenu na maumbile kuwaingilia wanaume kwa matamanio yenu, na mkwawacha wanawake? Ama kweli nyinyi mmesibiwa na upumbavu na ujinga wa kufudikiza, hata imekuwa hamwezi tena kuteuwa baina ya kiovu na chema.
Rudi kwenye Sura

56. Haikuwa jawabu ya watu wake alipo wakataza ila ni kusema: Mtoleeni mbali Lut'i na wafwasi wake katika mji huu. Kwani wao wanajitakasa hawataki kushirikiana nasi katika haya tuyatendayo.
Rudi kwenye Sura

57. Basi Sisi tukamwokoa yeye na ahali zake na ile adhabu walio pelekewa wale watu, isipo kuwa mkewe. Mwenyezi Mungu alimkadiria awe na walio baki nyuma ili apate kuangamia kwa adhabu pamoja na makafiri.
Rudi kwenye Sura

58. Na Sisi tukawanyeshea mvua hao mafisadi, mvua ya adhabu na nakama. Ilikuwa mvua ya kuwahiliki walio onywa kuwa watapata adhabu chungu, na wala wasisikie.
Rudi kwenye Sura

59. Ewe Mtume! Sema: Hakika mimi namhimidi Mwenyezi Mungu na namsifu Yeye peke yake. Na namwomba Mwenyezi Mungu salama na maamkio  kwa waja wake alio wateuwa kwa kuwapa Ujumbe wake. Na ewe Mtume! Waambie washirikina: Je! Kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, Aliye Mpweke,  ni bora kwa mwenye kuamini, au kuabudu masanamu mnayo mshirikisha naye, nayo hayawezi kukudhuruni wala kukufaeni?
Rudi kwenye Sura

60. Bali, ewe Mtume, waulize: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yake, na akakuteremshieni kutoka mbinguni mvua yenye manufaa, na kwa hiyo akakuotesheeni bustani nzuri zenye kupendeza. Msingeli weza nyinyi kuiotesha miti yake ya namna mbali mbali, na rangi mbali mbali, na matunda mbali mbali! Mipango hii iliyo umana sawa katika uumbaji inathibitisha kuwa hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu. Lakini makafiri ni watu walio potoka wakaiacha Haki na Imani, na wameelekea kwenye upotovu na ushirikina.
Rudi kwenye Sura

61. Bali waulize, ewe Mtume: Nani aliye itengeneza ardhi hata ikafaa   kukaliwa na watu wakatulia humo, na akaumba mito kati yake, na juu yake akaumba milima kuizuilia isiyumbe yumbe, na akayatenganisha maji matamu na maji ya chumvi hata yasichanganyike? Hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye  Mwenye kuumba peke yake. Lakini wengi wa watu hawanafiiki na ujuzi wa Haki kama ilivyo. Wamekuwa kama kwamba hawajui kitu.
Rudi kwenye Sura

62. Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye muitikia aliye shikwa na shida katika maombi yake, pale anapo shikwa na shida, akamtegemea Mwenyezi Mungu kwa unyonge na unyenyekevu, naye akamwondolea huyo mtu karaha iliyo msibu, na akakufanyeni warithi wa walio kutangulieni katika nchi? Hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu wa kukupeni neema zote hizi. Lakini nyinyi makafiri, ni kuchache kabisa kuwaidhika kwenu.
Rudi kwenye Sura

63. Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye waongoza katika nyendo za katika giza la usiku katika safari za nchi kavu na baharini?  Na nani anaye zipeleka pepo zinazo bashiria mvua, nayo ni rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu anaye fanya hayo? Mwenyezi Mungu Subhanahu ametakasika kuwa na mshirika.
Rudi kwenye Sura

64. Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye anzisha uumbaji tangu mwanzo, na kisha baada ya kupotea kwake akaurejesha kama ulivyo kuwa? Na nani anaye kuteremshieni riziki kutoka mbinguni, na akaitoa kwenye ardhi? Hakuna mungu pamoja na Mwenyezi Mungu atendaye hayo. Sema, ewe Mtume, kuwatahayarisha na kuwakanya: Kama nyinyi mnaye mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu basi tupeni hoja ya hayo, ikiwa mnadai kuwa nyinyi ni wasema kweli. Na wala hayataweza kuwa hayo kwenu.
Rudi kwenye Sura

65. Sema, ewe Mtume: Hakika mwenye kutenda yote haya peke yake ndiye Yeye Subhanahu  aliye tengeka peke yake kwa kuyajua mambo ya ghaibu yalioko mbinguni na duniani. Na Yeye huyo ndiye Mwenyezi Mungu wa pekee. Wala watu hawajui wakati gani watafufuliwa kutoka makaburini kwao kwa ajili ya kuhisabiwa na kulipwa.
Rudi kwenye Sura

66. Ujuzi wao wa Akhera umefuatana na ujinga, na huo ukawapelekea kuitilia shaka. Nao wamekuwa vipofu hawaitambui Haki katika jambo lolote, kwa sababu upotovu umefisidi fahamu zao.
Rudi kwenye Sura

67. Wakasema makafiri kwa kukanya kufufuliwa: Hivyo sisi tukisha kuwa mchanga, na ikisha oza miili yetu na ya baba zetu walio tutangulia, ndio tutarejeshwa tutolewe upya tuwe wahai?
Rudi kwenye Sura

68. Muhammad ametuahidi kuwa tutafufuliwa, kama Mitume walio tangulia walivyo waahidi baba zetu. Ingeli kuwa hayo ni kweli, basi yangeli kwisha kuwa. Haya si chochote ila ni uwongo tu wa watu wa kale.
Rudi kwenye Sura

69. Ewe Mtume! Waambie: Tembeeni duniani, na mtazame mabaki ya yaliyo wapata walio kadhibisha, nayo ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Huenda labda mkayazingatia haya, na mkaikhofu adhabu ya Akhera.
Rudi kwenye Sura

70. Ewe Mtume! Usiwahuzunukie makafiri wasio kufuata. Kwani kwa hakika waajibu wako ni kufikisha Ujumbe tu. Wala usiwe na dhiki kifuani mwako kwa sababu ya hila zao na vitimbi vyao. Kwani hakika Mwenyezi Mungu atakupa ushindi juu yao.
Rudi kwenye Sura

71. Na makafiri wanafanya ukomo wa juhudi yao kukanusha, na wanaihimiza adhabu kwa kusema: Lini, basi, itakuwa hiyo adhabu ambayo mnatutishia kuwa itakuja, ikiwa nyinyi mnasema kweli kuwa adhabu itawashukia wanao kanusha?
Rudi kwenye Sura

72. Ewe Mtume! Sema: Huenda ikakukuteni, na imekukaribieni baadhi ya adhabu mnayo ihimiza.
Rudi kwenye Sura

73. Na hakika Mwenyezi Mungu Mola wako Mlezi, ewe Mtume, ni Mwenye neema na hisani kwa watu wote. Na katika rehema zake ni kuakhirisha hiyo adhabu kwa hao wanao kadhibisha. Lakini watu wengi hawaelewi fadhila za Mwenyezi Mungu wala hawamshukuru.
Rudi kwenye Sura

74. Ewe Mtume! Hakika Mwenyezi Mungu, Mola wako Mlezi, hapana shaka anajua kila wanalo lificha na wanalo litangaza, ikiwa maneno au vitendo viovu. Naye atakuja walipa kwayo.
Rudi kwenye Sura

75. Na hapana kilicho fichikana cha ghaibu, na kiwe kidogo vipi au duni, mbinguni au katika ardhi ila Mwenyezi Mungu anakijua, na amekidhibiti katika Kitabu cha Haki kilioko kwake.
Rudi kwenye Sura

76. Hakika Kitabu hiki alicho teremshiwa Muhammad kinawawekea wazi Wana wa Israili ukweli wa yaliyo kuja katika Taurati, katika mambo ya itikadi na hukumu na hadithi. Na kinawarudisha kwenye kweli katika mambo waliyo khitalifiana kwayo.
Rudi kwenye Sura

77. Hakika Kitabu hichi ni Uwongofu wa kuokoa watu wasipotee, na ni Rehema ya kuwakinga na adhabu wote wenye kukiamini.
Rudi kwenye Sura

78. Ewe Mtume! Hakika Mola wako Mlezi atawapambanua watu wote Siku ya Kiyama kwa uadilifu wake. Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, basi hapana wa kuipinga hukumu yake. Yeye ni Mjuzi wa kila kitu, basi mbele yake kweli haiwezi kuchanganyika na uwongo.
Rudi kwenye Sura

79. Basi, ewe Mtume, mtegemezee mambo yako Mwenyezi Mungu, na shikilia wito wako kwa kuamini kuwa utashinda tu, kwa sababu wewe uko juu ya Haki iliyo wazi, na mapuuza ya makafiri kukupuuza wewe hakutakudhuru kitu.
Rudi kwenye Sura

80. Ewe Mtume! Hakika wewe huwezi kuwaongoa hao, kwani hao ni kama maiti kwa kuto tambua kitu, na kama viziwi kwa kutosikia. Basi hao hawako tayari kuusikia wito wako kwa vile walivyo shikilia kukupuuza.
Rudi kwenye Sura

81. Na wala huwezi kuwaongoa kwenye Haki wale ambao wamepofuka kuona kwao na kutambua kwao. Na huwezi kumfanya asikie ila mwenye kukubali kuziamini Ishara zetu. Hao ndio wenye kut'ii na wenye kuitikia.
Rudi kwenye Sura

82. Na itapo karibia kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu kuileta Saa ya Kiyama na kuwateremshia makafiri adhabu, Mwenyezi Mungu atawatolea watu mnyama kwenye ardhi atakaye waambia miongoni mwa atakayo sema: Hakika makafiri walikuwa hawaiamini miujiza yetu yote, na pia Siku ya Mwisho. Na hayo waliyo kuwa wakiyakanusha sasa yamekwisha kuwa. Na hichi basi kitisho cha hiyo Saa na yanayo fuatia!
Hii ndio tafsiri ya Aya hii kwa dhaahiri ya matamko yake. Na zipo tafsiri mbili nyengine ambazo za hii Aya zinazo weza kuwa: Kwanza ni kuwa makusudio ya "Dabbah" ni yeyote aendaye "yadibbu",  katika watu au wengineo. Na hapa inachukuliwa kuwa ni watu, watao kuja kabla ya Kiyama.  Na maana yake ni kuwa ikiwateremkia kauli juu yao na adhabu ikathibiti watakuja makundi ya Waumini wakiwaendea, wakienea kote kote, wakizitikisa nguzo za ukafiri. Tafsiri ya pili neno hilo "Dabbah" makusudio yake ni watu waovu, ambao kwa ujinga ni kama wanyama, kama alivyo sema Al As'fahan katika Muqarrarat yake. Na maana yake ni kuwa ikikaribia Siku ya Kiyama, uovu na ufisadi utazidi, na Kiyama wanacho kikanusha makafiri ndio kitakuja. Na hiyo kauli itakuwa, nayo si kauli ya kutamkwa kwa mdomo, lakini kwa kuwa hali yenyewe itakuwa hivyo ni kama iliyo semwa, kama maoni yaliyo kwisha tangulia.
Rudi kwenye Sura

83. Na ewe Mtume! Kumbuka siku tutapo wakusanya kutoka kila kundi la wenye kukadhibisha Ishara zetu, nao ni hao waongozi wanao fuatwa. Basi hao watachungwa wawe mbele ya kaumu zao kuendea hisabu na malipo.
Rudi kwenye Sura

84. Na pale watakapo simama mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabu, atasema Subhanahu kuwaambia kwa kuwadhili na kuwabinya:  Nyinyi mlizikadhibisha Ishara zangu zote, na mkazikataa bila ya kuzingatia wala kufahamu. Na khasa mlikuwa mkitenda nini nanyi hamkuumbwa kwa upuuzi?
Rudi kwenye Sura

85. Na adhabu itawateremkia kwa sababu ya kujidhulumu nafsi zao kwa ukafiri. Basi watakuwa hawawezi kujilinda wala kutaka udhuru.
Rudi kwenye Sura

86. Bila ya shaka wameshuhudia kuwa Mwenyezi Mungu ameufanya usiku ili wapate kupumzika, na akaufanya mchana una mwangaza, wapate kushughulikia kutafuta maisha yao. Hakika katika hayo zipo dalili wazi za Ungu wa Mwenyezi Mungu, na Upweke wake, kwa watu wanao zingatia wakaamini.
Rudi kwenye Sura

87. Na taja, ewe Mtume, Siku atapo puliza Israfil baragumu  kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na watapo ingiwa kiwewe walioko katika mbingu na katika ardhi kwa kitisho cha mpulizo huo, isipo kuwa huyo ambaye Mwenyezi Mungu atamtuliza na akamhifadhi na kitisho. Na  viumbe vyote watakuja kwa Mola wao Mlezi nao ni madhalili.
Rudi kwenye Sura

88. Na unaiona, ewe Mtume, milima na unadhani haitaharaki imetulia tu, lakini kwa hakika inakwenda mbio kama mawingu. Na haya ni katika uundaji wa Mwenyezi Mungu aliye umba kila kitu na akakizua. Hakika Yeye, Subhanahu, ni Mwenye kutimia ujuzi wake kwa yote wayatendayo watu, ya ut'iifu na maasi. Naye atawalipa kwayo.
"Na unaiona milima unaidhunia imetulia; nayo inakwenda kama mwendo wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza vilivyo kila kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo." Aya hii inathibitisha kuwa vitu vyote vinavyo fuata mvutano wa ardhi, kama milima, bahari, na funiko la anga n.k. vinashirikiana na dunia katika mzunguko wake wa kila siku juu ya msumari-kati wake, na mzunguko wake wa kila mwaka kulizunguka jua.   Lakini mzunguko huu hauonekani. Ni kama kwenda kwa mawingu angani.
Wanao tazama wanayaona, lakini hawasikii sauti yao, wala hawayagusi. Inaonyesha Aya hii tukufu kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliye tukuka, ameumba ulimwengu na mipango yake ya kuiendeshea. Naye ni Muweza wa kuifanya hii dunia imetulia tu haizunguki juu ya msumari-kati wake, au akaifanya kuzunguka juu ya msumari-kati wake sawa sawa na kuzunguka kwake kulizunguka jua. Na kwa hivyo ingeli kuwa nusu ya dunia imo kizani totoro kwa muda wa miezi sita, na kwa muda wa miezi sita ikawa nusu ya pili imo katika mwangaza moja kwa moja wa mchana. Na haya yangeli pelekea kuharibika mizani ya joto katika dunia yote. Na kwa hivyo uhai ulioko ungeli toweka duniani. Na Mwenyezi Mungu, Subhanahu wa Taa'la, ndiye aliye panga mpango huu uliopo kwa rehema yake na huruma zake kwa waja wake.
Na juu ya kuwa Aristakhoris, mtaalamu wa ilimu ya falaki wa Iskandaria (Alexandria) katika Misri, aliandika (310-230 K.K.) juu ya kuzunguka dunia wenyewe kwa wenyewe, maandishi haya ya kisayansi ya kale yalikuwa hayajawafikia Waarabu wakati wa Mtume Muhammad s.a.w. au kabla yake. Bali wa mwanzo wa kuashiria mambo haya katika wao alikuwa Albiruni katika mwaka 1000 B.K. (Baada ya Kuzaliwa Nabii Isa), baada ya kuingia kufasiriwa vitabu vya ilimu za zamani kwa lugha ya Kiarabu ulio kuweko katika enzi za Banul Abbas. Basi kutokea haya kwa ulimi wa Mtume Muhammad s.a.w. ambaye aliye kuwa hajapata ilimu hiyo, ni dalili kuwa haya yalifunuliwa kwake na Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura

89. Kila mwenye kuleta wema katika dunia, nayo ni Imani na usafi wa ut'iifu, atapata huko Akhera thawabu kubwa kabisa kwa ajili ya aliyo yatanguliza. Na wenye mema haya watasalimika na khofu na kufazaika Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura

90. Na kila mwenye kuleta uovu katika dunia - nao ni shirki na maasia - na akafa na hayo, basi malipo ya kundi hili ni kuwa Mwenyezi Mungu atawasukumiza juu ya nyuso zao katika Moto, na wataambiwa hapo kwa kuwatahayarisha: Hakika hii leo hamlipwi ila kwa sababu ya shirki yenu na maasi yenu.
Rudi kwenye Sura

91. Ewe Mtume! Waambie watu: Sikuamrishwa nimuabudu yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa mji wa Makka aliye utukuza, na akaufanya mtakatifu wenye amani, usio faa kumwagwa damu ndani yake, wala kuwindwa wanyama wake, wala kukatwa miti yake. Na vitu vyote viliomo ulimwenguni ni vya Mwenyezi Mungu kuvimiliki na kuvitawala, na mimi nimeamrishwa niwe katika wanao mnyenyekea Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura

92. Na nimeamrishwa nidumishe kuisoma Qur'ani, kwa ibada, na kuzingatia, na kuwaitia watu wafuate yaliomo humo. Basi mwenye kuongoka, akaiamini, na akakufuata wewe, basi kheri ya hayo na malipo yake ni kwa nafsi yake. Na mwenye kupotea asiifuate Haki, na asikufuate wewe, mwambie: Hakika mimi ni Mtume, naonya, na nafikisha Ujumbe tu.
Rudi kwenye Sura

93. Na sema, ewe Mtume: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu kwa neema ya Unabii na Uwongofu. Mwenyezi Mungu atakuonyesheni hapa duniani athari za uwezo wake, na Akhera atakuonyesheni ukweli wa aliyo kwambieni, na mtayajua vilivyo. Wala Mwenyezi Mungu hashindwi kukuhisabieni wala haghafiliki na vitendo vyenu.
Rudi kwenye Sura