') //-->
1. "Alif Mym Ra" hizi ni harufi za kutamkwa zimeanzia baadhi ya Sura za Qur'ani. Nazo zinaashiria kuwa huu ni muujiza juu ya kuwa ni harufi wanazo zitumia Waarabu katika maneno yao ya kawaida! Na harufi hizi zilikuwa zikitamkwa huwavutia Waarabu waisikilize Qur'ani! Kwani wale mapagani (washirikina) waliambizana wasiisikilize hii Qur'ani. Ikawa Waumini wakianzia harufi hizi huvutia masikio ya washirikina wakawa wanasikiliza.
Hakika hizo Aya au Ishara tukufu ndio hii Qur'ani, Kitabu chenye shani kubwa, uliyo teremshiwa wewe Nabii kwa haki na ukweli kutokana na Mwenyezi Mungu, aliye kuumba, na akakuteuwa. Lakini wengi wa washirikina walio yakanya yaliyo kuja ya Haki si watu wa kuikubali Haki. Bali wao wanaipinga kwa inda.
Rudi kwenye Sura
2. Hakika aliye kiteremsha hichi Kitabu ni Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye aliye zinyanyua hizi mbingu mnazo ziona zenye nyota zipitazo bila ya nguzo mnazo ziona, wala hazijui mtu ila Mwenyezi Mungu, ijapo kuwa amezifunganisha hizo na ardhi kwa funganisho zisio katika ila akipenda Mwenyezi Mungu. Na amedhalilisha jua na mwezi chini ya Ufalme wake na kwa ajili ya manufaa yenu. Na jua na mwezi yanazunguka kwa mpango maalumu kwa muda alio ukadiria Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la. Na Yeye Subhanahu anapanga kila kitu katika mbingu na ardhi, na anakubainishieni Ishara zake za kuumba kwa kutaraji mpate kuamini kuwa Yeye ni Mmoja wa pekee.
Rudi kwenye Sura
3. Na Subhanahu, Mwenyezi Mungu Aliye takasika, ndiye aliye kukunjulieni ardhi, akaidhalilisha ili muweze kutembea juu yake mashariki na magharibi. Na Yeye akajaalia katika hii ardhi milima iliyo simama imara, na mito ya maji matamu inayo miminika. Na akajaalia kwa hayo maji matunda ya kabila mbali mbali yanayo zaliana, na kati ya kabila hizo namna mbali mbali, mengine matamu na mengine makali, mengine meupe, na mengine meusi. Na Yeye Subhanahu huufunika mchana kwa usiku. Na hakika katika huu ulimwengu na ajabu zake zimo alama wazi za kuthibitisha uwezo wa Mwenyezi Mungu na Umoja wake kwa anaye fikiri akazingatia.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia katika kila mimea dume na jike ili ipate kupandishika sehemu ya uke kwa chembe za uzazi zilioko katika sehemu za ume. Na kwa hivyo ndio huzalikana namna kwa namna na kwa wingi.
Rudi kwenye Sura
4. Na hakika hiyo ardhi nafsi yake ina maajabu. Ndani yake vipo vipande vilivyo karibiana, navyo juu ya hivyo vina udongo mbali mbali. Vingine ardhi yaabisi, na vingine vya rutba, ijapo kuwa ni udongo ule ule. Ndani yake yapo mabustani yaliyo jaa miti ya mizabibu, na ndani yake mazao mengine yanavunwa, na mitende yenye kuzaa, nayo ama iliyo kusanyika au iko mbali mbali. Na yote hayo ijapo kuwa inanyweshwa maji yale yale yanakhitalifiana kwa utamu wao. Na hakika katika ajabu hizi zipo dalili wazi za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa mwenye akili ya kufikiria.
Aya hii tukufu inaonyesha ilimu ya ardhi (Geology) na ilimu ya mazingira (Ecology) na athari yao juu ya sifa za mimea. Inajuulikana katika ilimu kuwa rutuba ya ardhi inategemea juu ya chembe chembe za maadeni zinazo khitalifiana kwa namna na ukubwa, na maji yanayo toka kwenye mvua, na hewa, na vitu vyenye asili ya uhai, kama mimea na vyenginevyo, ambavyo hupatikana juu ya udongo au ndani yake. Huwapo hivyo kwa mamilioni vidogo vidogo hata havionekani kwa jicho tu. Kwa jumla ukizingatia haya utaona yanaonyesha uwezo wa Muumba na busara ya uumbaji, kwani ardhi kama wasemavyo wakulimu inakhitalifiana kila shubiri.
Na inajuulikana kwa wanazuoni wa sayansi kuwa ukipatikana upungufu katika hivyo vitu vya msingi katika udongo basi hudhihirisha upungufu wake katika mimea, na kwa hivyo wakulima hujalizia upungufu huo kwa kutia mbolea mbali mbali na hutengeneza hali ya mazingira. Na hayo yana athari zake juu ya mazao ikiwa kwa mmea wa namna moja au namna mbali. Ametakasika Mwenyezi Mungu ambaye katika mikono yake upo ufalme wa kila kitu, naye ni Muweza wa kila kitu.
Rudi kwenye Sura
5. Na hakika mambo ya washirikina juu ya dalili hizi ni ya ajabu. Ikiwa wewe Muhammad utas- taajabia jambo, basi la ajabu ni hiyo kauli yao wanapo sema: Ati baada ya kufa, na baada ya kwisha kuwa mchanga, tutakuwa wahai tena upya? Huu ndio mtindo wa wanao mkufuru Muumba wao. Akili zao zimefungwa na upotovu. Na marejeo yao ni Motoni watakapo dumu humo; kwani hao ni wenye kukanya juu ya kuwa mwenye kuweza kuanzisha anaweza kurejesha.
Rudi kwenye Sura
6. Na huko kupita mpaka upotovu kunawapelekea kutaka wateremshiwa adhabu haraka haraka badala ya kuomba hidaya itayo waokoa. Na wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu hawateremshii adhabu duniani akitaka. Na zimekwisha wapitia adhabu watu mfano wao kwa hayo, katika alio wateketeza Mwenyezi Mungu kabla yao. Lakini ni shani ya Mwenyezi Mungu kusamehe dhulma ya mwenye kutubia akarejea kwenye Haki, na kumteremshia adhabu kali anaye endelea na upotovu.
Rudi kwenye Sura
7. Na husema hao makafiri wasio amini muujiza mkubwa, yaani Qur'ani: Hebu na amteremshie Mola wake Mlezi alama ya unabii wake wa kuonekana kama kuiendesha milima akawa Mwenyezi Mungu anaonyesha wazi uhakika wa Nabii wake katika jambo hili! Na Yeye Subhanahu anamwambia: Hakika wewe ni Nabii wa kuwaonya kwamba kuna adhabu mbaya wakiendelea na upotovu wao. Na kila kaumu wanaye Mtume wa kuwaongoza kwenye Haki, na muujiza wa kubainisha ujumbe wake. Si wao wa kuchagua. Lao ni kujibu upinzani na kuleta mfano wake!
Rudi kwenye Sura
8. Aliye mpa Mtume huo muujiza mkubwa kabisa ni Yeye anaye jua kila kitu, na anazijua nafsi za binaadamu tangu kuumbwa kwao kutokana na mbegu za uzazi katika tumbo la mama mpaka wakati wa kufa kwao. Basi Yeye anaijua mimba anayo ichukua kila mwanamke kama ni mume au mke, kinacho punguka tumboni na kilicho zidi wakati, mpaka utimie muda wa mimba, na mtoto akamilike kukua, azaliwe. Kila kitu kwake Yeye Subhanahu kina kipimo maalumu, na muda maalumu.
Rudi kwenye Sura
9. Yeye anayajua ya ghaibu tusiyo yahisi, na tunayo yashuhudia kwa ujuzi zaidi kuliko tunavyo shuhudia sisi na kuona. Na Yeye Subhanahu ni Mwenye shani kubwa iliyo tukuka juu ya kila kiumbe.
Rudi kwenye Sura
10. Anazijua hali zenu zote katika maisha yenu, na maneno yenu na vitendo vyenu vyote. Basi anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza, vitendo na maneno. Na anajua vile mnavyo jificha usiku na kujitokeza mchana. Na yote ni sawa katika ujuzi wake.
Rudi kwenye Sura
11. Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika ndiye anaye kuhifadhini. Kila mtu anao Malaika wanao mlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu, na wanapeana zamu kumlinda mbele na nyuma yake. Na hakika Mwenyezi Mungu Subhanahu habadilishi hali ya watu kutoka shida kwendea neema, na kutoka nguvu wakawa dhaifu, mpaka wao wenyewe wageuze waliyo nayo kufuatana na hali wanayo iendea. Na Mwenyezi Mungu akitaka kuwateremshia watu maovu basi hawana wa kuwanusuru ataye walinda na amri yake, wala wa kuwatazamia mambo yao kuwakinga na yatayo wateremkia.
Rudi kwenye Sura
12. Na uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika ulimwengu unaonekana wazi, na athari zake zipo dhaahiri. Ni Yeye anaye kuonesheni umeme, ukakutisheni kuuona au mkakhofu isikujieni mvua wakati msio ihitaji ikakuharibieni mazao, au mkatumai kwa umeme itakuja mvua kubwa mnayo ihitajia kwa maslaha ya ukulima. Ni Yeye anaye yafanya mawingu yaliyo jaa mvua.
Rudi kwenye Sura
13. Na hakika radi zinamnyenyekea Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la kwa unyenyekevu ulio timia, mpaka ikawa sauti yake mnayo isikia ni kama kwamba inamtakasa na kumsabihi kwa kumhimidi, kumsifu na kumshukuru, kwa kuumba kwake kama ni ishara ya unyenyekevu wake. Na vile vile Roho safi msizo ziona, yaani Malaika, pia zinamtakasa Yeye. Na Yeye ndiye anaye peleka moto wa radi unao unguza ukampata amtakaye. Na juu ya kuwepo ishara hizi zinazo onekana zenye dalili ya uwezo wake Subhanahu wao bado wanabisha shani ya Mwenyezi Mungu Aliye takasika. Na Yeye ni Mwenye nguvu kubwa za kuvipinga vitimbi vya maadui.
Rudi kwenye Sura
14. Na hayo masanamu wanayo yaomba kwa woga na kutafuta amani badala ya Mwenyezi Mungu pekee hayawajibu wito na maombi yao. Hali yao ni kama mwenye kukunjua kiganja chake akinge maji ya kunywa na kiganja kisifike mdomoni. Na hali yao ikiwa ni hii, basi hizo dua zao haziwi ila kupotea na kukhasirika.
Rudi kwenye Sura
15. Na vyote viliomo mbinguni na duniani, vitu, watu, majini, na Malaika, vinamnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa matakwa yake na utukufu wake, vikitaka visitake. Hata vivuli vyao kadhaalika, vikirefuka na kufupika kwa mujibu wa nyakati za mchana adhuhuri na jioni, kwa kufuata anavyo amrisha Mwenyezi Mungu na anavyo kataza.
Rudi kwenye Sura
16. Mwenyezi Mungu amemuamrisha Nabii wake ajadiliane na washirikina kwa kuwaongoa na kuwabainishia. Akamwambia: Ewe Nabii! Waambie: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi, naye ndiye Mwenye kuzilinda, na Mwenye kuviendesha viliomo humo? Tena uwaeleze jawabu iliyo sawa hiyo wanayo ishindania. Waambie: Huyo ni Mwenyezi Mungu anaye abudiwa kwa haki, hana mwenginewe. Basi ni waajibu wenu mumuabudu Yeye peke yake. Tena waambie: Mnaziona dalili zilizo thibiti zinazo onyesha uumbaji wake kila kitu peke yake? Na juu ya hivyo mnawafanya masanamu kuwa ni miungu, bila ya kukubali kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja! Na haya masanamu hayajifai wenyewe kheri wala shari! Vipi basi mnayafanya sawa na Muumba Mwenye kupanga? Nyinyi mnafanya sawa baina ya Muumba wa kila kitu na asiye miliki kitu! Mmekuwa kama anaye fanya sawa baina ya viwili vinavyo gongana! Basi hebu ni sawa baina ya mwenye kuona na asiye ona? Je, giza totoro na mwangaza unao ng'aa ni sawa? Je, usawa huo unaingia akilini mwao? Au upotovu wao umepita hadi hata wanadai kuwa hayo masanamu yao ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika kuumba na kupanga, hata yakawadanganyikia wasijue mambo ya uumbaji, kama walivyo potea katika kuabudu? Waambie ewe Nabii! Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Muumba wa kila kiliopo. Na Yeye ni peke yake katika kuumba na kuabudiwa, Mwenye kushinda kila kitu.
Rudi kwenye Sura
17. Na hakika neema zake Mtukufu mnaziona, na masanamu yenu hayana athari yoyote katika neema hizo. Yeye ndiye anaye kuteremshieni mvua kutoka kwenye mawingu, na mito na mabonde yakamiminika maji, kila kitu kwa kadiri yake aliyo ikadiria Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa ajili ya kuzalisha mimea, na matunda ya miti. Na mito inapo miminika hubeba juu yake visio kuwa na manufaa, na huwa katika hivyo vyenye nafuu hubakia, na visio na faida hupita. Mfano wa hayo ni Haki na baat'ili, kweli na uwongo. Haki hubakia na baat'ili ikapita. Na katika maadeni yanayo yayushwa kwa moto kwa kufanyia mapambo, kama dhahabu na fedha, na yanayo tumiwa kwa manufaa mengine kama chuma na shaba, kadhaalika sehemu isiyo na faida huwa juu kama povu na hutupwa. Na yenye nafuu ndio hubakia. Kadhaalika katika imani. Potovu hupita, na iliyo ya kweli hubakia. Kwa mfano kama huu Mwenyezi Mungu Subhanahu anabainisha ukweli wa mambo, na hupiganisha mifano hii kwa hii ili yote yabainike wazi.
Rudi kwenye Sura
18. Watu kwa mujibu wa kupokea kwao uwongofu ni mafungu mawili. Fungu moja lilio itikia wito wa Mwenyezi Mungu Muumba Mwenye kupanga. Hilo litapata malipo mema duniani na Akhera. Fungu jengine lisilo itikia wito wa Aliye waumba. Hawa watapata malipo maovu Akhera. Na lau kuwa wanamiliki kila kiliomo duniani na mfano wake mara ya pili, hawawezi kujikinga na hayo malipo maovu! Lakini watapata kumiliki hayo? Kwa hivyo yao wao ni hisabu ya kuwaudhi, na wataishia katika Jahannamu, na huko ni pahali paovu mno pa kuishi.
Rudi kwenye Sura
19. Hakika walio ongoka na walio potoka hawawi sawa. Basi je, anaye jua ya kuwa uliyo teremshiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliye kulea akakuumba akakuteuwa kufikisha ujumbe wake, kuwa ni Haki isiyo na shaka yoyote...je huweza kuwa huyo kama aliye potea akaitupa Haki, hata akawa kama kipofu? Hakika hawatambui Haki wakazingatia utukufu wa Mwenyezi Mungu, ila watu wenye akili ya kufikiri.
Rudi kwenye Sura
20. Hao ndio wanao tambua Haki. Wao ndio wanao timiza ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyo juu yao kwa muujibu wa maumbile, na kwa muujibu wa maagano yao na ahadi zao walizo fungamana nazo; wala hawavunji maagano walio fungamana nayo kwa jina la Mwenyezi Mungu baina yao na waja wenzi wao, na kwa maagano makubwa walio jifunga nayo kwa maumbile yaliyo wafanya waitambue Haki na waamini, isipo kuwa walipo jipoteza wenyewe nafsi zao.
Rudi kwenye Sura
21. Hao ni Waumini; ada yao ni mapenzi na ut'iifu. Hao wanaamini mapendo baina ya watu, na wanahurumia jamaa zao, na wanawasaidia wenzi wao katika Haki, na wao wanaijua Haki ya Mwenyezi Mungu, na wanaiogopa hisabu ya kuwachusha Siku ya Kiyama, na kwa hivyo wanajikinga na madhambi kwa kadri wawezavyo.
Rudi kwenye Sura
22. Na wanavumilia maudhi wakitafuta radhi za Mwenyezi Mungu iwasaidie katika Njia ya kuwania Haki. Wanashika Sala kama inavyo pasa kusafisha roho zao, na kumkumbuka Mola wao Mlezi. Na wanatoa kutokana na mali aliyo wapa Mwenyezi Mungu kisirisiri na kwa dhahiri bila ya kutaka kuonyesha watu, na kwa maovu wanao tendewa wao wanalipa mema. Na wao kwa sifa hizi watapata malipo mema kwa kukaa katika ahsani ya nyumba, nayo ndiyo Pepo.
Rudi kwenye Sura
23. Hayo ndiyo malipo mema, ya ukaazi wa moja kwa moja katika Bustani za neema. Watakuwa wao humo pamoja na wazazi wao walio kuwa njema Imani yao na a'mali yao. Pamoja nao pia watakuwa na wake zao na dhuriya zao (wazao wao). Na Roho Safi zitawasalimu na kuwaingilia kila upande.
Rudi kwenye Sura
24. Hizo Roho zitawaambia: Amani ya milele ni yenu kwa sababu ya kuvumilia kwenu maudhi, na kusubiri kwenu katika kupambana na matamanio yenu. Ni mazuri mno haya malipo mnayo yapata, nayo ni kupata makaazi katika Nyumba ya Neema ya Peponi.
Rudi kwenye Sura
25. Hakika sifa za Waumini wema ni kinyume na sifa za washirikina waovu. Kwani washirikina huvunja ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo chukua kwao kwa mujibu wa maumbile na ambayo walijifunga nayo. Kwa hivyo wamekhalifu maumbile yao na akili zao kwa kuabudu mawe yasiyo wafaa wala kuwadhuru. Na wanavunja ahadi zao wanazo fungamana na waja wenzao, tena wanakata makhusiano yao ya mapenzi na watu, na makhusiano yao na Mwenyezi Mungu. Hawazifuati amri zake, wala hawamuabudu Yeye pekee. Na wanafanya uharibifu katika ardhi kwa uvamizi na kufanya uadui na kuvuka mipaka, na kuacha kuitengeneza dunia wakanafiika nayo! Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika hapendi uchafuzi na ufisadi.
Rudi kwenye Sura
26. Na ikiwa hao washirikina wanaona kuwa wao wamepewa mali mengi, na Waumini ni mafakiri, wanyonge, basi wajue kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu humpa riziki kunjufu amtakaye akizishika sababu na humdhikisha amtakaye. Basi Yeye humpa Muumini na asiye kuwa Muumini. Kwa hivyo msidhani kuwa wingi wa mali mikononi mwao kuwa ni dalili ya kuwa wao ndio wamo katika Haki. Lakini wao hufurahi kwa hayo mali walio pewa, juu ya kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu humpa dunia anaye mpenda na asiye mpenda. Na maisha ya duniani si chochote ila ni starehe duni yenye kupita!
Rudi kwenye Sura
27. Na hakika hao washirikina walio banwa na wingi wa pupa na papara husema: Je, huyu Nabii hakuteremshiwa muujiza mwengine kutoka kwa Mwenyezi Mungu? Ewe Nabii! Waambie: Sababu ya kutokuwa na Imani nyinyi si upungufu wa miujiza, bali ni upotovu tu! Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika na Aliye tukuka humwacha apotee anaye mtaka apotee, maadamu anaendelea katika njia ya upotovu. Na humwongoa aendee kwenye Haki yule ambae daima hurejea kwa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
28. Na hakika hawa wanao rejea kwa Mwenyezi Mungu, na wanaikubali Haki, ndio hao walio amini ambao nyoyo zao zinatua anapo tajwa na kukumbukwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Qur'ani au vyenginevyo. Na hakika nyoyo hazitulii na kutua ila kwa kukumbukwa utukufu wa Mwenyezi Mungu na uwezo wake na kuombwa radhi yake kwa kumt'ii.
Rudi kwenye Sura
29. Na hakika wanao inyenyekea Haki, na wakasimama kutenda vitendo vyema, hao watapata malipo mema, na mwisho mzuri.
Rudi kwenye Sura
30. Kama tulivyo wapelekea kaumu zilizo kwisha pita Mitume wakawaeleza yaliyo ya Haki, na wakapotea walio potea, na wakaongoka walio ongoka, na tukawapa miujiza ya kuonyesha Utume wao, kadhaalika tumekutuma wewe kwa umma wa Kiarabu na wenginewe, na kabla yao zimekwisha pita kaumu nyengine. Na muujiza wako ni hii Qur'ani uwasomee, uwawekee wazi maana yake na utukufu wake. Na wao wanaikanya rehema ya Mwenyezi Mungu walio pewa kwa kuteremshiwa Qur'ani. Basi ewe Nabii! Waambie: Mwenyezi Mungu ndiye aliye niumba, na anaye nilinda, na anaye nirehemu. Hapana mungu wa kuabudiwa kwa Haki ila Yeye. Namtegemea Yeye tu, na kwake ndio marejeo yangu na yenu.
Rudi kwenye Sura
31. Wao wanataka muujiza mwingine usio kuwa huu wa Qur'ani, juu ya ubora wa athari yake, lau kuwa kweli wanaitaka Haki na wanaikubali. Lau kuwa kuna Kitabu cha kusomwa kikaiendesha milima, kikapasua ardhi, au kikawasemeza maiti, basi Kitabu hicho kinge kuwa hii Qur'ani! Lakini watu hawa wana inda tu. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye amri yote katika miujiza na malipo ya hao wakanyao. Na katika hayo ana uwezo kaamili. Ikiwa hao wamo katika hali hii ya inadi, basi je walio it'ii Haki hawajakata tamaa bado na kuamini kwa hawa makafiri, na wakajua kwamba kufuru yao ni kuyakataa matakwa ya Mwenyezi Mungu? Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka waongoke watu wote basi wangeli ongoka! Na hakika uwezo wa Mwenyezi Mungu uko dhaahiri mbele yao. Basi haziachi balaa kali kali za kuwateketeza zikiwasibu, au kuwateremkia karibu yao, mpaka itimie ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo wapa. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu havunji miadi yake.
Rudi kwenye Sura
32. Na ikiwa hao wanao kanya wamekufanyia kejeli kwa hayo unao waitia na kwa Qur'ani, basi walifanyiwa maskhara vile vile Mitume walio tumwa kabla yako wewe, ewe Nabii. Basi usihuzunike, kwani mimi nawapa muhula tu hawa wanao kanya, kisha nitawatwaa, na hapo itakuwa adhabu kali isiyo wezekana kuelezwa wala kujuulikana hali yake.
Rudi kwenye Sura
33. Hakika washirikina wamefanya upumbavu katika kukanya kwao, wakamfanyia Mwenyezi Mungu washirika wa kuwaabudu. Kwani ati huyo ambaye ndiye Mwenye kuhifadhi na kuangalia kila nafsi, na kuipimia kwa kuilipa kheri na shari inayo ichuma, atakuwa wa kufananishwa na haya masanamu? Ewe Nabii! Waambie: Yaelezeni yalivyo kweli! Je, hayo masanamu ya hai? Yanaweza kujikinga na madhara? Yakiwa mawe hayanufaishi wala hayadhuru, basi mbona mnajidanganya nafsi zenu kuwa miungu hiyo ndio imemwambia Mwenyezi Mungu hayo ambayo mnadhani kuwa Yeye hayajui ya ardhi hii? Au mnaiweka kwenye cheo cha kuiabudu kwa maneno yanayo toka katika ndimi zenu? Hakika iliyopo ni kuwa watu hawa wamezugwa na mazingatio yao na mawazo yao ya upotovu. Na kwa sababu hiyo wameiacha Njia ya Haki wakabaki wakitanga tanga! Na wenye kupotea kama hao, basi hawana wa kuwaongoa yeyote, kwani wameziachisha nafsi zao Njia ya Uwongofu.
Rudi kwenye Sura
34. Duniani watapata adhabu kwa kushindwa na kutekwa na kuuliwa, ikiwa Waumini watakwenda katika njia ya Haki. Na hapana shaka adhabu ya Akhera itayo wateremkia ni kali zaidi na ya kudumu zaidi. Hapana wa kuwakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu Mwenye uwezo wa kila kitu.
Rudi kwenye Sura
35. Ikiwa hawa watapata adhabu hii, Waumini watapata Pepo na neema zake. Na hayo wamekwisha ahidiwa. Na hali ya Bustani walio ahidiwa wanao simama juu ya Haki na wakaweka kinga baina ya upotovu na Imani, ni kuwa itapitiwa chini ya miti yake maji matamu, na matunda yake ni ya daima hayasiti, na kivuli chake vilevile ni cha daima. Na haya ndiyo malipo ya wale wanao jikinga na shari. Ama makafiri wanao kanya, malipo yao ni kuingia Motoni.
Rudi kwenye Sura
36. Na wale ambao walio pewa ujuzi wa Vitabu vilivyo teremshwa ni waajibu wao wakifurahie Kitabu hichi ulicho teremshiwa wewe. Kwani hichi ni maendeleo ya ule ule ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Na wanayo ifanya dini kuwa ni sababu ya kufanya makundi mbali mbali wanayakataa baadhi ya uliyo teremshiwa kwa uadui na chuki tu. Basi ewe Nabii! Waambie: Hakika mimi sikuamrishwa ila nimuabudu Mwenyezi Mungu, na nisimshirikishe katika ibada yake na kitu chochote. Na kwendea kumuabudu Yeye peke yake ndio ninalingania, ninaita, na kwake Yeye peke yake ndio marejeo yangu.
Rudi kwenye Sura
37. Na kama vilivyo teremka Vitabu vya mbinguni, tumekuteremshia wewe hii Qur'ani ili iwe ni hakimu baina ya watu kwa yaliyo baina yao, na iwe ni hakimu wa Vitabu vilivyo tangulia kuwa ni vya kweli. Na hii Qur'ani tumeiteremsha kwa lugha ya Kiarabu. Wala usitake kuwafurahisha washirikina au Ahli Lkitab (watu wa Biblia), baada ya ufunuo na ilimu iliyo kufikia. Na ukitaka kuwaridhi basi hutakuwa na wa kukusaidia au kukulinda mbele ya Mwenyezi Mungu. Hapa anaambiwa Nabii, khasa wanasemezwa Waumini wote. Na mahadharisho ya Waumini ni kweli kweli hivyo; na kwa Nabii ni kwa ajili ya kubainisha kuwa juu ya kuwa yeye ni mteuliwa, na mtukufu wa daraja, bado anafaa kuhadharishwa.
Rudi kwenye Sura
38. Na ikiwa washirikina wanachochea watu wastaajabu kuwa wewe una wake na dhuriya, yaani wazao, na wanataka ulete muujiza mwengine usio kuwa Qur'ani, basi tulileta kabla yako Mitume wenye wake na wana vile vile. Kwani Mtume ni mwanaadamu, na ana sifa za kibinaadamu. Lakini yeye ni mbora kuliko wote. Wala Nabii hawezi kuleta muujiza kama apendavyo yeye au wapendavyo watu wake! Bali aletaye muujiza ni Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye anaye toa idhini. Kila kizazi katika vizazi kina amri yao aliyo waandikia Mwenyezi Mungu ya kuwasilihi. Na kila kizazi kina muujiza wake unao wanasibu. (Nabii Isa a.s. anasimuliwa katika Injili ya Yohana 5.30 kuwa alisema: Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe.)
Rudi kwenye Sura
39. Mwenyezi Mungu hufuta sharia na miujiza, na akaleta badala yake atakayo na akaithibitisha. Na kwake Yeye ipo asili ya Sharia zilizo thibiti zisio geuka, na ndio kwenye Umoja na asili ya fadhila zote, na mengineyo.
Rudi kwenye Sura
40. Na tukikuonyesha baadhi ya malipo au adhabu tulizo waahidi, au tukakujaalia ufe kabla ya hayo, ungeli ona kitisho kitacho washukia washirikina, na ungeli ona neema za Waumini! Lakini haya hayakukhusu wewe, juu yako wewe ni kufikisha Ujumbe tu, na kwetu Sisi peke yetu ndio hisabu.
Rudi kwenye Sura
41. Na hakika dalili za adhabu na kushindwa zipo! Hawaangalii kwamba Sisi tunazifikia nchi walizo kuwa wakizitawala zinachukuliwa na Waumini kidogo kidogo? Na kwa hivyo tunawapunguzia wao ardhi zilio wazunguka. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye wa kuhukumu kushinda na kushindwa, na thawabu na adhabu. Na wala hapana wa kuipinga hukumu yake. Na hisabu yake ni ya mbio mbio, haihitajii kupitiwa na wakati mrefu, kwani Yeye ni Mjuzi wa kila kitu. Basi ishara zipo!
Aya hii ina ukweli ulio fikiliwa na uchunguzi wa kisayansi za hivi sasa, ya kwamba imethibiti kuwa dunia inazunguka, na kuwa inayo mvuto kama simaku. Hayo yamepelekea kubabataa katika ncha mbili za kaskazini na kusini, North Pole na South Pole. Na hivyo ni kupunguka katika ncha mbili za ardhi. Na kadhaalika imejuulikana kuchopoka mbio za sehemu za gasi zilizo funika huu mpira wa dunia kukipindukia nguvu za mvuto wa ardhi, basi hutoka nje ya dunia. Na haya yanatokea mfululizo, na kwa hivyo ardhi, yaani dunia, inakuwa katika hali ya kupunguka moja kwa moja katika ncha zake. Haya yanakuwa kwa kuifasiri ardhi kuwa ni dunia, si nchi ya maadui wa Waumini. Yaelekea taf siri hii kwa Aya hii tukufu, ijapo kuwa wafasiri wengi wamefasiri kuwa muradi wa "ardhi" ni nchi za maadui.
Rudi kwenye Sura
42. Na walio kuwa kabla yao waliwapangia Mitume wao mipango ya uwovu. Lakini Mwenyezi Mungu Subhanahu ndiye Mwenye mipango yote kwa makafiri walioko sasa na walio watangulia. Na watapata malipo kwa wanayo yatenda, na Yeye anayajua ayatendayo kila kiumbe. Na ikiwa wao hawajui kuwa mwisho mwema ni wa Waumini, basi Siku ya Kiyama watajua kwa kuona nani atapata mwisho mwema kwa kukaa katika Nyumba ya neema.
Rudi kwenye Sura
43. Na hadi ya ushindani wao hao wanao kanya na hawaikubali Haki ni kukwambia: Ewe Nabii! Wewe si Mtume aliye toka kwa Mwenyezi Mungu! Basi waambie: Yanitosha mimi kuwa Mwenyezi Mungu ndiye wa kunihukumia mimi nanyi, na anaye ijua hakika ya Qur'ani na ajabu zake za miujiza ya kushangaza inayo ingia katika akili ziliyo nzima.
Rudi kwenye Sura