') //-->
1. Enyi watu! Tahadharini na adhabu ya Mola wenu Mlezi, na wekeni katika nyoyo zenu makumbusho ya Siku ya Kiyama. Kwani mtingishiko utao tokea hapo ni mkubwa, wenye kuhangaisha na kutikisa viumbe.
Rudi kwenye Sura
2. Siku mtapo kiona Kiyama mtaona kitisho chake kinafikilia ukubwa wake hata kama yupo mwanamke anaye nyonyesha na ziwa lake limo katika mdomo wa mwanawe, basi hapana shaka atamsahau na amwachilie mbali. Na kama yupo mwanamke ana mimba basi ataiharibu mimba kabla ya kufika wakati wake wa kuzaa kwa ajili ya fazaa na kitisho. Na ewe mwenye kuangalia! Ukiona hali ya watu Siku hiyo namna wanavyo onekana hawanazo, na wanapo kwenda wanayumba, utadhani wamelewa, na ilhali hawakulewa. Lakini kitisho walicho kishuhudia, na khofu ya adhabu kuu ya Mwenyezi Mungu ndiyo iliyo waondoshea utulivu wao.
Rudi kwenye Sura
3. Na juu ya onyo hili kali na la kweli bado wapo baadhi ya watu inadi yao au kufuata kwao kijinga huwapelekea katika mambo ya kubishana juu ya Mwenyezi Mungu na sifa zake, wakamsingizia kuwa ati ana washirika, au wakaukataa uweza wake wa kufufua na kuwalipa watu kwa vitendo vyao. Na kwa huo ubishi wao na kukataa kwao hawategemei ilimu sahihi, au hoja ya kweli; lakini wao hufuata tu nyayo za kila shetani aliye muasi Mola wake Mlezi, aliye baidika na uwongofu.
Rudi kwenye Sura
4. Mwenyezi Mungu amehukumu kuwa anaye mfuata Shetani na akamfanya kuwa ni rafiki yake na mlinzi wake, na mwongozi wake, basi humpotoa na njia ya Haki, na akamuelekeza kwenye upotovu unao pelekea kwenye Moto unao waka na kuripuka.
Rudi kwenye Sura
5. Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kukufufueni baada ya kufa, basi katika kuumbwa kwenu ipo dalili ya kuweza kwetu kufufua. Tulikuumbeni asili yenu kutokana na udongo, kisha tukaufanya tone ya manii, kisha baada ya muda tukaigeuza ikawa kipande cha damu iliyo gandana.(1) Kisha tukaifanya kipande cha nyama yenye sura ya kibinaadamu, au isiyo kuwa na sura, ili tukubainishieni uweza wetu wa kuanza uumbaji na kuendeleza kukuza kwa viwango na madaraja, na kugeuza kutoka hali hii na kuingia nyengine. Na katika viliomo katika matumbo ya mzazi vipo tunavyo viharibu tuvitakavyo na tunaviweka imara na madhubuti tuvitakavyo, mpaka utimie muda wa kuzaliwa. Kisha tunakutoeni kwenye matumbo ya mama zenu muwe watoto wachanga. Kisha tunakuleeni mpaka mkamilike akili na nguvu. Na baada ya hayo wapo katika nyinyi ambao Mwenyezi Mungu huwafisha, na wapo ambao umri wao hurefushwa mpaka wakafikia ukongwe wa kupiswa, ujuzi wao na kufahamu kwao mambo kukasita. Na aliye kuumbeni kwa sura hii tangu mwanzo hashindwi kukurudisheni tena. Na jambo jengine la kukuonyesha kudra ya Mwenezi Mungu kufufua ni kuwa wewe unaiona ardhi kavu yabisi; tukiiteremshia maji uhai unaitambalia, na hiyo ardhi hugutuka, na huzidi na hututumka kwa maji na hewa iliyo ingia ndani yake, na hapo tena hutokeza namna mbali mbali za mimea inayo furahisha kuiona, na uzuri wake ukazagaa, na mwenye kuiona roho yake ikakunjuka.
(1)(Maurice Bucaille, mtaalamu wa Kifaransa maarufu aliye silimu, amelifasiri neno A'laqa kwa maana ya "kitu kilicho tundikwa". Na hivyo ndivyo inavyo thibitisha Sayansi ya hivi sasa, kuwa mbegu ya uzazi ikisha pandikizwa huja ikaning'inia kama iliyo tundikwa kwenye tumbo la uzazi. Tazama pia 23.14, 40.67, 75.37-38 na kadhaalika Sura ya 5 ya Annisaa Aya 129, inayo eleza kuwa msimwache mke "kama aliye tundikwa")
Rudi kwenye Sura
6, 7. Hayo yaliyo tangulia ya kuumbwa binaadamu, na mimea ya kupanda, ni ushahidi ya kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mungu wa Haki. Na kwamba hakika Yeye ndiye anaye huisha maiti wakati wa kufufuliwa kama vile alivyo anza kuwaumba. Na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu, na kwamba hakika Kiyama kinakuja tu bila ya shaka kuhakikisha ahadi yake. Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu atawahuisha waliomo makaburini kwa kuwafufua kwa ajili ya hisabu na malipo.
Rudi kwenye Sura
8. Na juu ya yaliyo tangulia bado wapo baadhi ya watu wanao jadili juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu, na wanakanya kufufuka bila ya msingi wowote wa ki-ilimu, wala uwongozi wa kweli, au Kitabu kilicho toka kwa Mwenyezi Mungu cha kumwonyesha. Basi ubishi wake ni wa pumbao na inda tu.
Rudi kwenye Sura
9. Na pamoja na hayo hugeuka upande kwa kiburi na kukataa kuikubali Haki. Na watu wa namna hii itakuja wapata hizaya na udhalili duniani kwa ushindi wa Neno la Haki, na Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atawaadhibu kwa Moto wa kuunguza.
Rudi kwenye Sura
10. Na ataambiwa: Hayo unayo yapata ya hizaya na adhabu ni kwa sababu ya uzushi wako na kiburi chako; kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Muadilifu, hadhulumu. Wala hawaweki sawa Muumini na kafiri, na mwema na muovu; bali kila mmoja wao atamlipa kwa mujibu wa vitendo vyake.
Rudi kwenye Sura
11. Na miongoni mwa watu wapo wa namna ya tatu, ambao Imani bado haijatulia katika nyoyo zao, bali itikadi yao inayumba yumba. Maslaha ya nafsi zao ndiyo yanatawala katika Imani yao. Wakipata kheri hufurahi na hutulizana. Na wakipata shida yoyote katika nafsi zao, au mali zao, au wana wao, hurejea ukafirini. Hao huwa wamekosa duniani raha ya utulivu kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu na nusura yake, kama Akhera walivyo kosa neema ambayo Mwenyezi Mungu amewaahidi Waumini walio thibiti na wakasubiri. Hiyo khasara ya mara mbili ndiyo khasara ya kweli kweli iliyo wazi.
Rudi kwenye Sura
12. Mwenye kukhasiri hivi humuacha Mwenyezi Mungu na akayaabudu masanamu yasiyo weza kumdhuru pindi akito yaabudu, wala hayamfai kitu pindi akiyaabudu. Kitendo chake huyo ndio kupotelea mbali na haki na uwongofu.
Rudi kwenye Sura
13. Badala ya Mwenyezi Mungu anamwomba ambaye madhara yake kwa kuharibu akili na kutawala mawazo ovyo ni karibu zaidi kwa nafsi kuliko kuitakidi msaada wake. Muabudiwa huyo ni muovu mno wa kumtaraji msaada, na muovu mno kumfanya rafiki.
Rudi kwenye Sura
14. Hakika wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake kwa Imani yenye kuambatana na vitendo vyema, Mola wao Mlezi atawatia Siku ya Kiyama katika Bustani zipitwazo chini ya miti yake na mito. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendavyo kumuadhibu mharibifu na kumlipa mema mtenda mema.
Rudi kwenye Sura
15. Ikiwa miongoni mwa makafiri yupo anaye dhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamsaidia Nabii wake, basi na anyooshe kamba mpaka kwenye dari ya nyumba yake. Kisha ajinyonge, na akadirie katika nafsi yake na atazame, je, kitendo chake hicho kitaondoa hayo yanayo muudhi ya kuwa Mwenyezi Mungu anamnusuru Mtume wake?
Rudi kwenye Sura
16. Mfano wa tulivyo bainisha hoja zetu zi wazi katika tuliyo kwisha wateremshia Mitume. Tumemteremshia Muhammad Qur'ani yote, nayo ni Aya zilizo wazi ili ziwe ni hoja juu ya watu. Na hakika Mwenyezi Mungu humuongoa amtakaye kuwaongoa ili isalimike tabia yake na abaidike mbali na inadi na yanayo sabibisha hayo.
Rudi kwenye Sura
17. Hakika wanao muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake wote, na Mayahudi wanao nasibika na Musa, na waabuduo nyota na Malaika, na Wakristo wanao nasibika na Isa, na Majusi wanao abudu moto, na washirikina wanao abudu masanamu..hakika wote hawa Mwenyezi Mungu atakuja wapambanua mbali mbali Siku ya Kiyama kwa kumdhihirisha mwenye haki na aliye potea kati yao. Kwani Yeye anajua vyema vitendo vyote vya viumbe vyake. Na atawalipa kwa vitendo vyao.
Rudi kwenye Sura
18. Ewe mwenye akili! Hujui kwamba hakika Mwenyezi Mungu vinamnyenyekea na kumt'ii vyote viliomo mbinguni na katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi katika watu wanamuamini Mwenyezi Mungu na wanafuata maamrisho yake, na kwa hivyo wanastahiki Pepo? Na wapo wengi miongoni mwao wanao puuza na wala hawamuamini, wala hawayatendi maamrisho yake, na kwa hivyo wanastahiki adhabu na hizaya. Na anaye fukuzwa na Mwenyezi Mungu kutokana na rehema yake basi hawezi yeyote kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. Kwani Yeye hutenda ayapendayo.
Rudi kwenye Sura
19. Haya ni makundi mawili walio zozana kwa mambo yaliyo mkhusu Mola wao Mlezi, na yanayo mstahiki na yasio mstahiki. Kikundi kimoja kikamuamini na kikundi kingine kikakataa. Basi wale walio kataa na kukufuru Mwenyezi Mungu amewaandalia Siku ya Kiyama moto utao wazunguka na kuwapamba kila upande, kama nguo inavyo upamba mwili. Na kuzidi kuwaadhibu Malaika watawamiminia maji ya moto mno juu ya vichwa vyao!
Rudi kwenye Sura
20. Yatawapenya mpaka kwenye matumbo yao, viliomo ndani viyayuke kama zitavyo yayuka ngozi zao!
Rudi kwenye Sura
21. Na pia wataandaliwa marungu ya chuma.
Rudi kwenye Sura
22. Kila wakijaribu kutoka Motoni kwa wingi wa machungu na dhiki Malaika watawapiga nayo hayo marungu, na watarudishwa huko huko waliko kuwako. Na watawaambia: Onjeni adhabu ya Moto unao unguza kuwa ni malipo ya ukafiri wenu.
Rudi kwenye Sura
23. Ama walio amini na wakatenda vitendo vyema, hao bila ya shaka Mwenyezi Mungu atawaingiza kwenye Mabustani yanayo pita mito kati ya majumba yake na miti yake. Humo watastarehe kwa kila namna ya starehe, na Malaika watawapamba vikuku vya mikono vya dhahabu na watawapamba kwa lulu. Ama nguo zao za kawaida zitakuwa za hariri.
Rudi kwenye Sura
24. Na ziada ya starehe yao humo Peponi ni kuwa Mwenyezi Mungu atawajaalia wawe na kauli njema, na vitendo vizuri vya kusifika. Basi watakuwa wakimtakasa Mwenyezi Mungu na kumtukuza, na watakuwa wenyewe kwa wenyewe wakiamiliana kwa mapenzi na amani.
Rudi kwenye Sura
25. Hakika wale walio kufuru, yaani walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na pamoja na hayo wakawa mtindo wao kuwazuia watu wasiingie katika Uislamu, na kuwafanyia pingamizi Waumini kuingia kwenye Msikiti Mtakatifu wa Makka - na ilhali Mwenyezi Mungu ameufanya huo ni pahala pa amani kwa watu wote, mkaazi na mpita njia - atawapa watu hao adhabu kali. Na hali kadhaalika kila atakaye kengeuka na Haki, na akatenda udhalimu wowote katika pahala patakatifu, Mwenyezi Mungu atamuadhibu adhabu ya kutia uchungu.
Rudi kwenye Sura
26. Ewe Nabii! Watajie hawa washirikina wanao dai kuwa ati wanamfuata Ibrahim a.s. na wakaifanya Nyumba Takatifu kuwa ni pahala pa kuwekea masanamu yao; watajie kisa cha Ibrahim na Nyumba Takatifu tulipo mwongoza mpaka pahala pake, na tukamuamrisha aijenge, na tukamwambia: Usinishirikishe Mimi na kitu chochote katika ibada. Na isafishe Nyumba yangu na masanamu na uchafu, ili iwe ni pahala pa makusudi ya mwenye kuizunguka kwa kut'ufu, na mwenye kukaa hapo na akafanya ibada.
Rudi kwenye Sura
27. Ewe Nabii! Wajuvye watu kwamba hakika Mwenyezi Mungu amewalazimisha wawezao miongoni mwao waijie hii Nyumba. Basi waitikie wito wako, watakujia kwa miguu na kwa kupanda ngamia aliye konda kwa ajili ya safari ya kutoka mbali.
Rudi kwenye Sura
28. Ili wapate manufaa yao ya Kidini kwa kutekeleza Hija na manufaa ya kiduniani kwa kujuana na ndugu zao Waislamu na kushauriana nao katika mambo ya Dini yao na dunia yao. Nao wataje jina la Mwenyezi Mungu katika Siku ya Idi Kubwa na siku tatu zifwatazo, pale wanapo chinja walio jaaliwa, ikiwa ngamia, au ng'ombe au kondoo na mbuzi. Kuleni mpendacho katika hao, na muwalishe walio patwa na shida na ufakiri.
Rudi kwenye Sura
29. Tena baada ya hao yawapasa waondoe takataka na uchafu ulio wapata wakati ule wa Ih'ram (yaani kuharimia Hija), nao ni majasho na safari ndefu. Pia waondoe nadhiri walizo mwekea Mwenyezi Mungu, ikiwa wameweka nadhiri yoyote. Na waizunguke kwa kwenda kwa miguu ile Nyumba iliyo jengwa kwa ajili ya ibada ya Mwenyezi Mungu duniani.
Rudi kwenye Sura
30. Na mwenye kuzishika amri za Mwenyezi Mungu na makatazo yake katika Hija yake kwa kuzitukuza katika nafsi yake, hayo yatakuwa ni kheri yake katika dunia yake na Akhera yake. Na Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni kula nyama hoa, (mifugo) yaani ngamia, ng'ombe, kondoo na mbuzi, ila katika hali mnazo zijua kwa mlivyo kwisha somewa katika Qur'ani, kama vile nyamafu na nyenginezo. Basi epukaneni na kuabudu masanamu, kwani ibada hiyo ni uchafu wa kiakili na kiroho, na haimwelekei mwanaadamu kufanya hivyo. Na epukaneni na kusema uwongo, kumzulia Mwenyezi Mungu au mwanaadamu.
Rudi kwenye Sura
31. Na kuweni wenye kumsafia niya Mwenyezi Mungu, wenye pupa kutaka kuifuata Haki, bila ya kumfuata mshirika wowote na Mwenyezi Mungu katika ibada. Kwani mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu ameanguka huyo kutoka kwenye ngome ya Imani, na amesalitiwa na upotovu, na ameitia nafsi yake katika hilaki ya kutisha kabisa. Ikawa hali yake kama hali ya mtu aliye poromoka kutoka mbinguni na midege ikamrarua akakatika mapande mapande, asibakie hata alama. Au kama aliye peperushwa na upepo mkali, na mwili ukatawanyika mwahala mbali mbali.
Rudi kwenye Sura
32. Hakika mwenye kuitukuza Dini ya Mwenyezi Mungu na faridha ya Hija na a'mali zake na mihanga inayo pelekwa kwa ajili mafakiri wa Al-Haram, na wakachagua walio nona wazima, hawana ila, basi huyo ndio amemcha Mwenyezi Mungu. Kwani kutukuza kwake hayo ni matokeo ya unyenyekevu wa nyoyo zilizo amini, na alama katika alama za usafi wa niya.
Rudi kwenye Sura
33. Katika kutoa mihanga hii yapo manufaa ya kidunia. Mnawapanda na mnakunywa maziwa yake mpaka wakati wa kuwachinja. Kisha mnapata manufaa ya Kidini vile vile pale mnapo wachinja kwenye Nyumba Takatifu kwa kutafuta kujikaribisha kwa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
34. Hizi faridha za Hija hazikukhusuni nyinyi peke yenu. Kwani tumewajaalia jamaa wote walio amini mambo ya kuwakaribisha kwa Mwenyezi Mungu, na wanataja jina lake, na wanamtukuza wakati wanapo chinja kwa kumshukuru kwa neema aliyo waneemesha, na kuwasahilishia wanyama wa mifugo, nao ni ngamia, ng'ombe, mbuzi na kondoo. Na Mwenyezi Mungu aliye kuwekeeni sharia nyinyi na wao ni Mungu Mmoja. Basi yasalimisheni mambo yenu yote kwake Yeye peke yake. Na vitendo vyenu visafisheni kwake, wala msimshirikishe na yeyote. Na ewe Nabii! Wape bishara ya Pepo na thawabu nyingi wale walio safisha niya zao kwa Mwenyezi Mungu na wakawa wanamnyenyekea Yeye miongoni mwa waja wake,
Rudi kwenye Sura
35. Wale ambao akitajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hupapatika kwa kumkhofu, na hunyenyekea kwa kutajwa kwake, na ambao wanasubiri kwa masaibu ya karaha na shida yanayo wapata kwa kujisalimisha mbele ya amri yake na hukumu yake, na wakashika Sala kwa ukamilifu wake, na wakatoa baadhi ya mali aliyo waruzuku Mwenyezi Mungu katika njia za kheri.
Rudi kwenye Sura
36. Nasi tumefanya uchinjaji ngamia na ng'ombe n.k. katika Hija kuwa ni katika matukuzo ya Dini yalio dhaahiri. Na nyinyi kwa hayo mnajileta karibu na watu. Nanyi katika hao mnapata kheri nyingi katika dunia kwa kuwapanda, na kunywa maziwa yake. Na Akhera mnapata malipo na thawabu kwa kuwachinja na kuwalisha mafakiri. Basi tajeni jina la Mwenyezi Mungu wakati mnapo wapanga kwa safu kwa ajili ya kuwachinja. Mkisha wachinja kuleni sehemu mkitaka, na walisheni mafakiri walio kinai hawaombi, na ambao wanalazimika kuomba kwa haja. Na kama tulivyo fanya kila kitu kiwe kit'iifu kwa tuyatakayo kwa ajili ya manufaa yenu, na tumedhalilisha hivyo vikut'iini nyinyi ili mpate kuishukuru neema yetu kubwa iliyo juu yenu.
Rudi kwenye Sura
37. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu haangalii sura zenu wala vitendo vyenu, lakini anaangalia nyoyo zenu. Wala hataki kwenu mambo ya kujionyesha tu kwa kuchinja na kumwaga damu. Lakini anataka kwenu moyo wenye kunyenyekea. Basi hapati radhi yake mwenye kugawa hizo nyama wala damu. Lakini linalo pata radhi yake ni uchamngu wenu na usafi wa niya zenu. Kuwadhalilisha hao wanyama tulivyo wadhalilisha ni kwa ajili ya kukunafiisheni, mpate kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa vile alivyo kuongoeni hata mkatimiza ibada za Hija. Na ewe Nabii! Wape khabari njema watu wema walio tengeneza a'mali zao na niya zao kuwa watapata malipo makuu.
Rudi kwenye Sura
38. Hakika Mwenyezi Mungu huwalinda Waumini na huwahami na huwanusuru kwa Imani yao. Kwani Yeye hawapendi wenye kukhuni dhamana zao, wenye kupita mipaka katika ukafiri wao kumkataa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu hamsaidii yule asiye mpenda.
Rudi kwenye Sura
39. Mwenyezi Mungu amewaruhusu Waumini wanao pigwa vita na washirikina wawarejezee uadui wao, kwa sababu ya dhulma iliyo wapata nao wakasubiri kwa muda mrefu. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuweza kuwanusuru vipenzi vyake Waumini.
" Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia" Yaliyo tajwa na Qur'ani Tukufu kukhusu hukumu iliomo katika Aya 39 yamezitangulia kanuni zilizo kuja kuwekwa na madola baada yake, nayo ni kuwa mtu kujitetea nafsi yake ni sharia vyovyote vile itavyo kuwa matokeo yake. Na kwamba mwenye kuitetea nafsi yake, na mali yake, na nchi yake, hawi ni mkosa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya uadilifu, ijapo kuwa ameuwa mtu au ameteketeza roho nyingi. Aya hii imepasisha kuwa Waislamu wanayo ruhusa kujitetea pindi wakivamiwa. Na kwa hivyo tunafahamu kuwa vita vya Waislamu vilikuwa vita vya utetezi na kujilinda si vita vya kushambulia na kuvamia. Na kwamba Waislamu waliusimamisha Uislamu na wakaupa nguvu kwa hoja zilizo wazi, na dalili zilizo dhaahiri.
Rudi kwenye Sura
40. Hao ambao makafiri wamewadhulumu na wakawalazimisha waache mji wao wa Makka wauhame. Na wao hawakuwa na kosa lolote ila ni kuwa walimjua Mwenyezi Mungu na wakamuabudu Yeye pekee. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakuwatumilia kwa ajili ya Haki wasaidizi wa kumnusuru Yeye na wakamtetea kupinga jeuri za madhaalimu, basi hapana shaka upotovu ungeli enea, na majeuri wangeli endelea katika jeuri zao, na sauti ya haki wangeli inyamazisha. Wala wasingeli achiliwa Wakristo makanisa yao, wala mamonaki (wat'awa wa Kikristo) wasinge baki na monastari zao (nyumba zao za ibada), wala Mayahudi wansinge kuwa na masinagogi yao, wala Waislamu wasinge kuwa na misikiti yao, ambamo mote humo hutajwa kwa wingi jina la Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu amechukua juu ya nafsi yake ahadi ya nguvu ya kwamba atamsaidia na kumnusuru kila anaye isaidia Dini yake, na atamtukuza kila mwenye kulitukuza Neno la Haki katika ulimwengu. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu haiendi kinyume. Kwani Yeye ni Mwenye nguvu wa kutimiza alitakalo, Mtukufu hashindwi na yeyote.
Rudi kwenye Sura
41. Hao Waumini tulio waahidi kuwanusuru ndio hao ambao tukiwapa madaraka katika nchi wanalinda makhusiano yao na Mwenyezi Mungu na pia na wanaadamu wenzao. Kwa hivyo hushika Sala kwa utimilifu wake, na huwapa Zaka wanao stahiki kupewa, na huamrisha kila lenye kheri, na hukataza kila lenye shari. Na mambo yote hurejea kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Basi Yeye humtukuza amtakaye, na humdhalilisha amtakaye.
Rudi kwenye Sura
42. Ewe Nabii! Ukiwa unapata makanusho, kuambiwa mwongo, na maudhi kutokana na watu wako, basi usisikitike. Zingatia taarikh kwa yaliyo wapata Mitume wa kabla yako, utaona kwamba wewe si Mtume wa kwanza aliye kanushwa na kuudhiwa na watu wake. Kwani kabla ya hawa walio kukanusha wewe, kaumu Nuhu walimkadhibisha Mtume wao Nuhu, na kaumu ya A'ad walimkadhibisha Mtume wao Huud, na kina Thamud walimkanusha Mtume wao Saleh.
Rudi kwenye Sura
43. Na kaumu ya Ibrahim walimkanusha Mtume wao Ibrahim, na kaumu Lut'i walimfanyia hayo hayo Mtume wao Lut'i.
Rudi kwenye Sura
44. Na watu wa Madiana walimkanusha Mtume wao Shua'ib. Na Firauni na watu wake walimkanusha Mtume wa Mwenyezi Mungu Musa. Mitume hao wote yaliwapata yanayo kupata wewe. Na Mimi niliwapa muhula hao wakanushao ili wapate kutubia waongoke, na waitikie Wito wa Haki. Lakini wakazua na wakaendelea na kuwakadhibisha Mitume wao na kuwaudhi. Wakazidisha madhambi juu ya madhambi yao. Basi nikawaadhibu ukomo wa kuwaadhibu. Angalia taarikhi yao utaona kuwa adhabu yangu ilikuwa kali mno, pale nilipo ibadilisha neema ikawa nakama, na uzima ukawa ni maangamizo, na badala ya ujenzi ukawa uharibifu.
Rudi kwenye Sura
45. Basi tuliwatekeza watu wengi wa miji ambayo waliiamirisha, kwa sababu ya udhalimu wao na kukanusha kwao Mitume wao. Zikawa paa za nyumba zao zimeangukia kuta zake, hazina wakaazi. Kama kwamba jana hazikuwapo. Visima vingapi vilivyo bomoka na maji yake yakapotea, na majumba mangapi madhubuti yaliyo jengwa kwa mawe na saruji na chokaa, yamekuwa magofu hayana wakaazi!
Rudi kwenye Sura
46. Hivyo wao wanasema wayasemayo na wanahimiza waletewe adhabu, nao hawatembei ulimwenguni wakaona kwa macho yao walivyo teketea hao madhaalimu wakanushao? Huenda hapo nyoyo zao zikagutuka kutokana na ghafla iliyo wapamba, na wakatia akilini yanao wapasa wakafuata hayo ya wito wa Haki unao waitia. Na masikio yao yakisikia vifo vya hao makafiri huenda wao wakazingatia. Lakini wapi! Ya mbali hayo kuwa watu hawa waweze kuzingatia kwa wanayo yaona au kuyasikia maadamu nyoyo zao zimekuwa kama mawe. Kwani kipofu wa kweli siye yule aliye pofuka macho, lakini ni yule aliye pofuka moyo na hatambui kitu.
Rudi kwenye Sura
47. Na makafiri wa Makka wameshikwa na udanganyifu, na hawana wanalo litambua juu ya kuwepo dalili zote hizi. Kwa hivyo ndio wanakuhimiza, wewe Nabii, uwaletee adhabu ulio waahidi. Wanasema hayo kwa upinzani na kejeli. Na hayo hapana shaka yoyote yatawapata, lakini kwa wakati alio uweka Mwenyezi Mungu, ama duniani au Akhera. Naye hendi kinyume na ahadi yake, hata ikipita miaka. Kwani siku moja kwake ni kama miaka elfu mnayo ikadiria na kuihisabu.
"Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini Mwenyezi Mungu hatakwenda kinyume na ahadi yake kabisa. Na hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi." Qur'ani kwa Aya hii tukufu imeutangulia msafara wa wana sayansi kwa kueleza kuwa zama ni kipimo cha mnasaba, na kwamba fikra ya kuwa zama kwa ulimwengu ni moja kama watu wa zamani walivyo kuwa wakifikiri ni makosa.
Rudi kwenye Sura
48. Na wengi katika watu wa mijini walikuwa madhaalimu kama wao. Nami nikawapa muhula wala sikuwafanyia haraka kuwaadhibu. Na kisha nikawateremshia hiyo adhabu. Na ni kwangu Mimi tu ndio marejeo ya wote Siku ya Kiyama; na hapo nitawalipa kwa wanayo stahiki. Basi enyi makafiri! Msighurike kwa kuchelewa adhabu kukufikieni.
Rudi kwenye Sura
49. Ewe Nabii! Waambie hao wanao kanusha, wanao kuhimiza waletewe adhabu: Sio kazi yangu mimi kukulipeni kwa vitendo vyenu. Bali hakika mimi ni mwenye kukuhadharisheni kwa hadhari iliyo wazi kwamba kuna adhabu. Na Mwenyezi Mungu ndiye wa kukuhisabuni na kukulipeni.
Rudi kwenye Sura
50. Na wale walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakatenda vitendo vyema, watapata kutokana na Mwenyezi Mungu kusamehewa dhambi zao walizo ziingia, kama kadhaalika watavyo pata riziki ya ukarimu huko Peponi.
Rudi kwenye Sura
51. Na wale walio jikukusa nafsi zao katika kuipiga vita Qur'ani kushindana na Waumini na kuwapinga, wakitamani na kudai kwa uwongo, kwamba wao watapata wayatakayo - watu hao watabaki milele katika adhabu ya Motoni.
Rudi kwenye Sura
52. Ewe Nabii! Usihuzunike kwa hizi hila za makafiri. Yalimpata kama haya kila Mtume katika Mitume wetu, na kila Nabii katika Manabii wetu. Nayo ni kuwa kila wakiwasomea kitu kwa kuwaita waifuate Haki Mashetani wa kibinaadamu walio asi wakiyapinga ili waubat'ilishe Wito, na wawatie shaka watu kwa yale wanayo somewa. Makusudio yao ni kujiingiza kati baina ya Nabii na matamanio yake ya kutaka Wito wake uitikiwe. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa wayatakayo. Na mwishoe Haki ndiyo inayo shinda anapo isimamisha Mwenyezi Mungu sharia yake, na akamnusuru Mtume wake. Na Yeye ndiye Mwenye kuzijua hali za watu na vitimbi vyao, Mwenye hikima katika vitendo vyake. Anaweka kila kitu pahala pake.
Rudi kwenye Sura
53. Na hakika Mwenyezi Mungu amewawezesha waasi wanao kataa Haki waweze kutumbukiza shakashaka na vikwazo katika Njia ya Wito ili uwe ni mtihani na majaribio kwa watu. Makafiri ambao nyoyo zao zimegeuka mawe, na wanaafiki ambao nyoyo zao zina maradhi, huzidi upotovu kwa kueneza shakashaka hizi na kuziunga mkono. Na si ajabu madhaalimu hawa kusimama msimamo huu, kwani wao wamezama katika upotovu na wamevuka mpaka katika inadi na mfarakano.
Rudi kwenye Sura
54. Na ili walio pewa ilimu ya sharia na Imani wazidi Imani na kujua kwamba wayasemayo Mitume na Manabii hakika ni kweli iliyo teremka kutokana na Mwenyezi Mungu. Na kwamba Mwenyezi Mungu hakika anawalinda Waumini kwa hima yake kutokana na matatizo yote yanayo wapitikia. Na huwaongoa kwenye maarifa ya Njia Iliyo Nyooka nao wakaifuata.
Rudi kwenye Sura
55. Na walio kufuru hawatengenei. Bali wanaendelea kuitilia shaka Qur'ani mpaka wafikiwe na mauti, iwafikie adhabu ya Siku isiyo kuwa na kheri kwao wala rehema; nayo ni Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
56. Siku ambayo madaraka ya nguvu, na uendeshaji mambo usio na ukomo wote, ni wa Mwenyezi Mungu pekee. Siku hiyo ndipo atapo hukumu baina ya waja wake. Walio amini na wakatenda mema watadumu katika Bustani zilizo jaa kila namna ya neema.
Rudi kwenye Sura
57. Na walio kufuru na wakazikanusha Aya za Qur'ani tulizo mteremshia Muhammad, hao watakuta adhabu ya madhila na fedheha.
Rudi kwenye Sura
58. Na wenye kuacha nchi zao kwa ajili ya kutukuza shani ya Dini yao wakitafuta radhi za Mwenyezi Mungu, kisha wakauliwa katika uwanja wa Jihadi, au wakafa vitandani mwao, Mwenyezi Mungu atawalipa malipo mazuri kabisa. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kutoa thawabu za ukarimu.
Rudi kwenye Sura
59. Na hakika atawatia katika Pepo kwenye vyeo watavyo ridhika navyo na vitawafurahisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzijua vyema hali zao, basi atawalipa malipo bora, naye ni Mpole huyasamehe makosa yao madogo madogo ya kuteleza.
Rudi kwenye Sura
60. Huo ndio mwendo wetu katika kuwalipa watu. Hatuwadhulumu. Na Muumini mwenye kulipiza kisasi kwa aliye mfanyia uovu, na akalipiza kwa kadri ya alivyo tendewa bila ya kuzidisha, kisha yule mkosa akaja kumfanyia uadui tena baada yake, basi hakika Mwenyezi Mungu anatoa ahadi ya nguvu kuwa atamnusuru na kumsaidia yule aliye dhulumiwa. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kumsamehe mwenye kulipiza kama alivyo dhulumiwa. Hamtii makosani kwa hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, basi huyasitiri makosa ya kuteleza ya mja wake mt'iifu, wala hamfedhehi Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
61. Msaada huo ni mwepesi kwa Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ni Muweza wa kila kitu. Na katika Ishara za uwezo wake zilio wazi mbele yenu ni utawala wake juu ya ulimwengu wote. Huzungusha usiku na mchana, pengine huzidi huu au huzidi huu. Inakuwa baadhi ya kiza cha usiku pahala pa mwanga wa mchana. Na pengine huwa kinyume cha hivyo. Naye Subhanahu juu ya uwezo wake husikiliza kauli ya aliye dhulumiwa, na anaviona vitendo vya mwenye kudhulumu. Basi humtia adhabuni.
Rudi kwenye Sura
62. Huo ndio msaada wa wenye kudhulumiwa unao tokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na kutenda kwake katika ulimwengu kama atakavyo bila ya kiwango ni kama muonavyo matokeo yake; na kwa hakika Yeye ndiye Mungu wa Haki ambaye hapana mungu mwenginewe pamoja naye. Na kwamba masanamu wanayo yaabudu washirikina ni uwongo, hayana ukweli, na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye tukuka juu ya vyote isipo kuwa Yeye Mwenyewe kwa shani yake, na ni Mkuu wa madaraka.
Rudi kwenye Sura
63. Ewe mwenye akili! Huzingatii haya yalio kuzunguka uyaonayo kwa macho yenye kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu, ukamuabudu Yeye peke yake? Yeye ndiye anaye iteremsha mvua kutoka mawinguni, na ardhi ikageuka rangi ya kijani kibichi kwa mimea inayo chipuka, baada ya kuwa na ukame. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole mno kwa waja wake, na anajua vyema yanayo wanufaisha na kwa hivyo akawatengenezea kwa kudra yake.
Rudi kwenye Sura
64. Kila kiliomo mbinguni na katika ardhi ni chake Yeye, na kinamtumikia Yeye peke yake, na anakiendesha kama apendavyo. Na Yeye hawahitajii waja wake, bali wao ndio wanao mhitajia Yeye. Na Yeye ndiye anaye stahiki peke yake kuhimidiwa na kusifiwa na viumbe vyote.
Rudi kwenye Sura
65. Ewe mwenye akili! Huyaangalii yaonekanayo kwa macho ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, ukaona anavyo wasahilishia watu wote kunafiika na ardhi na viliomo ndani yake? Na akawatengenezea bahari za kwendea ndani yake marikebu kwa mujibu apendavyo Yeye? Na akazishika sayari zote ziliomo angani kwa kudra yake hata zisikosee mpango wake, au zikaangukia kwenye ardhi, isipo kuwa akitaka kwa mapenzi yake. Hakika Mwenyezi Mungu Aliye takasika ni Mwingi wa huruma na rehema kwa waja wake. Kwa hivyo amewatengenezea kila njia za maisha mema. Huwaje basi baada ya haya yote hamumsafii niya Yeye kwa kumshukuru na kumuabudu?
"Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu." Aya hii tukufu inakusanya maana za kisayansi za ndani. Mbingu, nayo ni kila kilicho juu yetu, inaanza kwa kuifunika ardhi kwa hewa, tena kwa anga, tena kwa vyombo vya mbinguni vinavyo toa mwanga kama nyota n.k. na visio toa mwanga wake mwenyewe kama mwezi, na sayari nyengine, na nyota mkia, na vumbi la ulimwengu, n.k. Vyote hivi vinakuwa vilivyo na vinashikana kwa athari ya nguvu mbali mbali. Muhimu wa hizo ni mvuto na nguvu inayo tokana na kule kuzunguka kwao.
Yamedhihiri mapenzi ya Mwenyezi Mungu na huruma zake kwa waja wake kuwa katengeneza kifuniko cha angani kina namna za gasi mbali mbali ambazo ni dharura kwa uhai. Kama pia anawalinda wakaazi wa duniani na mianga na vimondo n.k. vinavyo zunguka angani na ambavyo vinapo karibia kwenye ardhi huungua kabla havijafika chini.
Na katika mapenzi yake na rehema yake Mwenyezi Mungu ni kuwa hivyo vimondo vinavyo anguka kwenye ardhi ni nadra sana kutokea, na hutokea mwahala wasipo kaa watu. Jambo hili la dhaahiri laonyesha huruma na rehema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Na haya yanatilia nguvu na kusadikisha kauli yake Mwenyezi Mungu: " na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu."
Rudi kwenye Sura
66. Na Yeye ndiye aliye kupeni uhai. Kisha anakufisheni unapo malizika muda wenu. Kisha tena atakufufueni Siku ya Kiyama kwa ajili ya hisabu na malipo. Hakika mwanaadamu baada ya neema zote hizi na ushahidi wote huu ni mwingi wa kumkataa Mwenyezi Mungu na kuzikataa neema zake alizo mpa.
Rudi kwenye Sura
67. Tumewajaalia katika kila umma walio kwisha tangulia wawe na sharia zao makhsusi zinazo ambatana na zama zao, za kumuabudia Mwenyezi Mungu, mpaka zinapo kuja futwa na zijazo baadae. Na kwa hivyo tumewajaalia watu wako, ewe Nabii, wawe na Sharia ya kumuabudu Mwenyezi Mungu mpaka Siku ya Kiyama. Ilivyo kuwa hivi ndio amri yetu na mpango wetu, basi hao wanao jiabudia kwa dini zao zilizo pita, haiwafalii wao kutia mkazo katika kukupinga wewe. Kwani hakika sharia yako wewe imefuta sharia zao. Basi usijishughulishe na kujadiliana nao. Nawe endelea kuwaita watu wende kwa Mola wako Mlezi kwa mujibu wa unavyo pewa wahyi (ufunuo). Hakika wewe unafuata Uwongofu Ulio Nyooka wa Mola wako Mlezi.
Rudi kwenye Sura
68. Na wakishikilia kuendea kukujadili basi waachilie mbali, na waambie: Mwenyezi Mungu anajua zaidi vitendo vyenu, na malipo mnayo yastahiki.
Rudi kwenye Sura
69. Mwenyezi Mungu atahukumu baina yangu na nyinyi Siku ya Kiyama katika hayo mnayo khitalifiana nami. Atamlipa thawabu aliye ongoka na atamuadhibu aliye potoka.
Rudi kwenye Sura
70. Ewe mwenye akili! Jua kuwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu umekusanya kila kiliomo mbinguni na duniani. Hapana kitendo cha hawa washindani kinacho fichika kwake. Vyote hivyo vimekwisha andikwa katika Ubao ulio hifadhiwa (Lauhun Mahfuudh). Kwani kujua kwake Mwenyezi Mungu na kuvithibiti kwake ni kazi nyepesi kabisa kwake.
Rudi kwenye Sura
71. Na washirikina huabudu badala ya Mwenyezi Mungu masanamu na watu ambao haikuteremka hoja yoyote ya kuwaabudu hao katika Kitabu cha mbinguni chochote. Wala wao hawana ushahidi wowote wa kuingia akilini. Lakini wanafanya yote hayo kufuata pumbao na mila tu. Wala hao washirikina walio zidhulumu nafsi zao na wakazidharaulisha akili zao hawato pata msaidizi wa kuwanusuru, na kuwakinga na adhabu ya Moto Siku ya Kiyama, kama wanavyo jidai.
Rudi kwenye Sura
72. Ewe Nabii! Hawa washirikina mtu akiwasomea Aya zetu zilizo wazi, na ambazo ndani yake mna ushahidi wa ukweli wa hayo unao waitia, na ubaya wa ibada zao, utaona katika nyuso zao ghadhabu na chuki inayo wajaa, hata inakaribia kuwapelekea kutaka kumuuwa huyo anaye wasomea. Ewe Nabii! Waambie kwa kuwazindua na kuwaonya: Je! Mtanisikiliza nikwambieni yaliyo kuwa mabaya zaidi kuliko hiyo chuki inayo kuunguzeni roho? Ni Moto ambao Mwenyezi Mungu amewaahidi walio kufuru kama nyinyi Siku ya Kiyama. Na hapana mwisho mbaya na makaazi maovu kuliko hayo.
Rudi kwenye Sura
73. Enyi watu! Sisi tunakufahamisheni ukweli wa ajabu, basi hebu usikilizeni na muuzingatie. Haya masanamu hayataweza kabisa kuumba chochote hata kikiwa kitu duni kabisa kama nzi; hata ikiwa yote yakisaidiana katika kuumba huko. Bali huyu makhluku duni kabisa akiwanyang'anya chochote katika hizo sadaka wanazo pewa masanamu hawawezi kumzuia au kumfukuza. Unyonge gani basi huo wa kushindwa na nzi kutoweza kurejesha alicho pokonya. Na nzi ni kitu dhaifu mno! Wote wawili ni wanyonge. Bali hayo masanamu ambayo kama mnavyo ona ni dhaifu zaidi, basi huwaje mwanaadamu mwenye akili akenda kuyaabudu na kutaka yamnafiishe.
Rudi kwenye Sura
74. Hawa washirikina hawamjui Mwenyezi Mungu kama anavyo faa kujuulikana, wala hawamtukuzi kama anavyo stahiki kutukuzwa, walipo kwenda kumshirikisha katika ibada na vitu visio kuwa na maana kabisa. Na hali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muweza wa kila kitu, Asiye shindika na yeyote.
Rudi kwenye Sura
75. Mapenzi ya Mwenyezi Mungu na hikima yake yamempelekea kuteuwa Wajumbe kutokana na Malaika, na kutokana na wanaadamu, ili wafikishe sharia yake kwa viumbe vyake. Basi huwaje mkampinga aliye mchagua Mwenyewe kuwa ni Mjumbe wake kwenu? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia wayanenayo waja wake, Mwenye kuviona vitendo wavitendavyo. Naye atawalipa kwavyo.
Rudi kwenye Sura
76. Na Yeye Subhanahu anajua hali zao zilizo dhaahiri na za ndani. Hapana kinacho fichika kwake. Na kwake Yeye pekee ndiyo yanarejea mambo yote.
Rudi kwenye Sura
77. Enyi mlio amini! Msishughulikie upotovu wa makafiri. Nyinyi endeleeni na kutimiza Sala zenu kwa ukamilifu kwa kurukuu na kusujudu. Na muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni na akakuruzukuni. Wala msimshirikishe naye na yeyote. Na tendeni kila lenye kheri na manufaa, ili mpate kuwa watu wema, walio bahatika katika Akhera yenu na dunia yenu.
Rudi kwenye Sura
78. Na wanieni katika Jihadi ya kunyanyua Neno la Mwenyezi Mungu na kutafuta radhi zake mpaka mwashinde maadui zenu na myashinde matamanio yenu. Kwani Yeye Subhanahu amekukaribisheni kwake, na amekuteueni muinusuru Dini yake, na amekujaalieni muwe Umma wa katikati. Wala hakukulazimisheni katika aliyo kuwekeeni Sharia lolote lenye mashaka juu yenu msilo weza kulichukua. Na amekufanyieni mepesi katika yanayo kuleteeni mashaka, na katika msiyo yaweza amekufanyieni ruhusa namna mbali mbali. Basi ishikeni Dini hii, kwani hii ndiyo Dini ya baba yenu Ibrahim katika misingi yake. Na Yeye Subhanahu ndiye aliye kuiteni Waislamu, (yaani Wanyenyekevu) katika Vitabu vya mbinguni vilivyo tangulia, na pia katika hii Qur'ani kwa ut'iifu wenu kwa yale aliyo kutungieni sharia. Basi kueni kama alivyo kuiteni Mwenyezi Mungu ili muwe mwisho wenu mnamshuhudia Mtume kama amekufikishieni ujumbe nanyi mkatenda aliyo kufikishieni, mpate kufanikiwa, na muwe mashahidi kwa kaumu zilizo tangulia kwa yaliyo kuja katika Qur'ani kwamba Mitume wao nao walifikisha ujumbe. Na ilivyo kuwa Mwenyezi Mungu amekuchagueni nyinyi khasa kuwa ni wat'iifu kwake, mkashika Sala kwa ukomo wa ukamilifu wake, basi ni waajibu wenu kulipa hayo kwa kumshukuru na kumt'ii, mshike Sala kwa utimilifu wake, na mwape Zaka wanao stahiki, na mumtegemee Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote, na mchukue kwake msaada, kwani Yeye ndiye Msaidizi wenu na ndiye wa kuwanusuru.
Yeye ndiye Mbora wa ulinzi na Mbora wa kunusuru.
Rudi kwenye Sura