Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

104. SURAT AL-HUMAZAH

(Imeteremka Makka)

Katika Sura hii kipo kitisho kikubwa kwa mwenye kuzoea kuwakebehi watu kwa ishara au kwa maneno, mwenye kukusanya mali mengi, akayahisabu kwa ajili ya fakhari, na kudhani kuwa mali yake yatambakisha milele duniani.
Na humo vile vile lipo onyo kubwa kwa hao kuwa watatiwa kwenye Moto mkali unao vuruga miili yao na nyoyo zao, na wanafungiwa milango, na juu ya hivyo watafungwa pingu humo basi hawataweza kutaharaki wala kutoka.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Ole wake kila safihi, msengenyaji! *

2. Aliye kusanya mali na kuyahisabu. *

3. Anadhani ya kuwa mali yake yatambakisha milele! *

4. Hasha! Atavurumishwa katika H'ut'ama. *

5. Na nani atakujuvya ni nini H'ut'ama? *

6. Moto wa Mwenyezi Mungu ulio washwa. *

7. Ambao unapanda nyoyoni. *

8. Hakika huo utafungiwa nao *

9. Kwenye nguzo zilio nyooshwa.  *  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani