Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

107. SURAT AL-MAAU'N

(Imeteremka Makka)

Sura hii inahadithia khabari za mwenye kukadhibisha malipo ya Akhera. Ikataja katika sifa zake kuwa yeye anamdhalilisha yatima, na anamkemea kwa ukali, si kwa kumtengeza. Na kwamba yeye hamhimizi mtu yeyote, la kwa kauli wala kwa kitendo, kuwalisha masikini; kwa sababu huyo ni mchoyo kwa mali yake, bakhili kwa alicho nacho mkononi. Kisha Sura imewataja watu wa kikundi kingine wanao shabihiana na hawa wanao kadhibisha malipo. Hawa ni wale wanao ghafilika na Sala zao, ambao hawasali kama itakikanavyo, na ambao husimama kwa hayo kwa dhaahiri tu si kwa hakika. Ni wenye kuonyesha tu a'mali zao, wenye kuzuia msaada wao wasiwape wanao hitajia. Na Sura inawaahidi hao kuwa watapata misiba na maangamio, ili waache uasi wao.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Je! Umemwona anaye kadhibisha Malipo? *

2. Huyo ndiye anaye msukuma yatima, *

3. Wala hahimizi kumlisha masikini. *

4. Basi, ole wao wanao sali, *

5. Ambao wanapuuza Sala zao; *

6. Ambao wanajionyesha, *

7. Nao huku wanazuia msaada.  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani