1. Alif Lam Mim Ra - Kwa kuanzia harufi hizi ni kunabihisha muujiza wa Qur'ani, juu ya kuwa imeundwa kwa harufi hizi hizi zinazo tumiwa kwa kusemea. Na pia kuwazindua watu waisikilize. Haya yaliyo tajwa katika Sura hii ni Kitabu kilicho teremshwa kwako wewe, Muhammad, kutokana nasi, ili uwatoe watu wote kwenye kiza cha ukafiri na ujinga waendee kwenye nuru ya Imani na ilimu, kwa kusahilishiwa na Mola wao Mlezi. Na nuru hiyo ndiyo Njia ya Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kwa kuadhibisha, na Mwenye kuhimidiwa kwa kuneemesha.
Rudi kwenye Sura

2. Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Mwenye kuumba na kumiliki kila kiliomo mbinguni na kwenye ardhi. Ikiwa hii ndiyo hali ya Mungu wa Haki, basi makafiri, wenye kukanya, watahilikika kwa adhabu iliyo kali.
Rudi kwenye Sura

3. Hao ndio walio khiari uhai wa duniani kuliko Akhera, na wanawazuia watu wasifuate Sharia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotoa Sharia katika macho ya watu ili wapate kuikataa. Hao ndio wanao elezwa katika yaliyo tajwa kuwa wamepotelea mbali na Haki.
Rudi kwenye Sura

4. Na Sisi hatukumtuma Mtume yeyote kabla yako, ewe Nabii, ila kwa lugha ya kaumu yake ile tuliyo mtumia, ili apate kuwafahamisha aliyo kuja nayo, na wao wayafahamu, na wayaelewe kwa wepesi. Wala si juu yake yeye kuwa lazima waongoke. Mwenyezi Mungu Mwenyewe ndiye humwacha apotee anaye mtaka kwa kuwa huyo si tayari kuitaka Haki. Na humwongoa amtakaye kwa kuwa kajitayarisha vyema kufuata Haki. Naye Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu ambaye hashindiki kwa atakalo, na ambaye anayapanga mambo yote kwa mahala pao. Basi haachi kupotea wala haongoi ila kwa hikima yake.
Rudi kwenye Sura

5. Na tulimtuma Musa na tukamuunga mkono kwa miujiza yetu. Tukamwambia: Watoe watu wako, Wana wa Israili, kwenye kiza cha ukafiri na ujinga uwapeleke kwenye nuru ya Imani na ilimu, na uwakumbushe vituko na nakama aliyo wapelekea Mwenyezi Mungu kaumu za kabla yao. Hakika katika kukumbusha huko zipo dalili kubwa za kuthibitisha Upweke wa Mwenyezi Mungu, zinamlingania kwenye Imani kila mwenye kuthibiti kuwa na ukamilifu wa kuweza kuvumilia balaa, na kushukuru neema. Na hii ni sifa ya Muumini.
Rudi kwenye Sura

6. Ewe Nabii! Wakumbushe watu wako, huenda wakazingatia, wakati Musa alipo waambia watu wake kwa kufuata amri ya Mola wako Mlezi: Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu, pale alipo kuvueni kutokana na kaumu ya Firauni, nao wakikupatilizeni kwa adhabu ovu kabisa. Wakikufanyisheni kazi ngumu, wakiwachinja watoto wenu wa kiume, na wakiwaacha wa kike na kuwaweka katika unyonge na udhalili bila ya kuwauwa. Na mateso yote yaliyo tajwa na kuokoka ni mtihani mkubwa unao toka kwa Mwenyezi Mungu, ili upate kudhihiri uwezo wa kusubiri na kushukuru.
Rudi kwenye Sura

7. Na kumbukeni, enyi Wana wa Israil, pale Mola wenu Mlezi alipo kufunzeni, na akasema: Wallahi! Mkishukuru kwa neema niliyo kupeni ya kukuvueni, na mengineyo, kwa kuthibiti juu ya Imani na ut'iifu, basi hapana shaka nitakuzidishieni neema yangu. Na mkiikanya neema yangu kwa ukafiri na maasi, basi hakika nitakuadhibuni kwa adhabu ya kutia uchungu. Kwani adhabu yangu ni kali kwa wanao kanya.
Rudi kwenye Sura

8. Na Musa aliwaambia watu wake walipo mpinga na kumkanya: Mkizikanya neema za Mwenyezi Mungu, wala msishukuru kwa Imani na ut'iifu, nyinyi na wote waliomo duniani, basi hakika hayo hayatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, hahitajii shukra za wanao shukuru. Yeye ni Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa dhati yake, bila ya yeyote kumhimidi.
Rudi kwenye Sura

9. Je! Haijakufikilieni khabari za walio tangulia kabla yenu? Kaumu ya Nuhu, na A'adi, na Thamud, na kaumu nyenginezo zilizo kuja baada yao, ambao hapana anaye wajua ila Mwenyezi Mungu kwa wingi wao.  Hao walijiwa na Mitume wao kwa hoja zilizo wazi kuthibitisha ukweli wao. Na hao wakaweka mikono yao kwenye vinywa vyao, kwa mastaajabu na kukanya. Wakawaambia Mitume: Sisi tunaikataa miujiza na ishara mlizo kuja nazo. Na hakika sisi tuna shaka na hayo mnayo tuitia, mambo ya Imani na Tawhidi, ya kuwa Mungu ni mmoja. Sisi hatukuyakinika na chochote, na tuna shaka nayo!
Rudi kwenye Sura

10. Mitume wakawaambia watu wao, kwa mastaajabu, kuvunja shaka zao za kuwepo Mwenyezi Mungu na kuwa Yeye ni Mmoja peke yake: Hivyo katika kuwepo Mwenyezi Mungu Mmoja peke yake ipo shaka yoyote, na hali Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi bila ya kuwepo mfano wa kuigiza? Na Yeye anakuiteni apate kukusameheni baadhi ya madhambi mliyo yatenda kabla hamjaamini, na anakuakhirisheni mpaka umalizike muda wenu! Hao watu wakawaambia Mitume wao kwa kuudhi: Nyinyi si chochote ila ni watu tu, wanaadamu, kama sisi. Hamna ubora wowote wa kukufadhilisheni juu yetu hata mpewe Utume. Mnataka kwa huo wito wenu mtuzuie tusiabudu walio kuwa wakiabudu baba zetu! Basi tuleteeni hoja iliyo wazi katika tunazo kwambieni.
Rudi kwenye Sura

11. Mitume wao wakawaambia: Sisi si chochote ila ni watu kama nyinyi, kama mlivyo sema. Walakini Mwenyezi Mungu huwateua awatakaye miongoni mwa waja wake akawapa Unabii na Utume. Wala hatuna sisi uwezo wa kukuleteeni hoja mnayo taka ila Mwenyezi Mungu apendavyo. Na ni juu ya Mwenyezi Mungu tu peke yake ndio wategemee Waumini, na wamtegemee kwa kustahamilia inda zenu na upinzani wenu.
Rudi kwenye Sura

12. Na sisi tuna udhuru gani wa kuacha kumtegemea Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye aliye tuongoza kila mmoja wetu kwenye njia yake na maelekeo yake aliyo mwekea, na akamlazimisha afuate katika Dini? Na hakika sisi tunatilia mkazo tegemeo letu kwa Mwenyezi Mungu; na hapana shaka tutayavumilia maudhi yenu ya inadi na kutaka miujiza. Na juu ya Mwenyezi Mungu peke yake ndio humtegemea wanao tegemea.
Rudi kwenye Sura

13. Wakuu wa makafiri majabari wenye madaraka wakaazimia watumie nguvu walipo shindwa wote kupambana kwa hoja na dalili. Wakawaambia Mitume wao: Na liwe moja ya mawili. Ama tukutoeni katika nchi yetu, au muingie katika dini yetu. Mwenyezi Mungu akawafunulia Mitume kwa wahyi: Tutawateketeza hao makafiri kwa dhulma yao!
Rudi kwenye Sura

14. Na baada ya kuwateketeza tutakuwekeni nyinyi katika ardhi yao. Na huko kuwekwa kwa Waumini ni kweli, hakika, kwa mwenye kukhofu kusimama mbele yangu kwa ajili ya hisabu, na akakhofu ahadi yangu ya adhabu. Kwani mwenye kuingia na khofu huwa mt'iifu.
Rudi kwenye Sura

15. Hao Mitume waliomba nusura wawashinde hao watu wao wanao wapinga, baada ya kukata tamaa kuwa hawataamini tena. Mwenyezi Mungu aliwanusuru, na wakafuzu, na akakhasiri kila mwenye kiburi, akakataa kumt'ii Mwenyezi Mungu, akawa shadidi wa upinzani. (Haya yaliyo wapata Mitume huwapata watu wa Mungu wote wanao wania Haki hata katika zama zetu. Ushindi wa mwisho daima unakuwa kwa walio wema, hoja kuvumilia na kuendelea na kazi ya Mungu).
Rudi kwenye Sura

16. Kushindwa kwa hao madhaalimu kunatangulia hapa duniani, na baada yake Akhera ipo adhabu ya Jahannamu. Huko watanyweshwa maji yanayo kirihi kama usaha unao toka kwa watu wa Motoni!
Rudi kwenye Sura

17. Kunywa kwake ni taklifu, ni kama wanayagugumia, na wala hayeshi kiu, kwani hayumkini kuyaonea tamu kwa ukarihi wake na uchafu wake! Na mtu anakuwa ni kama amezungukwa na mauti kila upande kwa shida ziliopo, na wala huko katika Jahannamu hafi akapumzika na yanayo mfika, bali kila wakati anakuta adhabu nyengine kali zaidi.
Rudi kwenye Sura

18. Hakika hali za vitendo vya kheri wavifanyavyo makafiri duniani na pato lake, kwa kuwa havikujengwa juu ya msingi wa Imani, hali yake ni kama jivu. Ukaja upepo mkali ukalipeperusha siku ya kimbunga kilipo kaza. Siku ya Kiyama hawapati chochote kutokana na vitendo vyao vya namna hivyo vya duniani. Hayumkini wao kunafiika na chochote kutokana navyo, kwani hivyo havina thawabu, kama mtu mwenye vumbi linalo peperuka katika upepo asilo weza kulikamata. Na watu hawa wapotovu hujiona wenyewe ati kuwa ndio wanafanya mema, na ilhali vitendo vyao viko mbali kabisa na Njia ya Haki.
Rudi kwenye Sura

19. Ewe unae semezwa! Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi zisimame juu ya Haki kwa mujibu wa hikima yake? Na Mwenye kuweza haya basi anaweza kukuteketezeni, enyi makafiri, na akitaka akaleta viumbe wengine badala yenu nyinyi, ambao watakubali kuwepo kwake, na kwamba Yeye ni Mmoja wa pekee.
Rudi kwenye Sura

20. Na  kuondoa huko na kuleta si muhali wala si uzito kwa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura

21. Makafiri wote watadhihiri kutoka makaburini kwao, waonekane kwa ajili ya kuhisabiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na kudhihiri huko hakuna shaka, ni kama kwamba yametokea hivi sasa. Hapo wale wenye maoni ya kinyonge miongoni mwa wafwasi watawaambia waongozi wenye kiburi: Sisi tulikuwa wafwasi wenu katika kuwakanusha Mitume na kuwapiga vita, na kuzipuuza nasaha zao. Basi je, hii leo, hamtuondolei kidogo baadhi ya adhabu? Wakubwa walio takabari watasema: Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu ametuongoa  kwenye njia ya kuokoka, na akatuwafikia, basi nasi tungeli kuongozeni na tungeli kuitieni muifuate hiyo njia. Walakini sisi tumepotea na kwa hivyo tukakupotezeni nyinyi, yaani tumekuchagulieni tuliyo jichagulia nafsi zetu. Na leo hii sisi na nyinyi ni sawa sawa, tukisikitika au tukastahamili. Hapana pa kuikimbilia adhabu hii!
Rudi kwenye Sura

22. Mwenyezi Mungu atapo pitisha amri yake ya kuwaneemesha wat'iifu na kuwaadhibu wenye kuasi, Iblisi atawaambia wanao mfuata: Hakika Mwenyezi Mungu amekuahidini ahadi ya kweli kukhusu kufufuliwa na malipo, na ameitimiza. Na mimi nimekuahidini ahadi ya uwongo ya kwamba hakuna kufufuliwa, wala malipo, nami nimekwenda kinyume na ahadi yangu. Nami sikuwa na nguvu nanyi hata nikulazimisheni kunifuata. Lakini nimekuiteni kwa ushawishi wangu wa upotovu, nanyi mkaja mbio kunit'ii. Basi msinilaumu kwa sababu ya ushawishi wangu. Na zilaumuni nafsi zenu kwa kuniitikia. Wala mimi hii leo si wa kukuokoeni na adhabu. Na nyinyi hamwezi kuniokoa mimi! Mimi leo nakataa huko kunishirikisha mimi na Mwenyezi Mungu huko duniani mlipo kuwa mkinit'ii kama mtumwa anavyo mt'ii bwana wake. Hakika makafiri watapata adhabu chungu.
Rudi kwenye Sura

23. Na Akhera wataingizwa wenye kuamini, na wakatenda vitendo vyema, katika Mabustani yanayo pitiwa na mito chini ya majumba yake, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na amri yake. Maamkio yao humo kutokana na Malaika ni kufahamisha amani na utulivu.
Rudi kwenye Sura

24. Je, ewe mtu! Hujui vipi Mwenyezi Mungu alivyo fananisha neno la Haki lilio zuri, na neno la uwongo lilio baya?  Amelimathili neno zuri lenye faida kuwa ni kama mti wenye manufaa. Asili yake ni mizizi iliyo shikilia baraabara kwenye ardhi na matawi yake yamenyanyuka kuelekea mbinguni.
Rudi kwenye Sura

25. Hutoa matunda yake kila wakati aliyo uweka Mwenyezi Mungu yazae kwa mapendekezo ya aliye yaumba.  Hivyo hivyo ndio tamshi la Tawhid, Upweke wa Mwenyezi Mungu, ni lenye kuthibiti katika moyo wa Muumini. A'mali yake inapanda kwa Mwenyezi Mungu, na inamfikilia baraka zake na thawabu zake kila wakati. Na Mwenyezi Mungu anawabainishia watu kwa mifano, anashabihisha maana kwa vitu wavijuavyo ili Waumini wawaidhike.
Rudi kwenye Sura

26. Neno la uwongo baya mfano wake ni kama mti mbaya ulio ng'olewa, umetupwa juu ya ardhi. Haukusimama imara. Hali kadhaalika neno la uwongo lilio kataliwa halina uthabiti, kwa kuwa halikuungwa mkono na hoja.
Rudi kwenye Sura

27. Mwenyezi Mungu anawathibitisha imara wanao amini juu ya neno la Haki katika uhai wa duniani na Siku ya Kiyama pia. Na Mwenyezi Mungu huwabaidisha nalo neno hilo makafiri kwa kutojitengenezea wenyewe. Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo, akiwathibitisha baadhi na kuwaacha kupotea wenginewe. Hapana wa kumtoa kombo kwa hukumu yake, wala mwenye kuurudisha uamuzi wake!
Rudi kwenye Sura

28. Ewe msikilizaji! Hebu huwaangalii hao washirikina ambao, badala ya kushukuru neema ya Mwenyezi Mungu ya kumleta Muhammad na Dini yake, wakaingia kumkataa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na wakawasabibisha wafwasi wao kutumbukia katika nyumba ya hilaki kwa upotovu wao.
Rudi kwenye Sura

29. Na nyumba hiyo ndiyo Jahannamu wakiteswa kwa uvukuto wake. Na makaazi maovu mno ni Jahannamu.
Rudi kwenye Sura

30. Na wakamfanyia Mwenyezi Mungu Mmoja wa pekee mifano ya masanamu wakiyaabudu, kwa ajili ya kuwa natija ya vitendo vyao iwe kuwapoteza watu wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu! Ewe Nabii! Waambie hao walio potea: Stareheni na matamanio yenu, kwani marejeo yenu ni Motoni!
Rudi kwenye Sura

31. Ewe Muhammad! Waambie waja wangu walio sadiki, wakaamini, na wakatenda mema: Shikeni Sala, na toeni baadhi ya tuliyo kuruzukuni katika njia za kheri, kwa siri na kwa dhaahiri, kabla ya kufika siku ambayo haifai kitu kupatana kibiashara wala hisani ya urafiki.
Rudi kwenye Sura

32. Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye zianzisha mbingu na viliomo ndani yake, na ardhi na viliomo ndani yake. Na akateremsha kutoka mawinguni maji ya kumiminika. Na kwa sababu yake akakutoleeni riziki ya matunda, na mazao mengine na miti. Na Yeye akakufanyieni vyombo vya baharini vikufaeni vinakwenda na kupakia riziki zenu, na bidhaa zenu za biashara, kwa idhini yake na kutaka kwake. Na akaifanya mito ya maji matamu ikunufaisheni kwa kunywa nyinyi na kumwagia katika mashamba yenu.
Rudi kwenye Sura

33. Na akalifanya jua na mwezi yakufaeni daima dawamu, kwa mwangaza na maslaha ya mimea na wanyama. Na akajaalia usiku ukufaeni kwa kupumzika na mchana kwa kufanya kazi.
Rudi kwenye Sura

34. Na akakutengenezeeni yote mnayo yahitajia katika maisha yenu ambayo anastahiki kuombwa, sawa sawa ikiwa mmemuomba au la. Na mkizihisabu neema alizo kuneemesheni Mwenyezi Mungu, hamwezi kuzidhibiti namna zake, seuze idadi yake! Hakika huyo mwenye kukanya ambaye akalipa ukafiri kuwa ni malipo ya neema alizo pewa, basi ni mwingi wa udhalimu na ukafiri!
Rudi kwenye Sura

35. Ewe Nabii! Ili watu wako wapate kuzingatia  na waache ushirikina wao, wakumbushe kauli ya baba yao Ibrahim baada ya kuijenga Alkaaba. Alisema: Ewe Mola Mlezi! Ujaalie mji huu wenye Alkaaba uwe wa amani, ulindwe na wenye kudhulumu. Na unibaidishe, niwe mbali, mimi na wanangu na ibada ya masanamu.
Rudi kwenye Sura

36. Kwani masanamu yamepelekea kupotea watu wengi kwa kuyaabudu. Basi katika dhuriya zangu, wenye kunifuata mimi na wakakuabudu Wewe  kwa ikhlasi, basi hao ni watu wa Dini yangu. Na wenye  kuniasi kwa kushika ushirikina, basi Wewe ni Muweza wa kuwaongoa, kwani Wewe ni Mwingi wa maghfira na rehema.
Rudi kwenye Sura

37. Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewafanyia maskani baadhi ya dhuriya zangu katika bonde la Makka ambalo halioti mimea, kwenye Nyumba yako uliyo kataza isiingiliwe na kuvunjiwa hishima yake, na ukajaalia sehemu za jirani yake ziwe na amani. Ewe Mola wetu Mlezi! Wakirimu wapate kushika Sala karibu na Nyumba hii. Na zijaalie nyoyo za bora ya watu ziwapende  kwa kuizuru Nyumba yako. Na uwaruzuku matunda kwa kuletwa na hao watakao kuja, ili wapate kushukuru neema yako kwa Sala na Dua.
Rudi kwenye Sura

38. Ewe Mola wetu Mlezi! Ni sawa sawa kwako tunayo fanya siri na tunayo fanya dhaahiri. Kwani Wewe unajua maslaha yetu, na unatuonea huruma zaidi kuliko sisi wenyewe. Na hapana lifichikanalo kwako hata likiwa dogo, katika ardhi na katika mbingu. Basi hapana haja sisi ya kukuomba. Lakini juu ya hivyo tunaomba kwa kuonyesha kuwa sisi ni waja wako, twanyenyekea utukufu wako, na tunahitajia uliyo nayo, Wewe!
Rudi kwenye Sura

39. Alhamdulillahi, Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu, aliye nipa juu ya kuwa ni mzee wa miaka mingi, na nimekwisha kata tamaa ya kuzaa, Ismail na kisha Is-haq! Hakika Mwenyezi Mungu anasikia na ananipokelea maombi yangu.
Rudi kwenye Sura

40. Ewe Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nitimize Sala kwa inavyo takikana. Na wawezeshe watimilize kadhaalika wale walio wa kheri katika dhuriya zangu. Ewe Mola wetu Mlezi ipokee dua yangu kwa mapokezi ya kukubaliwa.
Rudi kwenye Sura

41. Ewe Mola wetu Mlezi! Nisamehe madhambi yaliyo niponyoka, na wasamehe wazazi wangu, na Waumini wote, Siku itapo hakikishwa hisabu, na baadae ikawa malipo.
Rudi kwenye Sura

42. Ewe Mtume! Wala usidhani kabisa kuwa Mola wako Mlezi ameghafilika na vitendo wafanyavyo wenye kudhulumu, kuupiga vita Uislamu na Waislamu wenyewe. Bali Yeye anaujua ukhalifu wao. Na amekadiria kuakhirisha kuwaadhibu mpaka Siku nzito. Macho yao yatabaki yamekodoka, hawawezi kuyafumba, wala kupepesa kwa kitisho watacho kiona.
Rudi kwenye Sura

43. Nao wako mbioni kumwendea anaye wita, vichwa vyao vimeelekea juu mbinguni, macho yao hayapepesi hata wakitaka, na nyoyo zao tupu hazina wazo lolote kwa wingi wa khofu.
Rudi kwenye Sura

44. Ewe Nabii! Waeleze watu khabari za vitisho vya Siku ya Kiyama watapo sema walio zidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na maasi: Mola wetu Mlezi, tuakhirishie adhabu, uturejeshe duniani, na utupe muhula kwa muda mdogo, walau tudiriki kuitikia wito wako wa Tawhidi na kuwafuata Mitume. Nao wataambiwa: Leo ndio mwasema haya? Na  mmesahau ya kwamba mliapa nyinyi ya kuwa mkifa neema hizi hazitokuondokeeni mtapo fufuliwa Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura

45. Na mkakaa duniani katika maskani zile zile za wale walio tangulia kuzidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na maasi miongoni mwa kaumu zilizo kuwa kabla yenu. Na ikadhihiri kwenu kwa kuona mabaki ya vile tulivyo waadhibu wao, na nyinyi msiwaidhike. Na tukakuelezeni waliyo yafanya wao, na nini kilicho wafika. Nanyi msizingatie.
Rudi kwenye Sura

46. Na wakapanga hao washirikina  njama zao kutaka kuvunja Daa'wa, yaani Wito. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hila zao.  Wala vitimbi vyao haviwezi kuiondoa Sharia iliyo thibiti imara kama milima.
Rudi kwenye Sura

47. Ewe Mtume! Usidhani kuwa Mwenyezi Mungu atawatupa Mitume wake kwa kwenda kinyume na ahadi aliyo wapa kuwa atawanusuru. Kwani Yeye daima ni Mwenye kushinda, hapana mmoja awezaye kumzuia kwa alitakalo, ni Mkali wa kulipiza kwa anaye mkanya na kumuasi.
Rudi kwenye Sura

48. Basi Mwenyezi Mungu atalipizia Siku ya Kiyama itapo geuzwa ardhi iwe ardhi nyengine sio hii ya sasa, na mbingu hali kadhaalika zigeuzwe ziwe nyengine, na viumbe watolewe makaburini mwao kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu asiye na mshirika, wala wa kumshinda.
Rudi kwenye Sura

49. Utawaona makafiri Siku ya Kiyama wamefungwa pingu pamoja na mashetani wao.
Rudi kwenye Sura

50. Ngozi zao zimepakwa lami inayo chiririka, imekuwa kama ndio nguo juu ya ngozi zao. Na moto umewapamba na kuwagubika nyuso zao.
Rudi kwenye Sura

51. Wanafanyiwa hayo ili Mwenyezi Mungu apate kumlipa kila mmoja wao kwa aliyo yachuma katika dunia. Na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu Siku ya Kiyama, wala hapana kitu cha kumshughulisha.
Rudi kwenye Sura

52. Hii Qur'ani ni Tangazo la kuwanasihi na kuwaonya na kuwakhofisha adhabu ya Mwenyezi Mungu, na ili wajue ya kwamba wakikhofu wakazingatia kuwa hakika hapana mungu ila Mungu Mmoja, na ili wenye akili wakumbuke utukufu wa Mola wao Mlezi, na kwa hivyo wajitenge mbali na yale yatayo waletea hilaki.
Rudi kwenye Sura