') //-->
1. Mambo ya Mwenyezi Mungu yametukuka, na kheri yake imezidi. Yeye ndiye aliye iteremsha Furqani, yaani Qur'ani, ya kufarikisha baina ya kweli na uwongo juu ya mja wake, Muhammad s.a.w., ili awe mwonyaji na mwenye kuifikisha hiyo Qur'ani kwa walimwengu wote.
Rudi kwenye Sura
2. Yeye Subhanahu ndiye peke yake aliye miliki mbingu na ardhi, aliye takasika na haja ya kuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika wowote katika ufalme wake. Na Yeye kaumba kila kitu na akakipima kwa kipimo baraabara kwa sharia zake ili kiweze kutimiza waajibu wake kwa nidhamu.
"Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo." Ilimu ya sayansi ya sasa imethibitisha kuwa vitu vyote vinakwenda kwa mujibu wa hukumu za uumbaji wake, na maendeleo yake namna mbali mbali kwa kufuata mpango madhubuti ambao hapana mwenye uwezo juu yake ila Muumbaji mwenye uwezo Mwenye kuanzisha kila kitu. Kwani katika kuwa kwake imebainika kuwa vitu vyote viumbe vyote na vinga khitalifiana umbo lake na sura yake kwa hakika vinatokana na madda chache za asli za kuhisabika, na hisabu ya madda hizo (elements) zinakaribia mia, nazo ni 96 zinazo juulikana mpaka sasa. Nazo zina khitalifiana kwa sifa zao za maumbile (physically ) na za Al Kimyaa (Chemically), na pia katika uzito wake wa chembe (Atomic Weight). Zinaanza kwa madda asli (element) Nambari 1. Nayo ni Hydrogen yenye Atomic weight 1, na kuishia na element ya nambari 96, Borium, ambayo atomic weight yake bado haijuulikani. Na element ya mwisho katika sayansi ni Uranium na atomic weight yake ni 238.57. Na hizi elements hujengeka na kufanyika Compounds kwa mujibu wa kanuni madhubuti zisio weza kuepukwa. Hali kadhaalika mimea na wanyama. Kila mmoja wao amegawika katika koo na makundi na namna (orders, families, species and sub-species) zinazo geuka sifa zake kwa madaraja ya viumbe vilivyo hai mpaka kuishia viumbe vyenye Khalaya au Cell moja (unicellular) kama microbes mpaka viumbe vyenye cells nyingi (multi- cellular) mpaka kufikia binaadamu, naye ndiye aliye kamilika kuliko wote. Na kila namna ya hizi sifa maalumu zinarithika katika kundi kizazi baada ya kizazi. Na yote haya yanakwenda kufuata kanuni na mipango iliyo thibiti madhubuti inayo onyesha kwa uwazi utukufu wa Mwenye kuumba na uwezo wake. Ametakasika, Subhanahu na ametukuka na hao wanao mshirikisha naye.
Rudi kwenye Sura
3. Na juu ya yote hayo makafiri wakaacha kumuabudu Yeye, wakenda kuchukua miungu mingine kuiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, katika masanamu, na nyota, na watu. Na hao hawanalo waliwezalo kuliumba, bali wao ni viumbe vya Mwenyezi Mungu. Wala hawawezi kujikinga nafsi zao na madhara, wala kujiletea kheri. Wala hawawezi kumfisha yeyote wala kumhuisha, wala kuwafufua maiti kutoka makaburini kwao. Na kila asiye miliki lolote katika hayo basi hastahiki kuabudiwa. Na mjinga wa kutupwa anaye waabudu. Mwenye kustahiki kuabudiwa ni yule Mwenye kumiliki haya yote.
Rudi kwenye Sura
4. Makafiri wakaitia ila Qur'ani, wakasema kuwa hiyo ati ni uwongo kauzua Muhammad mwenyewe, na akamsingizia Mwenyezi Mungu. Na wakamsaidia baadhi ya jamaa wengine katika Ahli-l-Kitab. Basi hawa makafiri wamefanya dhulma kwa kauli yao hiyo katika hukumu na kuishambulia Haki, wakaleta uzushi usio kuwa na ushahidi wowote. Kwani hao wanao waashiria katika Ahli-l- Kitab lugha yao hata si Kiarabu. Na Qur'an ni kwa lugha ya Kiarabu fasihi.
Rudi kwenye Sura
5. Wakaisema Qur'ani pia kuwa ati ni uwongo walio andika watu wa kale katika vitabu vyao, kisha akawataka wao wamuandikie na wamsomee asubuhi na jioni mpaka ahifadhi na apate kusema naye hayo hayo.
Rudi kwenye Sura
6. Ewe Nabii! Waambie: Hakika Qur'ani ameiteremsha Mwenyezi Mungu ambaye anazijua siri zilizo fichikana katika mbingu na ardhi. Na ameziweka katika Qur'ani ya muujiza kuwa ni dalili ya kwamba hiyo ni Ufunuo wake Subhanahu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa maghfira na rehema, anawasamehe wenye kuasi pindi wakitubu, wala hafanyi haraka kuwaadhibu.
Rudi kwenye Sura
7. Wakamkejeli Muhammad, wakasema: Kitu gani kinacho mtengua huyu anaye dai kuwa ni Mtume, hata anakula chakula kama tulavyo sisi, na anazururuka masokoni kutafuta maisha kama watu wengine? Angeli kuwa ni Mtume Mwenyezi Mungu angeli mtosheleza kwa hayo, na yeye angeli mwomba Mola wake Mlezi amteremshie Malaika kutoka mbinguni amsaidie katika uwonyaji na kufikisha Ujumbe, na amsadikishe katika wito wake, tupate sisi kumuamini.
Rudi kwenye Sura
8. Na hebu lau angeli mtaka amtosheleze chakula cha kutosha asihitajie kuzunguka masokoni, akamtupia khazina kutoka mbinguni ya kutumia, au akamjaalia na bustani ya kumlisha matunda yake? Na wakubwa wa makafiri walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri, wenye kuwapotoa watu wasimuamini Muhammad, na wenye kufanya hila za kuwaingiza shaka Waumini, walisema: Nyinyi hamumfuati ila huyu mtu aliye zugwa akili yake, basi anabwabwatika bila ya kuwa na hakika.
Rudi kwenye Sura
9. Hebu angalia, ewe Nabii! Vipi wanavyo kupigia mifano hawa! Mara wanakupigia mfano wa mwenye kurogwa, mara nyengine kuwa ati ni mwendawazimu, mara ya tatu kuwa ni mwongo, na mara yane kuwa unaipokea Qur'ani kutokana na wasio kuwa Waarabu. Hao kwa hayo hakika wameipotea njia ya haki, na kuhojiana kulio sawa. Basi hawaitambui njia ya kufikilia yote hayo.
Rudi kwenye Sura
10. Mwenyezi Mungu ametukuka, na izidi kheri yake! Yeye ndiye ambaye pindi akitaka atakujaalia duniani bora kuliko hayo wanayo pendekeza wao. Kwa Akhera Yeye amekwisha kujaalia kama alivyo kuahidi, nayo ni mabustani mengi yapitayo mito pembezoni mwake, na baina ya miti yake, na majumba ya fakhari madhubuti.
Rudi kwenye Sura
11. Na kwa hakika hawa wamepinga kila Ishara. Kwani wao wamekanusha kufufuliwa, na Siku ya Kiyama. Nao kwa hivyo wanayatia ila matakwa haya ili kuwageuza watu washughulikie upotofu wao. Na Sisi tumekwisha waandalia wanao ikanusha Siku ya Kiyama Moto wenye kuwaka vikali mno.
Rudi kwenye Sura
12. Wakiuona Moto, na huo Moto ukawaona, wataisikia sauti yenye hasira, yenye hamu kuwateketeza. Na katika hayo ni mfano wa mingurumo inayo toka kifuani mwa aliye kasirika kuwa ni alama ya ukali alio nao.
Rudi kwenye Sura
13. Na watapo tupwa katika pahali pembamba kwa kulingana na unene wao, nao wamefungwa pingu mikono yao kwenye shingo zao, watapiga kelele kuhimiza wateketezwe upesi upesi ili wapate kupumzika na kitisho cha adhabu.
Rudi kwenye Sura
14. Wataambiwa kwa kuwahizi na kuwakejeli: Msitake kuangamia mara moja tu, bali takeni muangamie mara nyingi. Hamtopata kusalimika na hayo mliyo nayo. Na hakika namna ya adhabu zao ni nyingi.
Rudi kwenye Sura
15. Ewe Nabii! Waambie makafiri: Je! Marejeo haya waliyo ahidiwa makafiri ni bora au Pepo yenye kudumu neema zake, na ambayo wameahidiwa Waumini, wachamngu, kuwa itakuwa yao kama ndio malipo na marejeo ya kwendea baada ya kufufuliwa na kuhisabiwa?
Rudi kwenye Sura
16. Humo watapata wakitakacho, wataneemeshwa kwa neema za daima, zisio katika. Na neema hizi ni ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao. Walimwomba Mola wao Mlezi itimie, naye akawaitikia kwa walilo liomba; kwani ahadi yake hayendi kinyume.
Rudi kwenye Sura
17. Na taja, kwa ajili ya mawaidha, Siku ambayo Mwenyezi Mungu atawakusanya washirikina kwa ajili ya hisabu katika Siku ya Kiyama, pamoja na hao ambao walikuwa wakiwaabudu duniani badala ya Mwenyezi Mungu, kama Yesu (Isa), Ezra (Uzair) na Malaika. Mwenyezi Mungu atawauliza hao waabudiwa: Je! Ni nyinyi ndio mlio wapoteza waja wangu, mkawaamrisha wakuabuduni, au wao wenyewe ndio walio potea Njia kwa khiari yao, wakakuabuduni?
Rudi kwenye Sura
18. Jawabu yao itakuwa: Umetakasika, na Umetukuka! Haikutafalia sisi kabisa tumtake mlinzi badala yako atunusuru na aangalie mambo yetu. Basi itakuwaje juu ya haya tumtake yeyote atuabudu sisi badala yako Wewe? Lakini sababu ya ukafiri wao hawa ni kuwa uliwastarehesha kwa muda mrefu duniani, wao na baba zao. Hayo yakawapandisha kichwa, wakasahau kukushukuru, na kukuelekea Wewe tu kwa ibada. Basi wakawa kwa jeuri hiyo na ukafiri huo wanastahiki kuangamizwa.
Rudi kwenye Sura
19. Wataambiwa wenye kuabudu, washirikina: Wamekukadhibisheni hao mlio kuwa mkiwaabudu, ambao mkidai kuwa wamekupotezeni. Basi nyinyi leo mnarejea kwenye adhabu. Hamna hila ya kuepukana nayo; wala hamyapati manusura ya kukutoeni. Na wajue waja wote kwamba mwenye kudhulumu kwa ukafiri na uasi kama walivyo fanya hao basi Sisi tutawaadhibu adhabu kali.
Rudi kwenye Sura
20. Na ikiwa washirikina wanakutia ila ewe Nabii, kwa kula kwako chakula, na kwenda kwako masokoni kwa ajili ya kazi na kuchuma maisha, basi huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa Mitume wake walio kuja kabla yako. Hatukumtuma yeyote kati yao ila alikuwa akila chakula, na anakwenda kwenda masokoni. Na enyi watu! Tumewafanya baadhi yenu wawe ni mitihani kwa wenginewe. Na mafisadi wanafanya hila kuziba Njia ya Uwongofu na Haki kwa namna mbali mbali. Basi, enyi Waumini, mtavumilia juu ya Haki yenu, na mtaishikilia Dini yenu, mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake kwa ushindi? Subirini! Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvizunguka vitu vyote, na atamlipa kila mtu kwa kitendo chake.
Rudi kwenye Sura
21. Na wakasema wanao kataa kufufuliwa na wala hawatumai kuwa yapo malipo kwa vitendo vyao: Kwa nini hatuteremshiwi Malaika wa kukuunga mkono, au Mwenyezi Mungu akajionyesha kwetu na akatwambia kwamba kweli Yeye kakutuma? Kiburi kimewajaa katika nafsi zao, na wamepita mpaka katika udhalimu na ujabari!
Rudi kwenye Sura
22. Siku ya Kiyama watawaona Malaika kama walivyo tamani, na hayo yatakuwa ni sababu ya kitisho kwao wala si jambo la kuwafurahisha. Watatafuta kujilinda nao, kama walivyo kuwa wakitafuta kujilinda na vinavyo watisha duniani.
Rudi kwenye Sura
23. Na Siku ya Kiyama tutawaletea waliyo yatenda katika mambo ya kuonyesha wema kwa dhaahiri na hisani katika dunia, na Sisi tutayafanya yaondokee patupu, na tutawaharimisha thawabu zake, kwa kuwa yamekosa Imani ambayo ni dharura ipatikane ili vitendo vitiwe maanani.
Rudi kwenye Sura
24. Watu wa Peponi Siku ya Kiyama ndio watao kuwa na utulivu bora, na mashukio mazuri, na makaazi ya starehe, kwa sababu hii ni Pepo walio andaliwa Waumini, si Moto walio andaliwa makafiri.
Rudi kwenye Sura
25. Ewe Nabii! Itaje Siku itapo pasuka mbingu na ikafunguka, na yakadhihiri kati yake mawingu, na Malaika wakashuka khasa kwa yakini.
Rudi kwenye Sura
26. Katika siku hii mali ya watu wenye mali yataharibika, madai yao wanao jidai yatakatika, na Ufalme wote utabaki ni wa Arrahmani , Mwingi wa Rehema, peke yake. Na itakuwa siku ya shida ngumu mno kwa makafiri.
Rudi kwenye Sura
27. Siku ya Kiyama mwenye kujidhulumu nafsi yake atajiuma mikono yake kwa hasira na majuto kwa ukafiri wake na kumwendea kinyume Mtume, na kwa kutamani atasema: Laiti lau ningeli mfuata Mtume, nikaifuata njia ya kwendea Peponi, na nikaiepuka njia ya kwendea Motoni!
Rudi kwenye Sura
28. Na atasema kwa kujuta kuwafuata walio mpoteza: Laiti ningeli kuwa sikumsadiki fulani, ambaye nimemwachia aniongoze.
Rudi kwenye Sura
29. Rafiki huyu amenibaidisha na Ukumbusho, Dhikr, kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kuikumbuka Qur'ani baada ya kwisha kuwa ni nyepesi kwangu. Ndio hivi Shetani anavyo mkhini binaadamu, na kumtokomeza kwenye hilaki yake.
Rudi kwenye Sura
30. Na Mtume alisema akimshitakia Mwenyezi Mungu kwa taabu anazo zipata kwa watu wake: Hakika hawa wameiacha Qur'ani na wameihama, na wameshikilia katika kuipuuza, na kuifanyia inda na uadui.
Rudi kwenye Sura
31. Kama tulivyo wajaalia watu wako, ewe Muhammad, wanavyo kufanyia uadui na kukukadhibisha, basi kadhaalika tulimjaalia kila Nabii ana maadui miongoni mwa wakosefu, wanao mfanyia uadui na wanaupinga wito wake. Na Mwenyezi Mungu atakunusuru, na atakuongoa mpaka uwashinde. Na Yeye anakutosha kwa uwongofu na kukunusuru.
Rudi kwenye Sura
32. Na makafiri kutaka kuikebehi Qur'ani walisema: Kwa nini haikuteremshwa kwa mara moja? Na Sisi hakika tumeiteremsha kwa mapande mapande ili moyo wako uthibiti kwayo kwa raha yako na ili uihifadhi. Na tumeisoma, yaani tumeigawa kwa Aya, au tumeisoma kwa ulimi wa Jibril, kidogo kidogo kwa utulivu na upole.
Rudi kwenye Sura
33. Na wala hawakujii na upinzani dhaifu, ila nasi tunakuletea Haki ya kubainisha, na bora ya maelezo.
Rudi kwenye Sura
34. Na walio ukataa Ujumbe wako watabururwa kupelekwa Motoni kifudifudi na madhalili. Hao ndio watu wa chini kabisa kwa cheo, na ndio walio zama mno katika upotovu.
Rudi kwenye Sura
35. Na Mtume s.a.w. anapozwa kwa yaliyo wapata Mitume wa kabla yake. Hakika Sisi tulimteremshia Musa Taurati, na tukamkalifisha afikishe Ujumbe wetu, na tukamuunga mkono kwa ndugu yake Harun, awe waziri wake na msaidizi katika kazi yake.
Rudi kwenye Sura
36. Tukasema: Nenda wewe na nduguyo kwa Firauni na watu wake. Tukamuunga mkono kwa miujiza inayo onyesha ukweli wake. Hawakumuamini, wakamkadhibisha. Mwisho wao ukawa tukawateketeza na tukawafutilia mbali!
Rudi kwenye Sura
37. Hali kadhaalika kabla ya Musa tuliwafanyia kaumu ya Nuhu walipo mkadhibisha, na aliye mkanusha Mtume mmoja basi amewakanusha Mitume wote. Nao tukawazamisha katika tufani, na tukawafanya wawe ni zingatio kwa watu. Na tukawajaalia hao na kila mshirikina kupata adhabu chungu Akhera.
Rudi kwenye Sura
38. Na kadhaalika tuliwahiliki A'di na Thamudi na watu wa Rass (1) walipo wakanusha Mitume wao. Na tuliziangamiza kaumu nyingi baina ya kaumu ya Nuhu na baina ya A'di, yakawapata malipo ya wenye kudhulumu.
(1) Rass, kama ilivyo elezwa katika Mufradaat ya Raaghib Al-As'fahani, ni bonde, na akatolea ushahidi ubeti wa shairi: (Nao ni bonde la Rass, kama mkono kwa mdomo.) Hao watu wa Rass, kama ilivyo kuja katika Aya tukufu, ni watu walio kuwa wakiabudu masanamu. Mwenyezi Mungu aliwatumia Shuaib. Basi hao ndio walio pelekewa Mtume Shuaib a.s. Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika amewaeleza hao kaumu ya Shuaib kuwa ni Watu wa Vichakani (Al-Aykat), napo ni pahali penye miti mingi panasifika kwa neema, na mara nyengine wanaitwa Watu wa Rass, nalo ni bonde lenye kheri kubwa, kuonesha neema alizo waneemesha Mwenyezi Mungu. Nao wakazikufuru neema za Mwenyezi Mungu, wakaabudu masanamu.
Rudi kwenye Sura
39. Na Sisi tumezionya kaumu zote hizi. Tukawakumbusha mawaidha, na mifano ya kweli yenye manufaa. Lakini hawakuwaidhika. Tukawashika wote kwa kuwaadhibu, tukawahiliki, na tukayabomoa majumba yao mpaka kifusi.
Rudi kwenye Sura
40. Na hawa Makureshi katika safari zao za kwenda Sham wanapita kwenye mji wa kaumu Lut'i, tulio unyeshea mvua ya shari na ovu kabisa, nayo ni mawe ya Motoni. Je! Hawauoni mji huo wakawaidhika kwa yaliyo wafika watu wake? Hakika wao wanauona huo, lakini si kwa macho ya kuwaidhika na kuzingatia. Kwani hawaamini ahadi (za Mwenyezi Mungu) wala kufufuliwa. Wala hawataraji kuwa ipo siku watakuja fufuliwa kwa ajili ya hisabu.
Rudi kwenye Sura
41. Na wakikuona watu hawa hawakuchukulii ila kukufanyia kejeli na maskhara. Na huambiana wao kwa wao: Ndiye huyu aliye mtuma kwetu Mwenyezi Mungu awe ni Mtume, na sisi tumfuate twende nyuma yake?
Rudi kwenye Sura
42. Mtu huyu hakika kajaaliwa kuwa na ufasihi mzuri, na hoja za kuvutia kwa wanao msikia. Na hapana shaka ameweza kuchota katika imani zetu hata alikaribia kututoa kwa miungu yetu tumfuate mungu wake. Lakini sisi tumesimama imara juu miungu yetu na dini yetu. (Mwenyezi Mungu anasema:) Tutakuja wabainishia ukweli wa mambo watapo kuja iona adhabu Siku ya Kiyama, na watajua nani huyo aliye thibiti katika upotovu na makosa.
Rudi kwenye Sura
43. Ewe Mtume! Umeona upotovu wa mwenye kufuata matamanio yake na pumbao lake hata akawa anaabudu mawe ambayo hayadhuru wala hayanafiishi? Na wewe umetumwa uwe mwonyaji na mbashiri, wala hukuwakilishwa kwa imani yao na uwongofu wao.
Rudi kwenye Sura
44. Na hivyo unadhani kuwa wengi wao wanasikia kwa sikio la kufahamu au wanaongoka kwa akili zao? Wamesha tupilia mbali kama walivyo amrishwa na ndoto zao. Wamekuwa kama wanyama wa kufuga, hawanalo linalo washughulisha ila kula, na kunywa, na kustarehe na maisha ya dunia. Wala hawana fikra yoyote baada ya hayo. Bali hali yao ni ovu zaidi kuliko ya wanyama, kwani wanyama huwafuata bwana zao katika yenye kheri nao, na wanayaepuka ya kuwadhuru. Lakini watu hawa wanajitokomeza wenyewe kwenye mambo ya kuwahiliki.
Rudi kwenye Sura
45. Tumesimamisha dalili za Tawhidi, Upweke wa Mwenyezi Mungu, za kuwaongoa wenye akili. Hebu kiangalie kivuli. Mwenyezi Mungu amekitandaza na akakifanya kimetulia mwanzo wa mchana. Kisha tukalipeleka jua likaondoa pahala pake kwa mwako wake. Likawa jua ni kama ndio linaongoza kivuli. Bila ya jua, kivuli kisingeli juulikana. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu ange penda angeli kifanya kivuli kitulie vile vile kimewang'ang'ania watu, na yakawaharibikia maslaha yao na mambo yao.
" Je! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na angeli taka angeli kifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi wake." Aya hii inadhihirisha hima ya Muumba na uwezo wake. Kwani kutandaza kivuli kunaonyesha mzunguko wa dunia na kuinama kwa msumari-kati (axis) wake. Na lau kuwa ardhi, yaani dunia, ingeli tulia tu, haitaharaki kulizunguka jua, na pia ikawa haizunguki wenyewe kwa wenyewe juu ya msumari-kati wake, basi kivuli kingeli tulia, na mwako wa jua ungeli piga juu ya nusu ya dunia, na nusu ya pili ikabaki ni usiku, moja kwa moja. Hayo yangeli leta khitilafu kubwa za baridi na joto, na ingeli pelekea kutoweka uhai kabisa katika dunia. Na kadhaalika ingeli kuwa hii ni hali ya dunia basi kivuli kingeli tulia. Na haya pia yange tokea ikiwa muda wa kuzunguka ardhi juu ya msumari-kati wake ndio muda ule ule muda wa kuzunguka kwake kulizunguka jua, yaani siku moja ikawa sawa na mwaka mzima. Lakini hapana awezaye kufanya hayo isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Haya licha ya kuwa kivuli nafsi yake ni neema miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu aliviumba vitu vyote vyapenyeza mwangaza (transparent) kisingeli kuwapo kivuli, na vitu visingeli pata fursa ya kuwepo ambavyo vinahitajia vivuli.
Rudi kwenye Sura
46. Na kukiondoa kwetu kivuli ni kwa utaratibu, kwa kipimo. Hakukuwa kwa mara moja. Na katika hayo yapo manufaa kwa watu.
Rudi kwenye Sura
47. Na katika Ishara za Tawhidi ni kuwa tumeufanya usiku ni sitara kwa kiza chake, ndani yake wanaingia viumbe ukawazunguka kama inavyo wazunguka nguo kwa mwenye kuivaa. Na tukawatengenezea malazi, ikawa ni mapumziko kupumzika na machofu, na kwa mwangaza wa jua wanazinduliwa watu watafute maisha yao na riziki zao.
Rudi kwenye Sura
48. Na Yeye ndiye aliye zifanya pepo zimtumikie, zikasukuma mawingu, nayo yakawabashiria watu itakuja mvua, ambayo ni rehema itokayo kwake kuwaendea wao. Na hakika Sisi tunateremsha kutoka mbinguni maji safi yanayo safisha kuondoa najisi na uchafu.
"Na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi." Katika Aya hii tukufu Mwenyezi Mungu anawasimbulia watu kwa kuwateremshia maji yaliyo safi kutoka mbinguni. Na Aya hii inafahamisha kuwa maji ya mvua katika asli ya kuumbwa kwake ni maji safi kabisa. Na juu ya kuwa baada yake yanabeba takataka nyingi katika anga, lakini bado yamo katika daraja ya usafi.
Rudi kwenye Sura
49. Tunaiteremsha mvua kwa sababu makulima yapate kumea na kukua, na ardhi ipate kufufuka baada ya kufa kwake, na wanyweshwe watu na wanyama walio umbwa.
Rudi kwenye Sura
50. Na hii Qur'ani tumeibainisha na tumeisarifu, tumeifanya, ili watu wamkumbuke Mola wao Mlezi, na wawaidhike, na watende kwa mujibu wake. Lakini wengi wa watu wanakataa isipo kuwa ukafiri na inda tu.
Rudi kwenye Sura
51. Na lau kuwa tumetaka basi tungeli mpeleka mwonyaji kwenye kila mji. Basi jitahidi na wito wako; na wacha maneno ya makafiri; na tupilia mbali wanayo yaleta.
Rudi kwenye Sura
52. Na endelea na kulingania kwako kwa Haki, na kufikisha Ujumbe wa Mola wako Mlezi. Na wao wakiupinga wito wako, na wakawavamia Waumini basi wapige vita, na kwa hayo pigana Jihadi kubwa.
Rudi kwenye Sura
53. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziendesha bahari mbili, bahari ya maji matamu na bahari ya maji ya chumvi. Na akafanya njia ya kila moja inakaribiana na nyengine. Na juu ya hivyo maji yao hayachanganyikani. Hiyo ni neema na rehema kwa watu.
"Naye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho." Yamkini Aya hii inaashiria neema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kwa kuto changanyika maji ya chumvi yanayo penya kutoka baharini kwenye miamba ya karibu na mwambao, na maji matamu yanayo penya kutoka bara, yasichanganyike kwa ukamilifu na hali nayo yanakutana. Matamu yanakuwa yako juu ya maji chumvi kama kwamba baina yao pana kinga kinacho zuia haya yasiingiane na haya, na kizuizi kizuiacho, yaani kizuizi chembamba tusicho weza kukiona.
Na haya si tu, bali ipo kanuni madhubuti inayo hukumu makhusiano haya, na inayo yahukumu kwa maslaha ya wanaadamu wanao kaa katika maeneo hayo, na maisha yao yanategemea kuwepo hayo maji matamu. Kwani imethibiti kuwa t'abaka ya maji matamu yalioko juu huzidi unene wake kwa mujibu wa kuzidi usawa (level) wa bahari kwa mpango maalumu. Hata inakuwa yawezekana kuhisabu kina cha mwisho cha maji matamu ambayo yamkinika kuyapata. Kwani hiyo ni sawa sawa na kadri ya khitilafu baina ya usawa (level) wa ardhi na usawa wa bahari mara arubaini.
Rudi kwenye Sura
54. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye umba kutokana na manii hawa watu, na akawajaalia wanaume na wanawake walio khusiana kwa nasaba ya kuzaana na kwa ushemeji wa kuoana. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza kwa atakayo, kwani kwa hiyo hiyo manii ameumba namna mbili mbali mbali.
Rudi kwenye Sura
55. Na baada ya Ishara hizi zenye kuonyesha kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anaye stahiki kuabudiwa, na kwamba hapana mungu isipo kuwa Yeye, wanatoka kikundi cha watu kuabudu masanamu yasiyo wafaa wala kuwadhuru. Na hawa kwa kujua kwao haya wanamsaidia Shetani, na yeye anawapoteza. Basi hao inakuwa wanasaidiana katika kuipinga Haki ambayo Mwenyezi Mungu anawaitia.
Rudi kwenye Sura
56. Na ewe Nabii! Huna jukumu ila kufikisha hayo ulio tumwa basi, na kuwabashiria Pepo Waumini, na kuwakhofisha makafiri kwa haya watayo yakuta. Baada ya hayo huna jengine unalo takiwa.
Rudi kwenye Sura
57. Na waambie: Hakika mimi sitafuti kwa huku kukuiteni muufuate Uislamu ujira wowote wala malipo. Ila nilitakalo ni mwongoke na muifuate Njia ya Haki mrejee kwa Mola wenu Mlezi.
Rudi kwenye Sura
58. Na katika mambo yako mtegemee Mwenyezi Mungu Aliye Hai, ambaye hayumkini kufa. Na mtakase na mtukuze kwa kuzisifu neema zake. Na waachilie mbali walio toka kwenye Njia. Kwani Mwenyezi Mungu anawajua vyema, na atawalipa kwa dhambi zao.
Rudi kwenye Sura
59. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao kwa siku sita. Naye ametawala juu ya A'rshi, Kiti cha Enzi, cha Ufalme wote, na madaraka yake yameenea kila kitu. Na Yeye ndiye Mwingi wa Rehema, Arrahman. Na ukitaka lolote katika sifa zake muulize ajuae atakujibu. Naye ni Mwenyezi Mungu Mwenye hikima.
"Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku sita. Kisha akatawala juu ya A'rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Ulize khabari zake kwa wamjuaye." Hizo Siku Sita ni usemi wa Mwenyezi Mungu, Mtukufu Aliye tukuka, kueleza wakati. Na Yeye Mtukufu ndiye Mwenye kujua zaidi kipimo cha hiyo Siku. Na kwa upande wa kiilimu za sayansi kazi ya kuumba ulimwengu unahitaji kupita vipindi na viwango mbali mbali. Na "Mbingu na ardhi na viliomo ndani yake" ni ishara ya vyombo vyote vya mbinguni, nyota, majua, sayari, miezi, mavumbi, gesi za namna mbali mbali, na nishat'i, Energy , na vyote hivyo vinavyo fanya ndio ulimwengu wa duniani na angani. Na kwa kuupanga ulimwengu wote, yaani uumbaji wote, kwa tafsili ya ukamilifu inayo kusanya kila kitu, ndio inaweka wazi, Utawala wa Mwenyezi Mungu, Subhanahu juu ya ulimwengu kwa jumla na kwa tafsili. "Uliza khabari zake kwa ajuaye". Katika kifungu hichi cha Aya hii tukufu pana uwongozi wa kisayansi kutokana na Mwenyezi Mungu kuonyesha dharura ya uchunguzi na utafiti wa mambo yanayo onekana ya uumbaji na mipango yake tuyaangalie ya ndani, ili tujue siri za uweza wa Mwenyezi Mungu katika kuanzisha huu ulimwengu.
Rudi kwenye Sura
60. Na wakiambiwa hawa makafiri: Mnyenyekeeni Arrahmani, Mwingi wa Rehema, na mumuabdu, wao husema: Nani huyo Arrahmani? Sisi hatumjui, hata tumsujudie. Basi tukufuate amri yako tu? Na wanazidi kuwa mbali na kutengeka na Imani.
Rudi kwenye Sura
61. Ametukuka Arrahman, Mwingi wa Rehema, na zimezidi fadhila zake. Ameziumba sayari mbinguni na akazijaalia na vituo vyake vya kupitia, na katika hizo akaumba jua kuwa ni taa yenye mwangaza, na mwezi wenye nuru.
"Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo taa na mwezi unao ng'ara." Aya hii tukufu inaashiria maana za ki-ilimu za sayansi zenye kukusanywa katika mpango wa ulimwengu alio uumba Mwenyezi Mungu, Aliye takasika, Aliye tukuka, na zikazidi fadhila zake. Na sisi tunashuhudia nyota za mbinguni kwa sura ya makundi ambayo takriban hayageuki sura na yangapitiliwa na karne, na Buruuj nayo ndio hayo makundi ya nyota, ni yale yale yanayo pitiwa mbele yake na jua katika mzunguko wake unavyo dhihiri kuizunguka ardhi. Hizo Buruuj ni kama vituo vya jua katika mzunguko wake katika mwaka. Na kila tatu katika hizo huwa ni musimu katika misimu ya mwaka. Nazo kwa kuzitaja moja moja kuanzia msimu wa Rabii' (Spring) unao kuja baina ya siku za baridi na joto, ni kama ifuatavyo kwa majina ya Kiarabu na Kizungu: Alh'aml (Aries, or Ram), Ath-thawr (Taurus), Aljawzaa' (Gemini), Assarat'aan (Cancer), Al Asad (Leo), Assunbulah (Spica), Al Miizaan (Libra), Al-A'qrab (Scorpion), Al Jadyu (Capricorn), Addalwu (Aquarius), Alh'uut (Pisces). Na jua ni moja katika nyota zenye nguvu za kati na kati. Nalo kama nyota zilizo baki lina mwangaza wake mwenyewe wa dhati kwa vituko vya kichembechembe (atomic reaction) vinavyo tokea ndani yake. Basi miale ya jua inayo toka kwenye nguvu hizo huangukia juu ya sayari, na ardhi, na miezi, na vyombo vilio baki vya mbinguni ambavyo havina mwanga wa nafsi yao. Kwa hivyo navyo hutoa nuru. Basi jua ndio Taa inayo waka kwa nafsi yake. Ama mwezi unarudisha nuru ya mwanga wa jua kutokana na uso wake, kama kiyoo. Hakika kwa kusifiwa Jua kuwa ni Taa, na ukasifiwa mwezi kuwa unatoa nuru, ni ishara ya kuwa Jua ndio chanzo cha nguvu, nishati, (T'aaqah, Energy) za joto.
Rudi kwenye Sura
62. Mwingi wa Rehema ndiye aliye ufanya usiku na mchana kufuatana, mmoja nyuma ya mwenzie. Na tumeyapanga haya ili mwenye kutaka akumbuke mpango huu, na ajue hikima ya Mwenyezi Mungu na uweza wake; au apate kushukuru kwa neema hii njema.
Rudi kwenye Sura
63. Na waja wa Mwenyezi Mungu ni wale wanao nyenyekea duniani. Wakitembea katika ardhi wanatembea kwa utulivu na staha. Hali kadhaalika katika mambo yao yote. Na masafihi katika washirikina wakiwasubu wanawaachilia mbali na shani yao, na wanawaambia: Hatuna shani nanyi. Letu sisi ni Assalamu Alaikum!
Rudi kwenye Sura
64. Na wale ambao wanakesha katika ibada na Sala, wakimdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi.
Rudi kwenye Sura
65. Na wale ambao khofu yao inashinda matarajio - nao ndio mwendo wa wachamngu. Basi wanaikhofu adhabu ya Akhera, na hawaachi kumwomba Mwenyezi Mungu awaepusha na adhabu ya Jahannamu. Kwani adhabu yake ikimteremkia mkosefu inamganda, wala haimwachi.
Rudi kwenye Sura
66. Na hakika Jahannamu ni kituo kiovu mno kwa mwenye kutua, na makao maovu kwa mwenye kukaa ndani yake.
Rudi kwenye Sura
67. Na katika alama za waja wa Mwenyezi Mungu ni kuwa wana kiasi katika kutumia kwao mali, kwa ajili ya nafsi zao na jamaa zao. Wao hawafanyi ubadhirifu, wala hawabanii matumizi bila ya kiasi. Bali kutoa kwao ni kati kati baina ya hayo.
Rudi kwenye Sura
68. Na katika sifa zao hao waja wa Mwenyezi Mungu ni kuwa wameisafia niya Tawhid, na wakatupilia mbali kila athari ya ushirikina katika kumuabudu Mola wao Mlezi. Na wakajizuia kuuwa nafsi aliyo kataza Mwenyezi Mungu kuuliwa, ila ikiwa imefanya uadui basi huuliwa kwa haki. Nao hujitenga mbali na uzinzi, na katika mambo ya starehe hawatendi ila lilio halali tu, ili waepukane na adhabu ya mambo yanayo angamiza. Kwani anaye tenda katika mambo hayo atakuta shari na adhabu.
Rudi kwenye Sura
69. Na Siku ya Kiyama atapata adhabu mardufu kuliko hiyo, na atadumu Motoni kwa udhalili na unyonge.
Rudi kwenye Sura
70. Lakini mwenye kutubu na madhambi haya na akawa mkweli katika Imani yake, na akafuatiliza hayo kwa ut'iifu na vitendo vyema, hao atawasamehe kwa rehema yake, na atawajaalia bora ya thawabu badala ya maovu yaliyo kwisha tangulia. Na hakika shani ya Mwenyezi Mungu ni kurehemu na kusamehe.
Rudi kwenye Sura
71. Na hivyo ndio mambo yetu yendavyo, yaani kuwa mwenye kutubu madhambi, na akaonyesha matokeo yake katika kukubali ut'iifu na kuepuka maasi, basi huyo Mwenyezi Mungu huikubalia toba yake. Na kwa hivyo hurejea kwa Mola wake Mlezi baada ya kumwacha kwake.
Rudi kwenye Sura
72. Na katika khulka za waja wa Mwingi wa Rehema ni kuwa wanajiepusha na kutoa ushahidi wa uwongo, na wakisadifu kukutana na mtu asiye kuwa na kauli au kitendo chema hawashirikiani naye katika hayo, na huacha kufuatana naye.
Rudi kwenye Sura
73. Na katika sifa zao ni kuwa mwenye kuwaidhi akiwapa mawaidha, na akawasomea Aya za Mwenyezi Mungu, humwelekea kumsikiliza, na nyoyo zao zikawaidhika, na macho yao hufunuka. Wala hawawi kama wale ambao wanatapatapa wanapo yasikia, wanapuuza, masikio yao hayapenyi kitu, wala macho yao hayafumbuki.
Rudi kwenye Sura
74. Na wao humwomba Mola wao Mlezi awajaalie wake zao na watoto wao wawe wa kuwapoza moyo kwa vitendo vya kheri, na awajaalie wawe ni waongozi katika kheri ili watu wema wawafuate.
Rudi kwenye Sura
75. Hawa wenye kusifiwa kwa sifa hizi tulizo zitaja ndio waja wa Mwenyezi Mungu wa kweli. Na malipo yao ni makao ya Peponi ya juu, kuwa ni jazaa ya kusubiri kwao juu ya ut'iifu. Na huko Peponi watakuta maamkio, na kusalimiwa.
Rudi kwenye Sura
76. Na neema zao za Peponi ni za daima, hazikatiki. Pepo ndio kituo na makao mema kabisa.
Rudi kwenye Sura
77. Ewe Mtume! Waambie watu: Mwenyezi Mungu hakutakini nyinyi ila mumuabudu Yeye, na mumwombe Yeye katika mambo yenu, wala msimwombe yeyote mwenginewe. Na kwa hayo ndio kakuumbeni. Lakini makafiri katika nyinyi wameyakanusha waliyo kuja nayo Mitume. Basi adhabu yao itawaganda hao, wala hapana wa kuwaokoa nayo.
Rudi kwenye Sura